Kutafuta Hazina Iliyofichika
KATIKA 1848 dhahabu iligunduliwa katika uwanja wa Sutter wenye kiwanda cha kupasulia miti huko Kalifornia, U.S.A. Kufikia 1849 maelfu ya watu walikuwa wakija kwenye eneo hilo wakitumaini kuwa matajiri upesi, na harakati kubwa zaidi ya kupata dhahabu katika historia ya United States ikaanza. Katika mwaka mmoja, ile bandari iliyokuwa karibu zaidi, yaani San Fransisko, ilikua kutoka mji mdogo likawa jiji la watu 25,000. Taraja la utajiri wa ghafula lilithibitika kuwa uvutano wenye nguvu.
Mfalme Sulemani wa Israeli wa kale alijua jinsi watu walivyochimba kwa bidii sana ili kupata hazina iliyofichika, na alirejezea hilo alipoandika hivi: “Naam, ukiita busara [uelewevu, NW], na kupaza sauti yako upate ufahamu; ukiutafuta kama fedha, na kuutafutia kama hazina iliyositirika; ndipo utakapofahamu kumcha BWANA [Yehova, NW], na kupata kumjua Mungu.”—Mithali 2:3-5.
Unaweza kufanya mambo mengi na dhahabu na fedha, lakini unaweza kufanya mengi zaidi na uelewevu na ufahamu. Hizo zaweza kukusaidia ufanye maamuzi yafaayo, kusuluhisha matatizo, kufanikiwa katika ndoa, na kupata furaha. (Mithali 2:11, 12) Vivyo hivyo, ujuzi na hekima ya kweli itakusaidia kumjua Muumba wako, kuelewa makusudi yake, na kumtii na kumpendeza. Dhahabu haiwezi kukupa yoyote ya mambo hayo.
Maneno ya Biblia ni ya kweli: “Hekima ni ulinzi kama vile fedha ni ulinzi, lakini faida ya ujuzi ni hii: kwamba hekima huhifadhi uhai wa yule aliye nayo.” (Mhubiri 7:12, New International Version) Ingawa wengi huota ndoto za kupata utajiri wa ghafula, ni jambo la hekima zaidi kama nini kuifungua Biblia na kuichimba ili kupata ufahamu, uelewevu, ujuzi, na hekima ambayo ni utajiri wa kweil.