Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w84 2/15 kur. 22-23
  • “Alasiri Yenye Furaha Nyingi Sana” Katika Abidjan

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • “Alasiri Yenye Furaha Nyingi Sana” Katika Abidjan
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1984
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1984
w84 2/15 kur. 22-23

“Alasiri Yenye Furaha Nyingi Sana” Katika Abidjan

“HII ni alasiri yenye furaha nyingi sana kwa nchi ya Ivory Coast,” akasema A. D. Schroeder, mshiriki wa Baraza Linaloongoza la Mashahidi wa Yehova, alipokuwa akifungua programu ya kuweka wakf jengo jipya la tawi la huko Abidjan. Wageni 500 waliokuwako siku hiyo ya Februari 27, 1982, walikuwa na kila sababu ya kufurahi sana. Si kwamba tu hilo jengo jipya la kupendeza lilikuwa lenyewe kisababishi cha shangwe, bali pia lilikuwa ushuhuda wa kwamba Yehova amebariki jitihada zao katika shamba la umisionari huko Ivory Coast na Upper Volta.

Mwaka wa 1971 Sosaiti ilianzisha tawi huko Abidjan lifanye uangalizi juu ya kazi ya kuhubiri katika nchi hizo mbili. Lilikuwa na afisi moja na makao ya watu wanne katika kijumba cha orofa ya tatu. Kazi ilisonga mbele kwa haraka sana mpaka afisi ndogo hiyo ikawa haiwezi kulichukua furushi hilo baada ya muda mfupi tu. Kwa hiyo, mwaka wa 1978, uwanja fulani huko Deux Plateaux, ambacho ni kisehemu kilichoko maili nane kutoka katikati ya mji, ulinunuliwa uwe wa tawi jipya.

Ujenzi ulianza Juni 1, 1980. Wenye kujitolea kutoka makundi kumi na sita katika Abidjan ndio walioifanya karibu kazi yote. Kila Jumapili makundi manne yalikuwa yakipeleka wenye kujitolea 25 kutoka kila kundi, kutia ndani akina mama wenye kubeba vitoto migongoni, ili wafanye kazi huko. Mwishowe, jumla ya saa walizotumia ikawa 30,000, au ikawa ni kama watu kumi na wanne wamefanya kazi saa 40 kwa juma muda wa mwaka mzima. Mashahidi wawili wenye ujuzi wa kujenga walitoka Ufaransa kuja kusaidia ujenzi kwa muda wa mwaka mmoja. Hatua hiyo, pamoja na vifaa vilivyotolewa ama bure au vikatolewa na akina ndugu na watu wa kupendezwa kwa bei fulani, viliwezesha jengo hilo limalizwe likiwa limegharimu nusu ya kiasi ambacho lingaligharimu hata kama lingalijengwa na wajenzi watozao pesa za chini zaidi.

Sasa na tulizuru jengo hilo kwa haraka. (Angalia ule mchoro ulio juu.) Tukiisha tu kuingia katika mlango mkuu wa kuingilia, tunapanda ngazi mbili za vidato, tunapita vyombo vikubwa vya kupandia mimea ya sehemu zenye joto na maua, kisha tunaingia moja kwa moja ndani ya sebule lenye sakafu ya marimari. Upande wa kulia kuna Jumba la Ufalme lenye nafasi ya kukaliwa na watu 200. Upande wa kushoto kuna afisi tatu na vyumba vitatu vya kulalia. Huko juu kuna vyumba vingine vitano vya kulalia, sehemu ya kufulia nguo na kuzipiga pasi, jiko, chumba cha kulia chakula na maktaba yenye kuelekeza kwenye nafasi wazi ya nje kwenye dari juu ya Jumba la Ufalme. Huko chini kabisa ya jengo iko idara ya usafirishaji wa vitabu, chumba cha kazi ya fundi wa mbao na nafasi ya kuweka magari.

Wageni waliohudhuria programu ya wakf walivutiwa sana, na wengi wao walikuwa wamevaa mavazi ya kienyeji ya kupendeza sana. Walijawa na msisimuko na moyo wa kuthamini, si kwa sababu ya jengo jipya hilo tu bali kwa sababu hasa linaleta sifa na utukuzo kwa yule Mungu mwenye furaha, Yehova, aliyewapa ongezeko. Kweli ilikuwa “alasiri yenye furaha nyingi sana.”

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki