Ishara Kwenye Barabara ya Uhai
KAMA ungekuwa ukisafiri kwenye barabara au njia usiyoifahamu, je, ungeona ishara kuwa kizuizi? Sivyo kabisa! Kwa hakika ungeziona kuwa msaada wa kukusaidia kutopotea njia inayoongoza mahali unapoenda.
Basi, namna gani kuhusu kusafiri kwenye barabara ya uhai? Je, yaweza kupitika kwa mafanikio bila ishara? Nabii wa kale wa Mungu alitambua upungufu wa mwanadamu kuhusu jambo hilo. Yeye alisema: “Najua, Ee BWANA, kwamba njia za mwanadamu si za kujichagulia mwenyewe; wala si juu ya mwanadamu kuamua mwendo wake maishani.”—Yeremia 10:23, The New English Bible.
Basi, ni wapi ambapo mwelekezo unaohitajiwa waweza kupatikana? Chanzo chenye kutegemeka cha mwongozo kama huo ni Muumba wa mwanadamu, nazo ishara za kitamathali zapatikana katika Biblia. Yehova, kupitia Neno lake, asema: “Na masikio yako yatasikia neno nyuma yako, likisema, Njia ni hii ifuateni; mgeukapo kwenda mkono wa kulia, na mgeukapo kwenda mkono wa kushoto.”—Isaya 30:21.
Naam, Neno la Mungu hutupa mwongozo unaotegemeka katika kila sehemu ya maisha yetu. (Isaya 48:17; 2 Timotheo 3:16, 17) Hata hivyo, kwa kusikitisha, wanadamu walio wengi husafiri kwenye njia ya uhai bila kutegemea mwelekezo wa kimungu. (Mathayo 7:13) Ingawa hivyo, ishara zimesimamishwa imara nazo zapatikana! Je, utazitii utembeapo kwenye barabara ya uhai?