Je! Waweza Kuitumaini Biblia?
IKIWA ungeokota Biblia, je ungetazamia kupata sarafu? Namna gani sarafu hii ya fedha ya kale?
Wengi huiona Biblia kuwa kitabu cha zamani kinachotoa hadithi za kale zenye kupendeza na adili zinazostahili kusifiwa. Hata hivyo, hawaamini kwamba masimulizi ya Biblia ni historia sahihi, kwa hiyo wao hukana kwamba ni Neno la Mungu. Lakini, kuna uthibitisho wa kutosha wa usahihi wa Biblia. Sarafu hii (inayoonyeshwa kwa ukubwa zaidi) ni kielelezo kizuri. Maandishi hayo yanasema nini?
Sarafu hii ilifanyizwa katika Tarso, jiji moja katika sehemu ya kusini-mashariki mwa nchi ambayo sasa ni Uturuki. Sarafu hiyo ilitokezwa wakati wa utawala wa gavana Mwajemi Mazaeus katika karne ya nne K.W.K. Inamtambulisha kuwa gavana wa mkoa wa “Ng’ambo ya Mto,” yaani, Mto Frati.
Lakini kwa nini fungu hilo la maneno ni lenye kupendeza? Kwa sababu utaona kichwa icho hicho cha cheo katika Biblia yako. Ezra 5:6–6:13 laonyesha barua kati ya Mfalme Mwajemi Dario na gavana aitwaye Tatenai. Suala lilikuwa juu ya kujenga upya kwa Wayahudi hekalu lao katika Yerusalemu. Ezra alikuwa mnakiliji stadi wa Sheria ya Mungu, na ungemtazamia kuwa dhahiri, sahihi katika yale aliyoandika. Utaona kwenye Ezra 5:6 and 6:13 kwamba alimwita Tatenai “liwali [gavana, NW] wa ng’ambo wa Mto.”
Ezra aliyaandika maneno hayo karibu 460 K.W.K., yapata miaka 100 kabla ya sarafu hii kuundwa. Ah, kuna watu wengine ambao huenda wakahisi kwamba kichwa cha cheo cha ofisa wa kale ni jambo dogo lisilo na maana. Lakini ikiwa unaweza kuwategemea waandishi wa Biblia katika hata mambo hayo madogo-madogo, je, hilo lisiongeze uhakika wako katika mambo yale mengine waliyoandika?
Katika makala za kwanza mbili katika toleo hili, utapata sababu zaidi za kuwa na uhakika huo.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 32]
Mkusanyo wa Israel Dept. of Antiquities Exhibited & photographed Israel Museum