Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w93 2/1 kur. 20-24
  • Maandalizi ya Kusaidia Huonyesha Upendo wa Kikristo

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Maandalizi ya Kusaidia Huonyesha Upendo wa Kikristo
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1993
  • Vichwa vidogo
  • Sweden
  • Finland
  • Denmark
  • Uholanzi
  • Uswisi
  • Austria
  • Italia
  • Chakula kwa Maelfu ya Wahudhuriaji
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1993
w93 2/1 kur. 20-24

Maandalizi ya Kusaidia Huonyesha Upendo wa Kikristo

“IWENI na upendo kwa ushirika wote wa akina ndugu,” mtume Petro aliwahimiza Wakristo wenzake. (1 Petro 2:17, NW) Upendo huo ulipaswa uvuke mipaka ya kirangi, kijamii, na kitaifa, ukivuta watu pamoja katika udugu wa kweli. Uhitaji wa kimwli ulipotokea miongoni mwa Wakristo wa mapema, upendo uliwasukuma wengi watoe michango kwa mitume ili igawanywe kwa wale wenye uhitaji. Rekodi yasema kwamba “walikuwa na vitu vyote shirika.”—Matendo 2:41-45; 4:32.

Upendo wa jinsi hiyo ulidhihirika mwishoni mwa 1991, wakati Baraza Linaloongoza la Mashahidi wa Yehova lilipoalika matawi kadhaa ya Watch Tower Society katika Ulaya ya Magharibi yaandae chakula na mavazi kwa ndugu zao wenye uhitaji katika Ulaya ya Magharibi, kutia na sehemu za uliokuwa Muungano wa Sovieti. Hapa twatokeza mfululizo wa ripoti kutoka baadhi ya matawi yaliyohusika.

Sweden

Katika Desemba 5, 1991, barua iliyoeleza uhitaji huo ilipelekwa kwa posta kwenye makundi yote 348 katika Sweden. Itikio lilikuwa la mara moja. Katika siku chache, lori la kwanza lilikuwa njiani kuelekea St. Petersburg, Urusi, likiwa limepakiwa tani 15 za unga, mafuta ya kupikia, nyama ya ng’ombe ya mkebe, maziwa ya unga-unga, na vitu kama hivyo. Mashahidi wa Yehova wa huko walipakua mizigo kutoka kwenye lori na upesi wakagawanya vifurushi hivyo 750 kuwapa wale wenye uhitaji. Baadaye, malori mengine mawili yalibeba chakula hadi Urusi. Kwa ujumla, tani zaidi ya 51.5 zilisafirishwa kutoka Sweden.

Nia ya kufanya utoaji wa mavazi na viatu ilipita kwa mbali matazamio yote. Marundo ya vifurushi vya mawazi yalilimbikana haraka katika Majumba ya Ufalme. Wakristo wengi walifanya utoaji wa mavazi yao wenyewe. Wengine walinunua vitu vipya. Ndugu mmoja alinunua suti tano. Mwenye duka mwenye kushangaa alipopata kujua kusudi lazo, alifanya utoaji wa suti nyinginezo tano. Ndugu mwingine alinunua boksi ya soksi, glavu, na skafu. Alipoeleza kusudi lazo, mwenye duka alimtolea shati mpya 30 kwa bei ya mbili. Mwenye duka la mavazi ya michezo alifanya utoaji wa jozi 100 za viatu na mabuti.

Vitu hivyo vyote vikaletwa kwenye tawi ili kuwekwa katika aina, kutiwa upya katika vifurushi, na kupakiwa. Mavazi—yaliyoweza kutoshea malori 40—yalijaa sehemu kubwa-kubwa za tawi! Akina ndugu na dada walifanya kazi kwa majuma kadhaa wakiyapanga katika marundo ya aina za wanaume, wanawake, na watoto na kuyatia katika katoni. Malori 15 tofauti yalitumiwa ili kubeba mavazi hayo kwa usalama hadi Urusi, Ukrainia, na Estonia.

