‘Miili Mingi ya Watakatifu Iliinuliwa’
“DUNIA ikatetemeka, na matungamo-miamba yakapasuliwa. Na maziara ya ukumbusho yakafunguliwa na miili mingi ya watakatifu iliyokuwa imelala usingizi ikainuliwa, (na watu, wakitoka miongoni mwa maziara ya ukumbusho baada ya kuinuliwa kwake, wakaingia ndani ya lile jiji takatifu,) nao wakawa wenye kuonekana kwa watu wengi.” (Mathayo 27:51-53, NW) Mwanachuo Mkatoliki Karl Staab huliita tukio hili lililotukia kwenye kifo cha Yesu “la kifumbo kabisa.” Kulitendeka nini?
Epifanio na Mababa wa Kanisa wengine wa mapema walifundisha kwamba watakatifu walihuika kihalisi wakaenda pamoja na Yesu mfufuliwa mbinguni. Augustino, Theofilakto, na Zigabeno waliamini kwamba wafu hao walipokea ufufuo wa muda lakini baadaye wakarudi kwenye maziara (makaburi) yao. Hata hivyo, maoni haya ya mwisho “hayakupata utambuzi mahali mengi,” aeleza mwanachuo Erich Fascher. Wakati zitafsiripo Mathayo 27:52, 53, tafsiri nyingi za ki-siku-hizi za Biblia hutoa wazo la kwamba ufufuo ulitukia. Sivyo ifanyavyo New World Translation, ambayo huelekeza kwenye matokeo ya tetemeko la dunia. Kwa nini?
Kwanza, hata iwe “watakatifu” hao walikuwa akina nani, Mathayo hakusema kwamba wao waliinuliwa. Alisema miili, au maiti zao ndizo zilizoinuliwa. Pili, hakusema kwamba miili hiyo ilihuika. Alisema iliinuliwa, na kitenzi cha Kigiriki e·geiʹro, kinachomaanisha ‘kuinua,’ hakimaanishi ufufuo sikuzote. Miongoni mwa mambo mengine, chaweza pia kumaanisha “kunyanyua kutoka ndani ya” shimo au ‘kuja juu’ kutoka chini. (Mathayo 12:11; 17:7; Luka 1:69, NW) Msukosuko wa kifo cha Yesu ulifungua maziara, ukitupa miili isiyo na uhai itokeze peupe. Matukio ya jinsi hiyo wakati wa matetemeko ya dunia yaliripotiwa katika karne ya pili W.K. na mwandikaji Mgiriki Aelio Aristide na majuzi zaidi, katika 1962, katika Colombia.
Maoni haya ya tukio hilo yapatana na mafundisho ya Biblia. Katika 1 Wakorintho sura ya 15, mtume Paulo hutoa uthibitisho wenye kusadikisha juu ya ufufuo, lakini yeye huacha kabisa Mathayo 27:52, 53. Ndivyo na waandikaji wengine wote wa Biblia. (Matendo 2:32, 34) Maiti zilizoinuliwa kwenye kifo cha Yesu hazingeweza kuwa zilikuja kwenye uhai kwa njia aliyofikiri Epifanio, kwa maana katika siku ya tatu baada ya hapo, Yesu alipata kuwa “mzaliwa wa kwanza katika wafu.” (Wakolosai 1:18) Wakristo wapakwa-mafuta, ambao pia huitwa “watakatifu,” waliahidiwa ushiriki katika ufufuo wa kwanza wakati wa kuwapo kwa Kristo, wala si katika karne ya kwanza.—1 Wathesalonike 3:13; 4:14-17.
Waelezaji wa Biblia walio wengi hutatizika kueleza mstari wa 53, ingawa baadhi yao hudokeza kwamba mstari wa 52 husimulia kufunguliwa kwa maziara na tetemeko la dunia na kufichuliwa kwa maiti zilizozikwa karibuni. Kwa kielelezo, mwanachuo Mjeremani Theobald Daechsel hutoa tafsiri inayofuata: “Maziara yakafunguka, na maiti nyingi za watakatifu wenye kulala pumzikoni zikainuliwa.”
Walikuwa nani wale ‘waliouingia mji mtakatifu’ muda mwingi baadaye, yaani baada ya Yesu kuwa amefufuliwa? Kama ionwavyo juu, miili iliyofichuliwa ilibaki bila uhai, kwa hiyo ni lazima Mathayo awe arejezea watu waliozuru maziara na kuleta habari za tukio hilo ndani ya Yerusalemu. Hivyo, fasiri ya New World Translation huongeza kina cha uelewevu wa Biblia wala haivurugi wasomaji kuhusu ufufuo.