Ni Nani Huamini Katika Roho Waovu?
JE! WEWE huamini kwamba roho wasioonekana waweza kuathiri maisha yako? Wengi wangekataa katakata. Ingawa wanakiri kuwako kwa Mungu, wao hudhihaki wazo la kuwako kwa wafanya uovu wanaozidi uwezo wa kibinadamu.
Kuenea sana kwa kutokuamini katika roho wasioonekana katika ulimwengu wa Magharibi husababishwa kwa sehemu na uvutano wa Jumuiya ya Wakristo, ambayo kwa muda wa karne kadhaa imefundisha kwamba dunia ilikuwa kitovu cha ulimwengu wote mzima, ikiwa kati ya mbingu na helo iliyo chini ya ardhi. Kulingana na fundisho hilo, malaika walijionea raha mustarehe ya mbinguni ilihali mashetani walisimamia mambo ya helo.
Mavumbuo katika sayansi yalipofanya watu wakatalie mbali mawazo yasiyofaa juu ya muundo wa ulimwengu wote mzima, kuamini katika viumbe vya kiroho kukawa jambo lisilo la kimambo-leo. The New Encyclopædia Britannica yasema hivi: “Baada ya mapinduzi ya Copernican ya karne ya 16 (yenye msingi wa nadharia za mwastronomia wa Poland Copernicus), ambayo katika hiyo . . . Dunia haikuonwa tena kuwa kitovu cha ulimwengu wote mzima bali, badala yayo, [ilionwa kuwa] sayari tu katika mfumo wa jua ambayo ni sehemu ndogo sana ya galaksi katika ulimwengu wote mzima usio na mpaka—mawazo ya [kuwako kwa] malaika na mashetani hayakuonekana tena kuwa yenye kufaa.”
Ingawa watu wengi hawaamini katika roho waovu, kuna mamilioni ya watu ambao huamini. Malaika waliotenda dhambi wana fungu la maana katika dini nyingi, za wakati uliopita na za sasa. Zaidi ya fungu lao wakiwa wenye kufisidi hali ya kiroho, malaika hao wabaya huonwa kuwa mawakili wa misiba, kama vile vita, njaa kali, na matetemeko ya dunia, na pia kuwa waenezaji wa ugonjwa, maradhi ya akili, na kifo.
Shetani Ibilisi, aliye roho mwovu mkuu katika Ukristo na Dini ya Kiyahudi, huitwa Iblis na Waislamu. Katika dini ya kale ya Kiajemi ya Uzoroaster, yeye aonekana kuwa Angra Mainyu. Katika dini ya Kignosti, iliyositawi katika karne za pili na tatu W.K., alionwa kuwa yule Demiurge, jina lililopewa mungu mwenye wivu na mwenye cheo cha chini aliyeabudiwa na sehemu kubwa ya ainakibinadamu bila wao kujua.
Roho waovu wenye cheo cha chini zaidi huhusika sana katika dini za Mashariki. Wahindu huamini kwamba wale asura (mashetani) hupinga wale deva (miungu). Wale ambao huhofiwa zaidi miongoni mwa asura ni wale rakshasa, viumbe vyenye kuchukiza ambavyo huzoelea makaburini.
Wabuddha huona mashetani kuwa kani zenye utu zinazowazuia watu wasifikie Nirvana, hali ya kutokuwa na tamaa. Mshawishi mkuu miongoni mwazo ni Mara, pamoja na binti zake watatu Rati (Tamaa), Raga (Anasa), na Tanha (Kutotulia).
Waabudu Wachina hutumia mioto mikubwa, mienge, na fataki ili kujilinda dhidi ya kuei, au mashetani wa asili. Dini za Kijapani huamini pia kwamba kuna mashetani wengi, kutia ndani wale tengu wenye kuhofisha, roho ambao hupagaa watu mpaka wapungwe na kuhani.
Miongoni mwa dini zisizo na elimu za Asia, Afrika, Oceania, na za mabara ya Amerika, viumbe vya kiroho huaminiwa kuwa vyenye kutoa msaada au vyenye kudhuru kulingana na hali na jinsi vinavyohisi wakati fulani. Watu huwapa roho hao heshima ya kiibada ili kuepuka msiba na kupokea mapendeleo.
Zaidi ya hayo yote ongeza kule kuenea sana kwa upendezi katika mizungu na uwasiliani-roho, na ni wazi kwamba imani katika roho waovu ina historia ndefu na yenye kuenea kotekote. Lakini je, yafaa kuamini kwamba viumbe hivyo viko? Biblia husema kwamba viko. Hata hivyo, ikiwa viko, kwa nini Mungu huviruhusu viathiri mwanadamu kwa hasara yake?