Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w92 2/15 kur. 21-25
  • Visiwa vya Bahari ya Hindi Vyaisikia Habari Njema

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Visiwa vya Bahari ya Hindi Vyaisikia Habari Njema
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1992
  • Vichwa vidogo
  • Kituo cha Kwanza—Rodrigzi
  • Visiwa vya Ushelisheli Vilivyo Mbali
  • Kurudi Réunioni
  • Mayotte—Kisiwa cha Manukato
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1992
w92 2/15 kur. 21-25

Visiwa vya Bahari ya Hindi Vyaisikia Habari Njema

VIKIWA vimepangwa katika nusu duara kuhusiana na Madagaska na kuenea kilometa za mraba zaidi ya milioni 3.9 za magharibi mwa Bahari ya Hindi ni vile visiwa Rodrigzi, Maurishasi, Réunioni, Ushelisheli, Mayotte, na Komorosi. Hata ingawa vina mweneo mkubwa kama huo, visiwa hivyo vya jumuika kuwa na eneo la bara la karibu kilometa za mraba 7,280 tu. Vikiwa na idadi ya watu milioni 2.3, vimo miongoni mwa visiwa vyenye wakaaji wengi sana katika ulimwengu.

Idadi hiyo ya watu inatia ndani Mashahidi wa Yehova karibu 2,900, wanaofanya kazi kwa bidii kuhubiri habari njema ya Ufalme wa Mungu kwa wakaa-visiwani. Wakiwa mbali na wengine, Mashahidi hao huthamini hasa ziara za waangalizi wasafirio na makusanyiko ya kila mwaka yanayopangwa na ofisi ya tawi ya Watch Tower Society katika Vakoasi, Maurishasi. Hizo ni pindi ambazo waweza kwa kweli kupendezwa na maana ya maneno ya Isaya 42:10: “Mwimbieni BWANA [Yehova, NW] wimbo mpya, na sifa zake tokea mwisho wa dunia; ninyi mshukao baharini, na vyote vilivyomo, na visiwa, nao wakaao humo.”

Hivi karibuni, wawakilishi kutoka ofisi ya tawi walisafiri kwenye visiwa hivyo kutembelea makundi na kufanya mfululizo wa makusanyiko ya pekee ya siku moja yanayofanywa kila mwaka, yaliyokazia kichwa “Iweni Watakatifu Katika Mwenendo Wenu Wote,” chenye msingi wa 1 Petro 1:15. Ili kueneza mapana makubwa ya bahari, safari ilikuwa hasa hewani—nyakati nyingine katika ndege za ki-siku-hizi za aina ya jumbo lakini mara nyingi katika ndege ndogo zenye kuendeshwa kwa propela. Majahazi na merikebu ndogo za matanga zilitumiwa pia. Njooni pamoja nasi, na kuona jinsi visiwa hivyo vya Bahari ya Hindi ya mbali vinavyoisikia habari njema!

Kituo cha Kwanza—Rodrigzi

Baada ya kusafiri hewani kwa muda wa saa moja na nusu kutoka Maurishasi, twaona kizingiti cha matumbawe. Kinatia alama ukingo wa wangwa mkubwa unaozunguka bara dogo sana katikati ya Bahari ya Hindi. Hicho ndicho kituo chetu cha kwanza, kisiwa cha Rodrigzi.

Kiwanja cha ndege kimejengwa kwenye eneo la matumbawe yenye kutokeza, liitwalo Point Coraille. Katika eneo hilo matumbawe ni mazito sana hivi kwamba yaweza kupasuliwa kwa msumeno kuwa mawe ya kutumiwa katika ujenzi. Basi dogo latupeleka kwenye barabara nyembamba yenye kupinda, kutoka kiwanja cha ndege hadi mji mkuu wa Port Matura (Mathurin). Wakati mmoja, twaweza kuona hadi ng’ambo ile nyingine ya kisiwa kuelekea vizingiti vya matumbawe vilivyo mbali, wangwa wa buluu, na ukingo wa bahari wenye miamba. Kwa kuwa majira ya mvua imekwisha hivi karibuni tu, pande za vilima zimetandikwa kwa nyasi nzito za yavuyavu na zenye kutapakaa ng’ombe, kondoo, na mbuzi walio malishoni.

Jumba la Ufalme dogo lililo nadhifu katikati ya Port Matura ndilo mahali pa kusanyiko letu la pekee la siku moja. Kazi katika Rodrigzi ilianza 1964. Sasa, miongoni mwa watu 37,000, kuna wahubiri wa habari njema 36. Ni shangwe kama nini kuona watu 53 wakiwa wamehudhuria na kijana mwenye umri wa miaka 18 akibatizwa. Mama yake, ingawa hakuweza kusoma wala kuandika, alikubali kweli katika 1969, naye ameendelea kumtumikia Yehova ujapokuwa upinzani kutoka kwa familia. Sasa wawili wa watoto wake wamejiweka wakfu kwa Yehova.

Baada ya kusanyiko hilo, tunatumia juma moja tukihubiri katika kisiwa hicho. Twasema lugha yetu ya Kreole ya Kimaurishasi, kwa kuwa ni lugha inayosemwa hapa Rodrigzi pia. Twaenda eneo letu kwa basi na kwa miguu—ni bonde lenye majani mabichi lenye kuenea kutoka barabara ya vilima hadi baharini. Ni mwono wenye kutazamisha kama nini—wangwa wa feruzi, kizingiti cheupe cha matumbawe, na bahari ya buluu nzito katika mandhari! Tukiwa tumechochewa na hewa tele isiyochafuliwa, tu tayari kwenda.

Twafuata vijia vidogo kupitia mashamba na kuvukavuka kijito chenye mabwawa ili kufikia zile nyumba nyingi ndogo zilizo bondeni. Tunapokewa kwa mikono miwili kwenye kila nyumba na kuweza kuongea na wenye nyumba juu ya mibaraka ya Ufalme iliyokaribu kuja. Kabla ya muda mrefu twafika chini sana katika bonde, na ni wakati wa kwenda nyumbani. Huko kwamaanisha kupanda zaidi na saa nyingi za kutembea, lakini ukaribishaji-wageni wa mahali hapo watusaidia—twapewa lifti nyuma ya gari ya aina ya jeep.

Baada ya matembezi hayo yenye kuchosha, tunafurahi kurudi kwenye ustarehe wa Makao ya Betheli yenye kupendeza katika Vakoasi. Siku mbili za kusanyiko la pekee zimeratibiwa kwenye Jumba la Manispaa. Siku ya kwanza, watu 760 waja. Wanatoka nusu za makundi 12 yaliyo kwenye kisiwa hicho. Siku ifuatayo, tunashiriki programu hiyo hiyo pamoja na watu 786 kutoka yale makundi mengine sita. Katika mwisho-juma huo, watu wanne wapya wanabatizwa. Kuna mapainia wa pekee 30 na mapainia wa kawaida 50 ambao hushiriki katika kuleta habari njema kwa wakaa-visiwani hao.

Visiwa vya Ushelisheli Vilivyo Mbali

Upesi wakati unafika wa sisi kuondoka kwa ndege tena, kwenda moja kwa moja kaskazini kilometa zaidi ya 1,600 juu ya bahari kuelekea kisiwa cha Mahé katika visiwa vya Ushelisheli, viitwavyo Zil Elwannyen Sesel katika Kikreole, linalomaanisha “Visiwa vya Ushelisheli Vilivyo Mbali.” Kwa sababu ya umbali huo, ofisi ya tawi yaweza kupanga ziara mbili tu kila mwaka. Siku ya kusanyiko la pekee na kusanyiko la mzunguko hufanywa siku tatu mfululizo katika masika. Mkusanyiko wa wilaya hufanywa baadaye katika mwaka. Sasa katikati ya Oktoba, tupo hapa kwa ajili ya mkusanyiko wa wilaya, utakaofuatwa na ziara ya juma moja kwenye kundi. Hapa tena twaweza kutumia lugha yetu ya Kreole ya Kimaurishasi.

