“Kuvua Samaki” Katika Maji ya Fiji
FIJI—jina hilo huleta mawazo ya paradiso ya Bahari ya Pasifiki. Maji ya rangi kijani-samawati, matumbawe, minazi yenye kusukasuka, milima ya kijani-kibichi, samaki wa tropiki, matunda na maua yasiyo ya kawaida. Waweza kupata hayo yote kwa wingi kwenye hiki kikundi cha visiwa 300, kilicho karibu kilometa 1,800 kaskazini mwa New Zealand katika Pasifiki Kusini. Hivyo, huenda ukakubali kwamba Fiji yaweza kuwa ndoto ya kila mtu ya paradiso ya kitropiki.
Hata hivyo, si uzuri wa asili tu unaofanya visiwa vya Fiji vivutie. Naam, kama vile kulivyo na unamna-namna mwingi wa samaki wa matumbawe, kuna unamna-namna mwingi pia barani. Visiwa vya Fiji vina makabila yenye kutofautiana sana hivi kwamba haina kifani katika Pasifiki Kusini. Vikundi viwili vikubwa zaidi ya vyote miongoni mwa wakazi wayo wapatao 750,000 ni Wafiji wenyeji, ambao ni wa asili ya Wamelanesia, na Wahindi wazawa wa Fiji, wazao wa wafanyakazi walioletwa kutoka India wakati wa siku za ukoloni wa Uingereza. Lakini pia kuna Wabanaba, Wachina, Wazungu, Wagilbert, Warotuma, Watuvalu, na wengineo.
Katika jamii hiyo ya utamaduni mbalimbali, Mashahidi wa Yehova wana shughuli nyingi katika kazi ya “kuvua samaki.” (Marko 1:17) Ni mwito kuhubiri habari njema za Ufalme wa Mungu katika jumuiya hiyo ya watu mbalimbali. Kwanza, kuna vizuizi vya kilugha na kitamaduni za kushinda. Ingawa Kiingereza ndiyo lugha isemwayo na wote, mara nyingi ni lazima Kifiji, Kihindi, Kirotuma, au lugha nyinginezo zitumiwe.
Ni lazima pia mifikio mbalimbali itumiwe ili kuzungumza na wale wanaotoka malezi mbalimbali ya kidini. Wengi wa Wafiji wenyeji na wanavisiwa wengine wametoka madhehebu mbalimbali za Kikristo. Wahindi walioko huko ni Wahindu, Waislamu, na Wasikh, huku Wahindu wakiwa wengi zaidi. Kuna makanisa mengi mijini na vijijini, lakini kwenye visiwa viwili vikubwa zaidi vya Fiji, mahekalu mengi ya Wahindu na misikiti ya Waislamu yatoa mandhari tofauti.
Mashahidi wengi wenyeji wamelelewa kusema lugha tatu kubwa—Kiingereza, Kifiji, na Kihindi. Kuwa na ustadi huo ni kwa faida kubwa katika kazi ya “kuvua samaki.” Nyakati nyingine watu hushangaa kusikia Mfiji akisema Kihindi kwa ufasaha na Mhindu akisema Kifiji kwa ufasaha. Kukiwa na tofauti za kitamaduni, kidini, na kilugha za kukabiliana nazo, yahitaji mfikio wenye kubadilika-badilika ili ‘kushiriki habari njema na wengine.’—1 Wakorintho 9:23.
“Kuvua Samaki” Katika Kijiji cha Fiji
Wafiji wenyeji ni watu wenye urafiki, na ukaribishaji-wageni. Ni vigumu kuwazia kwamba zaidi kidogo ya karne moja iliyopita, kulikuwako vita tele vya kikabila. Kwa kweli, Fiji viliitwa Visiwa vya Wala-Watu vilipotembelewa na Wazungu kwa mara ya kwanza. Hatimaye, baada ya kutawazwa kwa chifu mkuu na kugeuka kwake kuwa Mkristo, vita na kula watu kulikwisha. Tofauti za kikabila zapatikana tu miongoni mwa lahaja nyingi zipatikanazo katika mikoa mbalimbali, ingawa wengi waelewa lahaja ya Kibaua.
Kuongezea jiji kuu Suva, kuna majiji mengi kotekote Fiji. Wafiji wengi huishi katika jumuiya za vijijini chini ya udhibiti wa turaga ni koro, au mkuu wa kijiji. Mtu anapoingia kijiji fulani ili kuanza “kuvua samaki,” ni desturi kumfikia mtu huyo na kumwomba ruhusa ya kuzuru bures mbalimbali, au makao ya wenyeji. Ni mara chache sana, sanasana kwa sababu ya upinzani dhidi ya Mashahidi wa Yehova kutoka kwa makasisi fulani wa kijiji, ndipo ruhusa huwa haitolewi. Ikoje kuzuru nyumba ya Mfiji?
Tunapoingia bure, twaketi sakafuni miguu ikiwa imekingamanishwa. Utangulizi wa maneno yenye uangalifu, kama yanayotumiwa ili kunasa upendezi katika nchi za Magharibi, hauhitajiwi hapa. Yeyote anayekuja kusema juu ya Mungu akaribishwa. Anapoombwa achukue Biblia yake, mwenye nyumba huamka kwa utayari, na kwa kusema “tulou” (kunradhi), huenda kwenye rafu na kuchukua nakala ya Biblia ya Kifiji na kusoma kwa hamu maandiko mbalimbali ambayo mhudumu anayezuru ataja. Hata hivyo, mtazamo wa ukaribishaji-wageni na staha ya Wafiji hutokeza ugumu kwa njia tofauti. Utambuzi na busara nyingi yahitajiwa ili kuwavutia wenye nyumba kwenye mazungumzo, kuwatia moyo kufuatia wazo linalozungumzwa, au kuwasaidia kuona uhitaji wa kulinganisha itikadi zao wenyewe na mafundisho ya Biblia.
Kwa kawaida wenye nyumba Wafiji hupendezwa zaidi kuzungumzia mambo ya kimafundisho kuliko kuzungumzia hali au masuala ya kijamii. Kwa kweli, wengi kati ya Mashahidi wa Yehova zaidi ya 1,400 wenye bidii katika Fiji walipendezwa na kweli ya Biblia kutokana na mazungumzo juu ya maswali kama, Helo ni mahali pa aina gani? Ni nani wanaoenda mbinguni? na Je, dunia itaharibiwa? Hata hivyo, kufuatia upendezi ulioonyeshwa hutaka kubadilikana na udumifu. Mara nyingi mtu anaporudi katika wakati uliokubalianwa, yeye hupata mwenye nyumba alienda kwenye teitei (shamba) au mahali penginepo. La, si kwa sababu hawathamini ziara hiyo bali tu kwamba wao hawafuatii wakati sana. Bila shaka, kwa Mashahidi wenyeji, hilo halionekani kuwa jambo lisilo la kawaida. Wao hustahimili kwa kuzuru wakati mwingine. Hakuna majina ya barabara au nambari za nyumba unazoweza kuandika, kwa hiyo mtu ahitaji kumbukumbu nzuri anapofanya ziara za kurudia.
“Kuvua Samaki” kwa Mtindo wa Kipolinesia
Sasa, na twende “kuvua samaki” pamoja na mhudumu asafiriye, au mwangalizi wa mzunguko, azurupo kutaniko dogo katika Rotuma. Kikundi hiki cha visiwa vya volkeno kiko kilometa 500 kaskazini mwa Fiji. Ili kukifikia, twaenda kwa ndege yenye viti 19. Kisiwa kikuu kina ukubwa wa kilometa 50 tu za mraba, kikiwa na jumla ya watu wapatao 3,000. Barabara ya mchanga-mchanga yaenda sambamba na ufuo, ikiunganisha vijiji 20. Rotuma husimamiwa na Fiji lakini kina utamaduni na lugha tofauti. Wakazi wacho wakiwa wa asili ya Polinesia hutofautiana kwa sura na Wafiji ambao ni Wamelanesia. Kidini, wengi wao ama ni Wakatoliki wa Roma ama ni Wamethodisti.
Ndege ishukapo na kuzunguka ipate kutua, twaona uoto mzuri wa kijani-kibichi wa kisiwa. Kuti (matawi ya minazi) zilizo kama manyoya yaweza kuonekana kila mahali. Pana umati mkubwa wa kukaribisha ndege hiyo ya mara moja kwa juma. Miongoni mwao ni kikundi cha Mashahidi. Twasalimiwa kwa uchangamfu, na twapewa madafu kadhaa makubwa yaliyotobolewa matundu ili tuzime kiu yetu.
Baada ya safari fupi, twawasili mahali tutakapolala. Mlo uliopikwa katika jiko lililochimbwa ardhini. Nyama ya nguruwe iliyochomwa, kuku, samaki waliokaangwa, kamba, muhogo wa huko, mnyugwa, vyaandaliwa mbele yetu. Ni karamu na hali za kiparadiso zilizoje chini ya minazi michanga!
Siku inayofuata twazuru watu vijijini, viitwavyo ho’aga kwa Kirotuma. Tufikapo kwenye nyumba ya kwanza, mtoto wa nguruwe ambaye ametoroka kutoka mojapo mazizi atupita akikimbia, huku akitoa kilio chembamba. Mwenye nyumba ametuona tukija na kwa tabasamu afungua mlango, akitusalimu kwa kusema “Noya!” kwa Kirotuma, halafu atukaribisha tuketi. Sahani yenye ndizi zilizoiva yawekwa mbele yetu, na pia twakaribishwa kunywa madafu. Ukaribishaji-wageni ni jambo la maana katika Rotuma.
Hakuna wale wanaoamini kwamba ya Mungu hayajulikani au wanaoamini mageuzi huku. Kila mtu huamini Biblia. Habari kama vile kusudi la Mungu kwa dunia hunasa uangalifu wao kwa urahisi. Mwenye nyumba ashangaa kujua kwamba dunia haitaharibiwa bali itakaliwa na watu waadilifu watakaoishi juu yayo milele. (Zaburi 37:29) Yeye afuata kwa ukaribu maandiko ya Biblia yanayothibitisha jambo hilo yanaposomwa, na akubali kwa hamu fasihi ya Biblia tunayotoa. Tunapojitayarisha kuondoka, atushukuru kwa kumtembelea na kutupa mfuko wa plastiki uliojaa ndizi zilizoiva tunazoweza kula njiani. Mtu aweza kuongeza uzani kwa urahisi akihubiri huku!
Kubadilikana Ili Kufaana na Jumuiya ya Wahindi
Ingawa nchi nyingine nyingi za visiwa vya Pasifiki Kusini zina watu wa jamii mbalimbali, Fiji vinatokeza katika jambo hilo. Kwa kuongezea tamaduni za Wamelanesia, Wamaikronesia, na Wapolinesia kuna ile iliyotoka Asia. Kati ya 1879 na 1916, wafanyakazi wa mkataba kutoka India waliletwa ili kufanya kazi katika mashamba ya miwa. Mpango huo, ulioitwa girmit (makubaliano), ulifanya maelfu ya Wahindi waje Fiji. Wazao wa wafanyakazi hao hufanyiza kiasi kikubwa cha wananchi. Wamedumisha utamaduni wao, lugha yao, na dini yao.
Upande wa demani wa kisiwa kikuu cha Fiji kuna jiji la Lautoka. Hilo ni kitovu cha biashara ya miwa ya Fiji na ni makao ya sehemu kubwa ya idadi ya Wahindi wa nchi hiyo. Washiriki wa makutaniko matatu ya Mashahidi wa Yehova hapa wahitaji kuwa wenye kubadilikana sana katika kazi ya “kuvua samaki.” Mtu anapoenda nyumba kwa nyumba, ni lazima ajitayarishe kubadili habari ikitegemea jamii na dini ya mwenye nyumba. Na tujiunge na kikundi cha Mashahidi wenyeji wanapozuru makao yaliyotapakaa miongoni mwa mashamba ya miwa yaliyo nje tu ya Lautoka.
Tufikiapo nyumba ya kwanza, twaona fito ndefu za mianzi zenye vipande vyekundu vya nguo vilivyofungwa juu kwenye kona ya mbele ya ua. Hilo latambulisha familia hiyo kuwa ya Kihindu. Makao mengi ya Wahindu yamerembeshwa na picha za miungu yao. Wengi wao wana mungu wanayempenda, kama vile Krishna, na mara nyingi kuna kihekalu kidogo.a
Wahindu wengi waamini kwamba dini zote ni nzuri na kwamba ni njia mbalimbali tu za ibada. Hivyo, huenda mwenye nyumba akasikiliza kwa uungwana, akubali fasihi fulani, aandae viburudisho, na kuhisi kwamba amefanya wajibu wake. Kuzusha maswali yafaayo ili kuvuta wenye nyumba kwenye mazungumzo ya maana zaidi, mara nyingi husaidia kujua baadhi ya hadithi ambazo ni sehemu ya itikadi yao. Kwa kielelezo, baada ya kujua kwamba baadhi ya hadithi zao huonyesha miungu yao ikitenda mambo ambayo watu wengi wangetilia shaka, twaweza kuuliza: “Je! ungependa mke (mume) wako awe na mwenendo kama huo?” Kwa kawaida jibu ni: “La, hasha!” Halafu, mtu huyo aweza kuulizwa: “Je! mungu apaswa kutenda hivyo?” Mara nyingi mazungumzo ya aina hiyo hufungua fursa za kuonyesha thamani ya Biblia.
Itikadi juu ya kuzaliwa upya katika kiumbe kingine, sehemu nyingine ya Uhindu, ni habari ya maana ya kuzungumzwa. Mwanamke mmoja Mhindu mwenye elimu ambaye alikuwa amepoteza baba yake katika kifo karibuni aliulizwa: “Je! ungependa kumwona baba yako tena kama alivyokuwa mwanzoni?” Yeye alijibu hivi: “Ndiyo, ingekuwa vizuri ajabu.” Kutokana na itikio lake na mazungumzo yaliyofuata, ilikuwa wazi kwamba hakuridhika na itikadi kwamba baba yake sasa alikuwa hai katika sura nyingine na kwamba asingeweza kumjua tena. Lakini lile fundisho la Biblia zuri ajabu la ufufuo liligusa moyo wake.
Wahindu fulani wana maswali na wanatafuta majibu yenye kuridhisha. Shahidi mmoja alipozuru nyumba ya Mhindu, mtu huyo aliuliza hivi: “Mungu wako anaitwa nani?” Huyo Shahidi akamsomea Zaburi 83:18 na kueleza kwamba jina la Mungu ni Yehova na kwamba Warumi 10:13 yasema kwamba ili kupata wokovu ni lazima tuite juu ya jina hilo. Huyo mtu alivutiwa na alitaka kujua mengi zaidi. Kwa kweli, yeye alikuwa na hamu kubwa ya kuyajua. Alieleza kwamba baba yake, aliyejitoa sana kwa sanamu ya familia yao, aliugua baada ya kuiabudu na akafa muda mfupi baadaye. Jambo hilohilo lilikuwa limempata ndugu yake. Kisha akaongeza: “Sanamu hiyo inatuletea kifo, si uhai. Kwa hiyo ni lazima kuwe kuna jambo lisilofaa kwa kuiabudu. Labda Mungu huyu, Yehova, aweza kutusaidia kupata njia ya uhai.” Basi funzo la Biblia lilianzishwa pamoja naye, mke wake, na watoto wake wawili. Walifanya maendeleo ya haraka na upesi wakabatizwa. Wameacha sanamu zao na sasa wanatembea katika njia ya Yehova, Mungu wa uhai.
Halafu twaja kwenye nyumba ya familia ya Waislamu. Roho ileile ya ukaribishaji-wageni yaonyeshwa, na upesi twaketi huku tukiwa na vinywaji baridi mikononi mwetu. Hatuoni picha zozote za kidini ukutani isipokuwa maandishi ya Kiarabu yakiwa kwenye fremu ndogo. Twataja kwamba kuna mlingano kati ya Biblia na Qurani, yaani, Abrahamu aliyekuwa mzee wa ukoo, na kwamba Mungu alimwahidi Abrahamu kwamba kupitia mbegu yake mataifa yote yangebarikiwa. Ahadi hiyo itatimizwa katika Yesu Kristo, Mwanae. Waislamu fulani watapinga wazo la kwamba Mungu ana mwana. Hivyo, twaeleza kwamba kama vile mtu wa kwanza, Adamu, aitwavyo mwana wa Mungu kwa sababu ya yeye kuumbwa na Mungu, kwa njia iyo hiyo, Yesu ni Mwana wa Mungu. Mungu hahitaji mke halisi ili kutokeza wana hao. Kwa sababu Waislamu hawaamini fundisho la Utatu, twatumia habari hiyo tunayokubaliana ili kuonyesha kwamba Yehova Mungu ni mkuu zaidi ya wote.
Kufikia sasa ni wakati wa chakula cha mchana, na washiriki wa kikundi chetu wanarudi barabarani, kutoka mashamba ya miwa, ili kungojea basi la kurudi mjini. Ingawa wote wamechoka kidogo, wamesisimuka kwa sababu ya kazi ya asubuhi ya “kuvua samaki.” Jitihada iliyofanywa ya kubadilikana ili kufaana na hali tofauti na itikadi tulizokabili ilistahili.
Bahari na matumbawe ya Fiji yamejaa samaki wa aina nyingi. Ili kufanikiwa, gonedau (mvuvi) Mfiji ahitaji awe stadi katika kazi yake. Ni vivyo hivyo na kazi ya “kuvua samaki” ambayo Yesu Kristo aliwagawia wanafunzi wake. Ni lazima Wakristo “wavuvi wa watu” wawe stadi, wakibadilisha utoaji wao na hoja zao zifae itikadi mbalimbali za watu. (Mathayo 4:19) Hilo kwa kweli lahitajiwa katika Fiji. Na matokeo ni dhahiri kwenye mikusanyiko ya Mashahidi wa Yehova ya kila mwaka, ambapo Wafiji, Wahindi, Warotuma, na watu wa malezi ya kikabila yaliyochangamana, waabudu Yehova Mungu kwa umoja. Ndiyo, baraka zake zimo juu ya kazi ya “kuvua samaki” katika bahari za Fiji.
[Maelezo ya Chini]
a Ona kitabu Jitihada ya Ainabinadamu ya Kutafuta Mungu, kilichotangazwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc., kurasa 115-17.
[Ramani katika ukurasa wa 23]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Viti Levu
Vanua Levu
Suva
Lautoka
Nandi
0 Kilometa 100
0 100 maili
Digrii 18
Digrii 180
[Picha katika ukurasa wa 24]
“Bure,” au kao la kienyeji
[Picha katika ukurasa wa 24]
Hekalu la Kihindu katika Fiji
[Picha katika ukurasa wa 25]
“Kuvua” watu kwa mafanikio katika Fiji
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 24]
Fiji Visitors Bureau