Kupata Uhuru Katika “Kisiwa cha Wanaume Wapweke”
MOTABOTI iliyokuwa ikipita katikati ya mawimbi madogo kwenye Ghuba ya Nikoya haikujaa. Hata hivyo hii haikuwa kwa sababu ya uchache wa watalii. Hapa katika pwani ya Pasifiki ya Kosta Rika, ile anga isiyo na mawingu, maji rangi emeraldi-chanikiwiti, fuo zenye mchanga mweupe, na minazi yenye kuyumbayumba haijashindwa kamwe kuvutia wale wenye kufuatia paradiso ya kitropiki. Lakini mimi sikuwa likizoni hapa—wala wale abiria wengine.
“Kisiwa cha Wanaume Wapweke”
Tulikuwa tukielekea Kisiwa San Lucas, koloni ya gereza iliyosimamiwa na Wizara ya Mahakama ya Kosta Rika. Wakati mmoja, Kisiwa San Lucas kilikuwa mojapo magereza yenye sifa mbaya zaidi katika Amerika ya Kilatini. Walio wengi wa idadi yacho walikuwa wahalifu washupavu, na wale waliopelekwa huko walijifunza upesi magumu ya kuendelea kuishi. Wenye mamlaka walitoa mahitaji yaliyo ya lazima kabisa, hali wafungwa walijianzishia utaratibu wao wa kula chakula kidogo kidogo na wakang’ang’ana kufanya maisha yao yawe bora. Mara nyingi, wale waliojaribu kutoroka walichukuliwa mbali baharini na ile mikondo yenye nguvu, au wakauawa na papa.
Katika miaka ya mapema-mapema ya 1950, Jose Leon Sanchez, aliyekuwa hapo kwanza mfungwa wa Kisiwa San Lucas, aliandika kitabu kilichotegemea maisha yake binafsi katika koloni la gereza. Hadithi yake iliyofunua namna mambo yalivyo hasa, ya kinyama, lakini ya kweli, La Isla de los Hombres Solos (Kisiwa cha Wanaume Wapweke), upesi ikawa kitabu chenye kuuzwa zaidi katika Meksiko na Amerika ya Kati. Katika Kosta Rika kilianzisha kilio chenye nguvu kutoka kwa umma.
Wakati ule, serikali ilikuwa katika mwendo wa kufanya mashirika yayo ya gereza yawe ya ki-siku-hizi. Mkazo ulitiwa juu ya kugeuza tabia badala ya kuadhibu, nayo hukumu ya kifo iliondolewa. Kwa uangalifu ulioanzishwa na kitabu cha Sanchez, mabadiliko yalifanywa pia katika Kisiwa San Lucas. Wafungwa walifundishwa kufuga ng’ombe na nguruwe, kuvua samaki, na ufundi mwingine. Pia walikuza mimea ya kuleta pesa ya kuuzwa nao waliruhusiwa kushiriki faida. Maendeleo yalifanywa pia katika vifaa vya kuwapa wafungwa makao. Kufikia mwanzoni mwa miaka ya 1960, San Lucas kikawa kiolezo cha kitovu cha kugeuzia tabia kwa ajili ya wafungwa wasiohitaji ulinzi mkali.
Nilipokuwa nikishuka ile motaboti na kukanyaga ile gudi ndogo, mimi nilijua sana ile historia yenye sifa mbaya ya kisiwa hiki. Lakini mimi nilikuwa mlinzi wa wafungwa hapa, si mfungwa. Nilikuwa nimejiunga na Jeshi la Polisi la Taifa nilipokuwa na miaka 18, na kwa sababu nilikuwa mkubwa kwa mtu wa miaka yangu, mgawo wangu wa kwanza ulikuwa kazi ya ulinzi katika Kisiwa San Lucas.
Mfungwa, Hata Hivyo Huru
Nikiwa nimelelewa na watawa wa kike na mapadri Wakatoliki, sikuzote mimi niliogopeshwa sana na wazo la kuchomwa katika moto wa mateso. Kwangu mimi, jambo lililokuwa la maana zaidi maishani ni kuepuka kwenda katika moto wa mateso. Lakini mimi nilifadhaika kuona kwamba watu walio wengi hawakujali sana juu ya hilo. Padri aweza kulizungumza darasani, lakini nje ya darasa, hakuna mmoja aliyetaka kuongea juu ya dini au Biblia. Walidai kuamini moto wa mateso, lakini jambo hilo halikuzuia hata kidogo mwenendo wao.
Hali katika San Lucas haikuwa tofauti sana na hiyo. Ingawa wengi wa walinzi na wafungwa walidai kuwa na imani iyo hiyo, ilionekana kuwaathiri kidogo sana. Usemi mcha-fu-mchafu na mazoea machafu yalikuwa ya kawaida. Wakati mmoja mlinzi mwenzi alikamatwa akiingiza marijuana kisiwani kimagendo naye mwenyewe akawa mfungwa hatimaye! Msimamizi wangu wa karibu zaidi alikuwa mwenye hasira kali sana naye mara mbili aliwatolea mwito wafungwa waasi wapigane naye ngumi. Kwa kuwa mimi nilikuwa na wakati mwingi, mara nyingi nilifikiria sana mambo niliyokuwa nikiona kisiwani. Nikiwa kijana asiye na ujuzi, mimi nilikuwa nimevurugika na kuzinduka.
Jioni moja, Franklin, mfungwa mwenye kuaminika, alinialika nikasikilize mazungumzo ya Biblia. Hata ingawa sikuwa ninapendezwa sana, upesi mazungumzo yakasitawi.
“Lazima liwe jambo gumu kujifunza Biblia ukiwa mfungwa,” nikasema. Mimi sikusahau kamwe jibu la Franklin.
“Kimwili mimi ni mfungwa,” akasema, “lakini kiroho mimi ni huru.”
Lo! jinsi mimi nilivyotaka kuelewa aina hiyo ya uhuru!
Mashahidi Katika San Lucas
Ikawa kwamba Franklin alikuwa akijifunza Biblia na Mashahidi wa Yehova. Jumapili, watu wa ukoo na marafiki waliruhusiwa kuingia kisiwani. Mara nyingi, merikebu mbili au tatu zilikuwa zikileta Mashahidi wengi kufikia 30 kuvuka ghuba kutoka Kundi la Puntarenas. Nikiwa mpya pale, nilishangaa kuona wakuu wakiwapungia tu mkono Mashahidi wapite vituo vya ukaguzi hali kila mtu mwingineye alipekuliwa kikamili. Jambo la kushangaza hata zaidi ulikuwa uhakika wa kwamba Mashahidi waliwatendea kwa staha wafungwa na walinzi pia na waliongea na kila mmoja juu ya ujumbe wao wenye msingi wa Biblia.
Wafungwa wachache walikuwa na funzo la Biblia la kibinafsi pamoja na Mashahidi katika Jumapili hizi. Franklin alikuwa mmoja wao, na kulikuwako jambo moja lililonivutia kuhusu yeye. Nilijifunza kwamba Franklin alikuwa amehukumiwa muda wa miaka 12 gerezani kwa sababu ya kuua mshindani wa kibiashara. Huko gerezani alikuwa amejifunza utunzaji hesabu kwa njia ya barua. Kwa sababu yeye hakuwa akinywa, kuvuta sigareti, au kutumia dawa za kulevya, aliwekwa asimamie maktaba ya gereza. Baadaye, yeye alipewa chumba chake mwenyewe hata akapewa madaraka zaidi.
Alipokuwa shuleni, Franklin alikuwa amekuwa na marafiki fulani waliokuwa Mashahidi wa Yehova. Yeye aliona kwamba wao hawakujihusisha kamwe katika migogoro au mapigano, hata wakati wengine walipowachokoza. Ingawa yeye hakuchukua dini kwa uzito, alijua kwamba Mashahidi walikuwa watu wenye kuamanika na safi kiadili. Kwa hiyo wakati aliposikia kwamba alikuwamo Atalaya (“Mnara wa Mlinzi,” kama wengine walivyowaita Mashahidi wa Yehova) miongoni mwa wafungwa, akawa mwenye udadisi.
Siku moja kabla ya chakula cha mchana, Franklin aliona mfungwa akiketi peke yake nje ya jumba la kulia chakula. Sura yake nadhifu ilimfanya Franklin aulize kama yeye alikuwa ndiye yule Atalaya. Alipoambiwa kwamba alikuwa ndiye, tendo-mwitikio la kwanza la Franklin lilikuwa: “Kwa nini wewe upo hapa? ” Yule mwanamume akaeleza kwamba kwanza alikuwa amehukumiwa kufungwa katika Gereza la Kati katika San Jose, ule mji mkuu, naye alikuwa ameanza kujifunza Biblia pamoja na Mashahidi wa Yehova alipokuwa huko. Baada ya kuhamishiwa San Lucas, yeye aliendelea kujifunza na Shahidi mmoja kutoka Puntarenas. Baada ya wakati alibatizwa papo hapo kwenye Ufuo Coco katika Kisiwa San Lucas.
Mkutano huo ulibadili maisha ya Franklin. Tokea hapo na kuendelea, wakati wowote Mashahidi walipokuja kuzuru, alikuwa akiwatia katika mazungumzo machangamfu. Pia yeye alianza kuongea na wafungwa wengine na walinzi juu ya mambo aliyokuwa akijifunza. Mwenendo, mavazi, na kujipamba kwake kukapata maendeleo. Yeye na mwandamani wake aliyebatizwa wakapata staha ya kila mmoja.
Hatimaye, kifungo cha Franklin cha miaka 12 kilipunguzwa kikawa miaka 3 na miezi 4. Yeye pamoja na mwandamani wake waliendelea kujifunza Biblia. Yajapokuwa mazingira mabaya ya gereza, wao walikuwa na furaha, nazo nyuso zao zilionyesha hivyo. Kwa wazi waliona kwamba mimi nilikuwa tofauti na walinzi wengine, kwa kuwa mimi sikushiriki mizaha michafu na ucheshi wa matusi. Kwa hiyo wakanialika katika chumba chao kwa mazungumzo ya Biblia. Mambo niliyosikia kutoka kwao na kutoka kwa wale Mashahidi wageni yalinipendeza, hasa juu ya hali ya wafu na kwamba kwa kweli hakuna moto wa mateso wenye kuwaka. Nilipewa nakala moja ya kitabu Kweli Iongozayo Kwenye Uzima wa Milele na nikaanza kukisoma. Ijapokuwa mimi sikung’amua hivyo wakati ule, mbegu za ukweli zilikuwa zikipandwa katika moyo wangu ambazo baadaye zingezaa tunda.
Uhuru wa Kweli Hatimaye
Baada ya kuliacha Jeshi la Polisi la Taifa, mimi niliishi kwa muda mfupi katika Miami, Florida. Siku moja mfanya kazi mwenzi alianza kuzungumza nami juu ya Biblia. Usemi, mavazi, na kujipamba kwake kuliniambia kwamba nilikuwa nimekutana na Mashahidi wa Yehova kwa mara nyingine tena. Jambo hilo lilinikumbusha Kisiwa San Lucas, nami nikamwuliza ni kwa nini hakuna mtu aliyeonekana kupendezwa katika mazungumzo ya mambo ya kiroho. Yeye alinipa jibu fupi na akadokeza kwamba tuwe na mazungumzo nyumbani kwangu. Jambo hilo likaongoza kwenye funzo la Biblia la ukawaida na baadaye kwenye wakfu na ubatizo.
Nilirudi Kosta Rika katika 1975 na nikahudhuria mkusanyiko wa wilaya katika San Jose. Mimi ningali sina hakika ni nani aliyeshangaa zaidi wakati Franklin nami tulipokutana kwa nasibu katika mkusanyiko ule. Sasa yeye alikuwa huru kimwili na pia amebatizwa. Nilipoondoka San Lucas, Franklin hakuwa na hakika upendezi wangu katika Biblia ulikuwa imara kadiri gani. Lakini tulikuwapo hapa, aliyekuwa hapo kwanza mfungwa na aliyekuwa mlinzi, tukiwa tumeungana kikweli katika uhuru ambao hutokana na ibada ya Yehova yule Mungu wa kweli!
Kwa wengine gereza la “Kisiwa cha Wanaume Wapweke” lilimaanisha tu kumbukumbu zisizopendeza. Kwangu mimi lilimaanisha mwanzo wa uhuru wa kiroho. Sasa, nikiwa mzee Mkristo, mimi nashiriki kuleta uhuru kwa wale ambao hufikiri kwamba wao wako huru lakini ambao kwa kweli wamefungwa kama walivyokuwa wanaume hao niliozoea kulinda wakati mmoja.—Kama ilivyosimuliwa na David Robinson.
[Ramani katika ukurasa wa 25]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Nikaragwa
BAHARI YA KARIBEA
Kosta Rika
Puntarenas
Ghuba ya Nikoya
San Jose
Panama
BAHARI PASIFIKI
Km 0 50 100
mi 0 50 100