Ndugu mmoja aliyeendesha mojayapo malori ya Sosaiti mara nane hadi uliokuwa Muungano wa Sovieti alisema hivi: “Jinsi ambavyo akina ndugu walivyotupokea kwenye vituo ilikuwa thawabu kubwa. Walitukumbatia na kutubusu, na zijapokuwa nyenzo zao chache, walitupa sisi somo zuri katika ukarimu wa Kikristo.”

Finland

Ijapokuwa hali ya kiuchumi yenye kupungua sana, ukosefu wa kazi za kuajiriwa wenye kuenea, na matatizo ya kiuchumi ya Finland, nia ya akina ndugu karibu 18,000 wa Finland ya kuwasaidia ndugu zao katika uliokuwa Muungano wa Sovieti imekuwa kubwa. Walipeleka zaidi ya tani 58 za chakula katika katoni 4,850 hadi St. Petersburg, Estonia, Latvia, Lithuania, na Kaliningrad. Pia walijaza nafasi tupu katika malori mavazi kiasi cha meta za mjao 12. Magari 25 yaliyotumiwa yalitolewa pia kwa ajili ya matumizi katika kazi ya Ufalme.

Baadhi ya boksi za chakula zilifikia kundi moja la wahubiri 14 katika Slanti katika eneo la St. Petersburg. Walionyesha uthamini mkubwa katika barua. “Tuna akina dada kumi wenye umri mkubwa zaidi kundini mwetu. Wengi wetu ni wagonjwa sana na hatuwezi kusimama katika mistari kwa muda wa saa nyingi ili kupata chakula. Hata hivyo, Baba yetu wa kimbingu hatupi sisi sababu ya kuvunjika moyo katika nyakati hizi ngumu bali anajaza mioyo yetu shangwe. Tunaongoza mafunzo ya Biblia nyumbani 43.” Wakati dada mmoja katika St. Petersburg alipopata kifurushi chake cha msaada, alisukumwa sana hivi kwamba alilia machozi kwa muda wa saa mbili kabla ya kukifungua.

Denmark

Katika nchi hiyo ndogo iliyoko kwenye mwingilio wa Bahari ya Baltiki, Mashahidi wa Yehova 16,000 hivi walikusanyika na kupeleka Ukrainia malori 19 yenye tani 64 za chakula katika boksi 4,200; boksi 4,600 za mavazi yenye hali ya juu; na jozi 2,269 za viatu vipya. Ndugu mmoja katika Ujerumani aliruhusu tawi litumie malori matano, ambayo baadaye alitoa kuwa upaji kwa akina ndugu katika Ukrainia. Aliporudi nyumbani, mmoja wa madereva alisema hivi: “Tulikuta kwamba tulikuwa tumerudi na mengi zaidi ya vile tulivyokuwa tumepeleka. Upendo na roho ya kudhabihu iliyoonyeshwa na akina ndugu wa Ukrainia iliimarisha sana imani yetu.”

Madereva walilazimika kuwa macho kwa ajili ya wanyang’anyi wa barabarani katika uliokuwa Muungano wa Sovieti. Siku chache kabla ya lori moja la Denmark kupita, unyang’anyi ulikuwa umetukia kwenye njia hiyo. Msafara wa malori matano yenye chakula kutoka shirika jingine la msaada ulikuwa umesimamishwa na wanyang’anyi waliotumia helikopta na bunduki mimina-risasi. Walichukua malori yote matano, wakiwaacha madereva hao kando ya barabara. Ijapokuwa hatari hiyo, ugavi wote kutoka kwa tawi la Denmark uliwafikia akina ndugu kwa usalama. Kwa kurudisha, walimpa dereva mmoja achukue nyumbani kibarua kifuatacho, kilichoandikwa kwa shida sana katika Kiingereza: “Ndugu na dada wapendwa wa Denmark: Tumepokea msaada wenu. Yehova atawathawabisha.”

