Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w85 10/15 uku. 26
  • Mahakama Kuu Zaidi ya Uturuki Yaachilia Mashahidi wa Yehova

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mahakama Kuu Zaidi ya Uturuki Yaachilia Mashahidi wa Yehova
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1985
  • Vichwa vidogo
  • Mahakama Yaamua
  • Kuondolewa Mashtaka Kunatamaniwa
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1985
w85 10/15 uku. 26

Mahakama Kuu Zaidi ya Uturuki Yaachilia Mashahidi wa Yehova

KULIKUWA na furaha kuu kati ya Mashahidi wa Yehova 23 walioachiliwa huru Juni 14, 1985, baada ya kukaa mwaka mmoja gerezani katika Ankara. Mwaka 1984 walikuwa wamehukumiwa vifungo vya kuanzia miaka minne mpaka sita na Mahakama ya Serikali ya Usalama katika Ankara? Mahakama hiyo ilikuwa imewaona kuwa wenye hatia ya kuvunja kifungu cha 163 cha sheria za utekelezaji wa adhabu, ambazo zinakataza utendaji wa kidini wenye shabaha ya ‘kubadili utaratibu wa serikali wa kijamii, wa kiuchumi, wa kisiasa, au wa kisheria wa serikali.’ Mahakama ilikataa msimamo wao wa kuwa dini.​—Ona Mnara wa Mlinzi (Kiingereza), Aprili 1, 1985.

Hukumu hiyo ilikatiwa rufani, na Mei 29, 1985, kesi ikakubaliwa kusikiwa mbele ya Mahakama Kuu Zaidi ya Uturuki. Kwenye kesi hiyo, ombi lilifanywa kufuta hukumu hiyo kwa msingi wa kwamba kweli Mashahidi wa Yehova ni kikundi cha kidini na kwamba hakuna ushuhuda wa kuonyesha kuwa walitenda uhalifu walioshtakiwa.

Wakili mwenye kuwatetea alionyesha kwamba katika kesi zote za mahakamani zilizotangulia kufanywa nchini, Mashahidi wa Yehova walikuwa wamehesabiwa kuwa bila hatia, na kwamba wastadi wote wa kisheria waliochunguza utendaji wa Mashahidi wa Yehova muda wa miaka 20 iliyopita hawakuwapata wakiwa wamevunja sheria kwa njia yo yote. Pia watetezi hao wa kisheria walionyesha kwamba hukumu hiyo ilitegemea ubaguzi na habari za uwongo.

Mahakama Yaamua

Siku ya Juni 19, 1985, Mahakama Kuu Zaidi ilitoa uamuzi wake uliokubaliwa na wote kwa jumla. Ilifuta hukumu ya Mahakama ya Serikali ya Usalama kisha ikaagiza wale Mashahidi 23 waachiliwe huru bila kukawia. Mahakama hiyo ilikazia kwamba chini ya katiba ya Uturuku dini zote zina haki ile ile moja ya kuabudu na kueneza imani zao, mradi hazijiingizi katika mambo ya Serikali.

Mahakama Kuu Zaidi ikaonyesha kwamba washtakiwa walikuwa wamefanyiwa mashtaka “kwa sababu tu ya kuwa ni... Mashahidi wa Yehova.” Na hukumu hiyo ilikuwa imetegemezwa juu ya ripoti za “wastadi” wawili wenye ubaguzi wa kidini. Hao walikuwa wamesema kwamba Mashahidi wa Yehova ni “watu wasiopendeza juu ya msimamo wa umoja wa kidini na ibada.” Lakini Mahakama Kuu Zaidi ilionyesha kwamba kwa vyo vyote huo haukuwa ushuhuda kwamba vitendo vya Mashahidi hao vilivunja sheria ya kifungu cha 163.

Mahakama ilikata shauri kwamba Mashahidi wa Yehova hawakuruka mpaka wa uhuru wa kidini ambao umethibitishwa na katiba. Mahakama ilionyesha kwamba kwa sababu hiyo “uchafuaji na utumiaji mbaya wa uhuru kwa makusudi maovu haukuthibitishwa kuwa ulitendeka.”

Uamuzi huo unapatana na mambo hakika. Pia unapatana na uamuzi wa Mahakama Kuu Zaidi ya Rufani mwaka 1980. Mahakama hiyo ilisema wazi kwamba utendaji wa Mashahidi wa Yehova si wa kutaka kupindua serikali wala si hatari kwa nchi. Pia ilisema: “Ikiwa siku moja mambo ambayo washtakiwa wanaamini yatatukia na utawala wa Mungu usimamishwe juu ya ulimwengu, kuadhibu washtakiwa kwa sababu ya imani hiyo hakutazuia matukio hayo. Lakini ikiwa tazamio lao ni jambo wanalowazia-wazia tu na ni imani isiyo na msingi, imani yao haiwezi kwa njia yo yote kudhuru utaratibu wetu wa Serikali.”

Kwa hiyo mashtaka yote, na pia zile habari zilizotolewa na “wastadi” wale wawili wenye ubaguzi wa kidini, yamethibitishwa kuwa ya uwongo. Imethibitishwa tena kwamba hali ya kazi ya Mashahidi wa Yehova si ya kisiasa bali ni ya kidini kabisa.

Kuondolewa Mashtaka Kunatamaniwa

Ingawa hukumu hiyo imefutwa, kesi imepelekwa kwenye Mahakama ya Serikali ya Usalama ikachunguzwe tena. Inatumainiwa kwamba safari hii mahakama itahukumu kulingana na mambo hakika na kuondoa kabisa mashtaka juu ya washtakiwa hao.

Watu wanaopenda uhuru ulimwenguni pote wataendelea kutazamia matokeo ya jambo hilo. Wanataka kuona kama Mashahidi wa Yehova watafurahia uhuru kamili wa ibada. Ikiwa hivyo, hapo inaweza kwa haki kusemwa kwamba Uturuki inajaribu kutimiza dai lake la kwamba hiyo ni nchi ya kidemokrasi

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki