Ni Nani Asiyehitaji Faraja?
NYAKATI nyingine tunahitaji sana kufarijiwa na kutiwa moyo. Sababu ni kwamba kuna mambo mengi sana yanayotukia maishani yanayoweza kuleta huzuni.
Huenda wazazi wakafanya kazi kwa juhudi sana waruzuku watoto wao. Lakini watoto wanapokuwa wakubwa huenda wakaasi na kuwaletea baba yao na mama yao huzuni nyingi na wasiwasi mwingi sana.
Huenda mwanamume akawa chombo cha kusingiziwa na kudhulumiwa katika mahali pake pa kazi. Huenda asipandishwe cheo kwa sababu dhamiri yake haimruhusu ajitie katika siasa ajapokuwa mwaminifu na hufanya kazi yake kwa bidii. Hata huenda watu wasioijua kazi yake wakamwambia namna ya kuifanya. Mwanamume huyo huenda akaogopa sana kwenda kazini, kwa kuona ugumu wa kuvumilia mambo mengi sana yanayomwudhi.
Huenda mtu mzima mwenye bidii sana akazuiwa kutenda na ugonjwa wenye kudhoofisha au msiba wenye kulemeza. Mtu huyo hawezi tena kufanya mambo yaliyomsaidia sana kupata furaha. Huenda akalazimika kupunguza maumivu makali sana kwa kutumia dawa zenye nguvu sana.
Tena ni nani kati yetu ambaye hajapata kuona huzuni nyingi sana juu ya kifo cha rafiki mkubwa au cha mshiriki wa jamaa? Huenda tukawa tulishuka (tulivunjika) moyo sana, tukawa wapweke na kujiona bila msaada hata kidogo.
Katika hali kama hizo, tunaweza kugeukia wapi tupate faraja? Hakika lingekuwa jambo lenye kutia moyo ikiwa tungepata chanzo ambacho kinaweza kutuambia namna wengine walivyoshughulika na magumu haya kwa kufaulu na ni kitu gani kilichowasaidia kuendelea wakati huo wa dhiki yao. Biblia inafanya vivyo hivyo. Inatoa habari ya kweli kuhusu yale yaliyowapata wengine na namna walivyovumilia majaribu haya bila kuona uchungu.
Tunasoma habari za Mfalme Daudi, ambaye mwanawe Amnoni alipata kuwa na hatia ya kufanya zinaa za maharimu (na dada yake) kwa kumshika dada yake kwa nguvu na kufanya ngono naye. Tena mwanawe Absalomu alihusika katika mauaji na katika mipango ya kumpindua baba yake ajitwalie kiti chake cha enzi. Vilevile katika wakati wa maisha yake, Daudi alipata kushutumiwa sana na ndugu yake mkubwa, akalazimishwa kuishi maisha kama ya haramia kwa miaka kadha huku akiwindwa kama mnyama na Mfalme Sauli mwenye wivu, akapata kuchongezwa mara nyingi, akasalitiwa na mshauri wake aliyemtumaini, na akapata kuwa mgonjwa na dhaifu.
Mfalme Sulemani mwenye hekima alionyesha uhakika huu ulio wazi kuhusu maisha: “Wenye mbio hawashindi mashindano ya kukimbia, wala walio hodari kushinda vita, wala wenye hekima pia hawana chakula, wala wenye ufahamu pia hawana mali, wala hata wale walio na maarifa hawana kibali; kwa sababu wakati na tukio lisilotazamiwa huwapata wote.” “Mimi nimeona watumwa wamepanda farasi, na wakuu wakienda kwa miguu juu ya nchi kama watumwa.”—Mhu. 9:11, NW; 10:7.
Bila shaka, wanaume na wanawake wote waliotajwa katika Biblia hawakushindana na magumu yale yale. Hata hivyo, tangu wakati maisha ya Habili yalipokatizwa kwa jeuri na ndugu yake Kaini, wanadamu wamepata kujua linalowapata watu wanapompoteza mpendwa wao katika mauti. Ibrahimu alimwombolezea mkewe mpendwa Sara. (Mwa. 23:2) Yakobo alipokufa, “Yusufu akamwangukia babaye usoni, akamlilia, akambusu.” (Mwa. 50:1) Daudi alililia kifo cha rafiki yake Yonathani kwa maneno haya: “Nimesikitika kwa ajili yako, Yonathani, ndugu yangu, ulikuwa ukinipendeza sana; upendo wako kwangu ulikuwa wa ajabu, kupita upendo wa wanawake.”—2 Sam. 1:26.
Wajapokuwa walipatwa na mambo machungu sana pamoja na magumu, Daudi, Naomi, Hana, Ibrahimu, Yusufu na wengine wengi wanaotajwa katika Biblia hawakujiachilia washindwe na huzuni. Tumaini lao katika Mungu liliwadumisha.