Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w90 11/1 kur. 16-17
  • Samaria—Jiji Kuu Miongoni mwa Majiji Makuu ya Kaskazini

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Samaria—Jiji Kuu Miongoni mwa Majiji Makuu ya Kaskazini
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
  • Habari Zinazolingana
  • Alivumilia Licha ya Ukosefu wa Haki
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2014
  • Kitabu Cha Biblia Namba 11—1Wafalme
    “Kila Andiko, Lenye Pumzi ya Mungu, Lafaa”
  • Wamegundua Nini Huko Yezreeli?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2000
  • Ashuru Yenye Ukatili Ile Serikali Kubwa ya Pili ya Ulimwengu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1988
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
w90 11/1 kur. 16-17

Mandhari Kutoka Bara Lililoahidiwa

Samaria—Jiji Kuu Miongoni mwa Majiji Makuu ya Kaskazini

BABULONI, Ninawi, na Roma. Hayo yalikuwa majiji makuu nyakati za Biblia. Na bado, kusema Kibiblia, kando na Yerusalemu lenyewe, jiji kuu lenye kustahili kuangaliwa zaidi haielekei kuwa lilikuwa moja la hayo, bali Samaria. Kwa karibu miaka 200, lilikuwa ndilo jiji kuu la ufalme wa Israeli wenye makabila kumi, na jumbe nyingi za kiunabii zilikaza fikira juu ya Samaria. Lakini wewe wajua nini juu ya Samaria? Na kwa nini lilikuwa jiji kuu miongoni mwa majiji makuu ya kaskazini?

Kwa kurejezea ramani, kumbuka historia fulani baada ya makabila kumi ya Kiisraeli kuvunjika kutoka mfalme wa Yehova na hekalu kule Yerusalemu. Yeroboamu, aliyeongoza katika kufanyiza ufalme wa kaskazini, alitawala kwa muda mfupi akiwa Shekemu, katika njia ya mlimani ya kaskazini hadi kusini. Baadaye Yeroboamu alihamisha jiji kuu lake likawa Tirzah, ambayo ilikuwa upande wa juu wa Wadi Far῾ah. Njia moja ya kutoka Bonde la Yordani iliipita Tirzah na kuungana na ile barabara ya mlimani. Je! wewe ulijua kwamba Tirzah lilikuwa jiji kuu la ufalme wa makabila kumi wakati wa tawala za Nadabu, Baasha, Ela, Zimri, na hata Omri?—Mwanzo 12:5-9; 33:17, 18; 1 Wafalme 12:20, 25, 27; 14:17; 16:6, 15, 22.

Ingawa hivyo, baada ya miaka sita, Omri alifanyiza jiji kuu jipya. Wapi? Aliununua mlima ambao wauona upande wa kushoto, Samaria. (1 Wafalme 16:23-28) Ingawa sasa una matungazi mengi ya ukulima, yaelekea Omri aliuchagua kwa sababu kile kilima chenye kilele tambarare ambacho huchomoza kutoka kwenye uwanda kililindwa kwa urahisi. Mwana wake Ahabu aliendelea kujenga Samaria, kwa wazi akipanua maboma yalo kwa kuta zenye maki makubwa. Pia alijenga hekalu kwa ajili ya Baali na jumba la kifalme kwa ajili yake mwenyewe na mke wake Mfoinike, Yezebeli. Machimbuo yamefunua magofu ya jumba la kifalme la Ahabu, katika ukurasa ufuatao. Hilo jumba la kifalme lilijulikana kwa anasa na uovu wa kuzidi mno. (1 Wafalme 16:29-33) Wazia ukimwona nabii Eliya akipanda juu kwenda kwenye jiji hili na kuitembea ile barabara pana ya kwenda kwenye jumba la kifalme, huko akashutumu vikali uovu wa Ahabu wenye kumtegemea Baali.—1 Wafalme 17:1.

Katika 1910 wanaakiolojia walipata huko vigae vya vyungu vikiwa na mwandiko, vikiwa vinarekodi misafirisho ya divai na mafuta ya mzeituni au kodi zilizolipwa. Lakini mengi ya majina ya kibinafsi juu yavyo yalikuwa na kiunganisho baʹal. Huenda ikakupendeza kujua kwamba wanaakiolojia waligundua pia vijipande vya matandazo au mapambo ya kurembesha kuta kwa pembe, kama vile yameonyeshwa hapa. Kumbuka kwamba 1 Wafalme 22:39 ilitaja zamani za kale kwamba Ahabu alijenga “nyumba ya pembe.” Labda hii ilihusisha fanicha zenye mitandazo ya pembe zilizochongwa, kama “pembe ya malalo” yenye fahari ambayo nabii Amosi alirejezea karne moja baadaye. (Amosi 3:12, 15; 6:1, 4) Miongoni mwa virembesho vilivyokuwa juu yayo ni vichwa-simba-mtu vyenye mabawa na vifananisho vingine kutokana na ubuni wa hadithi za Kimisri.

Kutajwa kwa Ahabu na Yezebeli huenda kukakukumbusha jinsi walivyokufa. Ahabu alipoteza uhai wake katika vita ya kipumbavu pamoja na Siria (Shamu). Gari-vita lake lilipooshwa karibu na “birika la Samaria . . . mbwa wakaramba damu yake,” ikawa kweli kulingana na neno la Eliya. (1 Wafalme 21:19; 22:34-38) Malkia Yezebeli alitupwa hadi kifo chake kutoka kwenye dirisha la jumba la kifalme. Je! ilikuwa kutoka kwenye hili jumba la kifalme katika Samaria? Sivyo. Ahabu alikuwa na jumba la kifalme kule juu kaskazini pia katika bonde la Yezreeli. Yeye alilitamani kwa choyo shamba la mizabibu la Nabothi la hapo karibu. Wakiwa kwenye kimo cha hilo jumba la kifalme, wanaume walinzi wenye kutazama upande wa mashariki walimwona Yehu akiendesha kwa kiruu kule bondeni. Na hapo aliyekuwa malkia wa Samaria akatapanyika hadi mwisho wake ulio mbaya sana lakini wenye kustahikika.—1 Wafalme 21:1-16; 2 Wafalme 9:14-37.

Ingawa Samaria liliendelea kuwa jiji kuu, halikuwa na kibali wala baraka ya Mungu. Bali, lilionyesha ushindani na uhasama kuelekea jiji kuu Lake la upande wa kusini, Yerusalemu. Yehova alituma manabii wengi wakaonye watawala wa Samaria na watu walo juu ya ibada-sanamu yao, ukosefu wa adili, na kutostahi sheria zake, lakini wapi. (Isaya 9:9; 10:11; Ezekieli 23:4-10; Hosea 7:1; 10:5; Amosi 3:9; 8:14; Mika 1:1, 6) Hivyo basi katika 740 K.W.K., Samaria lilitozwa hesabu, likaharibiwa na Waashuri. Wengi wa watu walo walichukuliwa mateka, na mahali pao pakachukuliwa na watu wa kigeni.—2 Wafalme 17:1-6, 22-24.

Baadaye, hasa katika wakati wa Herode Mkubwa, Wagiriki na Waroma walilirudishia Samaria umashuhuri fulani. Hivyo basi hata Yesu na mitume walilifahamu hili jiji kuu miongoni mwa majiji makuu ya kaskazini.—Luka 17:11; Yohana 4:4.

[Ramani katika ukurasa wa 16]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Jezreel

Tirzah

Samaria

Shechem

Jerusalem

Jordan River

[Hisani]

Yategemea ramani ambayo haki ya unakili imetolewa na Pictorial Archive (Near Eastern History) Est. and Survey of Israel.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]

Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]

Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.

Garo Nalbandian

Picha-ndani: Idara ya Israeli ya Kumbukumbu za Kale na Majumba ya Makumbusho; foto kutoka Yerusalemu kwenye Jumba la Makumbusho la Israel

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki