Mwenye Kuamka Mapema
MIONGONI mwa miti ya matunda ya eneo la Mediterania, mlozi ni wenye kuvutia zaidi. Katika mwisho-mwisho wa Januari au Februari—muda mrefu kabla ya miti mingine mingi—unaamka kutoka usingizi wao wa majira ya baridi. Na huko ni kuamka kulikoje! Mti mzima unavikwa vazi la maua rangi nyekundu-nyeupe-nyororo au maua meupe, hayo meupe yakifanana kwa kadiri fulani na mvi wa wazee-wazee.—Linganisha Mhubiri 12:5.
Waebrania wa kale waliuita mlozi “aamkaye,” wakirejezea mchanuko wao wa mapema. Sifa hiyo ilitumiwa na Yehova kuonyesha ujumbe wa maana. Mwanzoni mwa huduma yake, Yeremia alionyeshwa katika njozi chipukizi cha mlozi. Hilo lilimaanisha nini? Yehova alieleza hivi: “Ninaliangalia [ninakaa macho kuhusu, NW] neno langu, ili nilitimize.”—Yeremia 1:12.
Kama vile mlozi ‘uamkavyo’ mapema, ndivyo Yehova alivyokuwa ‘akiamka mapema’ ili kuwatuma manabii wake kuwaonya watu wake juu ya matokeo ya kutokutii. (Yeremia 7:25) Naye hangepumzika—‘angekaa macho’—mpaka neno lake la kiunabii lilipotimizwa. Ndivyo ilivyokuwa katika 607 K.W.K., kwa wakati uliowekwa, hukumu ya Yehova ilikuja juu ya taifa la Yuda lenye kuasi-imani.
Neno la Mungu linatabiri kwamba hukumu iyo hiyo itakuja dhidi ya mfumo mbovu tunamoishi. (Zaburi 37:9, 10; 2 Petro 3:10-13) Akirejezea tendo hilo la hukumu, nabii Habakuki atuhakikishia hivi: “Maana njozi hii bado ni kwa wakati ulioamriwa . . . ingojee; kwa kuwa haina budi kuja, haitakawia.” (Habakuki 2:3) Ua zuri la mlozi linatukumbusha kwamba Yehova atakaa macho kuhusu neno lake ili kulitimiza.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 32]
Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.