Walikuja—Zijapokuwa Hali Zisizopendeza na Hatari
TAREHE ilikuwa Januari 2, 1992. Mahali—Makeke, Mkoa wa Inhambane. Kelele za usiku za Afrika huko Msumbiji zilikatizwa kwa ghafula wakati redio ilipofunguliwa. “Mashahidi wa Yehova wanafanya Mkusanyiko wao ‘Wapendao Uhuru’ katika mkoa wetu,” mtangazaji akasema. “Kusudi lao ni kuwafunza watu jinsi uhuru wa kweli uwezavyo kupatikana katika ulimwengu wa leo. Wote wanakaribishwa kuhudhuria.”
Huko katika pembe hiyo ya Afrika iliyo ya mbali, jambo lilikuwa likitukia ambalo litakumbukwa kwa muda mrefu! Kwa mara ya kwanza, mkusanyiko wa wilaya wa Mashahidi wa Yehova ulikuwa ukifanywa, na watu 1,024 walikuwako kuuonea shangwe. Miaka michache iliyopita, tukio la jinsi hiyo lisingeweza kutukia kamwe kwa uwazi jinsi hiyo katika Msumbiji, kwa kuwa kazi ya Mashahidi wa Yehova ilikuwa chini ya marafuku. Je! ungependa kusikia juu ya dhabihu za kijasiri zilizofanywa ili kuhudhuria mkusanyiko huo?
Mkoa wa Inhambane, sawa na sehemu nyinginezo nyingi za Afrika, ni yenye kupendeza sana. Mashua za kuvulia zilizo kama dau zenye matanga ya pembetatu huabiri baharini kwa kawaida karibu na pwani yayo. Minazi ni mingi. Lakini jambo lisilopendeza hunyemelea eneo la mashambani: vita ya wenyewe kwa wenyewe!
Kwa wale walalao ndani ya vibanda vya matawi ya minazi katika saa za mapema za asubuhi, si jambo lisilo la kawaida kuamshwa kwa mlio mzito wa mizinga mingi katika sehemu za mashambani zilizo karibu wakati vita inayopiganwa msituni inapoendelea usiku kucha. Mara nyingi sana ni raia wasio na hatia ambao huteseka. Nyakati nyingine watoto huonwa wakichechemea wakiwa bila viungo au viungo vikiwa vimekatwa-katwa. Hata baadhi ya Mashahidi wa Yehova wana kovu nyusoni na mwilini pao kutokana na ukatili waliopatwa nao.
Chini ya hali hizo Mkusanyiko “Wapendao Uhuru” ulithaminiwa sana na wote waliohudhuria. Ujapokuwa uwezekano wa kuviziwa njiani kuelekea mkusanyikoni, vikundi vingi vya familia kutoka maeneo ya mashambani vilikuwa vimeazimia kwa uthabiti kuja. Vivyo hivyo kwenda huko hakukuwa jambo la ustarehe, kwa kuwa usafiri wa watu wote mara nyingi ni kwenye sehemu ya nyuma ya malori makubwa yasiyofunikwa. Nyakati nyingine abiria wafikao 400 husongamana kwenye lori moja! Idadi fulani ya malori hayo hufuatana kwa mstari kufanyiza misafara inayoandamanwa na walinzi wa kijeshi wenye silaha.
Familia moja iliyohatarisha maisha ya washiriki wayo kwa kusafiri kwa njia hiyo ilikuwa ya Nora na mabinti wake watatu, wenye umri wa mwaka mmoja, miaka mitatu, na miaka sita. Alikuwa ameweka pesa akibani kwa miezi kadhaa iliyotangulia ili aweze kulipia safari hiyo. Jambo la kwamba mahali hususa pa kulala hapakupatikana kwenye mkusanyiko halikumzuia. Pamoja na wengine wengi, Nora na familia yake walipika, wakala, na kulala kwenye uwanja hapo hapo kwenye mahali pa mkusanyiko.
Hata joto kali ya kitropiki iliyofuatwa na mvua nyingi haikuweza kupunguza ile furaha isiyozuiwa ya akina ndugu wakionea shangwe karamu ya kiroho wakiwa pamoja. Walihisi kwamba hakukuwa jambo jingine lenye maana zaidi kwao kuliko kuwako kwenye mkusanyiko huo. Jumla ya watu 17 walionyesha wakfu wao katika maji yenye ujoto ya Bahari ya Hindi. Ubatizo ulipokuwa ukiendelea, umati mkubwa wa watazamaji wenye shangwe ulisukumwa kwa hiari kuimba sifa kwa Yehova.
Kikundi hicho cha waabudu kilikuwa kwa kweli kimegundua kile kinachomaanishwa na kuwa wapendao uhuru wa kimungu. Hans, mwakilishi kutoka mji mkuu, Maputo, alisema hivi: “Tumetoka tu kuona mwanzo wa muhula mpya katika kazi ya Mashahidi wa Yehova katika sehemu hii ya Afrika.”