Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w77 8/1 kur. 345-349
  • Chemchemi ya Ukweli Katika Jangwa

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Chemchemi ya Ukweli Katika Jangwa
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1977
  • Vichwa vidogo
  • NILIVYOMTAFUTA MUNGU
  • KUISHI KUPATANA NA KWELI YA BIBLIA
  • KUSHINDA UPINZANI
  • NJIA MPYA YA MAISHA YENYE FURAHA
  • YEHOVA ATUTIMIZIA MAHITAJI NYAKATI ZA MAGUMU
  • BARAKA ZISIZOTAZAMIWA
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1977
w77 8/1 kur. 345-349

Chemchemi ya Ukweli Katika Jangwa

MIMI nilizaliwa Khartoum, na hilo ni jina la Kiarabu linalomaanisha “Mkonga wa Ndovu.” Lakini kwa sababu gani mahali hapo nilipozaliwa pakaitwa hivyo? Ni kwa sababu sehemu hiyo ya nchi inayogawanya Mito White Nile na Blue Nile karibu na mahali inapokutana ni nyembamba. Baada ya kukutana, mito miwili hiyo inaungana kuwa mto mmoja mkubwa uitwao Nile, unaotiririka moja kwa moja kupita Jangwa la Sahara. Wapelelezi na watu wengine wamesema mambo mabaya juu ya Khartoum, lakini bado huko ndiko “kwetu.”

Kwa kawaida jua huwa kali sana. Nchi hapa iko futi 1,200 (mita 360) juu ya usawa wa bahari, nalo joto jingi sana linafanya kuwe na jangwa lenye mchanga, kilomita moja au mbili tu kutoka kingo za mito yenye maji. Huku pia tunakuwa na kazi nyingi ya kufukuza-fukuza mainzi nyakati zote. Upepo huleta mchanga na kuumwaga juu ya kila kitu. Nyakati nyingine mchanga huo hufanya mchana uonekane kama usiku. Mara nyingi jamaa yetu hupeleka vitanda nje tupumue kidogo, halafu kwa ghafula upepo mkali uitwao haboob unakuja kutuangushia mchanga mwingi! Asubuhi tunafuta mchanga machoni na kuamka, kisha tunaona mchanga umejichora kama miili yetu katika magodoro.

Ndivyo mambo yalivyo Khartoum. Hapa ndipo nilipoolewa nikiwa binti mwaminifu wa Orthodox Coptic Church, nikalea jamaa yangu yenye wana watatu na mabinti wawili.

NILIVYOMTAFUTA MUNGU

Sikuzote nilimtafuta Mungu. Kila asubuhi nilikumbushwa kwamba si mimi peke yangu niliyefanya hivyo. Kabla ya jua kupanda nilikuwa nikisikia mwenye kunadi sala au muezzin akiimba king’ong’o katika minara ya misikiti mingi iliyotapakaa katika mji wote, naye alifanya hivyo mara tano kwa siku, jua likiwa limepanda. Mji wa Khartoum wenye sehemu tatu, Khartoum, Kartoum ya Kaskazini na Omdurman ni wa Waislamu hasa, kwa hiyo sisi tuliodai kuwa Wakristo wa Coptic Church tulikuwa wachache sana.

Nilitaka sana kumtumikia Mungu hata nilipokuwa mtoto nikafikiria kujiweka wakf niwe mtawa wa kike katika kanisa langu. Lakini nilikuwa na tashwishwi juu ya imani zangu na sherehe za mapokeo za Coptic Church. Niliona kwamba maandamano yenye mapambo mengi na madoido mengi yaliyohusika katika sikukuu za kanisa hayakupatana na maisha ya Yesu Kristo ya kikawaida tu. Siku nyingi pia sikulala nikifikiria mateso mabaya sana ya moto wa milele na mafundisho yenye kuvuruga akili yasiyoelezeka juu ya Utatu, nami sikuyaamini kamwe. Baada ya kuoana, mume wangu hakupendezwa sana na mambo ya dini, lakini mimi nilikwenda kanisani kwa kawaida pamoja na watoto wangu. Kwa hiyo jirani na watu wa ukoo wetu waliona “tunafaa” tulipoendelea kuishi katika nyumba yetu ya matope yaliyochomwa ya mto Nile, iliyokuwa nyuma ya kanisa zuri la Coptic.

Siku moja ya mwezi Agosti 1958 nilikuwa nyumbani nikishona kwa cherehani wakatiwa joto jingi. Nilikuwa nikimwomba Mungu kwa kimya anisaidie niipate kweli ili niweze kumwabudu yeye. Halafu mgeni akaja kwangu! Bila shaka aliiona misalaba na sanamu za kidini nilizopamba nazo kuta zangu, kuonyesha nilikuwa mwanadini. Bibi aliyenitembelea alikuja kuzungumza nami habari za Biblia. Nilishangazwa sana na jinsi alivyofungua maandiko ya Biblia kwa urahisi, kunionyesha kwamba vifaa hivyo vya kutumia katika ibada havikuwa vya Ukristo wa kweli.

Alishinda vipingamizi vyangu upesi kwa kuniambia nilete Biblia yangu mwenyewe nilipomwambia yake ilitofautiana na tafsiri yangu ya Kiarabu. Basi nikatokeza Biblia yangu ya Kiarabu iliyochakaa na kuchafuka kidogo, kisha baada ya muda mfupi ikaonekana wazi sikujua kutafuta maandiko. Mapadre hawakunitia moyo kamwe nichunguze yaliyomo kwa njia hiyo. Lakini nilifurahi sana nilipoelezwa kweli za Biblia juu ya Yesu Kristo, tumaini la wafu na habari nyingine nilizothamini. Mazungumzo yalipokwisha nikachukua kwa furaha vitabu viwili vya kunisaidia kujifunza Biblia.

Mgeni wangu alipoondoka niliruka-ruka nikijua kwamba nimejibiwa sala zangu Niliburudishwa na maji ya kweli katika jangwa hili.

KUISHI KUPATANA NA KWELI YA BIBLIA

Maisha katika ujirani wetu, unaoitwa E1 Masalama, Omdurman, si yenye kufurahisha. Mgeni tusiyemkaribisha katika nyumba yetu yenye dari na matofali ya matope ya kahawia alihangaisha sana watu katika ujirani wote. Nyumba yetu ilikuwa ya kikale sana hata ikilinganishwa na hali za Omdurman, na hata sasa mwanangu mdogo akumbuka wakati upepo wenye mchanga mwingi ulipopeperusha madirisha yetu, na mvua nyingi ikamiminika ikiingilia darini. Hata hivyo, sikuzote nilikuwa nimejaribu kufurahi kwa kumtafuta Mungu, na nilifurahishwa sana na kujifunza Biblia kila juma. Lakini watu wa ukoo wangu na rafiki zangu wa zamani hawakufurahi, bali sasa walizidi kutoa malawama mengi kwamba nilipendezwa na mgeni wangu aliyekuwa mwanafunzi wa Biblia.

Mwanzoni mwa mazungumzo yetu habari ya msalaba ilitokezwa. Sikuzote nilikuwa nimefundisha watoto wangu kufanya ishara ya msalaba waziwazi kama ilivyowezekana, maana nilidhani wangepata ulinzi kwa kufanya hivyo. Kila mmoja alivaa msalaba shingoni, nao ulikuwa kitu cha maana sana katika maisha yetu ya kidini. Kwa hiyo sikutaka kuiondoa misalaba hiyo, ingawa mgeni wangu alinisadikisha kwamba halikuwa jambo la Kikristo kutumia msalaba. Habari hizo zilikuwa zikiwaingia washiriki wengine wa jamaa. Mume wangu alinishauri nijihadhari na mgeni wetu mpya, akapendekeza tumkaribishe kama rafiki tu. Halafu mwanangu mkubwa akaanza kueleza mwalimu wake wa ibada ya watoto habari za “mhubiri” aliyekuwa akija nyumbani kwetu, akaambiwa kwa mkazo mwingi tusiwe na uhusiano wo wote naye kwa sababu ‘hakuwa mwema.’ Lakini, mimi nilitaka sana kumpendeza Mungu, na baada ya kujifunza miezi miwili, niliichukua misalaba yote ya kidini na picha nikazitupa katika shimo la takataka katika ua wetu.

Furaha niliyokuwa nayo ya kujifunza kweli mpya juu ya Yehova na kusudi lake ilinifanya niongee na watu wa ukoo wangu, rafiki na jirani kila nilipopata nafasi. Kwa sababu hiyo jirani walitupia ua wetu na nyumba yetu mawe wakati tulipokuwa tukijifunza Biblia. Mapadre wa kanisa na watu wa ukoo walijaribu kutukomesha mara kwa mara tusijifunze.

Kila mwaka, jamaa yetu ilikuwa ikisherehekea Karamu ya Mariamu. Mimi nilikuwa nikioka keki maalum, halafu tukawa tukisherehekea wakati huo wa pekee. Lakini sasa nilikuwa nimejifunza katika Biblia kwamba Mariamu alipata watoto wengine pia baada ya Yesu kuzaliwa, nikashangaa sana. Niliposema nilikusudia kuacha kusherehekea Karamu ya Mariamu, binti yangu mkubwa alinihimiza sana niache kujifunza na mgeni mwenye kunifundisha Biblia. Nikaanza kuwaza, “Sababu gani niache kusherehekea karamu ya Mariamu?” Nikaamua hivi, “Bibi huyo akija tena, nitamwambia aweza kuwa akija kama mgeni, lakini si kuzungumza mambo ya dini.”

Nilihangaikia sana jambo hilo hivi kwamba, nilipoanguka katika sakafu ya jiko langu siku iliyotangulia muda wetu wa kujifunza tena Biblia, nilisema hiyo ilikuwa adhabu kutoka kwa Mungu kwa sababu ya nililokuwa nikifanya. Tazama tena! Mgeni wangu akafika tena. Badala ya kuja kesho yake alikuja siku iyo hiyo, akanikuta nikiwa na matope kila mahali kwa sababu ya kuanguka. Aliponisaidia nilimwambia nilivyokuwa nimekuwa nikiwaza, nami nikashangaa aliponikumbatia akanibusu. Baada ya kulizungumza jambo hilo tulisali pamoja tupate nguvu za kuendelea kuwa imara upande wa kweli ya Neno la Mungu. Ndipo tulipoacha kusherehekea karamu za Mariamu!

KUSHINDA UPINZANI

Jirani walianza kutuingilia, na wakati walipokuja nyumbani kwangu wakiwa na vijiti vya kumpiga rafiki yangu mpya, niliwakaribisha wao pamoja na mapadre walizungumze jambo hilo na mwanafunzi huyo wa Biblia katika nyumba yangu. Jioni iliyopangwa ilipofika, baada ya joto la mchana kumalizika, ilionekana kama kwamba watu wote wa El Masalama waliacha kwenda kwenye suks au masoko, wakaja kwangu. Nyumba ilijaa pomoni, na watu wengine walikuwa wakijazana nje katika ua, wengi wao wakiwa wamevaa kanzu nyeupe za Kisudan na vilemba. Mapadre hawakuja, lakini walisimama katika pembe ya barabara, na wakati mazungumzo yalipoendelea mashemasi na wajumbe wao wakawa wakikimbia-kimbia nje kupashwa habari wasizojua na wakuu hao wa dini.

Kulikuwa na makelele mengi jioni hiyo, huku mambo mengi yakizungumzwa, lakini nakumbuka mjumbe wa kanisa aliliambia kundi la watu, “Nyamazeni, mazungumzo haya yananifaidi.” Lakini, mwishoni akaniambia, “Usiache dini ya kanisa lako!” Huo ulikuwa usiku wa kukumbuka. Niliendelea kutetea kweli, ikaendelea kuniburudisha kiroho, kama kwamba ilikuwa chemchemi katika jangwa.

Lakini, jirani na kanisa halikutosheka. Waliendelea kuingilia mambo yetu. Walizidi kutupa mawe, hata wakatupa maji machafu mengi katika ua wetu wakijaribu kutisha jamaa yetu. Upinzani ulifikia upeo wakati jirani waliponishtaki kwa polisi juu ya kuingia nyumba zao bila ruhusa, kinyume cha sheria. Niliitwa mbele ya hakimu katika baraza ya mji, nikaelekeana na mawakili wawili wanaodhaniwa kuwa bora zaidi katika Omdurman. Adhabu ya kupatikana na hatia ingekuwa kifungo cha miezi mitatu na faini ya paundi 50 za Sudan (shilingi karibu 1,200 au 75Z). Lakini wakili mmoja alianza kuliepa suala, akisema utendaji wangu ulikuwa ndio “mwanzo wa mipango ya kuunda jamii yenye kufuata utaifa wa Kiyahudi katika Sudan.”

Akitoa hukumu yake, hakimu aliuliza, “Mbona ninyi nyote wateteaji mnamwonea mwanamke huyu?” Akaagiza kwamba nina uhuru wa kutangaza dini yangu katika Sudan yote nikitaka. Nilimshukuru Yehova kwa sababu ya matokeo ya kesi, lakini wakati huo sikujua jinsi ilivyokuwa kazi kubwa kuishuhudia kweli katika sehemu zote za nchi hii iliyo kubwa kupita nchi zote za Afrika. Lakini nilitaka kuzitangaza habari njema wakati wote kuonyesha nilimshukuru Yehova kwa sababu ya aliyokuwa amenifanyia.

NJIA MPYA YA MAISHA YENYE FURAHA

Sasa nikawa nikijifunza Neno la Mungu kila siku na kueleza wengine habari za ufalme wa Mungu. Nikawa nikiamka mapema na kufanya kazi zangu zote za nyumbani kabla ya saa 3 ya asubuhi; halafu baada ya kula fool, au kiamsha-kinywa cha maharagwe na mkate, nikawa nikiushuhudia Ufalme mpaka watoto wangu waliporudi kutoka shuleni saa 7:30 alasiri. Katika Sudan, shughuli za siku huamuliwa na joto la jua, nasi tuna rahat el zuhr, au kipindi cha adhuhuri cha kupumzika, kuanzia karibu saa 8 mpaka saa 11 jioni. Lakini niliweza kutoa ushuhuda saa 90 kila mwezi kwa kutumia vizuri nyakati za asubuhi. Nilikwenda na binti yangu mkubwa nyakati nyingi, nayo mikutano ya kujifunza Biblia ilifanywa nyumbani kwetu. Kikundi kilikuwa kidogo hata wakati huo, lakini kwa kusaidiwa na jamaa yangu kikaongezeka mara mbili. Mwanangu mdogo, aliyekuwa mwenye umri wa miaka saba wakati huo, akumbuka chai na keki tuliyokula baada ya mikutano hiyo. Alitazamia sana mikutano imalizike apate kula vitu hivyo ambavyo hatukula kwa kawaida nyumbani mwetu!

Mei 1959 mume wangu nami pamoja na watoto wetu wawili walio wakubwa zaidi tulibatizwa katika maji ya White Nile, kuonyesha tulikuwa tumejiweka wakf kwa Yehova. Siku chache baadaye, tulifurahi kutembelewa na msimamizi wa Watch Tower Society, Ndugu Knorr, aliyekuwa akipitia Sudan katika ziara ya kutumikia Afrika.

Hizo zilikuwa siku zenye shughuli nyingi. Sasa nilikuwa mhubiri “painia wa kawaida” wa habari njema. Karibu kila siku ningeweza kuonekana nikitembea haraka katika vichochoro vyenye kupitana vya barabara za mchanga za Omdurman zenye mashimo-mashimo na vinundu-vinundu​—nilipopitia kijia fulani ningeweza kuona mwuza-maziwa amemkalia punda wake kwa starehe akiwa amenyosha miguu na kukingamanisha nyayo zake shingoni mwa punda, huku madebe ya maziwa yakicheza-cheza kila upande, halafu nilipokwenda mahali pengine nilikuwa nikisimama kidogo ngamia avuke njia kuelekeza mzigo sokoni. Waislamu huweka vyungu vikubwa vya maji katika uvuli wa miti ya karibu barabara zote za Omdurman, yapate kunywewa na wasafiri wenye kiu. Lakini sasa sikuyathamini sana maji hayo. Nilikuwa nimeburudishwa na maji ya kweli, nikawa nimekaza nia kutafuta wengine waliotaka burudisho pia.

Nilijifunza na kila mmoja mmoja wa watoto wangu siku mbalimbali za juma. Mwanangu mdogo alijifunza kusoma Kiarabu kutokana na kitabu Kutoka Paradiso Iliyopotea Mpaka Paradiso Iliyopatikana, hata kabla hajaingia shule.

