Kufanya Kazi ya Mungu kwa Njia ya Mungu Katika Naijeria
ILIVUTIA macho. Marundo makubwa ya nguzo za chuma cha pua—zaidi ya kilo nusu milioni—vilikuwa vimelala forodhani Houston, Texas, tangu mwisho mmoja hadi ule mwingine. Kuli (mpakizi na mpakuaji) mmoja alikuwa na kazi ya kuchunguza shehena nyingi za kupakia. Alipokuwa akifanya kazi, alistaajabu kuona kwamba yote ilikuwa na alama “Mnara wa Mlinzi.” Mwishowe akamfikia mwanamume aliyekuwa na daraka la shehena hiyo akamwuliza: “Kwani huu mnara wa mlinzi ni mrefu namna gani?”
Ndipo kuli huyo alipojua kwamba chuma hicho cha pua hakingetengenezwa kuwa mnara wa mlinzi halisi. Badala yake, kingepelekwa Igieduma, Naijeria, ambako kingetumiwa kujenga kambi mpya ya tawi kwa ajili ya Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi—kwa halisi kijiji katikati ya pori la Afrika.
Miaka sita iliyopita kituo cha Igieduma kilikuwa hasa kichaka kikubwa na miti ya mpira. Sasa bara hilo linatunzwa na lapendeza; kuna maua, mabustani, na hata msitu wenye paa! Na hali, kwenye uwanja huo kuna matbaa iliyo kubwa zaidi ya ardhi yote iliyokuwa imejengwa tawi la awali katika Lagos. Ndani ya kiwanda, matbaa tatu hufanya kazi, moja ikiwa yaweza kutokeza magazeti 17,000 kwa saa moja. Majengo ya makao yaweza kukaliwa na watu zaidi ya 400. Jengo la kuhudumia lina chumba kikubwa cha kulia na meko na pia mahali pa kutunzia wagonjwa na ofisi ya daktari wa meno. Kuna ugavi wa maji na mifumo ya mabomba ya maji macha-fu ya kujitegemea. Nyumba ya umeme unaodhibitiwa na kompyuta hufanyiza umeme. Kuna Jumba la Ufalme, jengo la ofisi, na idara ya kuzima moto. Pia utakuta barabara na taa za barabarani. Haishangazi basi watu huliita jiji, hilo jengo-tata la Betheli kule Igieduma. Na yote ilijengwa na wafanya kazi wa kujitolea wasiolipwa na kugharimiwa kwa michango isiyo ya kuombwa-ombwa.
Mpanuko wa Haraka-Haraka
Ingawa Betheli hii ndiyo kubwa zaidi iliyopata kuwapo Naijeria, siyo ya kwanza. Ya kwanza ilisimamishwa na Ndugu William R. Brown, ambaye pamoja na mke wake na binti walihamia Lagos katika 1930. Vyumba kadhaa vilivyokodiwa ambamo waliishi vilitumika kuwa makao makuu ya tawi la Sosaiti la Afrika ya Magharibi, ambalo wakati huo liliangalia kazi ya Ufalme katika Naijeria, Ghana, na Sierra Leone. Wakati huo, kulikuwako wapiga mbiu wa habari njema watendaji saba tu katika Naijeria.
Bible Brown, kama alivyojulikana kwa wengi, alikuwa mhubiri wa habari njema mwenye nguvu na moyo mkuu. Akiwa hatosheki kwa muda mrefu kukaa kwenye kiti cha ofisini, yeye alizuru nchi hiyo kwa motokaa na gari-moshi, akitoa hotuba za peupe na kugawanya viasi vikubwa vya fasihi.
Kwa kadiri ujumbe wenye nguvu wa Ufalme ulivyotia mzizi katika akili na mioyo yenye kuitikia, watu zaidi na zaidi wakawa wapiga mbiu ya Ufalme wenye bidii. Muongo uliofuata ulikuwa kama kile kipindi katika karne ya kwanza katika Yerusalemu wakati “neno la Mungu li[li]enea; na hesabu ya wanafunzi ikazidi sana.” (Matendo 6:7) Kufikia 1940 hesabu ya wasifaji-watendaji wa Yehova katika Naijeria ilikuwa imeruka juu kutoka 7 hadi 1,051!
