Utendaji wa Ufalme Waanza Angola
MWAKA 1938 ndipo mbegu ya kwanza ya Ufalme ilipopandwa Angola. Eneo hili la karibu maili 481,000 ya mraba liko kati ya Afrika ya Magharibi-Kusini na Zaire, ambayo iko kaskazini mwake, na Zambia upande wake wa mashariki.
Mapainia wawili kutoka Cape Town walitembea huko 1938 wakafanya kazi kati ya weupe. Kwa miezi mitatu waliangusha Biblia, vitabu na vijitabu 8,158, wakaamsha kupendezwa kwa watu. Lakini, Vita ya Ulimwengu ya Pili ilitokea mwaka uliofuata ikawa vigumu sana kuendelea kuonana na wenye kupendezwa.
Miaka kumi na miwili baadaye, mwaka 1950, painia Mwafrika alifukuzwa nchi ya Msumbiji. Hakufanyiwa kesi, bali alipelekwa kwenye kisiwa kidogo cha Kireno cha São Tomé katika ikweta mbali na pwani magharibi ya Afrika. Eneo hilo lilitiwa ndani ya sehemu zilizostahili kufanywa na Angola. Baada ya miezi sita walikuwako wengine kumi na watatu wakishiriki pamoja naye kutoa ushuhuda katika kisiwa hicho.
Miaka miwili baadaye kikundi hicho kidogo katika São Tomé kiliongezeka kufika wahubiri 21. São Tomé na kisiwa jirani cha Principe zina eneo la maili 377 tu za mraba na zina jumla ya watu 64,000. Ni koloni la kuadhibia watu la Waafrika Wareno ambao wanafanya kazi kama watumwa katika mashamba ya mpira, ndizi na kahawa. Kwa hiyo kikundi kidogo cha wahubiri wa Ufalme wa huko kililazimika kuendesha shughuli chini ya magumu, bila ya kutembelewa wala kutiwa moyo na mtu. Mpaka hapo, hakukuwa na wahubiri wala tengenezo la kazi ya Ufalme Angola.
Lakini, mwaka wa 1954, barua zilipokewa katika tawi la Afrika Kusini kutoka kwa kikundi kidogo cha Waafrika katika Baía dos Tigres (makao ya kupashia adhabu yanayoshikamana na kituo cha kuvulia samaki kusini kabisa ya Angola). Mwandikaji, João Mancoca, alisema katika mojawapo ya barua zake hivi: “Kikundi cha mashahidi wa Yehova katika Angola ni chenye washiriki 1,000. Kiongozi wao ni Simão Gonçalves Toco.” Kuna hadithi ya kupendeza sana juu ya maneno hayo yenye kusisimua.
Mwaka wa 1943, Simão Toco huyo alikuwa kiongozi wa jamii ya waimbaji iliyohusiana na kanisa la Kibaptisti katika Léopoldville, Belgian Congo (Kinshasa, ambayo sasa yaitwa Zaïre). Alikuwa msimamizi hodari wa jamii ya waimbaji nacho kikundi kiliongezeka kikawa na mamia ya watu. Alipata vijitabu viwili vya Watch Tower Society akavisoma akipendezwa. Toco aliandikia ndugu wa Brooklyn apate vitabu zaidi vya Sosaiti. Kidogo kidogo, alitia mafundisho ya Ufalme katika nyimbo zake za kidini (alizotunga mwenyewe), na katika mazungumzo yake na washirika wake wakubwa wa uimbaji. Lakini, wafuasi wa Simon Kimbangu, waliozoea uchawi, walipenya katika vikundi vya Toco vya kujifunza. Mwaka wa 1949 walijisikia wakitaka kwenda wakaeleze wengine mambo hayo na wengi wao walikwenda kuhubiri katika mji wa Leopoldville. Lakini, muda si muda Toco na kikundi kikubwa cha wafuasi wake walikamatwa wakatiwa gerezani. Alipokuwa gerezani, Toco aliacha kutumia vitabu vya Sosaiti na hata Biblia, na kwa kuwa walitegemea ujumbe uliotoka kwa wachawi, kweli ilifunikwa na uchawi wa Kimbangu. Wengi waliokuwamo katika kikundi hicho walikuwa wa Angola. Kwa hiyo, baada ya kukaa miezi kadha jela, waliokataa kabisa kuacha kumfuata Toco walirudishwa Luanda. Walikuwa karibu 1,000.
Kati ya walioondolewa nchini wakapelekwa Angola alikuwako João Mancoca, Mwafrika mwenye akili na mwenye kujali mambo ya kiroho. Siku ya kujaribiwa kwake alishtakiwa kuwa mfuasi wa “Watchtower movement” (au Kitawala) iliyohusiana na dini ya Kimbangu, ambayo ilikuwa madhehebu marufuku ya Kiafrika. Hakimu alijaribu kumwachilia, mradi aikane imani yake. Ingawa Mancoca hakukubali baadhi ya mafasirio ya Toco, hasa mazoea yake ya uchawi, alijua kwamba Toco alikuwa amemweleza kiasi fulani cha kweli, tena alijua angeipoteza kweli akiacha aliyokuwa amekubali. Hivyo alionelea afadhali kutiwa gerezani kuliko kuacha kweli ndogo aliyokuwa nayo. Wakuu Wareno hawakuwa wameamua chanzo cha kikundi hicho na watakalowafanyia. Waliwadhani walitaka kupindua serikali kwa siri; hata hivyo washiriki wa kikundi hicho walielekea kuwa watu wanyofu sana wasiodhuru mtu. Mwishowe, walitawanyika vikundi vikundi kwenda sehemu nyingi za Angola. Toco na wengi wa kikundi chake walipelekwa kaskazini ya Angola wakafanye kazi katika shamba la kahawa. Mancoca, akiwa na kikundi kingine, alikuwa Luanda.
Katika Luanda, Mancoca alijaribu kuwasihi watumie Biblia na kuacha kuzoea uchawi. Akiwa pamoja na Sala Ramos Filemon na Carlos Agostinho Cadi, Mancoca alijitahidi kufanya kweli ya Biblia ishinde. Mwafrika mmoja alikuwa amepata vitabu vyetu “The Kingdom Is at Hand” na “The Truth Shall Make You Free” katika Kifaransa ili vitumiwe na mwanawe shuleni, lakini alipoona havikufaa kusudi hilo alimpa Mancoca. Hilo lilimsisimua sana pamoja na wenzi wake wachache waliothamini kweli kabisa. Halafu Toco alipelekwa kusini akapitia Luanda akielekea huko. Alikuwa mchawi thabiti sasa naye alikataza wafuasi wake wasitumie Biblia. Ilikuwa wazi wafuasi wake wa dini ya “Kimbangu” walikuwa wamemvuta sana wakamwondoa katika Neno la Mungu. Mancoca na kikundi chake hata hivyo walifadhaishwa na hilo wakasali kwa Yehova miezi mitatu awafungulie njia ya kupashana habari na Watch Tower Society.
Baadhi ya wafuasi wa Toco hawakupenda kweli alizokuwa akifundisha Mancoca. Kwa hiyo, walikana kwamba hawakuwa wa kikundi hicho kidogo mbele ya wakuu Wareno kisha wakakishtakia uongo wa kuwa watungaji wa mojawapo la mafundisho ya uongo ya Toco. Mancoca na rafiki zake walifungwa siku 21 katika kijumba cha jela chenye giza. Mlinzi mmoja aliwapelekea taipuraita kwa siri na mishumaa kadha. Walitumia nuru ya mishumaa kunakili kwa siri nakala za vijitabu vya Sosaiti kwa mfano wa hati. Waliondolewa wakapelekwa katika koloni la kuadhibia watu katika Baía dos Tigres, hukumu yao ya kifungo cha miaka minne ikarefushwa kuwa miaka sita—kwa sababu ya kushtakiwa uongo!
Mancoca na washiriki wake walikuta wafuasi wengine wa Toco katika Baía Tigres, wakawatia moyo wajifunze Biblia, lakini ilikuwa kazi bure. Ndipo Mancoca alipoamua kutafsiri sura kadha za “The Truth Shall Make You Free” (alichokuwa nacho cha Kifaransa) kukiingiza katika Kikongo, lugha yao wenyewe. Wakati huo mfuasi mmoja wa Toco aliandikia tawi la Sosaiti la Salisbury akajibiwa kwa Kispania, asiweze kusoma. Alimletea Mancoca barua hiyo. Hivyo Mancoca alipata anwani ya Sosaiti, basi yeye na wenzake wakaandikia tawi la Rhodesia kwa Kifaransa, nayo barua yao ikapelekwa kwenye tawi la Afrika Kusini. Kwa njia hiyo kikundi hiki katika Baía dos Tigres kiliandikiana barua na tawi hilo kwa miezi mitatu na kupokea vitabu pia.
Brooklyn walipofikiwa na habari za kikundi hicho kigeni, walipanga karibuni mmisionari Mwingereza, John R. Cooke, aliyekuwa amekaa Ureno miaka kadha akawa mfasaha kutosha wa lugha ya Kireno, aende Angola. Ndugu Cooke alifika Angola Januari 21, 1955. Mtu wa kwanza kuzungumza naye alikuwa wakili katika Luanda, akamshauri John ajiangalie sana, kwa maana kikundi cha Toco kilichukuliwa kuwa maharamia wa “Mau-Mau” au watu wenye kutumiwa na Wakomunisti.
Yalikuwa maono mageni kwa Ndugu Cooke kutembea katika barabara za miji kama Luanda na Benguela, kuona washiriki wa kikundi hiki wakiwa wamevaa nishani zao za nyota, wakamshangaza kama kweli walitazamiwa kuwa ndugu au walikuwa Wakomunisti waliojisingizia! Aliongea faraghani na wachache kati yao katika Lobito na Benguela, lakini zaidi ya kugundua kwamba walikuwa na Biblia, alipogundua walijua jina la Yehova na walifanya mikutano mara kwa mara, hakuweza kuendelea. Kulikuwa na kikundi kikubwa katika Luanda. Alisema nao na kuzungumza na halmashauri yao. Lakini watu hao walikuwa wafuasi wa Toco na kwa kweli hawakupendezwa na Watch Tower Bible and Tract Society. Aliyekuwa tofauti ni kijana Antonio Bizi, aliyefurahia sana ziara za Ndugu Cooke akasaidia wengine waandikishe magazeti ya Sosaiti.
Baada ya Ndugu Cooke kutolea tawi la Afrika Kusini katika Elandsfontein maoni yake ya kwanza, alipokea maagizo ajaribu kuonana na Mancoca na rafiki zake katika Baía dos Tigres. Lakini Baía dos Tigres ni kituo kidogo cha kuvulia samaki katika pwani ya jangwa lenye mchanga katika kusini kabisa ya Angola. Haina uhusiano mkubwa na nchi za nje, nayo husimamiwa kwa uangalifu sana na serikali, kwa maana ni koloni la kuadhibia watu. John Cooke alishangaa atakalofanya muda mrefu. Alisali kwa Yehova. Mwishowe, aliandikia Gavana Mkuu katika Luanda barua akamweleza agizo lake na kumwomba amhoji. Baada ya juma tatu za kutaka kujua matokeo, aliitwa amwone Bwana Santana Godinho, msaidizi mkuu katika usimamizi wa gavana. Wakati wa mazungumzo hayo marefu bwana huyo alimhoji Ndugu Cooke maulizo mengi juu ya kazi na imani za Mashahidi wa Yehova. Mwishowe, alikubali kwamba Ndugu Cooke aweza kwenda Baía dos Tigres. Ndipo alipomshangaza kwa kumwambia: “Hata tutakupa bure tikiti ya kwenda na kurudi kwa ndege!” Hiyo ilikuwa safari ya maili 1,200!
Siku chache baadaye, ndege ndogo yenye viti sita ilizungukazunguka juu ya makao yenye jua ya Baía dos Tigres ikatua katika kijia cha saruji kilichojengwa juu ya mchanga. John Cooke alitoka na abiria wengine. Baada ya magumu fulani, Ndugu Cooke alifanya mkutano wake wa kwanza na kikundi kidogo cha huko. Ilikuwa siku kuu kwa Mancoca. Alikuwa amesali akangoja miaka mingi aione siku hiyo—akutane mwishowe na Sosaiti iliyofundisha kweli! Alivaa mavazi yake bora akasoma karatasi ndefu ya kumkaribisha mjumbe wa Sosaiti. Lo! jinsi Ndugu Cooke alivyopendezwa kukuta wenye mfano wa kondoo waliotaka sana kujua habari za Ufalme! Alitumia kila jioni na Waafrika hao wanyenyekevu na wanyofu, akizungumza nao Neno la Mungu na kuwaeleza habari za kazi. Walimwonyesha kitabu kinene cha karatasi nyembamba. Kilikuwa na tafsiri ya lugha yao, Kikongo, ya vijitabu The Kingdom, the Hope of the World na The Last Days. Kitabu hicho kilikuwa kimefanywa na kuandikwa kwa mkono, nao walikitumia muda mrefu kama kimojawapo cha vitabu vyao vikuu vya mafundisho. Ndugu Cooke alishangaa kujua kwamba walikuwa wamekwisha pata ufahamu wa kutosha wa kweli kwa kusoma vitabu walivyopokea kutoka Elandsfontein.
