Mbona hizo Siri Zote?
“HAKUNA kitu chenye kulemea kama siri.” Au angalau ndivyo idaivyo mithali ya Kifaransa. Je, hilo lingeweza kueleza ni kwa nini sisi huhisi vizuri tujuapo siri fulani lakini twahisi kuvunjika moyo nyakati nyingine tusipoweza kuzungumza juu yayo? Hata hivyo, kwa karne nyingi watu wengi wamekubali kuweka siri, wakiungana wenyewe ili kufanyiza sosaiti za siri zenye kufuatia mradi uleule.
Miongoni mwa sosaiti hizo za siri za mapema zaidi mlikuwemo madhehebu za mafumbo zilizopatikana Misri, Ugiriki, na Roma. Baadaye baadhi ya sosaiti hizo zilikengeuka kutoka kwa uvutano wa kidini na kutwaa kisiri maelekeo ya kisiasa, kiuchumi, na kijamii. Kwa kielelezo, vyama vilipofanyizwa katika Ulaya ya enzi za kati, washiriki wavyo waligeukia siri kimsingi kwa ajili ya usalama wa kibinafsi wa kiuchumi.
Sosaiti za siri katika nyakati za kisasa mara nyingi zimefanyizwa kwa sababu zenye kuheshimika, labda kwa “makusudi mazuri na ya kijamii,” kulingana na Encyclopædia Britannica, na ili “kuendeleza programu za fadhili na za kielimu.” Mashirika fulani ya kirafiki, klabu za vijana, klabu za kijamii, na sosaiti nyingine pia ni za siri, au angalau ni za siri kwa sehemu. Kwa ujumla, sosaiti hizo huwa zisizo na miradi yenye kudhuru, washiriki wazo wakiona siri kuwa yenye kusisimua tu. Kuingizwa katika sosaiti hizo kisiri kuna uvutio wenye nguvu wa kihisia-moyo nao huimarisha vifungo vya urafiki na muungano. Washiriki hupata hisia ya kuwa washiriki na huhisi kwamba wana kusudi. Sosaiti za siri za aina hiyo kwa kawaida hazihatarishi wasio washiriki hata kidogo. Wasio washiriki hawapati hasara yoyote kwa kutojua hizo siri.
Siri Iashiriapo Hatari
Sosaiti mbalimbali za siri zina viwango vinavyotofautiana vya siri. Lakini sosaiti zilizo na “siri ndani ya siri,” kama kichapo Encyclopædia Britannica kielezavyo, hutokeza hatari mahususi. Chaeleza kwamba “kwa kutumia majina ya ziada ya kujibandika, masaibu au ufunuo mbalimbali,” washiriki wa ngazi za juu hufaulu “kujitenga,” hivyo wakichochea “wale wa ngazi za chini watie jitihada ihitajiwayo ili kufikia kiwango kilichokwezwa.” Hatari iliyo katika sosaiti hizo inaonekana wazi. Walio katika ngazi za chini huenda wasijue hata kidogo malengo ya hilo shirika wakiwa hawajapata kufanya maendeleo kufikia kiwango hicho cha ujuzi. Ni rahisi kuhusika katika sosaiti ambayo makusudi yayo na njia zayo za kuyafikia zatambulika kwa sehemu tu na, kwa kweli, labda hata hiyo sosaiti haijakufafanulia waziwazi makusudi yayo. Lakini mtu ambaye tayari ameingizwa katika sosaiti kama hiyo, huenda baadaye akaona ugumu wa kujiweka huru; akiwa amefungwa kitamathali kwa minyororo ya siri.
Hata hivyo, siri huashiria hatari kubwa hata zaidi sosaiti ifuatiapo miradi isiyo halali au ya uhalifu na hivyo kujaribu kuficha kuweko kwayo kwenyewe. Au ikiwa kuweko kwayo na makusudi yayo ya ujumla yajulikana, yaweza kujaribu kuweka washiriki wayo na mipango yayo ya punde tu ikiwa siri. Hiyo ni kweli kuhusu sosaiti za maharamia wanaochochewa sana ambao wanaushtua ulimwengu pindi kwa pindi kwa mashambulio yao ya uharamia.
Ndiyo, siri yaweza kuwa hatari, kwa watu mmoja-mmoja na pia kwa jamii nzima. Fikiria yale magenge ya siri ya matineja ambayo yanavizia kijeuri wahasiriwa wasio na hatia, mashirika ya wahalifu kama lile la Mafia la siri, sosaiti za mamlaka kuu ya watu weupe kama vile Ku Klux Klan,a kwa kuongezea zile sosaiti nyingi za maharamia ulimwenguni pote zinazoendelea kuzuia jitihada za kupata amani na usalama wa ulimwengu.
Zakusudia Kufanya Nini Sasa?
Miaka ya 1950, likiwa zaotuka la Vita Baridi, sosaiti za siri zilipangwa katika nchi nyingi za Ulaya Magharibi ili ziwe msingi wa kupinga harakati mbalimbali iwapo Wasovieti wangejaribu kushinda Ulaya Magharibi. Kwa kielelezo, kulingana na gazeti-habari la Kijerumani Focus, “vituo 79 vya silaha vya siri” vilianzishwa huko Austria katika kipindi hicho. Sosaiti hizo hata hazikujulikana na nchi zote za Ulaya. Gazeti-habari liliripoti hivi kwa uhalisi mapema katika miaka ya 1990: “Lisilojulikana bado ni idadi ya mashirika hayo ambayo bado yanatenda leo na mambo ambayo yamekuwa yakikusudia kufanya hivi karibuni.”
Ndiyo, kwa kweli. Ni nani awezaye kujua kwa kweli ni sosaiti ngapi za siri ambazo wakati huu huenda zikawa tisho kubwa zaidi ya lolote ambalo yeyote kati yetu aweza kuwazia?
[Maelezo ya Chini]
a Sosaiti hiyo ya Marekani ilidumisha baadhi ya mambo ya kidini ya sosaiti za siri za mapema ikitumia msalaba wenye kuwaka moto ukiwa ishara yazo. Zamani, ilifanya uvamizi mbalimbali wakati wa usiku, washiriki wayo wakiwa wamevalia kanzu na shiti nyeupe wakitoa hasira yao kali dhidi ya watu weusi, Wakatoliki, Wayahudi, wageni, na vyama vya wafanyakazi.