Ndugu kutoka visiwa vya karibu Prala na La Digue tayari wamewasili. Inasisimua kama nini kuwa na mataifa 12 yakiwakilishwa! Mahali pa kusanyiko hilo ni Jumba la Ufalme la hapo, gereji kubwa ambalo limegeuzwa lililo nyuma ya nyumba ya Shahidi mmoja. Kwa kuwa ni ndugu sita tu, kutia na wageni, wanaostahili kushiriki katika programu, wengine wana pendeleo la kutoa hotuba kadhaa muda wa siku hizo nne. Wahubiri 81 wanasisimuka kuona 216 wakiwapo kwenye siku ya mwisho ya mkusanyiko huo.

Baada ya mkusanyiko, tunasafiri kwa jahazi kuelekea Prala, kilometa 40 kaskazini mashariki mwa Mahé. Chombo hicho chenye urefu wa meta 18 kimefanyizwa kwa mbao wa mti uitwao takamahaka. Chombo hicho kizuri chaweza kubeba maabiria 50 na mizigo ya karibu tani 36. Tuondokapo bandari katika Mahé kuelekea ukingo wa Prala kwenye upeo wa macho ulio mbali, twaweza kuhisi msukumo injini ya dizeli unaosaidiwa na matanga meupe yanayojongea kutoka kwa ile milingoti miwili.

Muda wa saa mbili na nusu baadaye, tunaizunguka rasi yenye miamba na kuingia maji matulivu zaidi ya Ghuba ya St. Anne. Tunapokanyaga gati, twawaona ndugu zetu wakitungojea. Kuna wahubiri 13 kwenye kisiwa hiki kidogo, na wageni 8 waliokuja kutoka sehemu nyinginezo. Kwa hiyo ni shangwe kubwa kwamba twaona lile jumba dogo likiwa limejaa na watu 39 kwa ajili ya hotuba ya pekee. Ni uwezekano mzuri kama nini wa kuwa na ongezeko!

Tunapokuwa hapa Prala, ni lazima tuzuru lile bonde lenye kupendeza Vallée de Mai. Hayo ni makao ya mnazi wa aina ya Coco-de-mer, unaozaa mbegu iliyo kubwa zaidi ulimwenguni, kila moja ikiwa na uzito unaofikia kilo 20. Katika kivuli cha msitu huo kilicho na majani mabichi na chenye ubaridi, twaona mimea hiyo katika hatua zote za ukuzi. Maandishi rasmi yenye maelezo kwa wageni yaeleza kwamba ule mrefu zaidi ulikuwa na urefu wa meta 31 wakati ulipopimwa mara ya mwisho katika 1968. Mingine kati ya miti hiyo mirefu ilikadiriwa kuwa na umri wa miaka 800. Huchukua muda ya miaka 25 kabla ya mti kuanza kuzaa matunda na muda wa miaka 7 kabla ya nazi kukomaa. Haishangazi kwamba broshua hiyo yaonya hivi: “Piga picha tu, acha nyayo tu”!

