Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w92 5/15 kur. 18-27
  • Wahindi wa Goajiro Waitikia kwa Kupendezwa

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Wahindi wa Goajiro Waitikia kwa Kupendezwa
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1992
  • Vichwa vidogo
  • Maoni ya Kwanza
  • Kutafuta-tafuta Nyumba
  • Uso kwa Uso Wagoajiro
  • Hudhurio Lisilotazamiwa
  • Safari ya Pili Yenye Mafanikio
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1992
w92 5/15 kur. 18-27

Wahindi wa Goajiro Waitikia kwa Kupendezwa

AKIWA ameketi chini ya kivuli cha mti mkubwa mno na akiwa amevaa joho jeusi lenye urefu wa kufikia sakafuni, mwanamke huyo mzee-mzee alionekana kuwa ametoka kwa utamaduni tofauti kabisa. Alisema pia katika lugha iliyokuwa ya kigeni masikioni mwetu. “Rudini tena,” akasema kwa uchangamfu. Akielekezea watu wengine 50 wa jamii yake waliokuwa wameketi kumzunguka, aliongeza hivi: “Sisi sote twataka mrudi hapa tena. Mje kila juma!”

Hao watu walikuwa akina nani? Ni kwa nini walitaka sana turudi tena, ingawa hawakuwa wamekutana nasi kabla ya hapo? Turuhusuni tuwaambie juu ya siku moja tuliyotumia miongoni mwa Wahindi wa Goajiro wanaoishi Peninsula ya La Guajira katika Kolombia kaskazini-mashariki na Venezuela kaskazini-magharibi iliyo karibu.

Maoni ya Kwanza

Kuanzia Karakas, jiji kuu la Venezuela, kituo chetu cha kwanza kilikuwa Marakaibo. Tulipokuwa tukiingia mjini kwa gari, tuliona wanawake watatu vijana wakitembea kando ya barabara wakiwa wamevaa majoho marefu, yenye rangi-rangi. Sura zao zilikuwa tofauti na zile za Mvenezuela wa wastani—vituguta vya juu, ngozi ya kahawia, nywele nyeusi zilizonyoka. Tulipoona mwendo wao mzuri, wenye ustarehe, tulipendezwa sana kwa kuwaona kwa mara ya kwanza hao Wahindi wa Goajiro.

Siku ya safari yetu kwenda Peninsula ya La Guajira ilianza ikiwa nyangavu na yenye utulivu. Kabla ya jua la asubuhi kuwa lenye joto, sisi watu 50 tulipanda basi, tukisisimuka kwa sababu ya taraja la kushiriki sehemu katika kampeni ya pekee ya taifa zima ya kupeleka ujumbe wa Biblia hadi maeneo ya mbali huku Venezuela. Tulikuwa tukielekea mji wa Paragwachón, kwenye mpaka wa Kolombia.

Tukiacha mji wa Marakaibo nyuma, tulipitia miji na vijiji vingi vidogo vidogo, kila kimoja kikiwa na soko na vibanda vilivyouza makubazi yenye kufumwa na yale majoho marefu yenye rangi-rangi, yaitwayo manta. Kila kijiji kilikuwa na ua nadhifu katikati na kanisa lenye rangi nyangavu, zikifanya mandhari yote ionekane kuwa yenye kupendeza. Watu wote walikuwa na sura za Kihindi. Ingawa walionekana tofauti sana kwetu, tulihitaji kujikumbusha wenyewe kwamba hao ndio waliokuwa baadhi ya Wavenezuela wa asili.

Kutafuta-tafuta Nyumba

Hatimaye tulifika kituo chetu. Basi yetu ilielekezwa kando ya barabara na kuegeshwa karibu na ukuta mfupi chini ya kivuli cha mti wenye matawi yaliyotandaa sana. Kwenye upande ule mwingine wa ukuta kulikuwako shule ya kijiji hicho—iliyokuwa imefungwa kwa sababu ilikuwa Jumapili.

Tukigawanyika katika vikundi viwili, tulienda pande tofauti tukitafuta nyumba. Tulitakwa tualike kila mtu kwenye hotuba ya Biblia ambayo ingetolewa katika lugha ya Kigoajiro saa tisa za alasiri hiyo katika uwanja wa shule. Evelinda, Mhindi wa Goajiro mwenyeji, ndiye aliyekuwa mwandamani wetu. Tulitumaini kwamba, hilo lingefanya tukubalike zaidi, kwani ingawa tungeweza kusema Kihispania, hatukujua lolote kuhusu lugha ya Kigoajiro.

Tulipokuwa tumetoka kijiji hicho, tulilazimika kutembea mwendo mrefu katikati ya nyumba. Tulipokuwa kukitembea kwenye barabara ndefu, iliyonyoka yenye vichaka vingi kwenye kila upande, mvulana mmoja mwenye umri wa miaka kumi alijiunga nasi na kutukodolea macho akiwa na udadisi mwingi. Evelinda alitabasamu kwake na kueleza katika Kigoajiro kusudi la kuzuru kwetu eneo hilo. Jina lake lilikuwa Omar, naye aliondoka mbio baada ya sisi kumwalika kwenye hotuba.

Tukiacha barabara, tulifuata njia isiyo ya lami ambayo bado ilikuwa na matope-matope kutokana na mvua ya karibuni. Tulipata kujua kwamba njia hizo zilitumiwa na wenye kufanya magendo ya kusafirisha bidhaa haramu kati ya Kolombia na Venezuela. Hewa ilijaa harufu ya majani mabichi. Ingawa lile joto lenye unyevu-nyevu lilikuwa lenye kutumaliza nguvu kidogo, halikupunguza uchangamfu wetu. Kwa vyovyote vile, taabu yote ilisahauliwa wakati kile kijia chenye kupitia msitu wenye majani mengi kilipotuongoza ghafula kwenye uwanja mkubwa—kijiji halisi cha Wagoajiro.

Uso kwa Uso Wagoajiro

Mbuzi kumi na wawili hivi, wenye alama nyeupe, nyeusi na nyekundu zenye kupendeza, walikuwa wamelala chini ya kivuli, wakicheua kwa uradhi. Mwanamke mmoja alikuwa akilisha kitoto chake chakula, akiwa amelala katika wavu ulionyooshwa na kufungwa kati ya miti miwili. Vitoto viwili vilikuwa vikicheza karibu na hapo. Mwanamke huyo alikuwa nje tu ya ua wa vijiti na seng’enge iliyozunguka nyumba ya matope na henzerani yenye paa iliyoezekwa kwa majani. Kulikuwako vibanda vichache sahili katika eneo hilo. Kwa wazi, kimoja kilikuwa ndicho jikoni, ambamo moto wa kuni ulikuwa ukiwaka sakafuni miongoni mwa vyungu vikubwa vilivyofanana na marigedi. Ngozi za mbuzi zilikuwa zikining’inia karibu ili kukauka.

Alipotuona tukikaribia, mwanamume mmoja aliyekuwa amesimama karibu na lango alikimbia mbele na kutuwekea viti viwili karibu na mwanamke aliyekuwa kwenye ule wavu. Evelinda alisalimu mwanamume na mwanamke hao katika lugha yao na kueleza tumaini la Kimaandiko la wakati ujao akitumia ile broshua yenye picha Furahia Milele Maisha Duniani! Hali za amani katika eneo hilo zilituonyesha kwamba taabu za kimataifa au ongezeko la unyang’anyi katika majiji yenye watu wengi visingekuwa vichwa vyenye kufaa hapa. Shahidi mmoja katika kikundi hicho alikuwa ameeleza kwamba kwa kuwa Wahindi wa Goajiro walikuwa ni wanyamavu kiasili, ni jambo la maana kuonyesha uchangamfu na kupendezwa kibinafsi kikweli tangu mwanzoni. “Mara nyingi huwa tunauliza juu ya afya ya familia, juu ya mavuno, kama kumekuwa na mvua karibuni, na kadhalika,” akasema. “Hilo latufungulia njia ya kuwaambia juu ya Ufalme wa Mungu na kuwaonyesha kwamba Yehova karibuni ataondolea mbali kuteseka kwote na Shetani Ibilisi, ambaye wao humwogopa hasa.”

Evelinda alipokuwa akisema, wasikilizaji wake walionyesha kukubali, na upesi mwanamke mwingine na watoto kadhaa wakajiunga nasi. Tulikuwa tumepata kujua mapema zaidi kwamba sheria ya Goajiro humruhusu mwanamume kuwa na wake zaidi ya mmoja. Je! hali ilikuwa hivyo hapa? Hilo lilitufanya tumfikirie Yeni, Mgoajiro mwenye kuvutia aliye na umri wa miaka 21 anayeishi Marakaibo. Mwanamume tajiri Mgoajiro alikuwa ametoa mahari nyingi ili ampate. Lakini wazazi wake, ambao si Mashahidi wa Yehova, walikuwa na maoni tofauti. Ingawa mama yake alikubali mpango huo, babake Yeni alisema hapana. Mchumba huyo alikuwa tayari amemwoa dada wa Yeni.

