Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w91 2/1 uku. 31
  • ‘Taji Na Ushuhuda’

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • ‘Taji Na Ushuhuda’
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1991
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1991
w91 2/1 uku. 31

‘Taji Na Ushuhuda’

“NDIPO [Yehoyada kuhani] akamleta nje mwana wa mfalme, akamvika taji, na kumpa [akaweka juu yake, NW] ushuhuda; wakamfanya mfalme, wakamtia mafuta.” (2 Wafalme 11:12) Hivyo ndivyo kitabu cha Wafalme kinavyoeleza kutawazwa kwa Mfalme Yehoashi. Je! umeona kwamba zaidi ya lile “taji,” au vao la kichwani la kifalme, Yehoyada aliweka pia “ushuhuda” juu ya yule mfalme mchanga. Ushuhuda huo ulikuwa nini? Kwa nini ulikuwa sehemu ya sherehe hii ya kutawazwa?

Neno la Kiebrania lililotafsiriwa “ushuhuda” hapa kwa kawaida linamaanisha zile Amri Kumi au Sheria ya Mungu kwa ujumla. (Kutoka 31:18; Zaburi 78:5, Revised Standard Version) Kupatana na hili, usimulizi ule unaolingana na huo kwenye 2 Nyakati 23:11 unasomeka hivi katika The Jerusalem Bible (1966): “Ndipo Yehoyada akamleta nje mwana wa mfalme, akamvika taji, na kuweka ile Sheria juu yake.” Hata hivyo, kwenye 2 Wafalme 11:12, tafsiri hii inatumia neno “vikuku” badala ya “ushuhuda,” ingawa neno hilo hilo la Kiebrania linaonekana katika mistari yote miwili. Kwa nini?

Kitabu maarufu cha Biblia ya Kijerumani, Herders Bibelkommentar, kinaeleza kwamba watafsiri fulani hawawezi kuwazia kwamba mfalme angeivaa Sheria juu ya kichwa chake au juu ya mkono wake. Kwa kuwa, wakati wa kuzungumza juu ya Mfalme Sauli, 2 Samweli 1:10 inataja kikuku (au, bangili) pamoja na taji alilovaa, wanaamini kwamba andiko lililo kwenye 2 Wafalme 11:12 ni lazima hapo kwanza liwe lilisomeka “lile taji na vile vikuku.” Lakini huku ni kudhania tu. Kuweka “ushuhuda” badala ya “vikuku” kunawakilisha badiliko kubwa la kimaandiko.

Kwa hiyo The New Jerusalem Bible (1985) inarudisha wazo la ile Sheria, au agano la sheria, ikifasiri kifungu hicho cha maneno kuwa, “na kumpa nakala ya lile agano.” Lakini je! Yehoyada alimpa Yehoashi ule “ushuhuda”? Ni kweli, neno la Kiebrania linalotafsiriwa ‘aliweka’ linaweza pia kufasiriwa ‘akampa.’ Lakini katika Wafalme na Nyakati pia, linaonekana mara moja tu, likimaanisha taji na pia ule Ushuhuda. Zaidi ya hilo, linafuatwa mara iyo hiyo na neno la Kiebrania “juu ya.” Hivyo, ‘akaweka juu yake’ lazima iwe ndiyo tafsiri sahihi. Vyote viwili taji na Ushuhuda ‘viliwekwa juu ya’ Mfalme Yehoashi kijana, kama vile New World Translation inavyoonyesha.

Hivyo basi ni kwa nini—na jinsi gani—kuhani mkuu ‘aliweka’ ule Ushuhuda juu ya yule mfalme kijana? Fikiria maoni ya mwanachuo Mjerumani Otto Thenius: “Ile Sheria, kitabu ambamo maagizo ya Kimusa yaliandikwa. Hii ilishikiliwa kwa njia ya mfano juu ya kichwa cha mfalme, baada ya yeye kuwa amepambwa kwa lile taji.” (Die Bücher der Könige kilichotungwa na Otto Thenius) Vivyo hivyo, Profesa Ernst Bertheau anaeleza hivi: “Kuwekwa kwa Sheria [juu ya mfalme] kwa kweli kulikuwa na maana ya mfano, kwamba mfalme alikuwa na lazima ya kutawala kupatana nayo.”—Die Bücher der Chronik.

Mungu aliamuru kwamba wakati mfalme alipoketi juu ya kiti cha ufalme, alipaswa kujiandikia mwenyewe nakala ya ile Sheria, akijifunza hiyo na kuitumia maisha yake yote. (Kumbukumbu 17:18-20) Kuweka ule “ushuhuda” juu ya mfalme mpya huenda kukawa kulikuwa ishara fupi ya mfano kwamba hata ingawa sasa alikuwa mfalme, hakuwa na cheo cha juu kiasi cha kutofuata Sheria ya Yehova. Lisilofurahisha ni kwamba, baada ya kifo cha kuhani mkuu Yehoyada, Yehoashi alisahau somo hili la maana sana na pole kwa pole akaacha ibada ya Yehova, hatimaye akifa mikononi mwa wauaji.—2 Nyakati 24:17-25.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki