Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w79 9/15 kur. 21-24
  • Utendaji Wake Hodari Wakati Waamuzi Walipoongoza

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Utendaji Wake Hodari Wakati Waamuzi Walipoongoza
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1979
  • Vichwa vidogo
  • MTIWA MAFUTA WA YEHOVA
  • DALILI ZA MATENDO HODARI YA NYAKATI ZETU
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1979
w79 9/15 kur. 21-24

Utendaji Wake Hodari Wakati Waamuzi Walipoongoza

(Funzo la Kitabu hs 4:34-51)

1. Roho takatifu ilitendaje kazi kupitia kwa Mwamuzi Othnieli?

KWA sababu ya kuacha ibada safi, Waisraeli waliwekwa chini ya mamlaka yenye uonezi ya mfalme wa Shamu. “Kisha wana wa Israeli walipomlingana [Yehova], [Yehova] akawainulia wana wa Israeli mwokozi, aliyewaokoa, yaani, Othnieli mwana wa Kenazi, ndugu mdogo wa Kalebu.” Sasa ni nini lililotukia? “Roho ya [Yehova] ikamjilia juu yake, naye akawa mwamuzi wa Israeli; akatoka kwenenda vitani, naye [Yehova] akamtia huyo Kushan-rishathaimu, mfalme wa Mesopotamia, mkononi mwake; na mkono wake ukamshinda Kushan-rushathaimu. Nayo nchi ikawa na amani muda wa miaka arobaini.​​—⁠Amu. 3:9-11.

2. Roho takatifu ilitendaje kazi kupitia kwa Mwamuzi Gideoni?

2 Baadaye hali ziliharibika ikawa lazima Yehova ainue mwamuzi mwingine akomboe watu wake Israeli. “Wakati huo Wamidiani na Waamaleki, na hao wana wa mashariki walikutana pamoja; wakavuka na kupanga hema zao katika bonde la Yezreeli. Lakini roho ya [Yehova] ikaja juu ya Gideoni; naye akapiga tarumbeta; na Abiezeri Walikutanika na kumfuata.” (Amu. 6:33, 34) Kwa kumtumia mwanamume huyo mwenye imani, Yehova aliwapa watu wake ushindi mkuu, ushindi unaotajwa baadaye katika historia ya Biblia.​​—⁠Isa. 9:4-6; 10:26; Zab. 83:9-12; Ebr. 11:32, 33.

3. Roho takatifu ilitendaje kazi kupitia kwa Mwamuzi Yeftha?

3 Mara nyingi sana nguvu takatifu ya utendaji ya Yehova ilitenda kazi kwa ajili ya watu wenye imani ambao Yeye aliwatumia kufanya mambo yanayojulikana sana katika historia. Wakati mmoja ulikuwa ule Waisraeli wenye kuonewa walipokabiliwa na Waamoni wenye kutaka vita. ‘Ndipo roho ya [Yehova] ikamjilia juu yake Yeftha, naye akapita katika Gileadi . . . kuwaendea wana wa Amoni.” Akitaka sana kuona wakishinda na kuletea Yehova sifa, Mwamuzi Yeftha aliweka nadhiri yenye gharama (bei) nyingi kwake. Kwa hiyo Yehova akamtumia kuwapiga Waamoni.​​—⁠Amu. 11:29 mpaka 12:7.

4. Yehova aliinua nani aokoe Waisraeli mikononi mwa Wafilisti, naye alitumia nini?

4 Miaka mingi baadaye, Wafilisti waliwaonea Waisraeli sana. Kwa hiyo Mungu aliwezesha mwanamume mwingine asiye wa kawaida aliyeitwa Samsoni azaliwe. Alipaswa “kuwaokoa Israeli na mikono ya Wafilisti.” Kwa kusudi hilo, nguvu ya utendaji ya Mungu ilimwunga mkono. “Roho ya [Yehova] ikaanza kumtaharakisha katika mahane-dani, katikati ya Sora na Eshtaoli.” Hivyo Samsoni hakuonyesha nguvu nyingi kupita za mwanadamu ye yote aliyepata kuwa duniani akitumia uwezo wake mwenyewe.​​—⁠Amu. 13:5, 25.

5. Samsoni alifanya nini alipokutana na simba mwenye kunguruma, naye alimalizaje mambo wakati Wafilisti walipotumia hila kujua kitendawili chake?

5 Wakati mmoja, Samsoni alipokuwa akitembea peke yake, kwa ghafula alitokea mbele yake ,“mwana-simba akamngurumia.” Ikawaje kwa Samsoni? “Roho ya [Yehova] ikamjilia kwa nguvu, naye akampasua kana kwamba mwana-mbuzi, wala hakuwa na kitu cho chote mkononi mwake.” Muda mfupi baadaye Wafilisti walimdanganya wafanye kitendawili naye ili wamtie katika hasara kubwa. Badala ya kumshinda, Wafilisti wenyewe ndio walioshindwa. Tena, “roho ya [Yehova] ikamjilia juu yake kwa nguvu, naye akatelemkia Ashkeloni [katika Filistia], akapiga watu waume thelathini katika watu hao, na kuzitwaa nyara zao, na kuwapa hao waliokitambua kitendawili mavao hayo.”​​—⁠Amu. 14:5-19.

6. Jina la Samsoni lashirikishwa na nani katika Wae-wamemfunga kwa kamba mpya, mikononi mwa Wafilisti?

6 Hata kamba mpya hazikumshinda Samsoni nguvu alipokuwa akipelekwa, akiwa amefungwa kwa Wafilisti wenye chuki nyingi. “Ndipo roho ya [Yehova] ikamjilia kwa nguvu, na zile kamba zilizokuwa juu ya mikono yake zikawa kama kitani iliyoteketezwa kwa moto, na vile vifungo vyake vikaanguka mikononi mwake. Naye akaona mfupa mbichi wa taya ya punda, akautwaa, akapiga watu elfu kwa mfupa huo.”​​—⁠Amu. 15:11-15.

7, 8. Samsoni aliuaje Wafilisti wengi zaidi wakati wa kufa kwake kuliko wale alioua wakati wa kuamua Israeli?

7 Tendo kuu zaidi ambalo Mungu alifanya kupitia kwa Samoni juu ya Wafilisti waabudu wa mungu wa uongo Dagoni lilikuwa ndilo la mwisho. Lilionyesha kwamba roho ya Mungu haichoki wala kudhoofika.

8 Aliposalitiwa na mwanamke Delila akapofushwa na Wafilisti walipiza kisasi, Samsoni alisimama katikati ya nguzo mbili katika hekalu la Dagoni huko Gaza, Filistia. Akiwa hapo “Samoni akazishika nguzo mbili za katikati ambazo nyumba ile ilikaa juu yake, akazitegemea, moja kwa mkono wake wa kuume na moja kwa mkono wake wa kushoto. Samsoni akasema; Na nife pamoja na hawa Wafilisti. Akainama kwa nguvu zake zote; ile nyumba ikawaangukia hao wakuu, na watu wote waliokuwa ndani yake. Basi wale watu aliowaua wakati wa kufa kwake walikuwa wengi kuliko ,wale aliowaua wakati wa uhai wake.”​​—⁠Amu. 16:23-30.

9. Jina la Samsoni lashirikishwa na nani katika Waebrania 11:32-34?

9 Samsoni amepangwa kati ya watu wazamani waliomwamini Mungu, nayo imani ni tunda la roho Yake. “Nami niseme nini tena?” Ndivyo mwandikaji wa kitabu cha Waebrania anavyouliza katika sura ya kumi na moja, kisha ajibu hivi: “Maana wakati usingenitosha kuleta habari za Gideoni na Baraka na Samoni na Yeftha na Daudi na Samweli na za manabii; ambao kwa imani walishinda milki za wafalme, walitenda haki, walipata ahadi, walifunga vinywa vya simba, walizima nguvu za moto, waliokoka na makali ya upanga. Walitiwa nguvu baada ya kuwa dhaifu, walikuwa hodari katika vita, walikimbiza majeshi ya wageni.”​​—⁠Ebr. 11:32-34.

MTIWA MAFUTA WA YEHOVA

10. Ni badiliko gani lililotukia katika Daudi mara tu Samweli alipomtia mafuta Bethlehemu?

10 Jina mashuhuri ambalo mwandikaji wa Waebrania ataja ni lile la Daudi mwana wa Yese wa Bethlehemu. Alipokuwa mchungaji kijana, Daudi alitiwa mafuta na nabii Samweli awe mfalme-mkusudiwa wa makabila yote kumi na mawili ya Israeli. Mara tu baada ya kutiwa mafuta ikawaje? “Roho ya [Yehova] ikamjilia Daudi kwa nguvu tangu siku ile. Bali Samweli akaondoka, akaenda zake Rama. Basi, roho ya [Yehova] ilikuwa imemwacha Sauli [aliyekuwa mfalme wakati huo].” (1 Sam. 16:13, 14) Mwishowe Mfalme Sauli asiyeaminika aliendea mchawi-mke kwa kukata tamaa, ili amwezeshe kuongea na wafu, ikiwezekana. Muda mfupi baadaye alikufa katika vita waliyofanya na Wafilisti.

11. Mungu alishughulikaje na Daudi baada ya Mfalme Sauli kufia vitani?

11 Kwa habari ya Daudi, alianza kuingia katika ufalme ambao alikuwa ametiwa mafuta na Samweli awe nao. Mungu aliyemwabudu kwa uthabiti alimwezesha kufanya matendo hodari, hata kuitiisha Nchi ya Ahadi yote. Wala si hilo tu, bali Mungu alimwongoza kunena na kuandika unabii. Akawa nabii wa kweli: Kwa hiyo ‘ilipasa andiko litimizwe, ililolinena roho takatifu zamani kwa kinywa cha Daudi.’​​—⁠Matendo 1:16; 4:24, 25.

12. Sifa yaendea nani kwa sababu ya matendo hayo yote hodari, na kwa uhakikisho wa neno lake katika Zekaria 4:6, Zerubabeli na Kuhani Mkuu Yoshua walisherehekea tukio gani?

12 Lazima sifa imwendee Mungu mwenye nguvu nyingi mno zisizokwisha kwa sababu ya matendo hodari ajabu waliyofanya watu hao wa zamani. Matendo hayo ni pamoja na vitabu 39 vya Maandiko ya Kiebrania yaliyoongozwa na Mungu, kutoka Mwanzo mpaka Malaki. Katika kitabu cha unabii cha Zekaria, Gavana Zerubabeli atiwa moyo, ambaye alikabiliwa na kazi ya kujenga upya hekalu la Yerusalemu lililokuwa limeharibiwa na Wababeli mwaka 607 K.W.K. Alipewa agizo hili: “‘Si kwa kutumia jeshi, wala mamlaka, bali kwa kutumia roho yangu,’ Yehova wa majeshi amesema.” (Zek. 4:6, NW) Kwa kuungwa mkono na kitu chenye nguvu zaidi kuliko jeshi au nguvu nyingine yo yote ya kimwili, Gavana Zerubabeli na mfanya kazi mwenzake, Yoshua, Kuhani Mkuu, walistahimili upinzani wa adui na kwa hiyo wakapewa pendeleo la kusherehekea kukamilika kwa kujengwa upya kwa hekalu la Yehova Yerusalemu mwaka wa 515 K.W.K.

DALILI ZA MATENDO HODARI YA NYAKATI ZETU

13. Ni kwa njia gani matendo hodari wanayofanya wanadamu kwa nguvu za roho takatifu si mambo hakika ya historia tu?

13 Zerubabeli alipewa maneno yenye kumtia moyo yaliyoongozwa na Mungu zaidi ya nusu mileani (miaka elfu) kabla ya Wakati wa Kawaida wetu. Hata hivyo maneno hayo ni yenye maana kwetu leo sawa na yalivyokuwa huko nyuma siku za nabii Zekaria. Kwa sababu gani? Kwa sababu twaamini Yehova ndiye Chanzo cha Kimungu cha nguvu nyingi mno zipitazo za kibinadamu. Matendo hodari ya imani ambayo Mungu Mwenye Nguvu Zote alifanya kupitia kwa utendaji wa roho takatifu yake juu ya wanaume na wanawake wa zamani si mambo ya hakika tu. Yalikuwa dalili za matendo hodari ambayo Yeye angetimiza tangu wakati wa Masihi wake, Mtiwa Mafuta wake, na kuendelea mpaka kizazi chetu wenyewe.

14, 15. (a) Masihi aliyetabiriwa alijulishwa kwa watu na mtu aliyezaliwa kwa njia gani isiyo ya kawaida? (b) Mtangulizi wa Masihi angejazwa na nini tangu tumboni mwa mama yake, naye angefanya nini?

14 Masihi aliyetabiriwa alijulishwa kwa watu karne kumi na tisa zilizopita na mtu mwingine ambaye alizaliwa pia kwa mwujiza. Hakuzaliwa kwa nguvu za uzazi za baba na mama yake. Wakati huo walikuwa wamepita umri wa kuzaa. Nguvu zao za uzazi zilipaswa kufufuliwa ili wazae mtoto wao wa pekee, mwana ambaye baba yake, kuhani Zekaria, angemwita Yohana.

15 Alipokuwa akielezwa habari za kuja kwa mwana aliyetamaniwa sana, malaika Gabrieli alimwambia Zekaria hekaluni hivi: “Naye atajazwa [roho takatifu] hata tangu tumboni mwa mamaye. Na wengi katika Waisraeli atawarejeza kwa Bwana Mungu wao. Naye atatangulia mbele zake katika roho ya Eliya, na nguvu zake, ili kuigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto, na kuwatilia waasi akili za wenye haki, na kumwekea Bwana tayari watu waliotengenezwa.”​​—⁠Luka 1:5-17; linganisha Malaki 4:5, 6.

16. Kwa hiyo, Masihi wa kweli alipaswa kujijulisha mwenyewe kwa watu au alipaswa kujulishwaje?

16 Kwa kujulishwa kwa watu. na mtangulizi huyo, Masihi wa kweli hakupaswa kujitakia makuu na kujitangaza kwa taifa la Israeli kwamba ndiye Masihi akienda huku na huko kujitangaza ili awe na wafuasi. (Isa. 42:2-8). Bali, angejulishwa rasmi kwa wenye kutafuta Masihi na mtu aliyetumwa na Mungu na mwenye kuungwa mkono na Mungu.​​—⁠Isa. 40:3-5; Yohana 1:6, 7.

17. Yoeli 2:28-32 ilisema ni nini kingetukia baada ya Masihi kuja?

17 Baada ya Masihi kuja unabii wenye kuchochea wa Yoeli 2:28-32 ulipaswa kutimizwa: “Hata itakuwa, baada ya hayo, ya kwamba nitamimina roho yangu juu ya wote wenye mwili; na wana wenu, waume kwa wake, watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono; tena juu ya watumishi wenu, wanaume kwa wanawake, katika siku zile, nitamimina roho yangu. Nami nitaonyesha mambo ya ajabu katika mbingu na katika dunia, damu na moto na minara ya moshi. Jua litageuzwa kuwa giza, na mwezi kuwa damu, kabla haijaja hiyo siku ya [Yehova] iliyo kuu na itishayo. Na itakuwa ya kwamba mtu awaye yote atakayeliitia jina la [Yehova] ataponywa; kwa kuwa katika mlima Sayuni na katika Yerusalemu watakuwako watu watakaookoka kama [Yehova] alivyosema; na katika mabaki, hao awaitao [Yehova].”

18. (a) Kwa sababu ya unabii wa Yoeli, ni maulizo gani tunayopaswa kuuliza? (b) Kwa sababu gani mtu anapaswa sasa kuliitia jina la Yehova?

18 Sasa ndio wakati wa kuuliza, Ni nani wanaopokea kile ambacho Yehova aliahidi kumiminia kila namna ya mwili? Watu hao lazima watabiri wakiongozwa na nguvu ya kitu hicho chenye kumiminwa. Watabiri kwa wakati wake kwa kuwa matabiri yao yanapaswa kutangulia na kutabiri ‘kuja kwa siku ya Yehova iliyo kuu na itishayo.’ Watu wanaotii matabiri hayo huenda wakajikuta wakiwa kati ya waokokaji. Tukiamua kulingana na hali zote za nyakati zetu tangu mwaka wa 1914 W.K., ‘siku ya Yehova’ iliyoko mbele yetu yaonekana kuwa ‘kuu na itishayo’ kweli kweli. Je! sisi tunataka ‘kuokoka’? Ikiwa twataka, linakuwa jambo la maana ‘tuliitie jina la Yehova,’ Yeye ambaye roho yake inaendesha taratibu mpya inayokuja. ​—⁠Kutoka Holy Spirit​—⁠the Force Behind the Coming New Order, sura ya 4.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki