Jitihada za Ushujaa Zaendelea Angola
JUNI 1956, Mancoca na ndugu saba wengine wapya katika Baia dos Tigres walikuwa mashujaa wakachukua hatua ya kuandikia gavana wa Wilaya ya Mocamedes barua, ambako Baia dos Tigres ilikuwa. Walisema hivi, kwa ufupi: ‘Kwa heshima nyingi sana twakuomba ewe Mheshimiwa upendeleo wa kututambua kama washiriki halali wa Sosaiti ya mashahidi wa Yehova.’ Ndugu hao waliomba wawe na uhuru zaidi wa ibada, lakini walijibiwa kwa kuonewa zaidi. Hata hivyo, kumi kati yao walibatizwa mwaka wa 1956.
Wakati huo, katika kisiwa cha Sao Tome, ndugu kadha walikuwa wametoka katika kizuizi cha miaka saba. Kati ya waliofunguliwa wakarudishwa Msumbiji alikuwako mwangalizi-msimamizi wa zamani.
NURU HAIMALIZWI
Nuru ya kweli ilikuwa ikimulika Angola, nayo isingemalizwa yajapokuwako magumu. Tena, shamba lenye Wazungu lingepata faida ya nuru hiyo.
Oktoba 26, 1956, Mervyn Passlow, na mkewe, Aurora, walifika Luanda waendeleze kazi iliyoanzwa na John Cooke. Ndugu Cooke alikuwa amepelekea akina Passlow orodha yake ya waandikishaji na watu wenye kupendezwa Luanda. Lakini anwani zote za waandikishaji zilikuwa na visanduku vya barua, maana hakuna barua zinazopelekwa nyumbani kwa watu; kwa hiyo kwa muda fulani walishindwa kupata watu hao. Ndipo ilipokuja barua kutoka kwa Ndugu Britten, mwangalizi wa tawi katika Lisbon, akawaeleza mwanamke mwenye kupendezwa sana aitwaye Berta Teixeira anarudi Luanda. Mwanamke huyo alishangaa sana akina Passlow walipomtembelea mara tu alipofika. Walianza funzo la Biblia naye na jamaa yake bila kupoteza wakati. Naye aliwasaidia kuhusu anwani za waandikishaji, maana mmoja wa jamaa zake alikuwa mfanya kazi katika Afisi ya Posta. Hesabu kubwa ya waandikishaji walipendezwa sana kujifunza. Baada ya juma kadha wote hao walianza kuzungumza na rafiki na jirani zao. Akina Passlow walikaribishwa watembelee watu hao kila jioni na alasiri nyingi; baada ya muda wa miezi sita watu zaidi ya 50 walikuwa wakifunzwa.
Muda mfupi baada ya kufika, akina Passlow walianza kupokea barua pia kutoka kwa ndugu Waafrika na watu wenye kupendezwa katika sehemu mbalimbali za Angola. Ingawa Ndugu Mancoca alikuwa kizuizini bado katika Baia dos Tigres, aliandikia akina Passlow barua za kuwatia moyo. Ndugu Waafrika wa huko wenye kuhitaji msaada wa kiroho waliwatembelea pia. Kwa sababu ya hali iliyokuwako, na kwa sababu ya kuwa mgeni, Ndugu Passlow hakwenda katika mikutano yao. Lakini Antonio Bizi, aliyependezwa sana Ndugu Cooke alipokuwako, alikuwa akiwatembelea kwa kawaida afunzwe Biblia na kuzoezwa ili naye aweze kusaidia ndugu wengine Waafrika. Waafrika pia walipata vitabu vingi, nao walipeleka vingi sehemu za ndani ndani za nchi.
Miezi kadha baada ya akina Passlow kufika, walianza mafunzo ya kawaida ya gazeti Mnara wa Mlinzi katika chumba chao. Lakini kufika mwishoni mwa mwezi wa kwanza chumba hicho kilikuwa kidogo mno. Ndipo Dada Teixeira, aliyekuwa na shule ya kufunza lugha, alipowatolea darasa moja la ndani katika chuo chake. Kwa kuwa alifunza watu mpaka saa 3 ya usiku, mikutano yote ya wakati wa juma ilianza baada ya saa 3 ya usiku. Kwa njia hiyo wasingejulikana sana.
Barua ziliendelea kuja kutoka sehemu zote za Angola. Waandikaji walikuwa Waafrika, na wote walijidai kuwa ndugu. Lakini wakati huo vita ilikuwa ikivuma Angola na haikuwezekana kufikia watu hao.
Mara baada ya hapo, Bwana Vieira Goncalves na mkewe walianza kufunzwa. Mume alikuwa amejifunza upadre miaka sita, lakini alishangazwa sana na mwenendo wa vijana waliokuwa wakijifunza upadre hata akaacha kabla hajawa padre. Alifanya maendeleo haraka akawa akija mikutanoni na kuanza kuongea na rafiki zake. Baada ya miezi miwili alikuwa amekwisha anza kuongoza funzo na jamaa nyingine.
Baada ya Ndugu Passlow kukaa miezi minane katika Luanda, aliamua kwamba wakati ulikuwa umefika wa kuwa na ubatizo, kwa maana watu kadha walikuwa wamesema wanataka kuonyesha wamejiweka wakf. Jinsi walivyoshangaa na kufurahi ndugu mmoja wa Ureno alipofika siku hiyo—Ndugu Henrique Vieira, akielekea Afrika Kusini! Kwa hiyo, kabla ya ubatizo, Ndugu Vieira alitoa hotuba, akasimulia mambo yaliyoonwa kisha akawabatiza katika ghuba, Luanda.
Muda mfupi baadaye, Ndugu Passlow alikataliwa ombi lake la kuongezewa muda wa kukaa nchini. Alifanya haraka akamkaribisha Ndugu Gongalves aanze kuangalia kikundi hicho kidogo. Ndugu huyo mwaminifu aliendelea na kazi hiyo karibu miaka tisa mpaka alipokamatwa, akatiwa gerezani na mwishowe akafukuzwa aende Ureno, ingawa alikuwa kitoto katika kweli alipoanza kazi hiyo.
Ndugu Passlow alikuwa amechukua hatua wakati uliofaa kabisa. Siku chache baadaye gari la makachero (polisi wa siri) lilisimama kando ya akina Passlow wakiwa katika shughuli mjini, kisha mapolisi sita wakatoka na kuwazunguka kama kwamba walikuwa wahalifu wakubwa. Walipelekwa chumbani mwao wakanyang’anywa mali zao nyingi—kutia na maandishi ya Aurora yaliyohusu upishi, ati kwa sababu yalionekana kama kwamba yana mambo fulani ya siri! Mapolisi walipokuwa wakitoa nje akiba yao ya Biblia, Ndugu Passlow alisema: “Natumaini mtazisoma.” Mmoja akajibu: “Zinahusu mchezo wa mpira?”—wote wakacheka. Mapolisi walijua sana kwamba walikuwa wakitenda kama vibaraka wa askofu wa Luanda. Akina Passlew waligundua baadaye kwamba mwanamke mwenye kupendezwa alikuwa ameeleza askofu mambo yote mema aliyokuwa akijifunza.
Walitaka rufani kwa Balozi Mwingereza, aliyekuwa Mkatoliki thabiti, lakini ikakataliwa. Ndipo kamishna wa polisi alipowaita akina Passlow wafike afisini pake. Akawaambia lazima waondoke nchini juma hiyo. Maelezo yake yalionyesha wazi alikuwa akidhani akina Passlow walikuwa wa “Watchtower movement” (Kitawala) yenye sifa mbaya ya Afrika ya kati. Ilikuwa kazi bure kujaribu kumweleza.
Juni 27, 1957, akina Passlow waliingia melini kuelekea Afrika Kusini. Kwa sababu ya hali ya mapolisi, walionya ndugu, hasa Waafrika, wasije kuwaona wakiondoka. Lakini kifungo cha upendo kilikuwa kingi mno. Mapolisi waweko au wasiweko, akina ndugu, kutia na Waafrika wengi, walikwenda kusema ‘Adeus’ (Kwa heri)! Kabla hawajaanza kupanda ubao wa kuingia melini, mmoja wa ndugu hao Waafrika aliyekuwa ndiyo kwanza afunguliwe gerezani katika Baia dos Tigres alikaribia, akashindika bahasha katika mkono wa Ndugu Passlow kisha akatoweka katikati ya kundi hilo la watu. Bahasha hiyo ilikuwa na zawadi ya pesa za kumwaga, pamoja na ujumbe uliosema: “Za kununua mkate.” Meli ilipojikokota ikiondoka, akina Passlow walishukuru sana kwa furaha nyingi sana waliyopata wakisaidia wengine wapate kumjua Mungu wetu Yehova.
Muda fulani baadaye, akina Passlow walipata habari kwamba kesho yake radio ilitangaza nchi hiyo ilikuwa imeondoa hatari kubwa ya mume na mke wageni waliokuwa wakijaribu kuleta mambo ya Ukomunisti na ya “Mau-Mau,” “lakini, shukrani na apewe Mungu wetu, maana sasa hatari hiyo imeondolewa!” Miezi mingi baadaye, vita ya maharamia ilipozidi kuwa kali, magazeti ya Angola yalitangaza kwa uongo kwamba wamisionari wa Watchtower walikuwa wameongoza Waafrika waingie katika matendo ya kiharamia. Hata kulikuwa na picha zilizosemekana zilionyesha wamisionari wakiwapa Waafrika pesa za Kiamerika ili wapinge wakuu weupe!
