Kitabu Cha Biblia Namba 11—1Wafalme
Mwandikaji: Yeremia
Mahali Kilipoandikiwa: Yerusalemu na Yuda
Uandikaji Ulikamilishwa: 580 K.W.K.
Wakati Uliohusishwa: c. (karibu) 1040—911 K.W.K.
1. (a) Fanaka kubwa ya Israeli ilikujaje kuzorota kuwa uharibifu? (b) Hata hivyo ni kwa nini kitabu cha Wafalme wa Kwanza chaweza kuelezwa kuwa ni ‘chenye pumzi ya Mungu na chenye mafaa’?
USHINDI wa Daudi ulikuwa umepanua milki ya Israeli kufikia mipaka yayo iliyopewa na Mungu, tokea mto Frati upande wa kaskazini hadi mto wa Misri upande wa kusini. (2 Sam. 8:3; 1 Fal. 4:21) Kufikia wakati aliokuwa amekufa Daudi na mwana wake Sulemani akawa anatawala katika cheo chake, “Yuda na Israeli walikuwa wengi kama mchanga wa pwani kwa wingi, wakila, na kunywa, na kufurahi.” (1 Fal. 4:20) Sulemani alitawala kwa hekima kuu, hekima iliyozidi sana ile ya Wagiriki wa kale. Alijengea Yehova hekalu zuri sana. Hata hivyo, hata Sulemani alikengeuka kwenye ibada ya miungu bandia. Wakati wa kifo chake ufalme huo uligawanyika mara mbili, na uandamizi wa wafalme waovu katika falme zenye kushindana za Israeli na Yuda ulitenda kwa uharibifu, ukiletea watu msononeko, sawa na alivyokuwa ametabiri Samweli. (1 Sam. 8:10-18) Kati ya wale wafalme 14 waliotawala katika Yuda na katika Israeli baada ya kifo cha Sulemani na kama inavyopitiwa katika kitabu cha Wafalme wa Kwanza, ni 2 tu waliofaulu kufanya yaliyo haki machoni pa Yehova. Basi, je! maandishi hayo ‘yana pumzi ya Mungu na yafaa’? Ndiyo, bila shaka, kama tutakavyoona kutokana na maonyo yayo, unabii mbalimbali na vifananishi vyayo, na uhusiano wayo na habari kuu ya “kila andiko” juu ya Ufalme.
2. Maandishi ya kitabu cha Wafalme wa Kwanza na wa Pili yalikujaje kuwa katika makunjo mawili, nayo yalikusanywaje?
2 Kitabu cha Wafalme hapo awali kilikuwa kunjo, au buku moja, na kiliitwa Mela·khimʹ (Wafalme) katika Kiebrania. Watafsiri wa Septuagint walikiita Ba·si·leiʹon, “Falme,” na ndio waliokuwa wa kwanza kukigawanya kuwa makunjo mawili kwa minajili ya kuchukulika. Baadaye yakaitwa wafalme wa Tatu na Nne, mtajo ambao waendelea katika Biblia za Katoliki hadi wa leo. Hata hivyo, kwa ujumla sasa yajulikana kuwa kitabu cha Wafalme wa Kwanza na wa Pili. Vyatofautiana na kitabu cha Samweli wa Kwanza na wa Pili katika kutaja maandishi ya awali kuwa chanzo cha habari kwa mkusanyaji. Yule mkusanyaji mmoja, katika vitabu hivyo viwili, hurejezea mara 5 “kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda,” mara 18 kwa “kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli,” na pia “kitabuni mwa mambo yake Sulemani.” (1 Fal. 15:7; 14:19; 11:41) Ingawa maandishi hayo mengine ya kale yamekwisha potea kabisa, mkusanyo huu uliopuliziwa na Mungu ungalipo—simulizi lenye mafaa la kitabu cha Wafalme wa Kwanza na wa Pili.
3. (a) Bila shaka ni nani aliyeandika vitabu vya Wafalme, na kwa nini wajibu hivyo? (b) Uandikaji huo ulikamilishwa lini, na ni kipindi gani kinachohusishwa na kitabu cha Wafalme wa Kwanza?
3 Ni nani aliyeandika vitabu vya Wafalme? Mkazo wavyo juu ya kazi ya manabii, hasa Eliya na Elisha, hudokeza ni nabii fulani wa Yehova. Ufanani wa lugha, mtungo, na mtindo hudokeza mwandikaji yule yule wa kitabu cha Yeremia. Maneno mengi na semi nyingi za Kiebrania huonekana katika Wafalme na Yeremia peke yake, na mambo hayo hayamo katika kitabu kingine chochote cha Biblia. Hata hivyo, ikiwa Yeremia aliandika vitabu vya Wafalme, kwa nini hatajwi humo? Haikuwa lazima, kwa maana kazi yake tayari ilikuwa imezungumzwa katika kitabu chenye jina lake. Zaidi ya hayo, vitabu vya Wafalme viliandikwa ili kuadhimisha Yehova na ibada Yake, si kuzidisha sifa ya Yeremia. Kwa kweli, Wafalme na Yeremia vinakamilishana kwa sehemu iliyo kubwa, kila kimoja kikijazia mambo ambayo kile kingine kimeacha. Kuongezea hayo, kuna masimulizi yenye kulingana, kwa kielelezo kama 2 Wafalme 24:18–25:30 na Yeremia 39:1-10; 40:7–41:10; 52:1-34. Mapokeo ya Kiyahudi huthibitisha kwamba Yeremia ndiye aliyekuwa mwandikaji wa kitabu cha Wafalme wa Kwanza na wa Pili. Bila shaka alianza kukusanya vitabu vyote viwili katika Yerusalemu, na yaelekea kwamba kitabu cha pili kilikamilishiwa Misri karibu 580 K.W.K., kwa kuwa arejezea matukio ya mwaka huo katika umalizio wa maandishi yake. (2 Fal. 25:27) Kitabu cha Wafalme wa Kwanza hueleza historia ya Israeli kuanzia mwisho wa Samweli wa Pili na kuiendeleza hadi 911 K.W.K., alipokufa Yehoshafati.—1 Fal. 22:50.
4. Historia ya kilimwengu na akiolojia vyathibitishaje kitabu cha Wafalme wa Kwanza?
4 Kitabu cha Wafalme wa kwanza huchukua mahali panapokifaa katika yanayokubaliwa kuwa Maandiko ya Kiebrania. Zaidi ya hayo, matukio katika kitabu cha Wafalme wa Kwanza yathibitishwa na historia ya nchi za Misri na Ashuru. Akiolojia (uchimbuzi wa vitu vya kale) pia huunga mkono nyingi za taarifa za kitabu hicho. Kwa kielelezo, kwenye 1 Wafalme 7:45, 46 twasoma kwamba ilikuwa “katika uwanda wa Yordani . . . kati ya Sukothi na Sarethani” kwamba Hiramu alisubu (aliunda) vyombo vya shaba vya hekalu la Sulemani. Waakiolojia wanaochimba kwenye kituo hicho cha Sukothi ya kale wamechimbua ushuhuda wa kukalibu (uyeyushaji) huko.a Kuongezea hayo, mchoro kwenye ukuta wa hekalu kule Karnaki (Thebesi ya kale) hujivunia shambulio juu ya Yuda na mfalme Sheshonki (Shishaki) Mmisri, yanayorejezewa kwenye 1 Wafalme 14:25, 26.b
5. Ni ushuhuda gani uliopuliziwa na Mungu unaothibitisha uasilia wa kitabu cha Wafalme wa Kwanza?
5 Marejezo ya waandikaji wengineo wa Biblia na utimizo mbalimbali wa unabii huunga mkono uasilia wa kitabu cha Wafalme wa Kwanza. Yesu alinena juu ya matukio yaliyozunguka Eliya na mjane wa Sarepta kuwa uhalisi wa kihistoria. (Luka 4:24-26) Akinena juu ya Yohana Mbatizaji, Yesu alisema: “Yeye ndiye Eliya atakayekuja.” (Mt. 11:13, 14) Hapa Yesu alikuwa akirejezea unabii wa Malaki, aliyenena pia hivi juu ya siku za usoni: “Angalieni, nitawapelekea Eliya nabii, kabla haijaja siku ile ya BWANA [Yehova, NW], iliyo kuu na kuogofya.” (Mal. 4:5) Yesu alishuhudia zaidi juu ya kitabu cha Wafalme wa Kwanza kuwa chenye kukubaliwa aliporejezea yale ambayo yameandikwa katika kitabu hicho kuhusu Sulemani na pia malkia wa kusini.—Mt. 6:29; 12:42; linganisha 1 Wafalme 10:1-9.
YALIYOMO KATIKA WAFALME WA KWANZA
6. Ni chini ya hali gani Sulemani anakalia kiti cha enzi, na ni jinsi gani yeye anaimarika katika ufalme?
6 Sulemani awa mfalme (1:1–2:46). Maandishi ya kitabu cha Wafalme wa Kwanza yaanza na Daudi akiwa mahututi akaribiapo umalizio wa utawala wake wa miaka 40. Mwana wake Adoniya, kwa msaada wa Yoabu mkuu wa jeshi na Abiathari kuhani, atunga njama ya kutwaa ufalme. Nabii Nathani ajulisha Daudi juu ya hilo na kwa njia isiyo ya moja kwa moja amkumbusha kwamba tayari amekwisha teua Sulemani awe mfalme afapo. Kwa hiyo Daudi aagiza Sadoki kuhani ampake Sulemani mafuta kuwa mfalme, huku watunga njama wakisherehekea uandamizi wa Adoniya. Sasa Daudi amwagiza Sulemani awe mwenye nguvu na kujithibitisha mwenyewe kuwa mwanamume na kutembea katika njia za Yehova Mungu wake, kisha Daudi afa na kuzikwa “mjini mwa Daudi.” (2:10) Punde si punde Sulemani apeleka Abiathari uhamishoni na kuua wafanya matata Adoniya na Yoabu. Baadaye, Shimei auawa akosapo kuonyesha heshima kwa ajili ya mpango wa rehema uliofanywa wa kuponya uhai wake. Sasa ufalme wasimamishwa imara mikononi mwa Sulemani.
7. Ni sala gani ya Sulemani ambayo Yehova ajibu, na tokeo lawa nini kwa Israeli?
7 Utawala wa hekima wa Sulemani (3:1–4:34). Sulemani afanya mapatano ya ndoa pamoja na Misri kwa kuoa binti ya Farao. Asali kwa Yehova ampe moyo mtiifu kusudi ahukumu watu wa Yehova kwa ufahamu. Kwa sababu yeye haombi maisha marefu wala utajiri, Yehova aahidi kumpa moyo wa hekima wenye ufahamu na pia utajiri na utukufu. Katika utawala wake, Sulemani aonyesha hekima yake wakati wanawake wawili wajapo mbele yake wakidai mtoto yule yule. Sulemani aagiza wanaume wake ‘wamkate mtoto aliye hai vipande viwili’ na kumpa kila mwanamke nusu. (3:25) Ndiposa mama halisi anaposihi kwa ajili ya uhai wa mtoto, akisema yule mwanamke mwingine apewe. Kwa njia hiyo Sulemani atambua mama astahiliye, naye apata mtoto. Kwa sababu ya hekima ya Sulemani aliyopewa na Mungu, Israeli yote yafanikiwa na yawa yenye furaha na salama. Watu kutoka mabara mengi waja kusikia semi zake za hekima.
8. (a) Sulemani ajengaje hekalu? Eleza baadhi ya sehemu zalo. (b) Ni programu gani zaidi ya ujenzi anayotekeleza?
8 Hekalu la Sulemani (5:1–10:29). Sulemani akumbuka maneno ya Yehova kwa baba yake, Daudi: “Mwana wako, nitakayemweka katika kiti chake cha enzi mahali pako, ndiye atakayeijenga nyumba kwa jina langu.” (5:5) Kwa hiyo Sulemani afanya matayarisho kwa ajili ya hilo. Hiramu mfalme wa Tiro asaidia kwa kupeleka mbao za mierezi na miberoshi kutoka Lebanoni na kwa kuandaa wafanya kazi stadi. Wao, pamoja na wafanya kazi ngumu ya lazima ya Sulemani, waanza kazi ya nyumba ya Yehova katika mwaka wa nne wa utawala wa Sulemani, katika mwaka wa 480 baada ya Waisraeli kutoka Misri. (6:1) Hakuna nyundo, mashoka, au vyombo vyote vya chuma vinavyotumiwa kwenye kituo cha ujenzi, kwa kuwa mawe yote yatayarishwa na kulengetwa (kupambwa) kwenye shimo la kuchongea kabla ya kuletwa kwenye kituo cha hekalu ili kuunganishwa. Sehemu yote ya ndani ya hekalu, iliyofunikwa kwanza kwa mierezi kwenye kuta na mbao za miberoshi kwenye sakafu, sasa yafunikwa vizuri kwa dhahabu. Maumbo mawili ya makerubi yafanyizwa kwa ubao wa mzeituni, kila moja likiwa na kimo cha mikono kumi (meta 4.5) kwa urefu na mikono kumi toka ncha moja ya ubawa hadi ncha nyingine ya ubawa, nayo yawekwa katika chumba cha ndani zaidi. Makerubi wengine, pamoja na maumbo na michanuo ya mitende, yanakshiwa kwenye kuta za hekalu. Hatimaye, baada ya zaidi ya miaka saba ya kazi, hekalu zuri sana lakamilishwa. Sulemani aendelea na programu yake ya ujenzi: nyumba kwa ajili yake mwenyewe, Nyumba ya Msitu wa Lebanoni, na Ukumbi wa Nguzo, Ukumbi wa Kiti cha Enzi, na nyumba kwa ajili ya binti ya Farao. Pia ajenga nguzo mbili kubwa za shaba kwa ajili ya sebule ya nyumba ya Yehova, bahari ya subu kwa ajili ya baraza, na vichukuzi vya shaba, na pia mabakuli ya shaba na vyombo vya dhahabu.c
9. Ni udhihirisho gani wa Yehova na ni sala gani ya Sulemani inayotia alama kuingizwa kwa sanduku la agano?
9 Sasa wakati wawadia wa makuhani kuleta sanduku la agano la Yehova na kuliweka ndani ya chumba cha ndani zaidi, Patakatifu Zaidi, chini ya mabawa ya makerubi. Makuhani watokapo nje, ‘utukufu wa Yehova wajaza nyumba ya Yehova,’ hivi kwamba makuhani hawawezi kuendelea kusimama na kuhudumu. (8:11) Sulemani abariki kundi la Israeli, na abariki na kusifu Yehova. Akipiga magoti na viganja vyake vikiwa vimefumbuliwa kuelekea mbinguni, akiri kwa sala kwamba mbingu za mbingu haziwezi kumtosha Yehova, sembuse (itawezaje) nyumba hii ya kidunia aliyojenga. Asali kwamba Yehova atasikia wale wote wanaohofu Yeye wasalipo kuelekea nyumba hii, ndiyo, hata mgeni kutoka bara la mbali, “ili watu wote wa dunia wapate kulijua jina lako, na kukucha wewe kama watu wako Israeli.”—8:43.
10. Yehova ajibu sala ya Sulemani kwa ahadi na onyo gani la kiunabii?
10 Wakati wa karamu ya siku 14 inayofuata, Sulemani atoa dhabihu ng’ombe 22,000 na kondoo 120,000. Yehova amwambia Sulemani kwamba Yeye amesikia sala yake na kwamba Yeye ametakasa hekalu kwa kuweka ‘jina Lake humo milele.’ Sasa, ikiwa Sulemani atatembea kwa unyoofu mbele ya Yehova, kiti cha enzi cha ufalme wake kitaendelea. Hata hivyo, ikiwa Sulemani na wana wake baada yake wataacha ibada ya Yehova na kutumikia miungu mingine, basi, asema Yehova, “nitawakatilia Israeli mbali na nchi hii niliyowapa; na nyumba hii niliyoitakasa kwa jina langu, nitaitupilia mbali na macho yangu, na Israeli watakuwa mithali na neno la tusi katika mataifa yote. [Na nyumba hii yenyewe itakuwa vifusi vya mabomoko, NW].”—9:3, 7, 8.
11. Utajiri na hekima za Sulemani vyaenea kadiri gani?
11 Imemchukua Sulemani miaka 20 kukamilisha nyumba hizo mbili, nyumba ya Yehova na nyumba ya mfalme. Sasa achukua hatua ya kujenga majiji mengi katika milki yake yote, na pia merikebu za matumizi katika biashara pamoja na mabara ya mbali. Ndivyo malkia wa Sheba anavyosikia juu ya hekima kubwa ambayo Yehova amempa Sulemani, naye aja kumtia kwenye mtihani wa maswali yenye kutatanisha (magumu). Baada ya kumsikia na kuona fanaka na furaha ya watu wake, atamka hivi: “Sikuambiwa nusu.” (10:7) Yehova anapoendelea kuonyesha Israeli upendo, Sulemani apita “wafalme wote wa duniani kwa mali, na kwa hekima.”—10:23.
12. (a) Sulemani akengeuka kwenye nini, na ni mbegu gani za uasi zinazoanza kutokea? (b) Ahiya atabiri nini?
12 Ukosefu wa uaminifu wa Sulemani na kifo chake (11:1-43). Kinyume cha amri ya Yehova, Sulemani achukua wake wengi kutoka mataifa mengine—wake 700 na masuria 300. (Kum. 17:17) Moyo wake wakengeushwa utumikie miungu mingine. Yehova amwambia kwamba ufalme utararuliwa kutoka kwake, si katika siku yake, bali katika siku ya mwana wake. Hata hivyo, sehemu ya ufalme, kabila moja kuongezea Yuda, litatawalwa na wana wa Sulemani. Mungu aanza kutokezea Sulemani wapinzani kutoka mataifa ya karibu, na Yeroboamu wa kabila la Efraimu pia ajiinua kupinga mfalme huyo. Ahiya nabii amwambia Yeroboamu kwamba atakuwa mfalme juu ya makabila kumi ya Israeli, na Yeroboamu atorokea Misri aponye uhai wake. Sulemani afa baada ya kutawala kwa miaka 40, na mwana wake Rehoboamu awa mfalme katika mwaka 997 K.W.K.
13. Mgawanyiko watokeaje katika ufalme Rehoboamu aanzapo utawala wake, na Yeroboamu ajaribuje kufanya ufalme wake kuwa salama?
13 Ufalme wagawanyika (12:1–14:20). Yeroboamu arejea kutoka Misri na kwenda pamoja na watu kuuliza Rehoboamu awapumzishe kutoka kwa mizigo yote ambayo Sulemani alikuwa ameweka juu yao. Akisikiliza wanaume wachanga badala ya shauri la hekima la wazee katika Israeli, Rehoboamu azidisha magumu. Israeli wainuka katika maasi na kufanya Yeroboamu kuwa mfalme juu ya makabila kumi ya kaskazini. Rehoboamu, akiwa ameachwa na Yuda na Benyamini tu, akusanya jeshi apigane na waasi, lakini kwa amri ya Yehova arudi. Yeroboamu ajenga Shekemu kuwa mji mkuu wake, lakini bado hajioni salama. Ahofu kwamba watu watarudi Yerusalemu ili kuabudu Yehova na kwamba watakuja chini ya Rehoboamu tena. Ili kuzuia hilo, asimamisha ndama wawili wa dhahabu, mmoja katika Dani na mwingine katika Betheli, na ili kuelekeza ibada hiyo, achagua makuhani, si kutoka kwa kabila la Lawi, bali kutoka miongoni mwa watu kwa ujumla.d