Uholanzi

Tawi la Uholanzi lilipeleka tani 52 za chakula katika vifurushi 2,600. Vilipelekwa Ukrainia katika misafara miwili tofauti. Kila mara hayo malori sita yaliachwa huko, kwani yalitolewa kuwa upaji na akina ndugu katika Ujerumani kwa ajili ya kazi ya Ufalme katika Mashariki. Akina ndugu wa Ukrainia walipeleka kingi cha chakula hicho hadi Mosko, Siberia, na kwingineko ambako kulikuwa uhitaji mkubwa. Isitoshe, mavazi na viatu kiasi cha meta za mjao 736 vilitolewa na akina ndugu wa Uholanzi. Vililetwa Lviv katika Ukrainia kwa msafara wa malori 11 yakisindikizwa na gari la faragha.

Baada ya safari ndefu kwa gari kupitia Ujerumani na Polandi, msafara huo ulipitia forodha ya Ukrainia bila shida, na kufikia sehemu za nje-nje za Lviv saa tisa za usiku. Ripoti ya madereva ndiyo hii: “Kwa muda mfupi, kikundi cha akina ndugu 140 kilikuwako ili kupakua mizigo kutoka kwenye malori. Kabla ya kuanza kazi hiyo, ndugu hao wanyenyekevu walionyesha kumtegemea kwao Yehova, kwa kutoa sala ya pamoja. Kazi hiyo ilipomalizika, walikusanyika tena kwa ajili ya sala ya kutoa shukrani kwa Yehova. Baada ya kufurahia ukaribishaji-wageni wa ndugu wa huko, waliotoa kwa wingi yale machache waliyokuwa nayo, tulisindikizwa hadi barabara kuu, walikotoa sala kando ya barabara kabla ya kutuacha.

“Wakati wa safari ndefu kwa gari kurudi nyumbani, kulikuwa na mengi ya kufikiria—ukaribishaji-wageni wa akina ndugu katika Ujerumani na Polandi, na ule wa ndugu zetu katika Lviv; imani yao imara na mtazamo wao wa sala; ukaribishaji-wageni wao katika kuandaa makao na chakula huku wenyewe wakiwa na hali zenye uhitaji; wonyesho wao wa umoja na ukaribu; na shukrani yao. Tulifikiria pia akina ndugu na dada zetu nyumbani, waliokuwa wametoa kwa ukarimu sana.

Uswisi

Tawi la Uswisi lafungua ripoti yalo kwa kunukuu kutoka Yakobo 2:15, 16: “Ikiwa ndugu mwanamume au ndugu mwanamke yu uchi na kupungukiwa na riziki, na mtu wa kwenu akawaambia, Enendeni zenu kwa amani, mkaote moto na kushiba, lakini asiwape mahitaji ya mwili, yafaa nini?” Kisha ripoti yaendelea hivi: “Andiko hilo lilikuja akilini wakati Baraza Linaloongoza la Mashahidi wa Yehova lilipotualika tuandae msaada wa kimwili kwa ndugu zetu wenye uhitaji.

“Mara moja kila mtu akawa na shughuli! Katika siku mbili tu, tani 12 za chakula katika vifurushi 600 vilipelekwa Ukrainia kwa malori matatu kutoka Ujerumani, ambayo yangetolewa kuwa upaji kwa ajili ya kazi huko. Habari ya kwamba yote yalikuwa yamefika kwa usalama zilisababisha shangwe kubwa miongoni mwa ndugu zetu huku. Wakati uo huo, makundi yalikusanya mavazi, na upesi tawi letu lilijaa pomoni katoni, masanduku, na mikoba! Zile zenye nguo za watoto zilitia ndani vitu vya kuchezea kutoka kwa watoto Waswisi kwa ajili ya marafiki wasiojulikana katika Kaskazini ya mbali. Chokleti nyingi pia ziliwekwa kati ya matabaka ya mavazi.”

Hivyo vyote vingepelekwaje? Ripoti yasema hivi: “Tawi katika Ufaransa lilitusaidia kwa kutupa sisi malori mawili na madereva wanne. Kwa kuongezea, lori moja kutoka tawi letu na mengine manne ya ndugu wa huku yalihitajiwa ili kupeleka tani hizo 72 hadi Ukrainia.” Msafara, wenye meta 150 kwa urefu, ulifika depo katika Lviv kwa usalama, ambako karibu akina ndugu mia moja wa huko walingojea ili kupakua mizigo kutoka kwenye malori. Madereva waliripoti kwamba kizuio cha lugha hakikuwa tatizo kwa sababu nyuso zao zilionyesha uthamini wenye kina.

Austria

Akina ndugu wa Austria walipeleka tani 48.4 za chakula, katoni 5,114 za nguo, na jozi 6,700 za viatu hadi Lviv na Uzhgorod katika Ukrainia. Walipeleka pia tani 7 za chakula, boksi 1,418 za mavazi, na jozi 465 za viatu hadi Belgrade, Mostar, Osijek, Sarajevo, na Zagreb katika iliyokuwa Yugoslavia. Ripoti ya Tawi yasema hivi: “Tulikuwa na malori 12 yaliyopakiwa, yakisafiri kilometa 34,000. Sehemu kubwa ya usafirishaji huo ilifanywa na ndugu mmoja pamoja na mwana wake wenye biashara ya magari ya mizigo.”

Kwa habari ya mavazi yaliyotolewa, ripoti hiyo yaendelea hivi: “Tulitumia Jumba la Kusanyiko kuwa depo kuu. Mizigo baada ya mizigo ikafuliza kuja, mpaka hakukuwa na nafasi tena. Kama vile katika siku za Musa, watu walihitaji kuzuiwa wasilete zaidi. (Kutoka 36:6) Hata watu wengine ambao si Mashahidi wa Yehova walifanya utoaji wa fedha, ‘kwa sababu,’ kama walivyosema, ‘kwa njia hii twajua kwamba watu wenye uhitaji watazipata.’ Tulipata pia katoni tupu zilizohitajiwa sana kutoka kwa mashirika ya kilimwengu bila malipo.” Akina ndugu na dada waliopanga na kutia kila kitu katika vifurushi walikuwa kutoka miaka 9 hadi 80. Hata walijaribu kuweka pamoja tai na shati zifaazo kwa kila suti.

Ripoti hiyo yasema hivi: “Wenye mamlaka wa Austria na wale kwenye mipaka wamekuwa wenye msaada sana katika kuwezesha usafirishaji mbalimbali wa msaada na katika kutoa hati zinazohitajika ili usafirishaji wote uweze kufanywa bila ugumu.”

Italia

Kutoka Roma kiasi kifikacho tani 188 cha chakula kilipelekwa katika misafara ya malori mawili makubwa kuvuka Austria, Chekoslovakia, na Polandi hadi uliokuwa Muungano wa Sovieti. Kila timu ya msafara ilitia ndani madereva sita, mekanika, fundi-umeme wa magari, mkalimani, mmoja anayeshughulikia usafirishaji wa vitu, mpishi, daktari, kiongozi wa msafara katika gari la Jeep, na ndugu mwenye gari lililo kama makao.

Chakula kilinunuliwa kutoka mashirika saba yanayoandaa vifaa. Tawi laripoti hivi: “Mashirika hayo yaliposikia sababu ya utoaji huo, baadhi yayo yalitaka kushiriki. Mamia kadhaa ya kilogramu za pasta na mchele, pamoja na boksi za kuyatia ndani, zilitolewa na mashirika ya kilimwengu. Bado mengine yalifanya utoaji wa tairi za majira ya theluji kwa ajili ya malori au yalijitolea kuchanga fedha.

“Akina ndugu katika Italia walithamini fursa hiyo ya kusaidia. Watoto pia walitaka kuchanga. Mvulana wa miaka mitano alipeleka mchango mdogo ambao alitumaini ungeweza kununua ‘mkebe mkubwa sana wa samaki-tuna kwa ajili ya akina ndugu katika Urusi.’ Kwa ajili ya maksi zake za juu shuleni, msichana mmoja mdogo alipokea fedha kutoka kwa nyanya na babu yake za kuwanunulia wazazi wake zawadi. ‘Lakini,’ aliandika, ‘nilipotambua kwamba ndugu zangu wengi hawana vitu vyote vizuri nilivyo navyo vya kula, nilifikiri kwamba zawadi iliyo bora zaidi ambayo ningeweza kuwanunulia wazazi wangu ilikuwa kuwasaidia ndugu hao.’ Aliweka kiasi kikubwa cha fedha katika sanduku la michango. ‘Natumaini kuendelea kupata maksi nzuri, ili niweze kupeleka fedha nyingi zaidi,’ akasema.” Ripoti ya tawi inamalizia kwa kusema kwamba barua za uthamini wa moyo kutoka kwa akina ndugu katika Ukrainia, yale maneno mengi ya uthamini ya akina ndugu wa Italia, na maono mazuri katika kuandaa na kusafirisha ugavi huo yalikuwa yenye kugusa moyo, yenye kutia moyo, na yenye kuungamanisha.

Chakula kwa Maelfu ya Wahudhuriaji

Mkusanyiko wa kwanza wa kimataifa wa Mashahidi wa Yehova katika uliokuwa Muungano wa Sovieti ulifanywa kwenye stediamu ya Kirov katika St. Petersburg Urusi, Juni 28-30, 1992. Mkusanyiko huo wenye maana, wenye kichwa “Wachukuaji Nuru,” ulihudhuriwa na wahudhuriaji zaidi ya 46,200 kutoka nchi 28. Ulitoa nafasi nyingine ya kuonyesha upendo wa Kikristo kwa “ushirika wote wa akina ndugu.”—1 Petro 2:17, NW.

Tani za chakula kutoka Denmark, Finland, Sweden, na mabara mengine katika Ulaya ya Magharibi ziligawanywa bila malipo kwa maelfu ya wahudhuriaji wa mkusanyiko kutoka iliyokuwa U.S.S.R, cha kuliwa wakati wa mkusanyiko. Walipoondoka kwenye mkusanyiko baada ya kipindi cha mwisho, walipewa pia kifurushi cha chakula chenye maandalizi kwa ajili ya safari yao ya kurudi nyumbani.

Ripoti zilizotajwa hapa zinaonyesha kwamba utoaji huo umekuwa hauendi upande mmoja—kuelekea mashariki—tu. Kumekuwako badilishano la utoaji. Chakula na mavazi kuelekea mashariki, naam, lakini kuelekea magharibi maonyesho yenye kuchangamsha moyo yasiyohesabika ya upendo na maono yenye kuchochea imani yakionyesha udumifu na uaminifu wa maelfu ya waabudu wa Yehova katika miongo ya mbano na ugumu. Hivyo, pande zote mbili zimeona ukweli wa maneno haya ya Yesu: “Kuna furaha nyingi katika kutoa kuliko zilivyo katika kupokea.”—Matendo 20:35, NW.

[Mchoro/Picha katika ukurasa wa 21]

1. Kutoka Finland: St. Petersburg, Urusi; Tallinn na Tartu, Estonia; Riga, Latvia; Vilnius na Kaunas, Lithuania; Kaliningrad, Urusi; Petrozavodsk, Karelia

2. Kutoka Uholanzi: Lviv, Ukrainia

3. Kutoka Sweden: St. Petersburg, Urusi; Lviv, Ukrainia; Nevinnomyssk, Urusi

4. Kutoka Denmark: St. Petersburg, Urusi; Lviv, Ukrainia

5. Kutoka Austria: Lviv, Ukrainia; Belgrade, Mostar, Osijek, Sarajevo, Zagreb (katika iliyokuwa Yugoslavia)

6. Kutoka Uswisi: Lviv, Ukrainia

7. Kutoka Italia: Lviv, Ukrainia

[Picha katika ukurasa wa 23]

Katoni za mavazi katika tawi la Sweden

Kupakia maandalizi ya msaada

Vyakula katika kifurushi kimoja

Bekoni na hemu (nyamanguruwe) kutoka Denmark

Msafara wa malori 11 na gari moja

Vifurushi na masanduku kwenye tawi la Austria

Kupakua mizigo kutoka kwenye lori huko Lviv, Ukrainia ▸

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki