Muono-Ndani Juu ya Habari
“Kuteka Nyara Visukuku”
Chini ya kichwa hicho, Le Monde karatasi-habari ya Kifaransa iliripoti kisa cha mwanapalontolojia (mchunguzi wa visukuku) katika India ambaye “kwa miaka 20 . . . yaonekana alidanganya wenzake kuhusu asili ya visukuku ambavyo aliwapelekea ili wakadirie ubora wavyo.” ‘Utekaji nyara’ huo ulihusisha ndani kuwapelekea visukukuu [masalio ya vitu vya kale] ambavyo vilipatikana katika United States, Afrika, Chekoslovakia, na Visiwa vya Uingereza, akidai kwamba vilikuwa vimegunduliwa katika milima Himalaya. Mwanasayansi huyu alichapisha mavumbuo yake katika makala zaidi ya 300, mengi yayo yakiwa yametiwa sahihi na wanapalontolojia na kuchapishwa katika majarida ya kisayansi katika sehemu zote za ulimwengu. Ukopi huo ulifichuliwa na mwanasayansi Mwaustralia kupitia Nature jarida la kisayansi la Uingereza. Yeye alishangaa ‘ilikuwaje hata mavumbuo hayo ya mashaka-mashaka yakabaki bila kupingwa na wanasayansi.’
Kulingana na Le Monde, sababu moja yawezekana kuwa ni ile sheria ya kukaa kimya ambayo hutiiwa na washiriki wengi wa jumuiya ya kisayansi, hata iwapo wana mashaka juu ya mavumbuo ya wenzao. Vyovyote vile, makala hiyo iliarifu kwamba ‘utekaji nyara’ wa visukuku hivyo “umetangua karibu mambo yote ya uhakika yaliyokusanywa [muda wa miaka 20 iliyopita] kuhusu jiolojia ya milima Himalaya.”
Ni wazi kwamba kisa kipya hiki cha ukopi katika sayansi hakitilii shaka ulimwengu mzima wa kisayansi. Hata hivyo, chaandaa ushuhuda zaidi kwamba hoja za upalontolojia zilinganishwapo dhidi ya usahihi usiokosea wa maandishi ya Biblia huwa mara nyingi ni kama vile mtume Paulo alivyoziita, “mapinganisho ya ‘maarifa’ ambayo si maarifa hata kidogo.”—1 Timotheo 6:20, The New Jerusalem Bible.
“Imejaa Damu”
Katika Kolombia, Amerika Kusini, watu walio mashuhuri kwa kuuza dawa za kulevya hufanya mkataba pamoja na vijana ili wakomeshe washindani au kutia mbabaiko miongoni mwa wanasiasa na watu wote kwa ujumla. Sicario mmoja wa jinsi hiyo, au mwuaji wa kulipwa, aliambia waandishihabari wa Tiempo, gazeti-habari la Kihispania, kwamba ‘kuua bila huruma ni jambo lenye kutatiza,’ na kwa hiyo dhamiri yake humsumbua pindi kwa pindi. Yeye hutulizaje dhamiri yake? Alieleza hivi: “Mimi najua kwamba moja ya sheria za Mungu ni kwamba usiue, lakini kwa habari yangu mimi yanipasa kuua ili niishi. Mimi huua kidhamiri kwa sababu nazihitaji pesa. Kwani hamwoni kwamba ninafanya kazi kwa sababu ni lazima niishi kwa njia fulani? . . . Kabla sijaenda kuua mtu, mimi husali kwa Mungu na kwa Bikira ili wanilinde, nisipatwe na jambo baya, ili wanipe moyo mkuu, ili kila kitu kiwe kama kilivyopangwa.”
Ingawa bila shaka fikira ya namna hii ya kupunguza uzito wa mambo ingekataliwa katakata na wanatheolojia Wakatoliki, viongozi wa kanisa wamehalalisha pambano lenye silaha “kuwa ndio utatuzi wa mwisho wa kukomesha udhalimu wa wazi wenye kuendelea kwa muda mrefu.” Ikiwa wanatheolojia huachilia jeuri ifanywe kwa ajili ya ukosefu wa haki ya kisiasa, je! utakuwa mshangao kwamba Wakatoliki fulani, kama sicario huyu, hutetea kuua kwa sababu ya ukosefu wa haki ya kiuchumi? Ni hatari kama nini kutohoa mafundisho wazi ya Neno la Mungu!
Usiku ambapo ukosefu wa haki ulio mkubwa kupita mwingine wowote ulikaribia kutendwa—wenye kuhusisha kukamatwa, kujaribiwa, na kuuawa kwa Yesu Kristo—Yesu mwenyewe alikataa kufikiria jeuri ya namna yoyote. Alimwambia Petro hivi: “Wote wachukuao upanga watapotelea mbali kwa upanga.” (Mathayo 26:52, Revised Standard Version, Catholic Edition) Kimantiki, wenye kugeukia jeuri kuwa utatuzi wa mwisho wangewezaje kutarajia Mungu Mwenye Nguvu Zote awasikilize chini ya hali zozote, kwa maana unabii wa Isaya wataarifu wazi hivi: “Hata ingawa nyinyi mfanye sala nyingi, mimi sitasikiliza; mikono yenu imejaa damu”?—Isaya 1:15, RS, Catholic Edition.
“Vitu vya Kaisari kwa Kaisari”
Kuepa kodi ni tatizo linaloongezeka katika nchi nyingi. Kwa kielelezo, katika Hispania karatasi-habari El Diario Vasco yaripoti kwamba wanunuaji na wauzaji pia wana desturi ya kuficha kimakusudi bei halisi ya kununua mali. Shughuli ikiisha kufanywa, kodi hulipwa kulingana na thamani iliyoandikwa ya mali hiyo. Hata hivyo, ingawa huenda mnunuaji na mwuzaji wakaafikiana kuhusu bei moja kwa kitu kile hasa chenye kununuliwa, kiasi cha chini zaidi huandikwa katika hati ya umiliki. Hilo, nalo, hupunguza kodi itakayolipwa kwa kuhamisha hati ya umiliki. Kulingana na El Diario Vasco, msajili wa mikataba Jose Maria Segura Zurbano adai kwamba ingawa wasajili hawashiriki hasa katika ukopi, wao wajua kwamba thamani ya mali ambayo wao huandika si ile ya kweli. Akiarifu juu ya utofauti mmoja kwenye zoea hili la kutofuata haki, Zurbano alionelea hivi: “Katika nchi hii kila mtu na jirani yake husema uwongo, utofauti mmoja tu ukiwa ni Mashahidi wa Yehova. Wakati wao wauzapo au kununua, thamani [ya mali] ambayo wao hujulisha huwa ndiyo ya kweli kabisa.”
Mashahidi wa Yehova wajulikana kwa ukweli wao na ufuataji haki. Wao wajua kwamba Yehova Mungu hutarajia watumishi wake waonyeshe sifa hizo katika mishughuliko yao. Biblia yaonyesha wazi kwamba Mungu huchukia “ulimi bandia” na “shahidi bandia ambaye hutokeza mambo ya uwongo.” Kuhusu kulipa kodi, Yesu Kristo aliweka kiwango kwa wafuasi wake wa kweli aliposema: “Lipeni vitu vya Kaisari kwa Kaisari, lakini vitu vya Mungu kwa Mungu.”—Mithali 6:6-19; Marko 12:17, NW.