Historia ya Biblia Ni Sahihi Kadiri Gani?
“NASEMA kweli, sisemi uongo,” ndivyo alivyosema mwandishi mmoja wa Biblia kwa rafiki yake kijana. (1 Timotheo 2:7) Maneno kama hayo katika barua za Paulo hutokeza ugumu kwa wahakiki wa Biblia.a Zaidi ya miaka 1,900 imepita tangu barua za Paulo kuandikwa. Baada ya wakati huo wote, hakuna mtu ambaye ameweza kujitokeza na kuthibitisha kwa mafanikio hata jambo moja kuwa si sahihi katika barua zake.
Mwandishi wa Biblia Luka alionyesha pia alihangaikia usahihi. Yeye alirekodi usimulizi mmoja wa maisha na huduma ya Yesu uliofuatwa na usimulizi wake ulioitwa Matendo ya Mitume. “Nimejitafutia usahihi wa mambo hayo yote tangu mwanzo,” akaandika Luka.—Luka 1:3.
Shuhuda za Usahihi
Wahakiki wa Biblia wa miaka ya mapema ya karne ya 19 walipinga usahihi wa Luka akiwa mwanahistoria. Zaidi ya hayo, walidai kwamba ile historia katika Matendo ilibuniwa katikati ya karne ya pili W.K. Mwakiolojia Mwingereza Bwana William Mitchell Ramsay ni mmoja aliyeamini hivyo. Lakini baada ya kuchunguza majina na mahali-mahali panapotajwa na Luka, aliungama hivi: “Nilisadikishwa polepole kwamba katika mambo fulani madogo-madogo usimulizi huo ulionyesha ukweli wa ajabu.”
Ramsay alipoandika yaliyo juu, suala lililohusu usahihi wa Luka lilikuwa bado kusuluhishwa. Lilihusu yale majiji yaliyohusiana kwa ukaribu ya Ikonio, Listra na Derbe. Luka alidokeza kwamba Ikonio lilikuwa tofauti na Listra na Derbe, akiyasimulia hayo ya pili kuwa “[majiji] ya Likaonia.” (Matendo 14:6) Hata hivyo, kama vile ramani inayoandamana ionyeshavyo, Listra lilikuwa karibu zaidi na Ikonio kuliko Derbe. Baadhi ya wanahistoria wa kale walisimulia Ikonio kuwa sehemu ya Likaonia; kwa hiyo, wahakiki walimpinga Luka kwa ajili ya kutofanya hivyo pia.
Halafu, katika 1910, Ramsay akagundua nguzo moja ya ukumbusho katika mabomoko ya Ikonio ikionyesha kwamba lugha ya jiji hilo lilikuwa Kifirigia wala si Kilikaonia. “Hesabu kadhaa ya michoro mingine kutoka Ikonio na maeneo yaliyozunguka jiji hilo huthibitisha ukweli wa kwamba kijamii, jiji hilo lingeweza kusimuliwa kuwa la Kifirigia,” asema Dakt. Merrill Unger katika kitabu chake Archaeology and the New Testament. Kwa kweli, Ikonio la siku ya Paulo lilikuwa lenye utamaduni wa Kifirigia na lilikuwa tofauti na “[majiji] ya Likaonia,” ambako “[walisema] kwa Kilikaonia.”—Matendo 14:6, 11.
Wahakiki wa Biblia walibisha pia juu ya matumizi ya Luka ya neno “mapolitaki” kwa watawala wa jiji la Thesalonike. (Matendo 17:6, NW, kielezi-chini) Neno hilo halikujulikana katika fasihi ya Kigiriki. Halafu tao likapatikana katika jiji hilo la kale lililokuwa na majina ya watawala wa jiji waliosimuliwa kuwa “mapolitaki”—neno hasa lililotumiwa na Luka. “Usahihi wa Luka umetetewa na matumizi ya neno hilo,” aeleza W. E. Vine katika kitabu chake Expository Dictionary of Old and New Testament Words.
Safari ya Luka ya Baharini
Mabaharia wastadi wamechunguza yale maelezo madogo-madogo juu ya kuvunjikiwa merikebu kunakosimuliwa katika Matendo sura 27. Kulingana na Luka, ile merikebu kubwa ambamo yeye na Paulo waliabiri, ilishikwa na upepo wa nguvu uliotoka kaskazini hadi mashariki karibu na kisiwa kidogo cha Kauda, na mabaharia walikuwa wakihofia kuendeshwa ndani ya mafungu ya mchanga yaliyo karibu na pwani ya kaskazini mwa Afrika. (Matendo 27:14, 17, NW, kielezi-chini) Kwa ubaharia wenye ustadi, waliweza kukielekeza chombo hicho mbali na Afrika kwa mwendo wa kuelekea magharibi. Upepo huo wa nguvu uliendelea bila kupungua, na hatimaye merikebu ikakwama mwambani karibu na kisiwa cha Malta, ikiwa imesafiri mwendo wa karibu kilometa 870. Mabaharia wastadi wanafanya hesabu kwamba merikebu kubwa inayosafiri katika upepo wa nguvu ingechukua zaidi ya siku 13 kupelekwa mbali hivyo. Kufanya hesabu kwao kunakubaliana na usimulizi wa Luka, unaosema kwamba kuvunjikiwa merikebu huko kulitukia siku ya 14. (Matendo 27:27, 33, 39, 41) Baada ya kuyachunguza maelezo hayo yote madogo-madogo juu ya safari ya Luka ya baharini, baharia mmoja James Smith alikata maneno hivi: “Huo ni usimulizi wa matukio halisi, yaliyoandikwa na mtu aliyehusika nayo kibinafsi . . . Hakuna mtu ambaye si baharia ambaye angaliweza kuandika usimulizi wa safari ya baharini kwa upatano sana katika sehemu zayo zote, isipokuwa kwa kujionea mwenyewe.”
Kwa sababu ya magunduzi kama hayo, baadhi ya wanatheolojia wako tayari kutetea Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo kuwa historia sahihi. Lakini namna gani ile historia ya mapema zaidi inayopatikana katika Maandiko ya Kiebrania? Makasisi wengi hufuata falsafa ya kisasa na kujulisha kwamba maandiko hayo yanatia ndani ngano. Hata hivyo, kwa aibu ya wahakiki, mambo kadhaa madogo-madogo ya historia ya mapema ya Biblia yamethibitishwa pia. Kwa kielelezo, chunguza ule ugunduzi wa ile Milki ya Kiashuru iliyosahauliwa wakati mmoja.
[Maelezo ya Chini]
a Ona pia Warumi 9:1; 2 Wakorintho 11:31; Wagalatia 1:20.
[Ramani katika ukurasa wa 3]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
FIRIGIA
LIKAONIA
Ikonio
Listra
Derbe
BAHARI YA MEDITERANIA
KIPRO