Uzuri Ambao Haufifii
“UZURI hutoweka; uzuri hupita,” akaonelea mshairi mmoja Walter De la Mare. Hilo bila shaka hutukia kwa habari ya yale maua mazuri ajabu ya kakati ambayo yameonyeshwa hapa. Utukufu wayo hufifia upesi.
Mwanafunzi Mkristo Yakobo aliandika hivi: “Kama ua la majani [tajiri] atatoweka. Maana jua huchomoza kwa hari, huyakausha majani; ua lake huanguka, uzuri wa umbo lake hupotea; vivyo hivyo naye tajiri atanyauka katika njia zake.”—Yakobo 1:10, 11.
Katika ulimwengu huu usio na uhakika, utajiri waweza kwa kweli kutoweka katika usiku mmoja. Zaidi ya hayo, tajiri—kama kila mtu mwingine yeyote—‘siku zake za kuishi si nyingi kama vile ua.’ (Ayubu 14:1, 2) Yesu alitoa mfano wa mtu mmoja aliyekuwa amekuwa na shughuli nyingi akikusanya utajiri ili aweze kupumzika na kufurahi. Lakini alipofikiri kwamba alikuwa na kila kitu kilichohitajiwa ili kuwa na maisha ya starehe, alikufa. Yesu alionya hivi: “Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu.”—Luka 12:16-21.
‘Kujitajirisha kwa Mungu.’ Yesu alimaanisha nini aliposema hivyo? Mtu aliye tajiri kwa njia hiyo ana “hazina mbinguni”—jina zuri na Mungu. Hazina ya jinsi hiyo yaweza kukaa bila kufifia kamwe. (Mathayo 6:20; Waebrania 6:10) Badala ya kuwa kama ua linalonyauka, mtu wa jinsi hiyo analinganishwa katika Biblia na mti, ambao majani yao hayanyauki. Na, tunahakikishiwa kwamba, “kila alitendalo litafanikiwa.”—Zaburi 1:1-3, 6.