Evelinda alipomaliza utoaji wake, mwanamume huyo alichukua broshua. Mwanamke aliyekuwa amesimama nyuma yake aliomba moja pia, nasi tukafurahi kumpa. Kufikia wakati huo Mashahidi wale wengine walikuwa wametuacha. Kwa hiyo tulialika familia hiyo kwenye hotuba ya alasiri na kuondoka, tusitake kupotea katika eneo hilo la mashambani tusilolifahamu sana.

Shahidi mmoja katika kikundi hicho alisimulia lile alilolipata. Mwanamume aliyekuwa katika wavu alisikiliza kwa uangalifu wakati mke wake alipoenda kuleta viburudisho—gilasi mbili za chicha, kilichotengenezwa kwa mahindi. Ndugu yetu alikubali kwa heshima na kunywa. Baadaye, mwandamani wake Mgoajiro aliyeitwa Magali akaeleza jinsi kinywaji hicho kilivyotengenezwa. Kwa kawaida, mahindi husagwa kwa meno! Magali asingeweza kujizuia asiangue kicheko alipoona uso wa ndugu huyo aliposikia hivyo.

Mwanamume mwingine Mhindi, kwa wazi akivutiwa na jitihada ya ndugu yetu ya kufika kwenye nyumba yake na ujumbe wa Biblia, alishuka katika wavu wake. Akivaa shati, yeye binafsi alimpeleka ndugu huyo hadi makazi yaliyokuwa yamekosa kutembelewa.

Tukipitia uwanja ambapo ndugu zetu walikuwa wakizungumza na watu wazima wa familia, tuliona kikundi kidogo, watoto waliokuwa uchi wenye matumbo yaliyovimba wakiwa wamesimama kimya chini ya mti. Tulipata kujua kwamba hali hiyo ilikuwa kwa sababu ya ugonjwa wa kukosa chakula kinachofaa mwilini pamoja na minyoo. Walio wengi wa watu hao hawana maji ya mfereji wala umeme. Hilo, bila shaka, lamaanisha hawana friji, vipepeo, wala taa za stimu.

Hudhurio Lisilotazamiwa

Asubuhi hiyo ilikuwa imepita haraka sana. Tuliporudi kwenye basi ili kula chakula chetu cha mchana, tulitaka kujua ni watu wangapi kati ya wale tulioalika wangekuja kwenye hotuba ya Biblia alasiri hiyo.

Saa 8:45 za alasiri, tuliona labda ni sisi tu tuliokuja kwa basi ambao tungekuwa wasikilizaji wa ndugu yetu Mgoajiro, aliyekuwa ametayarisha hotuba ya dakika 45 katika lugha ya kienyeji. Lakini sivyo! Familia ndogo ya kwanza iliingia uwanja wa shule ya hapo kwa haya. Ni lazima walishangaa wakati kila mtu aliwafanya wahisi wamekaribishwa. Katika dakika chache zilizofuata, watu wengi zaidi wakafika, baadhi yao wakiwa kwa wazi wametembea mwendo mrefu. Ile familia iliyoishi katika uwanja ule uliokuwa na wale mbuzi kumi na wawili ilikuwapo pia! Mwanamke yule aliyekuwa katika ule wavu alionekana tofauti kama nini katika manta yake nyeusi maridadi! Hata Omar mdogo, tuliyesema naye barabarani, alikuwa amekuja, yaonekana akiwa peke yake. Wengine walipofika, ile ngazi ya saruji katika uwanja wa shule iliyotumika kuwa benchi ilijaa. Kisha dereva wetu wa basi mwenye urafiki akaanza kuondoa viti kutoka kwa basi ili watu wakalie wakati wa hotuba.

Jumla ya Wahindi wa Goajiro 55 waliketi na kusikiliza wakati Eduardo alipotoa hotuba ya Biblia. Lakini hawakuketi wakiwa wamenyamaza kimya. Walipokubaliana na jambo ambalo msemaji alisema, walionyesha kibali chao kwa kuvuma au kuguna. Aliposema juu ya mwisho unaokaribia wa uovu, yule mwanamke mzee-mzee aliyetajwa mwanzoni aliingilia. “Naam, kuna uovu mwingi,” akasema, kwa sauti kubwa vya kutosha ili wote wasikie. “Kwa kweli, kuna watu waovu ambao wameketi hapa sasa hivi. Kwa hiyo nina tumaini wanasikiliza!” Ndugu Eduardo alionyesha kwa busara shukrani kwa ajili ya elezo hilo na akaendelea na hotuba yake.

