Mwenye Hekima Alikuwa na Maana Gani?
KATIKA kitabu cha Mhubiri, Mfalme Sulemani mwenye hekima alitaja mingine ya mifululizo (mifuatano) isiyo na mwisho inayokamatana na dunia hii. Kizazi kimoja kinapita na kingine kinachukua mahali pake. Jua huchomoza na kutua. Upepo huendelea kuvuma toka pande mbalimbali. Maji ya mito huingia baharini wala hayaijazi.—Mhu. 1:4-7.
Baada ya hapo mwenye hekima alisema hivi: “Mambo yote yamejaa uchovu usioneneka, jicho halishibi kuona, wala sikio halikinai kusikia. Yaliyokuwako ndiyo yatakayokuwako; na yaliyotendeka ndiyo atakayotendeka; wala jambo jipya hakuna chini ya jua. Je! kuna jambo lo lote ambalo watu husema juu yake, Tazama, ni jambo jipya? Limekwisha kuwako, tangu zamani za kale zilizokuwa kabla yetu sisi. Hakuna kumbukumbu lo lote la vizazi vilivyotangulia; wala hakutakuwa na kumbukumbu lo lote la vizazi vitakavyokuja, miongoni mwao wale watakaofuata baadaye.”—Mhu. 1:8-11.
Kwa wazi Mfalme Sulemani alikuwa akikumbuka namna mambo yanavyotukia mara nyingi bila kuwa na mwisho aliposema hayo yaliyo juu. Kulikuwako mifululizo mingi sana ya mambo yaliyofanyika mara nyingi sana hivi kwamba mtu angejichosha ikiwa angejaribu kuyaeleza yote. Angekosa maneno ya kuyaeleza.
Mifululizo hiyo inaweza kuwa na matokeo juu ya mtu hivi kwamba tamaa yake ya kuona na kusikia haitoshelezeki bali awe anahitaji jambo jipya au la kiajabu. Hata hivyo, kwa kweli hakuna jambo jipya katika mifululizo ya asili au katika matukio ya kawaida ya maisha ya kila siku. Vizazi vya kale sana vilivyotutangulia vilipata kuona mifuatano iyo hiyo ya asili. Na katika mambo ya kibinadamu mambo yale yale yamepata kuonekana katika karne zote. Kumekuwa na maendeleo, kurudi nyuma, kukata tamaa, uonezi, upotovu, mapinduzi, yakifuatwa na uonezi na upotovu zaidi. Watu wamekuwa na matumaini, na tamaa zile zile pamoja na kujitakia makuu. Kisha, walipokufa, walisahauliwa na vizazi vilivyofuata baadaye. Hata watu waliojulikana sana walisahauliwa na waliokuwa wakiishi na mahali pao pakachukuliwa na wakuu waliokuwa wakiishi.
Habari hii ina faida gani? Inaweza kutulinda tusifuate sana isivyofaa miradi ya utafutaji wa mambo ya kimwili bila kumfikiria Muumba. Mambo yote ya kidunia tunayoweza kupata ni ya kitambo tu. Kwa hiyo, mahali pa kuyafanya kuwa miradi yetu mikubwa maishani, ni jambo bora zaidi kufurahia matunda ya kazi yako na kujifanyia jina jema na Mungu, awezaye kuturudishia uhai, na kutuwekea mbele yetu wakati ujao wa milele wenye furaha.