Saa moja ya asubuhi iliyofuata, tunakwenda kwa mashua kwenye kisiwa kidogo cha La Digue. Mashua nyingi ndogo zimekusanyika pamoja kuzunguka gati. Hiyo ndiyo njia ya pekee ambayo kwayo wakaaji zaidi ya 2,000 waweza kufikia ulimwengu wa nje. Tunalakiwa na wenzi wa ndoa wazee-wazee watokao Uswisi ambao wamekuwa katika visiwa hivyo tangu 1975. Badala ya kwenda kwa ‘teksi’ yenye kuburutwa na ng’ombe dume, twatembea ufuoni ulio na miamba ya graniti ya nyekundu nyeupe iliyolainishwa na bahari na mvua. Baada ya kuwa na kiamsha kinywa cha kuliwa nje, twaondoka kupitia eneo dogo la mashambani, ambako aina fulani ya shore kishungi asiyepatikana sana anakotaga, kuelekea nyumba ya watu fulani wenye kupendezwa. Watu 13 wanakusanyika huko kusikia hotuba inayotolewa katika Kikreole. Twakutana na wenzi wa ndoa waliokuwa wamefanya mipango yote ya kuhalalisha ndoa yao ili waweze kufanya maendeleo kiroho. Kwa kweli, Yehova anawaleta watu wa mataifa wenye kutamaniwa hata katika visiwa hivyo vya mbali sana.

Kurudi Réunioni

Réunioni ni kisiwa chenye kusitawi zaidi ya visiwa vyote tunavyozuru kwenye safari hii. Tunapokaribia bara, twaona barabara kuu yenye vijia vinne, yenye magari mengi kutoka mji mkuu, Saint-Denis. Majengo yenye orofa nyingi yajaza nafasi kati ya bahari na mlima. Kisiwa hicho ni makao ya watu 580,000 nacho kimethibitika kuwa shamba lenye kuzaa kwa ajili ya utoaji wa ushahidi wa Ufalme. (Mathayo 9:37, 38) Sasa kuna wahubiri wenye bidii wa habari njema karibu 2,000 katika makundi 21.

Siku ya kusanyiko la pekee linafanywa katika uwanja mkubwa wa michezo uliofunikwa. Twafurahi kuona watu 3,332 wakihudhuria, na ni jambo la kusisimua kama nini kuwa na watu 67 wapya wakijitokeza kwa ajili ya ubatizo! Baada ya kuonea shangwe ushirika pamoja na wamishonari walio kisiwani, twaelekea kwenye kituo chetu kinachofuata.

Mayotte—Kisiwa cha Manukato

Baada ya kusafiri hewani kwa muda wa saa mbili, ndege yetu yenye kubeba watu 40 yaanza kushuka kuelekea kiwanja cha ndege cha Pamanzi, kilicho kwenye kisiwa kidogo ambacho kimeunganishwa na Dzaoudzi, jiji kuu la Mayotte, kwa njia kuu ya mawe yenye urefu wa kilometa 1.9. Anga buluu, mawingu meupe, pande za milima yenye majani mabichi, na bahari ya buluu nzito zote zajumuika kutokeza picha ya paradiso ya kitropiki yenye amani. Kwa kufaa, Mayotte kinapewa jina la kupanga Kisiwa cha Manukato kwa sababu ya harufu yenye kupendeza sana ya mti ilangi-ilangi. Maji kutoka maua yao hupelekwa Ufaransa kuwa msingi wa manukato maarufu ulimwenguni.

Ni umbali wa muda wa dakika 15 tu kwa mashua kubwa kwenda kwenye kisiwa kikuu. Baada ya viburudisho kwenye nyumba ya wamishonari, tunaalikwa kwenye funzo la kitabu la umbali wa kilometa 19 kutoka hapo kwenye upande ule mwingine wa kisiwa. Hilo lilikomesha tumaini letu la kuwa na ziara yenye ustarehe! Twapanda gari ya aina ya jeep lililo wazi kwa safari yenye kuogopesha kwenye barabara nyembamba. Yaonekana kana kwamba twaepuka kidogo tu kugonga watu, ng’ombe, na magari mengine. Lakini dereva wetu Mfaransa ajua njia. Upesi, twawasili Shikone, ambako twakutana na familia ambayo katika nyumba yao funzo hufanywa.

Baba, aliyekuwa Mwislamu zamani, atujulisha watoto wake wanane. Mwana wake mchanga zaidi, mwenye umri wa miaka minne, atupa sisi lile ambalo baadaye twaarifiwa kwamba lilikuwa salamu ya kidesturi. Aweka upande wa nyuma wa mkono mmoja katika kiganja cha mkono ule mwingine na kusimama nayo ikiwa katika namna ya kikombe mbele yetu. Kwanza twajaribu kumsalimu kwa mkono, kisha mke wangu ajaribu kuweka mikono ya mvulana huyo juu ya kichwa chake. Kijana huyo mdogo mwenye macho makubwa ya mviringo angojea kwa saburi, bila shaka akishangaa juu ya yale tunayofanya. Mwishowe twafaulu—twaiweka mikono yake juu ya kichwa chake. Funzo laanza kukiwapo watu 14. Katikati ya funzo, mtu mwenye kupendezwa aingia na kuanza kusalimia kila mtu kwa mkono. Hilo pia yaonekana kuwa ni moja ya desturi zao.

Kwenye safari yetu ya kurudi kupitia eneo la mashambani lenye giza-giza, twaona popo wakubwa wa matunda wakielekea kwenye miti kwa ajili ya malisho yao ya usiku. Pia twanusa harufu ya fenesi chungu ambalo limeanguka kwenye barabara yenye kupinda na harufu tamu ya maembe, mapapai, na mapera. Hayo ni makao ya komba, wale wanyama wadogo walio kama tumbili wenye nyuso kama mbweha, na mikia mirefu, ya mviringo, yenye nguvu ya kushika. Tunapozunguka kwenye kilele cha kilima, twaona mwono wenye kupendeza sana. Mwezi mpevu wa rangi dhahabu-nyekundu umetokea tu juu ya ghuba, ukirudisha mwangaza wenye kumetameta kwenye maji matulivu. Hata dereva wetu aenda polepole ili kuustaajabia. Kwa baki ya safari hiyo, twautazama kila wakati barabara inapopinda.

Asubuhi inayofuata twaenda mahubiri pamoja na wamishonari. Kwanza, twazuru mwanamume kijana ambaye ni mwalimu na ambaye husema Kifaransa vizuri. Aketi sakafuni, nasi twaketi kwenye kitanda chake. Funzo lifuatalo ni pamoja na mwanamume kijana pia, naye atukaribisha tuketi kwenye kodoro lake lililo sakafuni mwa chumba chake kidogo. Baada ya wakati fulani twaanza kufurukuta, ijapokuwa tumejaribu kupuuza maumivu miguuni mwetu na jasho lenye kutiririka migongoni petu. Kukiwa na redio katika nyumba inayofuata yenye kutokeza muziki wa pop wa ki-siku-hizi kwa sauti kubwa sana, si jambo rahisi kukazia fikira kwenye funzo, linaloongozwa kwa sehemu katika Ufaransa na kwa sehemu katika Kimahoria.

Mtu tunayemtembelea mwisho ni kijana kutoka Visiwa vya Komorosi vilivyo karibu. Aomba msamaha kwa ajili ya kutosema Kifaransa vizuri sana, atoa broshua yake, na kuwa tayari kwa ajili ya funzo. Mishonari anapoendelea kunieleza jambo fulani, yeye aingilia na kusema kwamba atasoma kifungu. Anatuambia kwa adabu tunyamaze. Watu hao wote ni Waislamu, lakini wanathamini kweli kweli yale wanayojifunza kutoka kwa Biblia.

Tunashangaa ni kwa nini vijana wengi hujifunza, hali ni wanawake au wasichana wachache ambao hufanya hivyo. Hilo, twaambiwa, ni tokeo la mapokeo ya kijamii na familia. Kwa kuwa ndoa ya wake zaidi ya mmoja ni jambo linalokubalika kidini na kijamii na kila mke huishi katika nyumba yake mwenyewe, uvutano wa baba ni mdogo sana; mama ndiye anayeongoza mambo. Twajifunza pia kwamba kidesturi mabinti hubaki katika nyumba ya mama yao mpaka wanapoolewa. Wana, kwa upande ule mwingine, huondoka nyumbani wanapofika ubalehe na kujenga banga, au vibanda, vyao wenyewe au kuishi pamoja na wavulana wengine katika banga. Chini ya hali hizo wanaume vijana wako huru kujifunza wakitaka, lakini ni wasichana wachache walio na uhuru wa jinsi hiyo.

Jumapili ndiyo itakayokuwa siku ya kusanyiko la pekee. Hali ya anga yaanza ikiwa nzuri, lakini kufikia saa sita mchana mawingu yaanza kukusanyika, na upesi mvua nyingi yaanza kunyesha. Hakuna yeyote anayeonekana kujali sana, kwani inapunguza joto tu. Hapa tena twapata mibaraka tele ya kiroho wakati wahubiri 36 na mapainia wanapoonea shangwe kuona watu 83 wakihudhuria na watu 3 wapya wakibatizwa.

Kutolewa kwa broshua Furahia Milele Maisha Duniani! katika lugha yao ni jambo kuu. Si kwamba tu ni kichapo cha pekee cha Watch Tower katika Kimahoria bali pia kichapo cha pekee cha aina yoyote hadi sasa katika lugha hiyo. Kina maandishi ya Kiarabu chini ya maandishi ya Kiroma. Watu hujifunza maandishi ya Kiarabu shuleni lakini si lugha ya Kiarabu. Waweza kusema kwa moyo sala za Kiarabu na kusoma Korani katika Kiarabu; hata hivyo hawaelewi lile wanalotamka. Wanaposoma maandishi ya Kiarabu katika broshua hiyo, wanashangaa kwamba waweza kuielewa. Ile wanayosoma ni lugha yao ya Kimahoria hasa iliyoandikwa kifonetiki (kwa kuwakilisha sauti za Kimahoria) katika maandishi ya Kiarabu. Ni shangwe kuona nyuso zao zikiangaza wanapoelewa yale wanayosoma.

Ni rahisi kuangushia watu broshua hizo. Katika kijiji kimoja cha nje, mwanamume mmoja atukaribia tunapohubiria mwanamke mmoja. Aanza kuongea na ndugu wetu kwa nguvu sana katika Kimahoria. Yaonekana kwetu kwamba apinga sana. Mwanamume huyo aendelea kwa muda fulani, kwa kufanya ishara tele za mkono. Ndugu aeleza baadaye kwamba mwanamume huyo alikuwa akilalamika hivi: “Mnatazamiaje tukumbuke yale mnayotuambia huku mkitutembelea mara moja tu kwa mwaka? Mnawezaje? Mwapaswa kuja mara nyingi zaidi kuongea nasi juu ya mambo haya.”

Maneno hayo ya mwisho yaonyesha hisi zetu pia. Yehova kwa hakika anakusanya vitu vinavyotamaniwa vya mataifa kwa njia ya habari njema ya Ufalme. Ingawa wametengwa na mapana ya bahari, wakaa-visiwani wanaongeza sauti zao kwa kupaza sauti kwa nguvu kwa sifa inayotolewa kwa Mfanyi na Baba yao wa kimbingu, Yehova Mungu.—Hagai 2:7.

[Ramani katika ukurasa wa 21]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa.)

USHELISHELI

BAHARI YA HINDI

KOMOROSI

MAYOTTE

MADAGASKA

MAURISHASI

RÉUNIONI

RODRIGZI

[Picha katika ukurasa wa 23]

Rasi yenye miamba kwenye Ghuba ya Prasin, St. Anne

[Picha katika ukurasa wa 24]

‘Teksi’ yenye kuburutwa na ng’ombe dume kwenye La Digue, Ushelisheli

[Picha katika ukurasa wa 25]

Kuhubiri na broshua mpya katika Mayotte

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki