Habari Njema Kutoka Malawi!
MNAMO Novemba 15, 1993, Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania liliandikishwa rasmi katika nchi ya Malawi iliyoko kusini-mashariki mwa Afrika. Kufanya hivyo kutawapa Mashahidi wa Yehova utambuzi wa kisheria na uhuru wa kuhubiri kweli za Biblia kwa watu wa Malawi.
Kule nyuma katika 1948, ofisi ya tawi ya Watch Tower Society ilifunguliwa nchini Malawi ili iratibishe kazi ya Mashahidi wa Yehova katika nchi hiyo. Mnamo Januari 8, 1957, Watch Tower Society liliandikishwa huko kwa mara ya kwanza. Kwa miaka kadhaa Mashahidi wa Yehova walifurahia ukuzi wa haraka. Lakini mnyanyaso mkatili ukatokea katika 1964. Kwa nini?
Kwa kumtii Mungu, Mashahidi wa Yehova walidumisha msimamo wao wa kutokuwamo kabisa kwa habari za siasa. (Yohana 17:16) Kwa wazi, wengine hawakuelewa vizuri msimamo huo wa Kimaandiko na wakachukulia Mashahidi vibaya kuwa dini ya uzushi na wavunja-sheria. Kwa hiyo, wengine walihisi wana sababu nzuri ya kunyanyasa Wakristo hao wenye kupenda amani. Mashahidi wengi walifukuzwa kazini mwao, walipigwa, na kuaibishwa kwa njia nyinginezo. Wengine walitenganishwa na watoto wao kwa nguvu.
Katika 1972 zaidi ya Mashahidi 30,000 na wengine waliokuwa wakijifunza Biblia pamoja nao walilazimishwa wahame nchi hiyo kwa kuhofia uhai wao. Maelfu waliishi katika kambi za wakimbizi katika nchi jirani ya Msumbiji. Lakini katika 1975 wakimbizi hao walirudishwa Malawi, walikolazimishwa kukabili mnyanyaso zaidi. Wakimbizi wengi waliwekwa katika kambi za mateso. Katikati ya mivurugo hiyo, Watch Tower Society lilifutiliwa mbali lisiwe katika orodha ya mashirika halali nchini Malawi. Tangu wakati huo Mashahidi wa Yehova na mashirika yao ya kisheria wamepigwa marufuku katika nchi hiyo.
Wajapotendewa mambo hayo yote, Mashahidi hawakulipiza kisasi. Hawakufanyiza umati wenye ghasia wala kufanya maandamano yenye jeuri wakiteta dhidi ya serikali. Badala ya hivyo, kwa kusali wao walidumisha takwa lao la Kikristo la kuonyesha staha na heshima ifaayo kwa “mamlaka iliyo kuu” ya kiserikali. (Warumi 13:1-7; 1 Timotheo 2:1, 2) Mashahidi vilevile walidumisha viwango vya juu vya kuishi kwa njia ya Kikristo kama inavyoonyeshwa katika Biblia na hivyo wameweka kielelezo bora cha tabia.
Wakiwa na uhuru wao mpya, Mashahidi wa Yehova nchini Malawi wameazimia kuendelea kuhubiri kweli za Biblia kwa uharaka, katika “wakati ufaao.”—2 Timotheo 4:2.
[Picha katika ukurasa wa 31]
M. G. Henschel akiwa na familia ya Betheli ya Malawi katika miaka ya 1960