14. Ni onyo gani la kiunabii linalovumishwa juu ya nyumba ya Yeroboamu, na ni misiba gani yaanza?
14 Yeroboamu akiwa anatoa dhabihu kwenye madhabahu katika Betheli, Yehova apeleka nabii mmoja amwonye kwamba Yeye atainua mfalme kutoka kwa nasaba ya Daudi, jina lake Yosia, ambaye atachukulia madhabahu hiyo ya bandia hatua kali. Ili kuwa dalili, madhabahu yapasuliwa papo kwa hapo. Huyo nabii mwenyewe auawa baadaye na simba kwa ajili ya kukosa kutii agizo la Yehova la kutokula wala kunywa akiwa kwenye utume wake. Sasa msiba waanza kupiga nyumba ya Yeroboamu. Mtoto wake afa ikiwa ni hukumu kutoka kwa Yehova, na Ahiya nabii wa Mungu atabiri kwamba nyumba ya Yeroboamu itakatiliwa mbali kabisa kwa sababu ya dhambi kubwa yake ya kusimamisha miungu bandia katika Israeli. Baada ya kutawala kwa miaka 22 Yeroboamu afa na mwana wake Nadabu awa mfalme mahali pake.
15. Ni matukio gani yanayotokea wakati wa tawala za wafalme watatu wanaofuata katika Yuda?
15 Katika Yuda: Rehoboamu, Abiyamu, na Asa (14:21–15:24). Wakati ule ule, chini ya Rehoboamu, Yuda pia wanafanya yaliyo mabaya machoni pa Yehova, wakizoea ibada ya sanamu. Mfalme wa Misri avamia na kuchukua hazina nyingi za hekalu. Baada ya kutawala miaka 17, Rehoboamu afa, na mwana wake Abiyamu awa mfalme. Yeye pia aendelea kumtenda Yehova dhambi, na afa baada ya kutawala kwa miaka mitatu. Mwana wake, Asa, sasa atawala na, kinyume chake, atumikia Yehova kwa moyo kamili na kuondoa sanamu zenye kuchukiza sana kutoka kwenye bara. Kuna mapigano ya kudumu baina ya Israeli na Yuda. Asa apata msaada kutoka Shamu, na Israeli walazimika kujiondosha. Asa atawala kwa miaka 41 na mwandamizi wake awa mwana wake Yehoshafati.
16. Ni matukio gani yenye mchafuko yanayotukia sasa katika Israeli, na kwa nini?
16 Katika Israeli: Nadabu, Baasha, Ela, Zimri, Tibni, Omri, na Ahabu (15:25–16:34). Umati mwovu ulioje! Baasha amwua Nadabu baada ya yeye kutawala kwa miaka miwili tu na kufuatia hilo aangamiza nyumba yote ya Yeroboamu. Aendelea katika ibada bandia na katika kupigana na Yuda. Yehova atabiri kwamba Yeye atafagia kabisa nyumba yote ya Baasha, sawa na alivyoifanya ya Yeroboamu. Baada ya utawala wa Baasha wa miaka 24, mwandamizi wake awa mwana wake Ela, ambaye auawa miaka miwili baadaye na mtumishi wake Zimri. Punde tu achukuapo kiti cha enzi, Zimri apiga dharuba nyumba yote ya Baasha. Watu wasikiapo hilo, wafanya Omri, mkuu wa jeshi, kuwa mfalme na kuja kupigana na Tirza, mji mkuu wa Zimri. Aonapo kwamba hakuna tumaini, Zimri ateketeza nyumba ya mfalme akiwemo, naye afa hivyo. Sasa Tibni ajaribu kutawala akiwa mfalme mshindani, lakini baada ya muda wafuasi wa Omri wamshinda nguvu na kumwua.
17. (a) Utawala wa Omri wajulikana kwa ajili ya nini? (b) Ni kwa nini ibada ya kweli yashuka kabisa wakati wa utawala wa Ahabu?
17 Omri anunua mlima wa Samaria na kujenga huko jiji la Samaria. Aendelea kutembea katika njia zote za Yeroboamu, akimwudhi Yehova kwa ibada ya sanamu. Kwa kweli, yeye ni mbaya zaidi ya wengine wote waliomtangulia. Baada ya kutawala miaka 12, afa na Ahabu mwana wake awa mfalme. Ahabu aoa Yezebeli, binti ya mfalme wa Sidoni, na kisha asimamisha madhabahu ya Baali katika Samaria. Awazidi katika uovu wote waliomtangulia. Ni katika wakati huu Hieli Mbetheli anapojenga upya jiji la Yeriko hilo likigharimu uhai wa mwana mzaliwa wake wa kwanza na mwana wake mchanga zaidi. Ibada ya kweli imeshuka kabisa.