YEHOVA ATUTIMIZIA MAHITAJI NYAKATI ZA MAGUMU

Ndipo tulipopatwa ghafula na magumu. Mume wangu alifutwa kazi, tukawa hatuna mapato. Tungefanya nini? Niliuza vipambo vya dhahabu, mikeka mitatu na vitu vingine. Halafu tukaingilia njiwa wetu, nao walizaana kimwujiza muda huo. Mwanangu mdogo aliweza kupeleka sokoni wanne au sita kila siku, na kuwauza wawili wawili piaster 15 (karibu shilingi 3.15) Hata tulikuwa na njiwa wa kutosha kutupa sehemu kubwa ya chakula chetu cha kila siku. Yehova alitutimizia mahitaji yetu katika hali hizo karibu mwaka mmoja. Siku moja nilipokuwa nikijitayarisha kwenda katika utumishi wa Ufalme, niliona kwamba hatukuwa na piaster yo yote. Sasa ningefanyaje? Binti yangu aligundua mkebe wa zamani tuliokuwa tumetumia kuweka akiba ya piaster. Ulikuwa na pesa! Zilitosha kunipeleka katika eneo langu nikafanye utumishi na kununua chakula chetu cha siku.

Mwezi Machi 1962 nilikaribishwa niwe mmoja wa “mapainia wa pekee,” wanaotumia saa 140 au zaidi kila mwezi kueleza watu habari za Ufalme. Tangu wakati huo nimelifurahia pendeleo hilo.

BARAKA ZISIZOTAZAMIWA

Ndugu mmoja alitutembelea nyumbani kwetu mwanzoni mwa 1963 akanieleza habari za kusanyiko la Kikristo ambalo lingefanywa baadaye mwaka huo katika Munich, Ujeremani. Nilitaka sana kwenda huko nikawe pamoja na ndugu zangu wengine wa Kikristo, lakini ilielekea kutowezekana! Halafu, siku sita baadaye, binti yangu mkubwa akapata kazi ya kusafiri kwa ndege akiwa mtumikia-abiria. Hivyo niliweza kupata tikiti ya kwenda na kurudi kwa kiasi cha chini sana, nikafurahi sana kwamba ningeweza kukusanyika na watu wengi wenye imani kama yangu huko Munich.

Mwanangu wa pili na binti yangu mdogo walibatizwa 1962, naye mwanangu mdogo akabatizwa 1965. Nimefurahi kuona wakitia juhudi wamtumikie Yehova. Binti huyo alianza kutaka kumtumikia Yehova wakati wote naye amekuwa Shahidi “painia wa kawaida” tangu 1968. Mwaka 1971 alijiunga nami kuwa “painia wa pekee,” na ameendelea kuwa na pendeleo hilo hata alipoolewa na mtumishi wa huduma wa kundi letu. Mwanangu aliye mdogo zaidi kati ya wale watatu ana kazi inayompatia riziki pamoja na mkewe na kumwezesha afurahie pendeleo la kutumikia kama mtumishi wa huduma kundini.

Maisha yetu yamekuwa na maendeleo mengi wakati ambao tumetanguliza faida za ufalme wa Mungu. Sikuzote tumejaribu kutanguliza mambo ya kiroho mbele ya mambo ya kimwili, nasi tumebarikiwa kusaidia watu zaidi ya 30 waweke maisha zao wakf kwa Yehova na kubatizwa. Lakini tumefanikiwa katika njia nyingine pia. Tangu nilipohudhuria kusanyiko huko Munich, washiriki wa jamaa yangu na mimi mwenyewe tumehudhuria makusanyiko mengine ya Kikristo ya mataifa yote katika Ulaya na sehemu mbalimbali za Afrika. Baada ya upungufu wetu wa pesa kumalizika, tulitoka Omdurman tukahamia Khartoum, na sasa tuna nyumba kubwa kiasi cha kuweza kuwa na mikutano humo ya kundi linalozidi kupanuka nyakati zote.

Mwanangu wa pili aliamua kuwa na masomo ya juu shuleni kwa kuingia chuo kikuu Misri. Lakini baada ya mwaka mmoja tu alirudi nyumbani kwetu kushirikiana kabisa na jamaa atumie nguvu zake kuendeleza ibada ya kweli Sudan. Sasa yeye ni mzee, nao ujuzi wake na kujitoa kwake kunasaidia sana na kuthaminiwa na kundi.

Mtu mwenye kiu nyingi peke yake ndiye anayejua hasa ubora wa kupata chemchemi katika jangwa. Anafurahi hata zaidi kuona wengine wakiburudika. Hivyo ndivyo maji ya ukweli yamenibariki mimi na jamaa yangu, nasi twamshukuru sana Chemchemi ya Ukweli, Yehova Mungu wetu.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki