Kudhabihu Vijana—Hakutoki kwa Mungu
NJE YA kuta za Yerusalemu, katika nyakati za kale kulikuwa na mahali palipoitwa Tofethi. Hapo, Waisraeli, waasi-imani, kutia na Wafalme Ahazi na Manase, walikuwa wakizoea ile desturi mbaya sana ya kudhabihu watoto. Mwishowe kabisa, yule mfalme mwaminifu Yosia alikomesha zoea hilo kwa kufanya Tofethi pawe mahali pasipofaa kwa sherehe za kidini.—2 Wafalme 23:10; 2 Nyakati 28:1-4; 33:1, 6.
Kwa sababu gani mahali hapo paliitwa Tofethi? Asili ya neno hilo inabishaniwa, lakini inapendeza kuangalia yale ambayo mwanachuo wa Kiyahudi David Kimhi (karibu mwaka 1160 mpaka karibu mwaka 1235) alikuwa amesema juu ya mahali hapo. Akizungumza juu ya 2 Wafalme 23:10, ambapo Tofethi pametajwa, yeye aliandika: “Jina la mahali ambapo wao walisababisha wana wao wapite katika [ule moto] kwa kumpa Moleki. Jina la mahali hapo lilikuwa Tofethi, na wao walisema paliitwa hivyo kwa sababu wakati ule wa ibada wao wangecheza dansi na kupiga matari [Kiebrania, tuppim’] ili kwamba yule baba hangesikia vilio vya mwana wake wakati wao walipokuwa wakisababisha yeye apite katika ule moto, na kwamba moyo wake usije ukataharuki mno juu ya mwana wake na yeye amchukue kutoka mkono wao. Na mahali hapa palikuwa bonde ambalo lilikuwa mali ya mwanamume mmoja jina lake Hinomu, na liliitwa ‘Bonde la Hinomu’ na ‘Bonde la Mwana wa Hinomu’ . . . Yosia alipanajisi mahali hapo, akapapunguzia hadhi pakawa mahali pasipo safi, pa kutupiwa mizoga na utovu wote wa usafi, kwamba pasije kamwe tena kuingia ndani ya moyo wa mwanadamu kusababisha mwana wake na binti yake wapite katika ule moto kwa kupewa Moleki.”
Katika nyakati za ki-siku-hizi, yule mungu Moleki amekuwa historia tu ambayo inastaajabisha sana, na bila shaka watu wengi wanaona ugumu wa kufahamu kwa nini watu waliua watoto wao kwa ajili yake. Hata hivyo, leo watu wazima bado wanaelekea kuwa tayari kuua vijana wao wakati inapowafaa wao. Wakati wa karne hii, mamilioni ya vijana wamedhabihiwa juu ya madhabahu ya vita. Kila mwaka, mamilioni ya wasioelezeka ya vitoto visivyozaliwa vinauawa kwa makusudi katika visa vya kutoa mimba, vingi kati yavyo vikiwa ni kwa sababu kutungwa mimba kwa vitoto hivyo kulitokana na ngono ya vivi hivi tu au kwa sababu kuzaliwa kwavyo kungevuruga mtindo wa maisha wa wazazi wavyo. Hivyo, watoto hao wamekuwa dhabihu ya miungu wa uhuru wa kufanya ngono na utafutiaji wa vitu vya kimwili.
Yehova alisema kwamba kuteketeza watoto ili kumpa Moleki lilikuwa jambo la kuchukiza sana. (Yeremia 7:31) Je! yeye anauona kwa utofauti wo wote ule uuaji ovyo-ovyo wa vijana katika kizazi chetu?
[Pichas katika ukurasa wa 31]
Dhabihu ya Watoto kwa Moleki yule mungu-bandia, kama ilivyoonyeshwa miaka yapata 75 katika ile sinema “Drama-Picha ya Uumbaji”
Bonde la Hinomu la siku hizi, likitazama upande wa Mashariki