Baada ya hotuba hiyo kuisha, mmoja katika kikundi chetu alipiga picha. Wagoajiro walipendezwa na hilo wakauliza kama wangepaswa kuinua broshua zao za Furahia Maisha katika picha ambayo ingefuata. Baadhi yao wakaanza kuondoka polepole, lakini karibu nusu yao walibaki na kututazama tukipanda basi. Walitushurutisha tuahidi kwamba tungerudi, kisha wakasimama na kutupungia mkono mpaka walipokuwa hawawezi kuiona basi.

Tulipokuwa tukiondoka kwa gari, kwa hakika tulihisi kwamba lilikuwa pendeleo kuchukua habari njema za Ufalme wa Mungu kwa watu hao. Katika visa vingi walikuwa wamezisikia kwa mara ya kwanza kabisa. Mashahidi katika Marakaibo walikuwa tayari wakiongea juu ya ziara yao ifuatayo. Je! hadithi hiyo ingekuwa na sehemu ya pili?

Safari ya Pili Yenye Mafanikio

Ndugu walirudi majuma mawili baadaye. Vichapo vingi vya Biblia vikaangushwa, ziara za kurudia zikafanywa kwa waliopendezwa, na mafunzo ya Biblia nyumbani yakaanzwa. Isitoshe, Wahindi 79 walihudhuria mkutano wa watu wote wa pili uliofanywa peupe. Katika pindi hiyo ndugu walieleza kwamba wangerudi katika muda wa majuma matatu badala ya mawili kwa sababu ya kusanyiko la mzunguko. Wahindi hao walishtuka. “Huenda tukafa kabla ya wakati huo!” akasema mmoja wao. Wakauliza kusanyiko la mzunguko ni nini. Lilisikika kuwa jambo zuri sana hivi kwamba waliamua kwamba walitaka kuwapo pia! Mipango ikafanywa, na 34 wao wakaweza kuhudhuria kusanyiko katika Marakaibo, ambako ndugu wenye kusema Kigoajiro waliwasaidia waelewe programu ya Kihispania.

Mapenzi ya Yehova ni kwamba ‘watu wa aina zote wapate maarifa sahihi ya kweli.’ (1 Timotheo 2:3, 4, NW) Ni shangwe kama nini kuona itikio zuri miongoni mwa Wahindi hao wenye kutafuta kweli katika Peninsula ya La Guajira!

[Picha katika ukurasa wa 18]

Maisha Yaliyotajirishwa na Kweli ya Biblia

Iris na Margarita, matineja wawili Wagoajiro, walipendezwa kuona ile broshua Furahia Maisha Milele Duniani! Lakini walikuwa na tatizo. Hawakujua kusoma. Shahidi aliyewatembelea alijitolea kuwasaidia kwa kutumia kile kijitabu Jifunze Kusoma na Kuandika. Upesi, wasichana hao wakasisimuka kuweza kuandika na kutamka jina Yehova ifaavyo.

Walipofanya maendeleo, walishangazwa na lile tumaini zuri ajabu linalotolewa na Biblia. Waliguswa moyoni hasa na ile ahadi kwamba ainabinadamu yote itaonea shangwe uhuru. “Maisha hapa ni yenye huzuni sana kwetu sisi matineja,” wakaeleza. “Kwa kawaida tunaozwa tukiwa wachanga sana, na kulalwa kinguvu ni hatari ya daima.”

Jambo kuu kwa Iris na Margarita lilikuwa kuhudhuria kusanyiko la mzunguko katika Marakaibo. Nyuso zao zilionyesha ile shangwe waliyohisi mioyoni mwao, hasa wakati wa kuimba nyimbo. Walikuwa wakingojea mlangoni kwa hamu sikuzote wakati yule Shahidi alikuja kwa ajili ya funzo lao la Biblia, na hawakukosa kamwe hotuba ya watu wote iliyotolewa katika kijiji chao. Wasichana hao wachanga huhisi kwamba kwa kweli maisha yao yametajirishwa kwa kupata maarifa kuhusu Yehova Mungu na kusudi lake.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki