Haki ya Kweli Lini na Jinsi Gani?
WASIO na hatia hapaswi kuwa na sababu yoyote ya kuhofu haki ya kweli. Kwa kweli, karibu kila mahali raia wana sababu ya kushukuru ikiwa nchi yao ina mfumo wa sheria ambao hujaribu kuhakikisha kwamba kuna haki. Mfumo wa namna hiyo huhusisha muundo fulani wa sheria, jeshi la polisi ili kuzitekeleza, na mahakama za kutekeleza haki. Wakristo wa kweli hustahi mfumo wa kihukumu wa sehemu ambamo huishi, kwa kupatana na onyo la upole la Biblia la “[kuwa] katika ujitiisho kwa mamlaka zilizo kubwa.”—Waroma 13:1-7.
Hata hivyo, mifumo ya kihukumu katika nchi mbalimbali imefanya makosa yenye kudhuru na yenye kuaibisha.a Badala ya kuwaadhibu wenye hatia na kuwalinda wasio na hatia, nyakati nyingine watu wasio na hatia wameadhibiwa kwa ajili ya uhalifu ambao hawakuufanya. Watu wengine wamekaa gerezani kwa muda wa miaka mingi, wakiachiliwa tu kabla ya kukamilisha kifungo chao kukiwa na shaka kubwa kama walikuwa na hatia na kama kupatikana kwao na hatia kulikuwa halali. Kwa sababu hiyo, wengi wanauliza, Je, kutakuwako na haki ya kweli kwa ajili ya kila mtu? Ikiwa ndivyo, ni lini na jinsi gani? Ni nani tuwezaye kutumaini awalinde wasio na hatia? Na kuna tumaini gani kwa ajili ya wahasiriwa wa ukosefu wa haki?
Haki Yenye Kasoro
Katika miaka ya 1980, Ujerumani ilishuhudia “mojawapo ya taratibu za kisheria zenye kushtusha zaidi za kipindi cha baada ya vita,” wakati ambapo mama fulani alihukumiwa kifungo cha maisha kwa kuua kimakusudi binti zake wawili. Hata hivyo, miaka kadhaa baadaye, ushahidi uliotolewa dhidi yake ulichunguzwa tena, naye akaachiliwa akisubiri kufanyiwa kesi upya. Gazeti la habari la Die Zeit liliripoti katika mwaka wa 1995 kwamba, hukumu ya kwanza “ingeweza kuthibitika kuwa kosa la kihukumu.” Hata kufikia wakati wa kuandika makala hii, mwanamke huyo alikuwa amekaa gerezani muda wa miaka tisa akiwa hana uhakika kama yeye ana hatia au hana hatia.
Jioni moja katika Novemba 1974, sehemu ya kati ya jiji la Birmingham, Uingereza, ilisukwasukwa na mlipuko wa mabomu mawili yaliyowaua watu 21. Lilikuwa tukio ambalo “hakuna mtu yeyote katika Birmingham atalisahau kamwe,” akaandika Chris Mullen, ambaye ni Mbunge. Baadaye, “wanaume sita ambao hawakuhusika na mlipuko huo walipatikana na hatia ya uuaji kimakusudi ulio mkubwa zaidi katika historia ya Uingereza.” Baadaye kupatikana kwao na hatia kulifutiliwa mbali—lakini baada tu ya wanaume hao kukaa gerezani kwa muda wa miaka 16!
Mshauri wa mambo ya sheria, Ken Crispin aliripoti kuhusu kesi ambayo “katika historia ya sheria ya Australia, ilivutia akili za umma katika njia ya pekee.” Familia fulani ilikuwa imepiga kambi karibu na mwamba uitwao Ayers Rock, wakati mtoto wao mchanga alipotoweka, asionekane tena kamwe. Mama yake alishtakiwa kuua kimakusudi, akapatikana na hatia, na kuhukumiwa kifungo cha maisha. Katika mwaka wa 1987, baada ya kufungwa jela kwa muda wa miaka zaidi ya mitatu, uchunguzi rasmi uligundua kwamba ushahidi uliotolewa dhidi yake haungetosha kumtia hatiani. Aliachiliwa na kusamehewa.
Mwanamke mwenye umri wa miaka 18 aliyekuwa akiishi kusini mwa Marekani, aliuawa mwaka wa 1986. Mwanamume wa makamo alishtakiwa, akapatikana na hatia, na kuhukumiwa kifo. Alikaa katika chumba cha wanaohukumiwa kifo kwa muda wa miaka sita kabla ya kuthibitishwa kwamba, hakuwa amehusika na huo uhalifu.
Je, hivi ni vielelezo nadra vya makosa ya kihukumu? David Rudovsky wa Chuo Kikuu cha Shule ya Sheria ya Pennsylvania asema hivi: “Nimekuwa katika mfumo wa sheria kwa miaka ipatayo 25 na nimeona kesi nyingi sana. Ningesema kwamba wale wenye kupatikana na hatia na ambao kwa kweli hawana hatia . . . ningewakadiria kuwa kati ya asilimia tano na asilimia 10.” Crispin auliza swali hili lenye kusumbua: “Je, kunao watu wengine wasio na hatia ambao wanaketi kwa kuvunjika moyo katika seli za magereza?” Je, makosa kama hayo yenye kuhuzunisha yanawezaje kutokea?
Mifumo ya Kihukumu ya Kibinadamu—Yenye Udhaifu Mbalimbali wa Kibinadamu
“Hakuna mfumo wa kibinadamu uwezao kutarajia kuwa mkamilifu,” ikakazia Mahakama ya Rufani ya Uingereza katika mwaka wa 1991. Mfumo wa kihukumu waweza kuwa tu wenye haki na wenye kutegemeka sawa na vile watu wenye kuubuni na kuutekeleza walivyo. Watu wana mielekeo ya kukosea, kutofuata haki, na ubaguzi. Kwa sababu hiyo, haipasi kushangaza kwamba mifumo ya kihukumu ya mwanadamu hudhihirisha dosari hizohizo. Fikiria maoni yafuatayo.
Kulingana na Hakimu Rolf Bender wa Ujerumani, katika asilimia 95 ya kesi zote za uhalifu, taarifa kutoka kwa wenye kutoa ushahidi zaweza kutumiwa kuamua kesi sawa na vile ushahidi utumiwavyo. Lakini je, watu hao wenye kutoa ushahidi mahakamani huwa wenye kutegemeka sikuzote? Hakimu Bender hafikiri hivyo. Yeye akadiria kwamba nusu ya wenye kutoa ushahidi wanaoenda mahakamani husema uwongo. Bernd Schünemann, profesa kamili wa sheria ya jinai kwenye Chuo Kikuu cha Munich, Ujerumani, alikuwa na maoni hayohayo. Katika mahojiano na gazeti la habari la Die Zeit, Schünemann alithibitisha kwamba taarifa za wenye kutoa ushahidi—hata ingawa hazitegemeki—ni aina kuu ya ushahidi. “Ningesema sababu ya kawaida ya kufanya makosa katika utekelezaji wa haki ni kwamba, hakimu hutegemea taarifa za wenye kutoa ushahidi zisizotegemeka.”
Wenye kutoa ushahidi wanaweza kukosea; ndivyo ilivyo pia na polisi. Hasa kufuatia uhalifu ambao husababisha hasira za umma, polisi huwa chini ya mkazo wa kuwataka wawakamate wahusika. Chini ya hali za namna hiyo, polisi mmoja-mmoja wameshawishiwa kubuni ushahidi au kumlazimisha mshukiwa kuungama kosa. Wanaume sita waliopatikana na hatia ya kushambulia Birmingham kwa mabomu walipoachiliwa, gazeti la habari la Uingereza, The Independent lilikuwa na kichwa cha habari: “Polisi Wafisadi Walaumiwa kwa Kupatikana na Hatia kwa Watu Sita.” Kulingana na gazeti la habari la The Times: “Polisi walisema uwongo, wakala njama, na kudanganya.”
Katika visa fulani, ubaguzi waweza kuwafanya polisi wawashuku watu wa jamii, dini, au taifa fulani. Kama gazeti la habari la U.S.News & World Report liripotivyo, kutatua uhalifu kwaweza kuzorota kuwa “suala la ubaguzi wa kijamii badala ya kuwa suala la kufuata haki.”
Kesi ifikapo mahakamani, maamuzi yaweza kuathiriwa si na yale wenye kutoa ushahidi wasemayo tu, bali pia na ushahidi wa kisayansi. Katika nyanja inayozidi kuwa tata ya mambo ya hakika ya kitiba, hakimu au baraza la mahakama laweza kuombwa liamue kama mtu ana hatia au hana hatia kwa kutegemea uchunguzi wa silaha zilizotumiwa au, kutambuliwa kwa alama za vidole, mwandiko, aina za damu, rangi ya nywele, nyuzi za nguo, au sampuli za asidi za DNA. Mwanasheria mmoja alionelea kwamba, mahakama zinakabiliwa na “wanasayansi wenye fahari wakifafanua taratibu zenye utata unaoduwaza.”
Isitoshe, gazeti la Nature laonelea kwamba si wanasayansi wote ambao hukubaliana na kufasiriwa kwa ushahidi wa mambo ya hakika ya kitiba. “Kwaweza kuwa kutokubaliana kwa kweli kati ya wanasayansi wa mambo ya hakika ya kitiba.” Yasikitisha kusema, “mambo ya hakika ya kitiba yenye kasoro tayari yamesababisha kupatikana na hatia kwingi kuliko na kasoro.”
Hata tuwe twaishi wapi, mifumo yote ya kihukumu ambayo sasa inafanya kazi hudhihirisha kasoro za kibinadamu. Hivyo, ni nani tuwezaye kumtumaini awalinde wasio na hatia? Je, twaweza kutumaini kuwa na haki ya kweli wakati wowote? Na kuna tumaini gani kwa wahasiriwa wa kosa la kihukumu?
“Mimi, BWANA, Naipenda Hukumu ya Haki”
Wewe au mshiriki wa jamaa yako akiwa mhasiriwa wa utekelezwaji wa haki wenye kosa, Yehova Mungu na Mwana wake, Yesu, hutambua unayokabili. Ukosefu wa haki mbaya zaidi uliowahi kutokea ulifanywa wakati Kristo alipofishwa juu ya mti wa mateso. Mtume Petro atuambia kwamba Yesu “hakufanya dhambi.” Hata hivyo, alishtakiwa na wenye kutoa ushahidi usio wa kweli, akapatikana na hatia, na kufishwa.—1 Petro 2:22; Mathayo 26:3, 4, 59-62.
Wazia Yehova lazima alikuwa na hisia zilizoje kuhusu kutendwa vibaya hivyo kwa Mwana wake! Haki ni mojawapo ya sifa za msingi za Yehova. Biblia hutuambia hivi: “Njia zake zote ni haki.”—Kumbukumbu la Torati 32:4; Zaburi 33:5.
Yehova aliwapa Israeli mfumo wa kihukumu ulio wa kutokeza. Katika kisa cha kuua kimakusudi ambacho hakikuwa kimetatuliwa, kifo kilifunikwa kwa dhabihu. Hakukuwa na mkazo wa kutatua kila uhalifu kukiwa na hatari ya kumpata na hatia mtu asiye na hatia. Hakuna yeyote ambaye angeweza kupatikana na hatia ya kuua kimakusudi kwa kutegemea hali au ushahidi wa kisayansi; angalau watu wawili walioshuhudia walihitajika. (Kumbukumbu la Torati 17:6; 21:1-9) Vielelezo hivyo vyaonyesha kwamba Yehova ana viwango vya juu na yeye hujishughulisha kuona kwamba haki inatekelezwa ifaavyo. Kwa kweli, yeye asema hivi: “Mimi, BWANA, naipenda hukumu ya haki.”—Isaya 61:8.
Bila shaka, mfumo wa kihukumu wa Israeli ulikuwa mikononi mwa wanadamu waliokuwa na kasoro sawa na zetu. Kulikuwa na visa ambapo sheria ilitumiwa kwa makosa. Mfalme Solomoni aliandika hivi: “Ujapokuwa unaona maskini kuonewa, na hukumu ya haki kuondolewa kwa jeuri katika jimbo, usilistaajabie jambo hilo.”—Mhubiri 5:8.
Yehova alikuwa na uwezo wa kusahihisha ukosefu wa haki uliofanyiwa Mwana wake. Uhakika wa jambo hilo ulimwimarisha Yesu, ambaye “kwa ajili ya shangwe iliyowekwa mbele yake alivumilia mti wa mateso.” Vivyo hivyo, matazamio yenye kufurahisha ya kuishi katika dunia iliyo paradiso chini ya utawala wa Mesiya, haki ya kweli ikienea pote, yaweza kutuimarisha tuvumilie kusikia au hata kupatwa na ukosefu wa haki katika mfumo huu wa kale. Hakuna dhara au ubaya wowote ambao Yehova hawezi kurekebisha katika wakati wake. Hata wale wanaokufa kupitia kosa la kihukumu waweza kufufuliwa.—Waebrania 12:2; Matendo 24:15.
Tukiteseka tukiwa wahasiriwa wa ukosefu wa haki, twaweza kushukuru kwamba mifumo mingi ya kihukumu ina njia za kisheria ambazo huenda zikatuwezesha kusahihisha hali hiyo. Wakristo wanaweza kutumia njia hizo. Hata hivyo wao hukumbuka jambo hili la hakika: Mifumo ya kihukumu isiyo mikamilifu ni udhihirisho wa jamii ya kibinadamu inayohitaji urekebishaji mkubwa. Jambo hilo litatukia karibuni—kwa mkono wa Mungu.
Karibuni Yehova ataondolea mbali mfumo huu wa mambo usio na haki na mahali pake pachukuliwe na mfumo mpya ambamo “uadilifu utakaa.” Twaweza kuwa na uhakika kamili kwamba Muumba wetu atatekeleza haki wakati huo kupitia Mfalme wake wa Kimesiya, Yesu Kristo. Haki ya kweli kwa kila mtu inakaribia! Jinsi tuwezavyo kuwa wenye shukrani kwa ajili ya matazamio hayo.—2 Petro 3:13.
[Maelezo ya Chini]
a Katika visa ambavyo vimetajwa hapa, gazeti la Mnara wa Mlinzi halidokezi kwamba mtu yeyote ana hatia au hana hatia, wala haliungi mkono mfumo wa sheria wa nchi moja kuwa mzuri zaidi kuliko wa nchi nyingine. Isitoshe, gazeti hili halitetei aina moja ya adhabu dhidi ya nyingine. Makala hii yataja tu mambo ya hakika kama yalivyojulikana wakati wa kuandikwa.
[Blabu katika ukurasa wa 27]
Mifumo ya kihukumu yenye kasoro—pamoja na serikali yenye ufisadi, dini iliyoshushwa, na biashara isiyo na kanuni—hudhihirisha jamii ya kibinadamu ambayo yahitaji urekebishaji mkubwa
[Sanduku katika ukurasa wa 28]
Faraja kutoka katika Maandiko Matakatifu
Katika Novemba 1952, Derek Bentley na Christopher Craig walivunja na kuingia katika ghala la bidhaa za biashara huko Croydon, karibu na London, Uingereza. Bentley alikuwa na umri wa miaka 19 naye Craig alikuwa na umri wa miaka 16. Polisi waliitwa, na Craig akampiga risasi na kumwua mmoja wa polisi hao. Craig alikaa gerezani kwa muda wa miaka tisa, ilhali Bentley alinyongwa katika Januari 1953 kwa kuua kimakusudi.
Iris, dada ya Bentley, amefanya kampeni kwa miaka 40 ili kuliondolea jina la Derek hatia ya uuaji kimakusudi ambao hakuufanya. Katika mwaka wa 1993, Mamlaka ya Kifalme ilitoa msamaha kuhusiana na hiyo hukumu, ikikiri kwamba Derek Bentley hangalipaswa kamwe kunyongwa. Iris Bentley aliandika juu ya hiyo kesi katika kitabu Let Him Have Justice:
Mwaka mmoja hivi kabla ya huo ufyatuaji wa risasi, Derek alikutana na Shahidi wa Yehova barabarani . . . Dada Lane aliishi katika Fairview Road, mahali palipokuwa karibu na kwetu, naye alimwalika Derek nyumbani kwake kusikiliza hadithi za Biblia. . . . Jambo lililosaidia lilikuwa kwamba Dada Lane alikuwa amerekodi hizo hadithi za Biblia, ambazo alimwazima [kwa kuwa Derek hakujua kusoma vizuri]. . . . Alikuwa akirudi kuniambia mambo ambayo huyo dada alikuwa amemwambia, mambo kama vile sisi sote tutafufuliwa baada ya kufa.”
Iris Bentley alimzuru ndugu yake katika chumba cha wanaohukumiwa kifo kabla hajafishwa. Alihisije? “Mambo hayo ambayo Dada Lane alimwambia yalimsaidia kukabiliana na siku hizo chache za mwisho.”—Italiki ni zetu.
Ukipatwa na shida kutokana na utekelezwaji wa haki wenye kosa, ingekuwa vema kusoma na kutafakari juu ya kweli za Biblia. Kufanya hivyo kwaweza kuandaa faraja, kwa kuwa Yehova Mungu ni “Baba ya rehema nyororo na Mungu wa faraja yote, ambaye hutufariji katika dhiki yetu yote.”—2 Wakorintho 1:3, 4.
[Picha katika ukurasa wa 29]
Ukosefu wa haki ulio mbaya zaidi ulifanywa Kristo alipofishwa