Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w95 6/15 kur. 24-27
  • Kukwea Mlima Mrefu Zaidi Kuliko Ile ya Himalaya

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kukwea Mlima Mrefu Zaidi Kuliko Ile ya Himalaya
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1995
  • Vichwa vidogo
  • Nepal—Ufalme wa Mlima
  • Mianzo Midogo
  • Mpanuko Yajapokuwa Matatizo
  • Nepal Leo
  • Kwea Juu Zaidi Kuliko Milima ya Himalaya
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1995
w95 6/15 kur. 24-27

Kukwea Mlima Mrefu Zaidi Kuliko Ile ya Himalaya

MILIMA ya Himalaya! Maneno haya yanakufanya uwazie nini? Je, ni vilele virefu ajabu vyenye barafu na pepo kali zenye nguvu? Je, unahisi msisimuko wa ushindi ukiwa umesimama kwenye kilele cha mlima ulio mrefu zaidi duniani? Kwa wengi wetu, kukwea Mlima Everest, katika Milima ya Himalaya katika Nepal, ni jambo lisilowezekana. Hata hivyo, leo watu wengi katika Nepal wanakwea mlima ulio mrefu zaidi kuliko ile ya Himalaya! Kabla ya kuchunguza safari hii ya kwenda kwenye mlima mtukufu, ebu tuangalie Ufalme wa Nepal ulio mdogo lakini wenye kupendeza.

Nepal—Ufalme wa Mlima

Ufalme wa Nepal ni ufalme usio wa kawaida kwa sababu ni mmoja wa falme chache zilizobaki ulimwenguni na pia kwa sababu huo ni ufalme wa kidini. Nepal ndilo taifa la Kihindu pekee ulimwenguni. Idadi kubwa ya wakazi wake milioni 20 ni Wahindu. Hata hivyo, watu walo wametokana na makabila mengi mbalimbali. Wale waishio upande wa kaskazini wenye milima-milima hasa ni mchanganyiko wa Watibet na Burma, na katika nyanda za kusini, watu hasa ni wa mchanganyiko wa Wahindi wa Waarya. Kinepal ndiyo lugha ya taifa ya nchi hiyo na ndiyo lugha ya asili ya watu karibu asilimia 60. Waliobaki huzungumza zaidi ya lugha 18 mbalimbali.

Nepal ni kama ina umbo la pembe nne za mraba, ikiwa kilometa 880 kutoka mashariki hadi magharibi na kilometa 200 kutoka kaskazini hadi kusini. Milima ya Himalaya yenye kuvutia sana, inayofanyiza mpaka wa upande wa kaskazini, inatia ndani Mlima Everest, wenye kilele kirefu zaidi kupita vyote ulimwenguni cha meta 8,848, na vilele vingine vinane vyenye vimo vinavyozidi meta 8,000. Katika Nepal ya kati kuna milima mifupi kidogo na maziwa ya maji na mabonde. Mbali kusini, kwenye mpaka wa India, kuna Tarai yenye rutuba, mahali pa ukulima hasa.

Jiji kuu, Kathmandu, lililo kwenye sehemu ya kati, kwa kweli ni mahali pa kufurahisha watalii. Lina mipango ya kupelekwa kwa ndege juu ya milima hiyo mitukufu, ya kwenda kwenye mbuga za wanyama, na mambo mengi ya kujionea. Wakati mwingine Nepal huitwa bonde la miungu kwa sababu dini ina fungu kubwa katika maisha ya watu wayo. Dini pia ndiyo sababu inayofanya mamilioni ulimwenguni pote kukwea “mlima” ulio mrefu zaidi kuliko milima ya Himalaya.

Karibu miaka 2,700 iliyopita, nabii Mwebrania Isaya alipuliziwa kutabiri kwamba “katika siku za mwisho, mlima wa nyumba ya BWANA utawekwa imara juu ya milima . . . Na mataifa mengi watakwenda na kusema, Njoni, twende juu mlimani kwa BWANA . . . naye atatufundisha njia zake, nasi tutakwenda katika mapito yake.” (Isaya 2:2, 3) Hapa ibada safi iliyoinuliwa ya Yehova, Muumba na Mtawala Mwenye Enzi Kuu ya ulimwengu wote mzima, inafananishwa na mlima, ulioinuliwa juu sana ya aina nyinginezo za ibada zinazofanana na mlima. Ndiyo mada ya habari ya kazi ya kuelimisha ya ulimwenguni pote inayosaidia watu wenye njaa ya kweli kujifunza juu ya njia za Yehova. Kazi hii ilianzishwaje Nepal?