18. Eliya aanza kazi yake ya kiunabii kwa tangazo gani katika Israeli, naye aonyeshaje sababu halisi ya taabu za Israeli?
18 Kazi ya kiunabii ya Eliya katika Israeli (17:1–22:40). Ghafula mjumbe kutoka kwa Yehova ajitokeza. Ni Eliya Mtishbi.e Tangazo lake la kwanza kwa Mfalme Ahabu ni lenye kushtua kweli kweli: “Kama BWANA [Yehova, NW], Mungu wa Israeli, aishivyo, ambaye ninasimama mbele zake, hakutakuwa na umande wala mvua miaka hii, ila kwa neno langu!” (17:1) Kwa ghafula jinsi iyo hiyo, Eliya arudi kwa mwelekezo wa Yehova kwenye bonde fulani mashariki mwa Yordani. Kuna ukame katika Israeli, lakini kunguru wamletea Eliya chakula. Kijito cha bonde hilo kinyaukapo, Yehova apeleka nabii wake akakae Sarepta katika Sidoni. Kwa sababu ya fadhili za mjane kuelekea Eliya, Yehova ajaza kimwujiza ugavi wake mdogo wa unga na mafuta hivi kwamba yeye na mwana wake hawafi njaa. Baadaye mwana huyo apatwa na ugonjwa na kufa, lakini Yehova arudisha uhai wa mtoto huyo Eliya amsihipo. Kisha, katika mwaka wa tatu wa ukame, Yehova apeleka Eliya kwa Ahabu tena. Ahabu ashtaki Eliya kwa kuletea Israeli taabu, lakini Eliya amwambia Ahabu kwa ujasiri hivi: “Ni wewe, na nyumba ya baba yako” kwa sababu ya kufuata Mabaali.—18:18.
19. Suala la uungu latokezwaje wazi, na ukuu wa Yehova wathibitishwaje?
19 Eliya apeleka mwito kwa Ahabu akusanye manabii wote wa Baali kwenye Mlima Karmeli. Haitawezekana tena kuchechemaa kwenye kauli mbili. Suala ni wazi: Yehova kukabiliana na Baali! Mbele ya watu wote, makuhani 450 wa Baali watayarisha fahali, wamweka kwenye kuni juu ya madhabahu, na wasali moto ushuke na kuteketeza sadaka hiyo. Tangu asubuhi hadi alasiri, wamwitia Baali lakini wapi, huku Eliya akiwadhihaki. Wapiga kelele na kujikatakata, lakini hakuna jibu! Kisha, yule nabii mmoja, Eliya, ajenga madhabahu katika jina la Yehova na kutayarisha kuni na fahali kwa ajili ya dhabihu. Aambia watu wachovye sadaka na kuni mara tatu ndani ya maji, na kisha asali hivi kwa Yehova: “Unisikie, Ee BWANA [Yehova, NW], unisikie, ili watu hawa wajue ya kuwa wewe, BWANA [Yehova, NW], ndiwe Mungu [wa kweli, NW].” Kisha, moto kutoka mbinguni wamweka, ukiiteketeza sadaka hiyo, kuni, mawe ya madhabahu, mavumbi, na maji. Watu wote waonapo, bila kukawia walala kifudifudi na kusema: “BWANA [Yehova, NW] ndiye Mungu [wa kweli, NW], BWANA [Yehova, NW] ndiye Mungu [wa kweli, NW]!” (18:37, 39) Kifo kwa manabii wa Baali! Eliya binafsi ahakikisha mauaji hayo, hivi kwamba hakuna yeyote anayeponyoka. Kisha Yehova atoa mvua, kumaliza ukame katika Israeli.
20. (a) Yehova amtokeaje Eliya katika Horebu, na Yeye atoa agizo na faraja gani? (b) Ni dhambi na uhalifu gani unaofanywa na Ahabu?
20 Habari za kuvunjiwa heshima kwa Baali zimfikiapo Yezebeli, atafuta kumwua Eliya. Kwa kuhofu, yeye atoroka pamoja na mtumishi wake kwenye nyika, na Yehova amwelekeza kwenda Horebu. Kule Yehova amtokea—la, si kwa tamasha katika upepo wala mtetemo wala moto, bali kwa “sauti ndogo, ya utulivu.” (19:11, 12) Yehova amwambia apake mafuta Hazaeli kuwa mfalme wa Shamu, Yehu kuwa mfalme juu ya Israeli, na Elisha kuwa nabii mahali pake. Amfariji Eliya kwa habari kwamba 7,000 katika Israeli hawajasujudia Baali. Eliya achukua hatua ya mara moja kupaka mafuta Elisha kwa kutupa vazi lake rasmi juu yake. Sasa Ahabu apata ushindi mara mbili juu ya Washami lakini akemewa na Yehova kwa ajili ya kufanya agano pamoja na mfalme wao badala ya kumwua. Kisha chaja kile kisa cha Nabothi, ambaye shamba lake la mizabibu alitamani Ahabu. Yezebeli aagiza Nabothi asingiziwe na mashahidi bandia na kuuawa ili Ahabu atwae shamba hilo la mizabibu. Jinsi huo ulivyo uhalifu usiosameheka!
21. (a) Eliya atangaza maangamizi gani juu ya Ahabu na nyumba yake, na juu ya Yezebeli? (b) Ni unabii gani unaotimizwa penye kifo cha Ahabu?
21 Kwa mara nyingine Eliya atokea. Amwambia Ahabu kwamba mahali alipofia Nabothi, mbwa wataramba damu yake pia, na kwamba nyumba yake itaangamizwa kabisa kama zile za Yeroboamu na Baasha. Mbwa watamla Yezebeli katika shamba la ardhi ya Yezreeli. “Hapakuwa na mtu kama Ahabu, aliyejiuza atende maovu machoni pa BWANA [Yehova, NW], ambaye Yezebeli mkewe alimchochea.” (21:25) Hata hivyo, kwa sababu Ahabu ajinyenyekeza asikiapo maneno ya Eliya, Yehova asema kwamba msiba huo hautakuja katika siku zake bali katika siku za mwana wake. Ahabu sasa ajiunga na Yehoshafati, mfalme wa Yuda, katika pigano juu ya Shamu, na kinyume cha shauri la Mikaya nabii wa Yehova, waenda kwenye pigano. Ahabu afa kwa majeraha aliyopata kwenye pigano. Gari-farasi lake la vita lioshwapo kwenye kidimbwi cha Samaria, mbwa waramba damu yake, sawa na alivyotabiri Eliya. Ahazia mwana wake awa mfalme wa Israeli mahali pake.
22. Ni nini kinachokuwa sehemu ya utawala wa Yehoshafati katika Yuda na wa Ahazia katika Israeli?
22 Yehoshafati atawala katika Yuda (22:41-53). Yehoshafati, aliyeandamana na Ahabu kwenye pigano na Shamu, ni mwaminifu kwa Yehova kama Asa baba yake, lakini akosa kuondoa kabisa sehemu za juu za ibada bandia. Baada ya kutawala kwa miaka 25, yeye afa, na Yehoramu mwana wake awa mfalme. Kule kaskazini, katika Israeli, Ahazia afuata nyayo za baba yake, akimwudhi Yehova kwa ibada yake ya Baali.
KWA NINI NI CHENYE MAFAA
23. Ni uhakikisho na kitia-moyo gani vinavyotolewa na kitabu cha Wafalme wa Kwanza kwa habari ya sala?
23 Mafaa makubwa yapatikana katika agizo la kimungu katika kitabu cha Wafalme wa Kwanza. Kwanza, fikiria jambo linalohusu sala, ambalo lajitokeza mara nyingi katika kitabu hiki. Sulemani, alipokabiliwa na daraka kubwa la ufalme katika Israeli, alisali kwa unyenyekevu kwa Yehova kwa namna ya mtoto. Aliomba tu ufahamu na moyo wa utiifu, lakini kuongezea kumpa hekima ya kipimo chenye kufurika, Yehova alimpa pia utajiri na utukufu. (3:7-9, 12-14) Sisi na tuwe na uhakikisho leo kwamba sala zetu za unyenyekevu za kuomba hekima na mwelekezo katika utumishi wa Yehova hazitakosa kujibiwa! (Yak. 1:5) Daima na tusali kwa bidii toka moyoni, tukiwa na uthamini wa kina kirefu kwa ajili ya wema wote wa Yehova, sawa na Sulemani wakati wa hekalu kuwekwa wakfu! (1 Fal. 8:22-53) Daima sala zetu na ziwe na muhuri wa tegemeo kamili na uhakika katika Yehova, sawa na zilivyokuwa sala za Eliya katika wakati wa jaribu na alipokabiliana uso kwa uso na taifa lenye kuabudu roho waovu! Yehova husaidia kwa utele sana wale wanaomtafuta katika sala.—1 Fal. 17:20-22; 18:36-40; 1 Yn. 5:14.
24. Ni vielelezo gani vya onyo vinavyotolewa katika kitabu cha Wafalme wa Kwanza, na kwa nini, hasa, waangalizi wapaswa kuelekeza uangalifu?
24 Zaidi ya hayo, twapaswa kuonywa na vielelezo vya wale ambao hawakujinyenyekeza mbele ya Yehova. Lo! jinsi ‘Mungu apingavyo wenye kiburi’! (1 Pet. 5:5) Kulikuwa Adoniya, aliyedhani angeweza kujitanguliza mbele ya mwekwa-kitheokrasi wa Yehova (1 Fal. 1:5; 2:24, 25); Shimei, aliyedhani angeweza kuvuka mipaka na kurudi tena (2:37, 41-46); Sulemani katika miaka yake ya baadaye, ambaye ukosefu wake wa utii ulileta maadui kutoka kwa Yehova (11:9-14, 23-26); na wafalme wa Israeli, ambao dini yao bandia ilipata kuwa yenye maafa (13:33, 34; 14:7-11; 16:1-4). Zaidi ya hayo, kulikuwako yule Yezebeli mwenye tamaa mbovu, aliyekuwa mamlaka iliyotegemeza kiti cha enzi cha Ahabu, ambaye kielelezo chake chenye sifa mbaya sana kilitumiwa miaka elfu moja baadaye katika kuonya kundi katika Thiatira: “Lakini nina neno juu yako, ya kwamba wamridhia yule mwanamke Yezebeli, yeye ajiitaye nabii na kuwafundisha watumishi wangu na kuwapoteza, ili wazini na kula vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu.” (Ufu. 2:20) Ni lazima waangalizi watunze makundi yakiwa safi na bila ya uvutano mbalimbali wa Kiyezebeli!—Linganisha Matendo 20:28-30.
25. Ni unabii gani mbalimbali wa kitabu cha Wafalme wa Kwanza umetimizwa kwa njia ya kutokeza, na kuukumbuka kwaweza kutusaidiaje sisi leo?
25 Uwezo wa Yehova wa unabii waonyeshwa waziwazi katika utimizo wa unabii mwingi uliotolewa katika kitabu cha Wafalme wa Kwanza. Kwa kielelezo, kuna utabiri wenye kutokeza, uliotolewa zaidi ya miaka 300 kimbele, kwamba Yosia ndiye angevunja-vunja madhabahu ya Yeroboamu kule Betheli. Yosia alifanya hivyo! (1 Fal. 13:1-3; 2 Fal. 23:15) Hata hivyo, wenye kutokeza sana ni ule unabii mbalimbali unaohusu nyumba ya Yehova, iliyojengwa na Sulemani. Yehova alimwambia Sulemani kwamba kukengeuka kwenye miungu bandia kungetokeza kukatiliwa mbali kwa Israeli kutoka kwenye uso wa nchi na kwamba Yeye angetupilia mbali kutoka mbele ya uso Wake nyumba ambayo Yeye alikuwa ametakasa kwa jina lake. (1 Fal. 9:7, 8) Kwenye 2 Mambo ya Nyakati 36:17-21 twasoma jinsi unabii huo ulivyothibitika kuwa kweli kabisa. Zaidi ya hayo, Yesu alionyesha kwamba lile hekalu la baadaye lililojengwa na Herode Mkuu kwenye kituo icho hicho lingepatwa na ayo hayo na kwa sababu ile ile. (Luka 21:6) Jinsi hilo pia lilivyopata kuwa kweli! Twapaswa kukumbuka misiba hiyo na sababu yayo, na hayo yapasa kutukumbusha sisi tutembee daima katika njia za Mungu wa kweli.
26. Ni maono gani ya kimbele yenye kusisimua ya hekalu na Ufalme wa Yehova yanayotolewa katika kitabu cha Wafalme wa Kwanza?
26 Malkia wa Sheba alitoka nchi yake ya mbali ili astaajabie hekima ya Sulemani, fanaka ya watu wake, na utukufu wa ufalme wake, kutia na nyumba nzuri sana ya Yehova. Hata hivyo, hata Sulemani alikiri hivi kwa Yehova: “Tazama, mbingu hazikutoshi, wala mbingu za mbingu; sembuse nyumba hii niliyoijenga!” (1 Fal. 8:27; 10:4-9) Lakini karne nyingi baadaye Kristo Yesu alikuja kutekeleza kazi ya ujenzi wa kiroho hasa kuhusiana na kurudishwa kwa ibada ya kweli kwenye hekalu kuu la kiroho la Yehova. (Ebr. 8:1-5; 9:2-10, 23) Kwa huyu, aliye mkuu zaidi ya Sulemani, ahadi ya Yehova ni kweli: “Ndipo nitakapokifanya imara kiti cha ufalme wako juu ya Israeli milele.” (1 Fal. 9:5; Mt. 1:1, 6, 7, 16; 12:42; Luka 1:32) Kitabu cha Wafalme wa Kwanza chatoa maono ya kimbele ya utukufu wa hekalu la kiroho la Yehova na ya fanaka, shangwe, na furaha yenye kupendeza ya wote watakaokuja kuishi chini ya utawala wa hekima wa Ufalme wa Yehova kupitia Kristo Yesu. Uthamini wetu wa umaana wa ibada ya kweli na wa mpango mzuri sana wa Yehova wa Ufalme wake kupitia Mbegu waendelea kukua!
[Maelezo ya Chini]
a The International Standard Bible Encyclopedia, Buku 4, 1988, kilichohaririwa na G. W. Bromiley, ukurasa 648.
b Insight on the Scriptures, Buku 1, kurasa 149, 952.
c Insight on the Scriptures, Buku 1, kurasa 750-1.
d Insight on the Scriptures, Buku 1, kurasa 949-50.
e Insight on the Scriptures, Buku 1, kurasa 947-8