‘Mdogo alikuwa amekuwa elfu,’ lakini huo ulikuwa ni mwanzo tu. (Isaya 60:22) Katika 1947 Sosaiti ilipeleka wamisionari watatu waliozoezwa Gileadi kwenda Lagos. Mmoja wao, Anthony Attwood, yungali atenda katika mgawo wake. Akumbuka Betheli ya wakati huo: “Ilikuwa nyumba ya orofani juu ya duka la viatu. Kulikuwako vyumba viwili vya kulala, sebule/ofisi, na chumba cha kulia. Ndugu na Dada Brown na familia yao walikaa kwenye vyumba viwili vya kulala, na sisi misionari watatu tulijazana katika chumba cha tatu. Kulikuwako nafasi tu ya kutosha vitanda vitatu vya mtu mmoja mmoja na kabati lililojengwa ukutani.”
Uhitaji wa nafasi zaidi ulichochea hatua ya kwenda kwenye jengo lenye orofa tatu katika 1948. Kufikia wakati huo hesabu ya wahubiri katika Naijeria ilikuwa imefika 6,825. Miaka minane baadaye, hesabu hiyo ilikuwa imeongezeka mara tatu, kwa hiyo Betheli ilihamishwa tena, hadi Shomolu, Lagos. Huko, kwa mara ya kwanza katika Naijeria, Sosaiti ilijenga Makao ya Betheli yayo yenyewe, jengo lenye vyumba vinane kwenye ardhi ya hektari 0.6. Serikali ya mji iliita barabara hiyo Barabara ya Mnara wa Mlinzi. Bustanini mlikuwa na miti mingi, kutia ndani mitende ya nazi na pia jamii ya michungwa, mifenesi, miavokado, na miembe. Lakini wakati wa miaka 33 iliyofuata, majengo yaliongezwa na kupanuliwa. Kufikia miaka ya katikati ya 1970, majengo yalienea karibu ardhi yote hiyo. Ilikuwa lazima kuhama tena.
Kumbukumbu za Ujenzi
Kwanza, sehemu ya ardhi yenye hektari 31 ilipatikana kule Otta, kaskazini mwa Lagos. Lakini matatizo yakazidi kuzuia maendeleo yasifanywe. Hatimaye, ikawa wazi kwamba hayakuwa mapenzi ya Yehova tuhamie huko. Kisha utafutaji wa ardhi ulienezwa katika sehemu yote ya kusini mwa nchi hiyo, na katika 1983 Sosaiti ilipata kisehemu cha ardhi ya hektari 57 kule Igieduma, katika Jimbo la Bendel.
Wakati wa miaka sita iliyofuata, chatu na fira walihama wakati ndugu na mashine kubwa-kubwa walipohamia. Tatizo kubwa kwa kazi hiyo lilikuwa kwamba ilikuwa vigumu, au karibu haiwezekani, kununua nchini vingi vya vyombo na vifaa vya ujenzi. Msaada wa nje ulihitajiwa. Kwa hiyo jopo la Mashahidi katika United States liliulizwa litafute, kununua, na kupeleka vifaa. Terry Dean, mratibu wa shughuli kubwa hiyo, asimulia hivi: “Kilichofanya kazi hii kuwa kubwa sana ilikuwa kwamba karibu kila kifaa kilipasa kipelekwe kutoka nje. Ndugu katika Naijeria walituambia kwamba vifaa vya ujenzi pekee walivyokuwa navyo ni mchanga, saruji, na maji!”
Ilikuwa vizuri kwamba vifaa hivyo vya msingi vilipatikana, kwa kuwa kazi ya ujenzi ilitumia kilo 7,500,000 za saruji, kilo 55,000,000 za mchanga, na kilo 35,000,000 za kokoto. Pia mbao zilipatikana kwa utele. Hata hivyo, wakati wa miaka mitano iliyofuata, kilo milioni 4.5 za vifaa zilipelekwa kutoka United States, kiasi cha kujaza meli za mizigo 347, ambazo kama zikishikanishwa zingekuwa na urefu wa kilometa 3.5!
Matawi mengine pia yalichanga ugavi kwa ukarimu. Uingereza ilitoa mfumo wote wa umeme, kutia ndani jenereta sita kubwa za kutoa nguvu hizo. Uswedi ilitoa krini (mtambo wa kunyanyulia mizigo) ya mnara, matinga (trekta), mashine ya kuchimbua, lori, vyombo vya kazi, vyombo vya jikoni, na mfumo wa simu. Wakati duka la vitu vya chuma lilipopigwa mnada, ndugu Waswedi walilinunua na kupeleka vitu vyote hadi Naijeria. Vifaa pekee ambavyo hawakupeleka kutoka duka hilo ni beleshi za theluji—kwa wazi zikiwa ni zenye mafaa zaidi katika Uswedi kuliko katika Afrika!
Bila shaka, Mashahidi wa nchini pia walichanga kwa kulingana na uweza wao. Zaidi ya 125,000 walionyesha uungaji-mkono wao kwa ajili ya kazi hiyo kwa kuja kwenye kituo wakati wa ujenzi. Wengi walisaidia kifedha. Mchango mmoja wa senti 20 (za U.S.) ulitoka kwa mvulana wa miaka saba. Alipataje pesa hizo? Baba yake alimpa kiazi kikuu apike ale; badala yake mvulana huyo alikihifadhi na kukipanda wakati wa majira yanayofaa. Baadaye yeye alivuna kiazi kikuu chake, akakiuza, na kuchanga pesa hizo kwa ajili ya kazi ya Igieduma.
Mashahidi wa Yehova wengine walichanga ujuzi wao, hata kuzoeza wengine wajue stadi za ujenzi. Wengi, kufikia 500 kwa wakati mmoja, walichanga kazi ngumu, wakitaabika chini ya jua lenye kukaanga na katika mvua za tropiki ili kumaliza kazi hiyo. Kwa kielelezo, fikiria kazi yenyewe iliyohusika katika kujenga ukuta unaozunguka kituo hicho. Katika miezi saba iliyotumiwa kukamilisha ukuta huu wa karibu kilometa 3, akina ndugu walitengeneza na kufinyanga matofali moja moja ya zege zaidi ya 57,000! Ndugu mmoja alifanya ucheshi hivi: “Kilichonifanya nisiache ni kuona ndege wala mzoga wakizunguka juu kichwani wakingojea nianguke!” Kwa kweli, sawa na wale maelfu wengine walio-changia kufanikiwa kwa Igieduma, yeye alichochewa na kutegemezwa na roho takatifu ya Yehova.
Kutambuliwa Rasmi
Maofisa wa serikali walishirikiana kwa kuunga mkono kazi hiyo. Ofisi ya Rais ilifanya hisani ya kwamba ugavi wote wa ujenzi ulioingizwa nchini usitozwe ushuru wa forodha. Maofisa wa mji huo walifutilia mbali ada za usitawi na utiaji sahihi ramani. Ada ndogo tu ya ujenzi ndiyo iliyohitajiwa. Pindi moja, kulipokuwa ubishi juu ya ardhi, Omo N’oba, au mfalme, wa eneo lote hilo alijiingiza na kutoa amri hii: “Kazi hii haipasi kusimamishwa kwa sababu hii ni kazi ya Mungu.”
Ilitambuliwa na wengine ambao hawakuwa Mashahidi wa Yehova kwamba kazi hii ilikuwa na utegemezo wa kimungu. Wakati kampuni moja ya Kiamerika ilipotoa chuma cha pua cha kujengea gereji, walituma mmoja wa watu wao, Mkatoliki, asaidie kupajenga. Wakati wa ukaaji wake wa majuma mawili kule Igieduma, upesi akahisi yuko nyumbani, hata akawa anaita wafanya kazi wenzake ndugu na dada. Baada ya kurudi nyumbani, yeye aliandikia ofisi yetu ya Naijeria hivi: “Sijapata kamwe kuonea kazi shangwe ya kadiri kubwa kama wakati nilipokuwa huko nikifanya kazi ya Mungu katika njia ya Mungu.”
Siku ya Kuweka Wakfu
Mnamo Januari 20, 1990, jengo-tata hili la Betheli lenye kupendeza liliwekwa wakfu kwa Yehova Mungu, ambaye roho yake ilikuwa na daraka la ukamilisho wayo. Wageni walikuja kutoka sehemu zote za Naijeria, ingawa ilipasa mialiko iwe kwa wale ambao walikuwa wamebatizwa kwa angalau miaka 35 au ambao walikuwa wametumia miaka isiyopungua 20 katika utumishi wa wakati wote. Akina dada walikuwa wamejipamba katika marinda marefu, yenye rangi nyingi pamoja na vitambaa vya nywele vyenye kushabihi, na wengi wa akina ndugu walivaa majoho ya Kiafrika ya kupendeza. Kwa ujumla, 4,209 kutoka nchi 29 walihudhuria wakfu huo. Miongoni mwao kulikuwako wamisionari angalau 80, wengi wao wakiwa wametoka katika nchi nyingine za Afrika ya Magharibi. Katika programu zilitiwa ndani ripoti za wawakilishi watano wa tawi waliozuru, ambao walikazia umoja wa kusudi na hisia-mwenzi uliopo miongoni mwa watu wa Yehova. Salamu zilizoandikwa na telegramu zilitoka kwa ndugu katika nchi 21, kutia ndani ujumbe wenye kuchochea moyo kutoka kwa “ndugu na dada 40 katika Mosko, Urusi.”
Washiriki wawili wa Baraza Linaloongoza la Mashahidi wa Yehova katika Brooklyn, New York, walikuwapo pia. Albert Schroeder alinena juu ya habari “Kinachotafutwa Ni Kupatikana Mwaminifu,” akikazia uhitaji wa uaminifu mwendelevu upande wa watu wa Mungu. (1 Wakorintho 4:2) Hotuba ya kuweka wakfu ilitolewa na Lyman Swingle, aliyezungumza juu ya ujenzi wa hekalu tukufu la siku za Solomoni. Ingawa hekalu hilo lilikuwa na utegemezo na kibali cha Mungu, Yehova alionyesha wazi kwamba lenye maana zaidi ya ujenzi ulikuwa ni uaminifu-mshikamanifu na utii wa watu wake walio wakfu. Kwa njia hiyo Ndugu Swingle alionyesha kwamba jengo-tata la tawi lenye kupendeza kule Igieduma halikuwa kikomo chenyewe bali njia ya kusogeza mbele ibada ya kweli.
Siku iliyofuata, mikutano ya pekee kuhusiana na wakfu ilifanyika katika miji mitatu ya Naijeria. Zaidi ya 60,000 walihudhuria vipindi hivyo.
Katika nyakati za kale, wakati watu wa Naijeria wenye kusema Kiedo walipokuja kumstahi chifu mkuu, kulikuwako mwadhimisho na shangwe kubwa. Igieduma (hapo awali ugie dunai) lilikuwa neno lililotumiwa kueleza umalizio wenye kufaulu wa ukusanyikaji kama huo wenye shangwe. Kwa watu wa Yehova waliokuja siku hiyo ya kuweka wakfu ili kustahi Chifu wa Ulimwengu Wote, Yehova Mungu, maneno hayo machache yalifaa sana. Kwa wale wahubiri wa Ufalme 139,150 katika Naijeria, neno “Igieduma” lakumbusha mahali ambapo kutoka hapo mwelekezo na ushauri wa kitheokrasi hububujikia, na pia vifaa vilivyochapishwa vitakavyowasaidia kuendelea kufanya kazi ya Mungu katika njia ya Mungu.
[Picha katika ukurasa wa 24, 25]
1. Majengo ya makao
2. Jumba la Ufalme
3.Jengo la Kutumikia
4. Ofisi
5. Kiwanda
6. Gereji
7. Nyumba ya jenereta
[Picha katika ukurasa wa 26]
Ndugu na Dada Brown mbele ya ofisi ya tawi katika miaka ya 1940
Sebule ya upokezi ya kiwanda kwenye tawi jipya
Chumba cha Betheli
[Picha katika ukurasa wa 27]
Matbaa ya ofseti ya rangi mbili
Kupakia fasihi
Jumba la Ufalme
Idara ya Utumishi