Mianzo Midogo

Mwanajeshi mmoja katika Jeshi la Uingereza katika Vita ya Ulimwengu ya 2 alikuwa akitafuta dini ya kweli. Wazazi wake waliokuwa Wahindu wa Nepal walikuwa wamebadili dini na kufuata Ukatoliki. Alipokuwa akikua, aliona utupu wa ibada ya sanamu, akakataa mafundisho kama lile la moto wa helo, akaanza kuchunguza itikadi za makanisa ya Kiprotestanti. Lakini hakuridhika.

Alipokamatwa na Wajapani katika ile iliyokuwa Rangoon, Burma, mwanajeshi huyu alisali kwamba ikiwezekana aokoke ugumu wa kambi za kazi ngumu ili aendelee kutafuta ibada ya kweli. Baadaye, aliweza kutoroka waliomkamata akasaidiwa na mwalimu wa shule ambamo nyumbani mwake alipata kijitabu Where Are the Dead?, kilichoandikwa na J. F. Rutherford. Alipotambua ukweli, alikubali kwa hamu nyingi kujifunza wakati Mashahidi wa Yehova walipomtembelea huko Rangoon katika 1947. Baada ya miezi michache, alibatizwa, na baada ya muda mfupi mkeye mchanga akabatizwa pia. Waliamua kurudi India, na kukaa nyumbani kwao Kalimpong, kwenye milima ya kaskazini-mashariki. Hapo watoto wao wawili walizaliwa na kuelimishwa. Katika Machi 1970, walihamia Kathmandu.

Katiba ya Nepal ilikataza uongofu. Yeyote aliyepatikana akiendesha ile iliyokuwa ikiitwa dini ya kigeni alipaswa kufungwa jela miaka saba, na mtu aliyejiunga na dini kama hiyo angehukumiwa kifungo cha miaka mitatu gerezani pamoja na faini kubwa. Hivyo kutoa ushahidi kulipaswa kufanywe kwa busara. Huduma ya nyumba kwa nyumba ilimaanisha kubisha nyumba fulani, kisha kwenda katika eneo lingine na kubisha mlango mwingine huko. Inaeleweka kwamba, ushahidi wa vivi hivi ulichukua nafasi kubwa katika kuhubiri habari njema.

Maendeleo yalikuwa ya polepole. Kukiwa na idadi ya watu karibu milioni kumi, shamba hilo lilionekana lenye kuvunja moyo. Mbegu za kweli zilipandwa familia hii pekee ilipotolea ushahidi marafiki, watu waliowajua, waajiri, na waajiriwa wenzi. Walifanya mikutano kwa ukawaida nyumbani kwao na kuwaalika wenye kupendezwa wajiunge nao. Mwishowe katika Machi 1974, baada ya miaka minne ya kupanda na kutia maji kwa bidii, tunda la kwanza kutoka Nepal likatokea—nalo lilitoka sehemu isiyotazamiwa kama nini!

Alipokuwa akitembelea nyumba fulani, mhubiri alizungumza na mtu mmoja tajiri aliyekuwa katibu wa mshiriki fulani wa familia ya kifalme. “Zungumza na mwanangu,” mtu huyo akasema. Mwanaye alikubali funzo la Biblia. Baada ya muda alibadili kazi yake, kwa kuwa alifanya kazi katika jumba la kamari. Baba yake, aliyeshikilia sana dini ya Hindu, alimpinga. Na bado, huyu kijana mwanamume alichukua msimamo wake kwa Yehova. Tokeo likawa nini? Baba yake baadaye akaacha kumpinga, na kikundi cha watu wa ukoo wa karibu kikakubali kweli ya Biblia. Sasa yeye anatumika akiwa mzee wa kutaniko la Kikristo.