Ni kweli kwamba wamisionari wa Jumuiya ya Wakristo na viongozi wa dini walihusika sana katika uharamia Angola. Lakini sivyo mashahidi wa Yehova! Asante kwa fadhili zisizostahilika za Yehova, maana wamisionari wa Watchtower walikuwa wamefaulu kuingia nchini. Ingawa kulikuwa na matatizo na upinzani mwingi, ilikuwa imewezekana kuanza tengenezo dogo la ndugu 54 waliokuwa wamekaza nia kusimama imara na kuangaza nuru ya kweli Angola.
Baada ya wasiwasi uliotokea Ndugu na Dada Passlow walipoondoka, ndugu waliendelea mbele kwa unyamavu na uaminifu. Hawakuwa na mtu aliyekomaa wa kuwafundisha, lakini walifanya mikutano na kuhubiri kadiri ambavyo ndugu waliweza katika hali hizo zenye magumu.
Mwaka wa 1958, Harry Arnott, mwangalizi wa eneo la dunia, aliwatembelea kifupi, akatia Waafrika na Wazungu pia moyo mwingi. Mwaka wa 1959 alirudi Luanda tena akiwa mwangalizi wa eneo la dunia. Alipofika katika uwanja wa ndege, mapolisi walitokea ghafula wakamkamata pamoja na wote waliokuwa wakimlaki wakati uo huo. Ndugu Arnott alitenganishwa na wengine apate kuulizwa maulizo. Mkoba wake ulipekuliwa sana. Alisali orodha ya waandikishaji wa Mnara wa Mlinzi katika mji wa Luanda isionekane na mapolisi. Orodha hiyo yenye thamani nyingi ilikuwa katika kifuko cha tikiti cha Ndugu Arnott. Ingawa mkuu mwenye kuchunguza aliitazama tikiti, hakuiona orodha. Baada ya kumwuliza maulizo mengi sana, mkuu huyo alisema: “Bw. Arnott, wewe kumbuka hivi: Ukiwa Angola umekwisha, ukaisha, ukaisha, nalo tengenezo Watchtower limekwisha, likaisha, likaisha!”
Muda mfupi baadaye alipelekwa kwenye jengo jingine walikokuwa ndugu wale wengine, kutia na Ndugu Mancoca. Mkuu wa uchunguzi alimgeukia Ndugu Mancoca, akamtukana na kusema: “Wajua utakalotendewa?” Ndugu Mancoca alimtazama tu mtesi wake machoni na kusema: “Nimekwisha vumilia mengi, kwa hiyo jambo la pekee unaloweza kunifanyia ni kuniua, lakini sitaacha imani yangu.” Ndipo alipomtazama Ndugu Arnott akatabasamu kwa njia ya kumtia moyo. Ndugu Arnott asema: “Alionekana hakujali litakalompata na kwamba alitaka kuhakikisha mimi mwenyewe sikuvunjwa moyo na hali hiyo. Nilifarijika sana kumwona ndugu huyu Mwafrika akichukua msimamo huo wa imara na ushujaa baada ya kukaa gerezani miaka mingi.”
Ndugu Arnott alirudishwa katika ndege akalazimishwa kuondoka nchini bila kukawia. Kwa sasa, polisi walikuwa wamegundua kwamba kundi lilikutana katika nyumba ya Dada Teixeira. Kwa hiyo, wengine wao walikwenda huko bila kukawia wakapekue. Walitafuta, lakini wakashindwa kufungua mlango wa kwenda katika orofa ya chini, ambako karibu ndugu 50 na watu wenye kupendezwa walikuwa wakimsubiri Ndugu Arnott awatolee hotuba.
Wakati huo ndugu hao waliokuwa wamemlaki Ndugu Arnott, hata Mancoca mwenyewe, hawakupatwa na madhara makubwa. Alihojiwa kwa saa saba, na wakati huo mkuu mmoja aliagiza apelekwe gerezani. Lakini mwishoni mkaguzi alibadili nia akamwambia Ndugu Mancoca: “Nenda zako, Mancoca, na ujihadhari. Kesho niletee vitabu vyote vya Watch Tower ulivyo navyo nyumbani kwako. . . . Wewe iache shughuli hii ya Watch Tower ujitunze mwenyewe na watoto wako.”
Tukio hilo lilifanya kikundi hicho kidogo kibadili mahali pa kukutania, na baada ya hapo Waafrika wakaanza kujisimamia. Lakini, tengenezo la hapo lilikuwa dogo sana. Kilele cha wahubiri walioripoti mwaka wa 1960 kilikuwa 17 tu. Wakati huo ndipo Angola ilipoanza kusimamiwa na afisi ya Watch Tower Society katika Lisbon, Ureno.
Mwaka wa 1971, hesabu kubwa ya ndugu walikamatwa wakatiwa gerezani Luanda, kutia na ndugu yetu mwenye kujitoa sana, Mancoca. Lakini jitihada za adui ni ndogo sana zikilinganishwa na makusudi yasiyoshindika na uwezo mwingi sana wa Yehova. Hakuna kitu, hata kiwe nini, kiwezacho kuzuia ujumbe wa Ufalme usihubiriwe katika dunia yote inayokaliwa na watu, kutia na Angola.—1976 Yearbook.