Kwa sasa Ndugu Cooke alikuwa katika mnara wa kuongoza wasafiri usiku, akikaa na mwangalizi wa hapo. Mtu huyo alipendezwa akaandikisha magazeti yote mawili na kuagiza Biblia. Akasema: “Bwana Cooke, wewe hutumia wakati wako wote ukiwa na Waafrika. Namna gani sisi weupe? Mbona usitupangie mkutano?” Aliwapangia, na Jumapili moja hotuba ya watu wote ilipotolewa katika kimojawapo cha viwanda vyenye kunuka samaki, watu 80 walihudhuria—weupe 10 na weusi 70. Huo ulikuwa ndio mkutano wa kwanza wa watu wote katika Angola! Kesho yake Ndugu Cooke aliwaacha akaruka kwa ndege kama alivyokuwa akifanya kila juma, akifurahia sana kikundi hicho kidogo, akiwa na barua kiliyoandikiwa kikundi cha Toco kuwaeleza alikuwa nani na kuwatia moyo wamkubali kama mjumbe wa Sosaiti. Alitumaini kusikiwa zaidi na vikundi hivyo mbalimbali.
Ndugu Mancoca akumbuka ziara hii ya Ndugu Cooke, akisema: “Sikuwa na shaka tena kwamba hili ndilo tengenezo la kweli lenye kusaidiwa na Mungu. Sikuwa nimewaza wala kuamini kwamba tengenezo lo lote jingine la kidini lingefanya jambo kama hilo: bila malipo, kupeleka mmisionari kutoka mbali akatembelee mtu asiye wa maana ati kwa sababu aliandika barua tu.”
Lakini huko Luanda, halmashauri ya Toco haikupendezwa na barua ya Mancoca. “Yeye ndiye nani atuambie la kufanya? Sasa, kama Toco ndiye angalikupa barua kama hiyo, mambo yangalikuwa tofauti.” Kwa hiyo aliamua kumtembelea Toco mwenyewe.
Bwana Santana Godinho alipelekewa ripoti kumweleza kifupi yaliyotukia katika safari, na maoni ya John Cooke juu ya watu aliokuta. Karibuni aliitwa ahojiwe tena. Santana Godinho aliithamini ripoti hiyo. Alieleza kwamba, ingawa maoni ya wakuu yalikuwa kwamba madhehebu ya Toco ilikuwa ikitaka kweli kupindua serikali, yeye na wengine walitilia mashaka maoni hayo. Kwa hiyo, walifurahi kuwa na mtu ambaye angeweza kuwaendea wapate kujua habari za kweli. Ndipo alimpomtolea Cooke toleo jingine la kushangaza. “Sasa, ungependa kwenda wapi kwingineko, Bwana Cooke? Wewe sema tu unakotaka nasi tutakupa bure tikiti ya kwenda na kurudi!” John aliomba akamwone Toco mashambani karibu na Sá de Bandeira, mji mkubwa kiasi katika sehemu ya kusini ya kati ya Angola. Aliruhusiwa.
Muda mfupi baadaye, Ndugu Cooke alihojiana sana na Toco mara mbili, mkuu wa serikali akiwapo. Toco, ambaye alikuwa kijana mrefu na mwenye akili, alisema kwamba alifurahi kukutana na mtu wa Watch Tower Society. Yeye na Ndugu Cooke walizungumza Maandiko na habari za kuundwa kwa kikundi, kisha akaandikia wafuasi wake wote wa Angola barua, akawaambia kwamba Bw. Cooke ni mjumbe wa Watch Tower Society alikotoa vitabu. Baada ya matembezi kadha ya sehemu hiyo akiwa mgeni wa Gavana. Ndugu Cooke alirudi Luanda akidhani pengine kikundi hicho cha watu 1,000 kingekubali kweli kwa urahisi zaidi.
Lakini huko Luanda halmashauri ya Toco haikutaka kusikia lo lote juu ya kweli. Wao ndio waliokuwa mabwana-wakubwa na hawakutaka mtu mwingine ye yote aanze kuwasimamia. Hiyo ndiyo iliyokuwa nia ya kiongozi wa hapo, David Dongala, ingawa watu wengi walipendezwa kutosha. Lakini, wakati uliotumiwa Luanda haukupotea bure. Ndugu Cooke alitoa ushuhuda mwingi akafanikiwa sana, akapata maandikisho 22 siku moja. Vilevile, alikuwa ndiyo kwanza aanze kupata mafunzo ya Biblia kwa jamaa moja au mbili za weupe na washiriki wa kikundi cha Toco.
Baada ya safari yenye matukio ya kwenda Cela, koloni jipya la ukulima, hali ilibadilika sana. Santana Godinho aliondolewa katika cheo chake cha kuwa msimamizi wa serikali. Alikuwa amemsaidia sana Ndugu Cooke katika mgawo wake mgumu akiwa mwenye urafiki sana. Sasa asingepata tena tikiti za kusafiri bure, na ombi lake la kukaa miezi mitano zaidi lilikataliwa. Ndugu Cooke aliondoka Juni 1955, akimshukuru sana Yehova kwa msaada aliopewa na pendeleo la kufikia watu kwa njia bora na kupanda mbegu nyingi katika eneo jipya.