“Machozi ya Uthamini”
“HUKU nikilia machozi ya uthamini, ni sasa tu nimemaliza kusoma ile makala ‘Jinsi ya Kusaidia Walioshuka Moyo Wapate Shangwe Tena.’” (Mnara wa Mlinzi Machi 15, 1990, kurasa 26-30) Hivyo ndivyo ilivyoanza moja ya barua nyingi za uthamini zilizopokewa na Sosaiti kwa ajili ya makala zinazohusu mshuko wa moyo zilizoonekana katika matoleo yetu ya Machi 1 na Machi 15, 1990. Hata hivyo, maoni haya hasa yalitoka kwa dada mmoja katika Japani ambaye mwana wake mchanga alisumbuliwa na skizofrenia hivi majuzi. Mama huyo anaeleza hivi:
“Nikiwa kila siku ninaifariji na kuitia moyo mkuu nafsi iliyoshuka moyo, nyakati fulani najisikia nimechoka mno nisiweze kuendelea. Giza linapoingia, mwana wangu anashikwa na hofu na wasiwasi. Hivyo basi mimi ninampa vibonge vya kulala na kuketi kando yake kitandani nikisugua mikono yake na kuweka mkono wangu juu ya kipaji cha uso wake mpaka anapolala. Ni kama kufanya mtoto mchanga alale, na baada ya karibu saa moja, yeye mwishowe analala usingizi mzito. Hapo ndipo mimi najisikia nikiwa na kitulizo, lakini wakati uo huo, najiambia kwamba asubuhi ya kesho italeta siku nyingine ya kupambana nayo mpaka iishe.
“Mwana wangu huwa anasema, ‘Mimi sina faida yoyote. Hakuna tumaini kwangu.’ Kila siku yeye anauliza kwa huzuni, ‘Je! mimi nitaponywa ugonjwa wangu? Ni wakati gani nitakuwa huru na dawa? Aina hii ya maisha itaendelea kwa muda gani?’ Nyakati kama hizo mimi natumia maswali kubadili kufikiri kwake kama vile magazeti yaliyodokeza, na hii inamsaidia apate nguvu kwa kadiri fulani. Lakini sisi huwa tunarudia hayo hayo siku nenda, siku rudi.
“Pia kuna nyakati ambapo mwana wangu anaita wazee [kutoka kundi la mahali petu] katikati ya usiku anapoona wasiwasi kabisa na kuwaomba watoe sala kwa ajili yake. Jambo hili linaonekana kuwa la faraja kubwa kwake na kutuliza akili yake. . . . Mara nyingi, hali ya mwana wangu inakuwa mbaya zaidi wakati mume wangu (asiyeamini) anapokuwa ameenda safari za kikazi. Ninapoomba msaada katika simu, ndugu wengi wanakuja mbio nyumbani kwetu.
“Nawapa asante nyinyi, akina ndugu, kutoka kwenye kina cha moyo wangu kwa kuchapisha kwenu makala za aina hii mara kwa mara na kuonyesha mnajali mahitaji ya walio dhaifu.”
[Imetiwa sahihi] H. H.