Kuleta Nuru Kwenye Mahali Palipo Mbali Katika Bolivia
KASKAZINI na mashariki ya milima iliyoinuka sana ya Bolivia kuna nyanda za chini za kitropiki, zenye majani-majani mengi. Zimegawanywa na mito yenye msukosuko ambayo hujipinda kupita katika misitu na nyika. Mambo huwa namna gani kwa kuhubiri habari njema za Ufalme katika maeneo ya ndani kama hayo?
Jiwazie ukiwa katika mtumbwi mkubwa, ulioundwa kutokana na gogo la mti uliotobolewa shimo, wenye kuendeshwa kwa mota iliyo nyuma. Hilo ndilo lililopata wahudumu sita wa wakati wote kutoka Trinidad, jiji moja katika sehemu ya El Beni ya Bolivia. Walikuwa wamepanga safari hii ili waweze kutoa ushahidi kwenye makao ya mtoni yasiyopata kamwe kufikiwa kwa ‘habari njema za ufalme.’ (Mathayo 24:14) Baada ya kupita katika utandao mpana wa maji yenye kung’aa, chombo chao kilianza kupita katika kijito chembamba upande wa Mto Mamoré.
Mmoja katika kikundi hicho asimulia hivi: “Tulikuwa ni kama tumeufikia Mamoré tulipogundua kwamba sehemu ya mwisho ya kijito ilikuwa kavu. Kwa kutoka mashuani, tukajikuta tukizama katika utopetope hadi kwenye mapaja yetu! Mke wangu alipoteza viatu vyake akijaribu kujiondoa humo. Lakini kwa msaada wa wapita-njia, tuliweza kuvuta ule mtumbwi mzito kutoka kwenye matope na kuuleta kwenye nchi kavu imara zaidi. Baada ya saa mbili za kazi ya jasho, tukaufikia Mamoré.
“Halafu tukawasha mota kwenda upande wa juu katika mto, ambao kandokando yao ulikuwa na kingo zilizoinuka zikiwa na majani-majani ya kitropiki mengi. Kwa kusikia mvumo wa mota, kasa (kobe) wakubwa walichomoka kwenye magogo yenye kuelea majini, huku dolfini wenye madaha wakichomoza-chomoza kutoka majini. Kituo chetu cha kwanza kilionyeshwa na kishungi cha moshi kutoka kwenye moto uliowashwa kando ya mto kufukuza wadudu. Baada ya kuegesha mtumbwi wetu katikati ya matawi yaliyoshikamana, tuliongea na wale watu wenye urafiki juu ya baraka za Ufalme unaokuja. Kwa uthamini wakatupa matunda na mayai tele.
“Siku ilipopita, tulifanya vituo vya ziada ili kupanda mbegu zaidi za ukweli. Ilikuwa giza tulipofika San Antonio. Wanakijiji walikuwa wameenda kulala. Hata hivyo, habari ilipoenea kwamba filamu ingeonyeshwa, taa zikaanza kuwashwa. Farasi na gari-farasi vikaungwa pamoja ili kuleta vifaa vyetu mjini. Watu wengi wakajuana na Mashahidi wa Yehova kwa filamu na kibinafsi.
“Kesho yake tukaendelea kuzuru mahali pageni. Katika ukingo ulioinuka, wanawake walikuwa wakifua nguo zao, na hata kuosha mtoto mchanga mmoja, ndani ya mafuniko makubwa sana ya kasa. Walikuwa hawajapata kamwe kusikia ujumbe wetu wa Biblia. Mahali pamoja samaki wadogo waliruka juu kutoka kwenye maji yaliyo karibu na ile mashua, na wengi wakaanguka ndani humo. Hivyo basi baada ya kuionyesha filamu, kabla ya kulala tukala samaki waliokaangwa. Kufikia mwisho wa safari, vitabu vingi vikawa vimeachwa katika eneo hili la ndani, nasi tukaridhika kuwa tumesaidia wengi kusikia habari njema kwa mara ya kwanza.”—Linganisha Warumi 15:20, 21.
Ushuhuda wa Mwelekezo wa Kimalaika
Sasa piga picha ujione ukiwa katika utume wa kwenda kutafuta mtu mmoja katika mji wenye watu 12,000, ambao unauzuru kwa mara ya kwanza. Hujui zaidi juu yake isipokuwa jina lake. Hilo ndilo lililokuwa tatizo lenye kuwaelekea wahudumu wawili wa wakati wote waliowasili Guayaramerín wakitumaini kupata mtu fulani ambaye hapo kwanza alikuwa amejifunza Biblia na alihudhuria mikutano katika mji mwingine lakini akahamia mji huu. Baada ya kutulia, mapainia wawili hao waliamua kutembea-tembea kwenye uwanja mkuu wa pitapita za mji, ambako umati wa watu walikuwa ama walikuwa mezani wakila au wakiongea tu. Karibu mara hiyo hiyo mwanamume mmoja akawafikia mume na mke hao wawili na kuanzisha maongezi. Wakamwuliza kama alimjua mwanamke waliyekuwa wakimtafuta. “Sivyo,” akasema, “lakini mama-mkwe wangu ni mmoja wa Mashahidi wa Yehova.” Kwa kuwa hakuna Mashahidi wowote waliojulikana kuwa katika mji huo, wakafikiri angeweza kuwa amevurugika.
Hata hivyo, kesho yake walimzuru bibi huyu wa umri mkubwa, asiyetoka kitandani akiwa na mguu uliovunjika. “Mimi ni mmoja wa Mashahidi wa Yehova, lakini sijabatizwa bado,” akasema. Alipoulizwa nani alimfunza ukweli, alielekeza kidole kwenye picha ya binti mjukuu ukutani na kusema: “Ni yeye.” Walishangazwa na walichoona! Alikuwa ni yule mwanamke kijana waliyekuwa wakimtafuta! “Kwa nini mwana-mkwe wako alikana kwamba hamjui?” wakauliza. “Oh, yeye sasa ameolewa, na mwana huyo ajua jina lake la ndoa tu,” akajibu. Binti mjukuu huyo hakuwako wakati huo, lakini funzo la Biblia liliongozwa baada ya hapo kwa kuandikiana barua. Tokeo likawa nini? Yeye na nyanya yake walifanya maendeleo wote wawili kufikia hatua ya kubatizwa. Nyumba yao ikatumika kuwa Jumba la Ufalme kwa ajili ya kundi lenye kukua, na akiwa mhudumu wa wakati wote, mwanamke kijana huyo ameelekeza wengi kwenye tengenezo la Yehova.
Kuhubiri Katikati ya Tropiki
Halafu, wazia ndege yenu ikitua kwenye mkimbilio wa ndege ulio na nyasi-nyasi kule San Joaquín, ndani sana katikati ya zile tropiki za Bolivia. Wewe wapatwa na wasiwasi ufikiriapo tauni ya kifumbo ambayo, miaka miwili mapema kidogo, ilifagia sehemu moja kwa tano ya wakaaji wa mji huu.
Mume na mke mapainia wenye kuwasili kutoka Trinidad kwa ndege walikuwa tayari wamepata mwonjo wa ukaribishaji-wageni wa watu kule. Mume huyo asimulia hivi: “Maongezi ya Biblia yaliyofanywa wakati wa mruko wetu yaliongoza kwenye mwaliko wa kukaa kwenye nyumba ya faraghani, bila malipo. Wakaribishaji wetu hata walitutolea vyakula kwa gharama ya chini, ikituwezesha kutumia wakati wetu wote kwenye kazi yetu ya kuhubiri. Muda mfupi baada ya kuwasili, tuliambiwa tukapige ripoti kwenye makao ya wanajeshi moja kwa moja. Ofisa alipojua kwamba hatukuwa wanamapinduzi bali Mashahidi wa Yehova, akaonyesha kupendezwa kusiko kwa kawaida na kujipatia Biblia, na pia vitabu vya Biblia na maandikisho kwa magazeti Mnara wa Mlinzi na Amkeni! Baada ya hapo, karibu kila mtu mjini alisikiliza kwa makini ahadi ya Biblia juu ya afya kamilifu karibuni.—Ufunuo 21:4.
Wahudumu wanne wa wakati wote walitaka kutoka San Joaquín kwenda San Ramón, lakini namna moja tu ya usafiri iliyopatikana ilikuwa mkokoteni-ng’ombe. Walitumia katoni za vitabu kuwa viti. Baada ya muda mfupi zikapondeka kwa sababu ya miruko-ruko na mitikisiko ya mkokoteni, wenye magurudumu ya mbao yaliyoinuka juu. Hata kuku wenye kubebwa walionekana wakiwa na kizunguzungu kutokana na kichefuchefu cha kutukushwa.
Baada ya saa kumi za kupitapita kati ya miti kwa kutembea katika vichaka vya chinichini, walifikia mahali ambapo hakuna hata kipito kimoja kilichoonyesha alama ya njia, na giza lilikuwa likiingia. Dereva alikishtua kikundi kwa kusema, “Nafikiri tumepotea!” Walikuwa wameanza tu kushangaa, ‘Twawezaje kukaa huku nje katika vichaka vya chini vyenye nyoka na wanyama-mwitu hatari?’ wakati dereva alipoongezea, “Lakini msifanye wasiwasi. Wanyama hawa wamepata kuifunga safari hii wakati mwingine.” Ikawa hivyo. Katika muda wa saa moja wakaibuka kutoka kwenye vichaka vya chinichini wakiwa San Ramón kwenyewe!
Hapa, pia, siku nyingi zilitumiwa kutangaza kwenye masikio ya wasiopata kusikia juu ya Paradiso inayokuja. Hakuna Mashahidi walioishi hapa; hata hivyo jambo fulani lilitukia lililobadili hilo.
Mwanamke mmoja mmisionari Mkatoliki alikuwa amekuwa akiwafuata Mashahidi walipokuwa wakienda mlango kwa mlango. Kwa njia fulani miendo yao ikagongana na wakamkuta ghafula katika nyumba ile nyingine waliyokuja. Kwa kushangazwa na urafiki wa mwanamke huyo, wao walimwachia kitabu Kweli Iongozayo Kwenye Uzima wa Milele. Ingawa yeye mwenyewe hakupendezwa kikweli, alimpa dada-mkwe wake kitabu hicho, ambaye aliyamaliza yote yaliyomo, akajifunza zaidi, na baadaye akawa Shahidi aliyebatizwa.
Wasiwasi Katika Mito ya Kitropiki
Sasa piga picha ujione kwenye usukani wa mashua-abiria ya mtoni yenye kupita katika maji hatari, yenye msukosuko. Miamba iliyofichika, kingo zenye matope, mashina ya miti, pamoja na kutokea ghafula kwa dimbwi kubwa la maji ya kisulisuli, ni chache tu za hatari zilizopo. Mapiranha, mikunga yenye kuwaka umeme, na samaki-ubapa wenye maumo makali ni tele katika maji haya. Hayo ndiyo matatizo yaliyowaelekea ndugu wale waliokuwa na kazi ya kuwatolea ushahidi wakaaji wa mtoni katika eneo hilo katika Riberalta.
Ili kufika mahali-mahali hapa palipotengeka, walijenga mashua-abiria iliyopewa jina Luz de los Ríos (Nuru ya Mito). Wakati wa ziara ya waangalizi wa wilaya na mzunguko, iliamuliwa kupeleka mashua-abiria hiyo ikakimbizwe kwa majaribio. Mambo yote yakawa sawasawa mpaka paa iliponaswa na tanzu la mti lenye kuning’inia. mkondo imara uliyumbisha mashua-abiria hiyo dhidi ya mti ulioanguka. Kama upanga, tawi lenye kuchongoka lililovunjika likaichoma mashua kwa upande—karibu kumtundika mke wa mwangalizi wa wilaya! Maji yakamiminika ndani, nayo mashua-abiria ikapinduka, ikibwaga abiria wayo ndani ya yale maji yenye kuzunguka vururu-vururu. Na tena mwangalizi wa wilaya na mke wake hawakujua kuogelea! Kwa msaada wa wale ambao wangeweza, walifika nchi kavu salama. Lakini mashua-abiria hiyo ikatokomea. Siku kadhaa baadaye ilipatikana kilometa 5 kule chini ya mto. Mali zote, kutia na katoni 20 za vitabu, zikawa zimepotezwa.
Jeshi-Bahari la Bolivia lilisaidia kuieleza tena majini, na baada ya majuma ya marekebisho, mashua-abiria hiyo ikawa tayari tena kumaliza safari yayo ya kwanza. Safari hiyo yenye wasiwasi ilianza na hali mbaya ya hewa na matatizo ya injini.
Mahali pa kwanza ambapo akina ndugu walitia nanga, walikabiliwa na kikundi cha Waevanjeli, waliodhihaki hivi: “Mashua yenu ndogo haifai katika mto huu!” Jaribio la kuonyesha slaidi likavurugwa na jenereta yenye kasoro. Waliporudi mtoni, Mashahidi hao wakapata kujua kwamba mashua-abiria nyingine zilikuwa zimekuja zikiwa na vikuza-sauti kuonya juu ya “manabii bandia” wanaokuja. Kwa wazi, hii ilikuwa kazi ya wale Waevanjeli. Hata hivyo, iliongezea tu udadisi wa watu.
Ingawa ziara hii ilimaliza ile propaganda kutoka kwa wale waliokuwa manabii bandia kikweli, akina ndugu walijisikia wenye wasiwasi, kwa maana bado walikuwa na safari ya siku 21 mbele yao ili kufika Fortaleza.
Njiani, walimtolea ushahidi chifu wa kabila moja la sehemu ya ndani-ndani; alisikiliza kwa makini. Kupitia hotuba ya Biblia iliyotolewa na mmoja wa mapainia, kikundi cha waombolezi katika kiwanja kimoja kilicho mahali palipotengeka kilifarijiwa kwa lile tumaini la kweli kwa ajili ya wafu. Mwanamume mmoja mwenye umri mkubwa mwenye ndevu ndefu nyeupe alionyesha uthamini wake wa kujisikia moyoni, naye akauliza angewezaje kufanya andikisho la kupata gazeti letu kwa miaka kumi! Katika Fortaleza, watu 120 walinufaika na programu ya Sosaiti ya slaidi.
Mapainia hawa walijisikia wametosheka kama nini kuwa wameleta nuru ya ukweli mahali-mahali pa ndani-ndani! Kwa uhakika, hakuna njia iliyo salama na yenye kutosheleza ya mtu kutumia maisha yake kuliko kumtumikia Muumba wa uhai wenyewe, Yehova Mungu.—Zaburi 63:3, 4.
[Ramani/Picha katika ukurasa wa 26]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
BOLIVIA
Guayaramerín
Riberalta
Fortaleza
San Joaquín
San Ramón
Trinidad
San Antonio