“Sijapata Kamwe Kuona Lolote Kama Hili!”
KATIKA mwaka 1993 ofisi ya Watch Tower Society katika Argentina iliulizwa kutuma wajumbe elfu moja kwenda Santiago, Chile, kwa ajili ya “Ufundishaji wa Kimungu” Mkusanyiko wa Wilaya wa siku nne wa Mashahidi wa Yehova. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwamba Mashahidi Waargentina walikuwa wameombwa kusafiri wakiwa kikundi kikubwa kwenda kwenye mkusanyiko wa kigeni.a Itikio lilikuwa nini? Zaidi ya maombi 8,500 yalipelekwa kwa wingi, ambapo wajumbe 1,039 walichaguliwa.
Jumla ya mabasi 14 yalikodiwa ili kufunga safari hii ya kilometa 1,400 kutoka Buenos Aires hadi Santiago. Safari hii ya saa 26 iliongezewa uvutio na mandhari yenye kutazamisha. Wakivuka Milima ya Andes, wajumbe hao walipita karibu na Aconcagua, wenye kimo cha meta 6,960 ukiwa kilele cha juu zaidi katika Kizio cha Magharibi. Wenye kukumbukwa hasa ni ule mteremko mkali na wenye kupinda-pinda kuingia Chile. Madereva walipigiwa makofi sana kwa ustadi wao katika kuendesha mabasi kwenye barabara yenye miinuko na mipindo-pindo!
Hata hivyo, tamasha yenye kupendeza zaidi, ilikuwa ipatikane katika mkusanyiko wenyewe. Katika ulimwengu wenye ugomvi wa kitaifa na mabishano ya kikabila, jinsi ilivyoburudisha kuona umati uliounganika wa watu 80,000 kutoka nchi 24 wakihudhuria—kwa kweli udugu wa kimataifa! Baada ya kujionea wao wenyewe umoja miongoni mwa wakusanyikaji, madereva fulani wa basi walionyesha upendezi katika kujifunza zaidi juu ya Mashahidi wa Yehova. “Sijapata kamwe kuona lolote kama hili!” mmoja wao akapaaza sauti kwa mshangao.
[Maelezo ya Chini]
a Vizuizi vya kiserikali katika Argentina kutoka mwaka 1949 hadi 1982 vilifanya jambo hilo lisiwezekane.