“Mashahidi wa Yehova Wamenilinda!”
KATIKA siku hizi za mwisho, wengi wamekuwa “wakali, wasiopenda mema.” (2 Timotheo 3:1, 3) Isaac, mhudumu wa kujitolea katika ofisi moja ya tawi ya Watch Tower Society nchini Afrika Magharibi, alipata jambo hilo kuwa kweli. Yeye aeleza:
“Mnamo Januari 1992, nilikuwa nikisafiri katika barabara moja yenye upweke katika teksi moja nikiwa pamoja na abiria wengine watano. Nilianza mazungumzo pamoja na mwanamke mmoja aliyekuwa ameketi kando yangu, naye akakubali kwa furaha broshua yenye msingi wa Biblia niliyompa.
“Kwa ghafula, karibu saa kumi alasiri, gari jipya bila nambari za leseni ikakata mbele yetu, nalo gari letu likashika breki kwa kelele nyingi. Watu watatu wenye nguvu, kila mmoja wao akiwa na bunduki kubwa, wakaruka nje ya gari lile jingine na kufungua milango yetu kwa nguvu. ‘Tokeni nje, nyinyi nyote,’ mmoja wao akanguruma.
“Mtu mwingine akashika mfuko wangu wa vitabu. Alipoona kwamba mfuko huo ulikuwa tu na fasihi za Biblia, aliutupilia mbali. ‘Una kitu gani kingine?’ akauliza, akinielekezea bunduki. Nikampa fedha nilizokuwa nazo mfukoni haraka. ‘Ni hizo tu?’ akauliza. Nikamwambia kwamba mimi ni mmoja wa Mashahidi wa Yehova na kwamba Mashahidi hawasemi uongo. Akanyakua mfuko wangu wa kuwekea fedha, akaona kitambulisho changu cha Watch Tower kisha akasema, ‘Naam, Watchtower. Ngoja hapa.’
“Kisha akamgeukia yule mwanamke niliyekuwa nimezungumza naye katika teksi. Akampa haraka mkufu wake wa shingo na fedha alizokuwa nazo katika kibeti chake. Mnyang’anyi huyo alipoona ile broshua katika mikono yake yenye kutetemeka, alidhani ya kwamba tulikuwa pamoja, na hivyo akamwambia akae nami.
“Wakati uo huo, wale majambazi wengine waliwashambulia kikatili wale wasafiri wenzetu wengine. Waliwapiga na kuwanyang’anya vitu dereva na yule mtu mwingine aliyekuwa akisafiri na sisi. Jambazi mmoja alishika mkufu wa shingo wa mwanamke wa pili. Yule mwanamke alipokataa, walimpiga kikatili kichwani na kifuani wakitumia sehemu za mwisho za bunduki mpaka akafa. Walimvuta mwanamke wa tatu nje ya gari na kumpiga risasi kifuani. Inasikitisha kwamba yeye naye akafa. Ni mimi pekee na yule mwanamke mchanga aliyekuwa nami ambao hatukujeruhiwa kwa namna yoyote.
“Tulipochukuliwa baadaye na gari moja lililokuwa likipita, mwanamke huyo aliyekuwa ameogofya sana alikuwa akirudia-rudia kusema, ‘Mashahidi wa Yehova wamenilinda!’”