Kesi Dhidi ya Mashahidi wa Yehova Yaamuliwa
BAADA ya kuahirishwa mara nyingi, Mahakama ya Rufani katika Thessalonica, Ugiriki, mwishowe iliketi katika Juni 8, 1995, kusikiliza kesi dhidi ya wanawake wanne walio Mashahidi wa Yehova. Walishtakiwa juu ya kosa gani? Kugeuza watu kidini, jambo ambalo sheria ya Ugiriki ilikuwa imekataza kwa zaidi ya miongo mitano.
Hata hivyo, kufikia wakati mahakama ilipoketi, shahidi mkuu wa upande wa mashtaka—kasisi aliyechochea hiyo kesi dhidi ya hao wanawake wanne—tayari alikuwa amekufa. Kasisi mwingine alijaribu kutoa ushahidi kwa niaba yake, lakini mahakama haikukubali ushahidi wake. Hivyo, haishangazi kwamba kusikilizwa kwa kesi hiyo kulichukua muda wa dakika 15 pekee! Hakimu aliwahoji mashahidi wengine wa upande wa mashtaka, akapata kwamba washtakiwa hawakuwa na hatia ya zoea la kugeuza watu kidini kinyume cha sheria. Uamuzi huo waonyesha kwamba mahakama za Ugiriki ziko tayari kuheshimu na kufuata uamuzi uliofikiwa katika 1993 na Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu.
Lilikuwa jambo la kushangaza hasa kuona hao wanawake watatu waliotoa ushahidi kwa upande wa mashtaka wakiwaendea hao Mashahidi walioshtakiwa, wakiwapongeza kwa moyo wote. “Twaomba msamaha kwa mambo hayo yote yaliyotendeka,” mmoja wao akasema. Akaongeza hivi: “Halikuwa kosa letu. Kasisi alitulazimisha kuwashtaki. Kwa kuwa sasa amekufa, tunataka mje kijijini mwetu na nyumbani mwetu.”
Hivyo, kwa mara nyingine tena Yehova ametoa ushindi wa ajabu kwa watu wake katika Ugiriki. Sheria zinazokataza kubadili watu kidini zilipitishwa katika Ugiriki katika 1938 na 1939. Katika 1993 Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu iliamua kwamba kutumia sheria hii kunyanyasa Mashahidi wa Yehova ni kosa.—Ona Mnara wa Mlinzi, Septemba 1, 1993, kurasa 27-31.