Ili kibaki kikiwa na nguvu kiroho na kutii amri ya Kimaandiko ya kutoacha kukutanika pamoja, kikundi kidogo cha Kathmandu kilifanya mikutano kwa ukawaida katika nyumba ya binafsi. Lakini sanasana, ndugu hawakuweza kufika kwenye makusanyiko makubwa. Wale walioweza kufanya hivyo walisafiri hadi India kwa makusanyiko—safari ndefu na ya gharama kubwa juu ya milima.

Lilikuwa tukio lenye shangwe kama nini wakati programu yote ya mkusanyiko wa wilaya ilipofanywa katika nyumba ambayo walifanyia mikutano! Ebu wazia ndugu wanne, kutia ndani mshiriki wa tawi la India, wakiendesha programu hiyo yote! Hata drama ya Biblia ilifanywa. Jinsi gani? Picha za slaidi zilikuwa zimepigwa kwenye majaribio ya mavazi ya drama katika India. Katika Nepal, slaidi hizi zilionyeshwa kwenye kiwambo, zikiandamana na maneno katika kaseti. Wasikilizaji waliipenda. Wasikilizaji hao walikuwa wengi kiasi gani? Watu 18!

Msaada wa kazi ya kuhubiri kutoka nje ya nchi hiyo ulikuwa haba. Kazi ya mishonari haikuwezekana, na haikuwa rahisi kwa wageni kupata kazi ya kuajiriwa. Hata hivyo, Mashahidi wawili Wahindi, waliweza kupata kazi katika Nepal nyakati tofauti-tofauti, wakakaa kwa miaka kadhaa katika Kathmandu na kusaidia kuimarisha kutaniko hilo lililokuwa jipya. Kufikia 1976 kulikuwa na wahubiri wa Ufalme 17 katika Kathmandu. Katika 1985 ndugu walijenga Jumba la Ufalme lao. Wakati Jumba la Ufalme hilo lilipomalizika, mikusanyiko ya wilaya ya kila mwaka, pamoja na makusanyiko mengine, yalianza kufanywa huko kwa ukawaida. Jumba hilo lilikuwa kwelikweli kitovu cha ibada safi katika eneo hilo la mbali, lenye milima.

Mpanuko Yajapokuwa Matatizo

Katika miaka hiyo ya mapema, kazi ya kuhubiri, iliyofanywa kwa busara sana, haikuwa imejulikana sana na wenye mamlaka. Ingawa hivyo, kuelekea mwisho wa 1984, makatazo yalianza kuwekwa. Ndugu mmoja na dada watatu walishikwa na kuwekwa korokoroni kwa siku nne kabla ya kufunguliwa na kuonywa wasiendelee na utendaji wao. Katika kijiji kimoja, watu tisa walishikwa walipokuwa wakijifunza Biblia nyumbani kwao. Sita walifungwa jela kwa siku 43. Wengine kadhaa walishikwa, lakini hakuna hatua ya kisheria iliyochukuliwa.

Karibuni kama mwaka wa 1989, ndugu na dada wote katika Funzo la Kitabu la Kutaniko walishikwa, wakazuiliwa kwa siku tatu, kisha wakaachiliwa. Nyakati nyingine, waliambiwa watie sahihi taarifa iliyosema kwamba hawatahubiri. Walikataa. Wengine waliachiliwa baada tu ya kutia sahihi taarifa ya kwamba wangekuwa tayari kukabili adhabu yoyote ile ambayo ingetokea kama wangeshikwa wakihubiri tena.

Yajapokuwa magumu kama hayo, ndugu waliendelea kuhubiri habari njema za Ufalme kwa bidii. Mathalani, katika 1985, mwaka mmoja baada ya kuingilia mambo kwa serikali kuanza, kulikuwa na ongezeko la asilimia 21 la idadi ya wahubiri. Wahubiri hao 35 walitumia muda wa saa 20 kila mwezi wakizungumza na wengine juu ya ibada safi.

Kadiri wakati ulivyopita, pepo za mabadiliko ya kisiasa zilianza kuvuma katika Nepal. Maofisa wa serikali wakaanza kutambua kwamba Mashahidi wa Yehova si tisho. Kwa kweli, kazi yao ya kuelimisha Biblia ilifaidi na kujenga watu, ikiwafanya kuwa wananchi bora. Maofisa waliona kwamba unyoofu, kazi ya bidii, na tabia nzuri za adili zilikaziwa zikiwa matakwa ya msingi kwa waabudu wa Yehova.

Ushahidi mzuri ulitolewa wakati mwanamke mmoja aliyekuwa ameshikilia sana dini ya Hindu alipokuja kuwa Shahidi na kukataa kutiwa damu mishipani. Madaktari walishangazwa na uamuzi wake, wenye ufahamu na uthabiti. Mwanamke huyu alisaidiwa kujifunza Biblia kwa kutumia broshua Furahia Milele Maisha Duniani! Ajapopingwa na kudhihakiwa na familia yake, alibatizwa katika 1990 akikaribia umri wa miaka 70. Baadaye alivunjika mguu na, akiugua magonjwa mengine pia, ilibidi afanyiwe upasuaji mkubwa. Kwa majuma mawili alikinza mkazo wa madaktari na watu wa ukoo wa kukubali kutiwa damu. Mwishowe, madaktari wa upasuaji walimfanyia upasuaji uliofaulu bila kutumia damu. Ingawa sasa hawezi kutembea kama kawaida, dada huyu mwaminifu hukaa kwenye lango lake kila asubuhi na kukaribisha wapita njia wakae naye na kusikia habari njema zenye kupendeza.

Nepal Leo

Nepal iko vipi leo? Mashahidi wa Yehova hufurahia uhuru wa ibada wa kadiri fulani kama ilivyo na ndugu zao ulimwenguni pote. Tangu wakati mtu mmoja au wawili wenye kukwea kitamathali walipojiunga na wakweao mlima wa ibada ya kweli, idadi inayoongezeka ya watu imesema, “Njoni, twende juu mlimani kwa BWANA.” Kufikia 1989 kulikuwa na idadi ya watu 43 kila mwezi walioshiriki katika kazi ya kuhubiri, na 204 walihudhuria Ukumbusho wa kifo cha Kristo mwaka huo.

Kisha, kama ilivyoahidiwa, Yehova akaanza kuharakisha kukusanya watafutaji kweli kwenye nyumba yake. (Isaya 60:22) Muda usio mrefu uliopita kutaniko la pili lilifanyizwa katika Kathmandu, na sasa kuna vikundi viwili vilivyo peke yavyo nje ya jiji hilo. Katika Aprili 1994, kulikuwa na Wakristo 153 walioripoti kazi ya kuhubiri—ongezeko la asilimia 350 katika miaka mitano! Waliongoza mafunzo ya Biblia nyumbani 386 pamoja na watu wenye kupendezwa. Kwenye Ukumbusho 1994, kulikuwa na hudhurio lenye kusisimua la watu 580. Wakati wa siku ya kusanyiko la pekee, watu 635 walijaza jumba, na 20 walijitoa kwa ubatizo. Hivyo maongezeko makubwa yanayofurahiwa na Mashahidi wa Yehova ulimwenguni pote yanatokea pia katika Nepal iliyo ndogo.

Katika miaka ya karibuni kiasi cha fasihi inayotolewa kwa lugha ya Kinepal kimeongezeka sana, ikisaidia wanyenyekevu kuishika kweli imara. Watafsiri walizoezwa katika ofisi ya tawi ya India katika mbinu za utafsiri na kutumia kompyuta sasa wanatumika wakati wote katika Kathmandu. Wakiwa tayari kwa mpanuko, wapandaji milima wa kitheokrasi wa Nepal wanafanya maendeleo!

Kwea Juu Zaidi Kuliko Milima ya Himalaya

Wewe pia unaweza kuonea shangwe kukwea juu ya mlima ulio juu kuliko Himalaya. Ukifanya hivyo, utakuwa ukijiunga, si na wale walioko Nepal pekee, bali pia mamilioni ya watu “wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha.” (Ufunuo 7:9) Pamoja nao, utafurahia kuagizwa na Muumba wa milima mitukufu kama ile ya Nepal. Wewe utaona Muumba ‘akirekebisha mambo,’ nawe utaweza kutazamia kuishi milele katika dunia iliyosafishwa na kurembeshwa.—Isaya 2:4, NW.

[Ramani katika ukurasa wa 24]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Kathmandu

Mlima Everest

[Picha katika ukurasa wa25]

Nje ya Jumba la Ufalme katika Kathmandu

[Picha katika ukurasa wa26]

Wanepal wengi wananufaika kutokana na mafunzo ya Biblia

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki