Tunaweza Kuishi Muda Mrefu Kadiri Gani?
Kwa ujumla, watu wanaishi muda mrefu zaidi na zaidi, hilo likiwafanya wengi waulize, ‘Tunaweza kuishi muda mrefu kadiri gani?’
KULINGANA na The New Encyclopædia Britannica (1995), wakati uliopita, ilikubaliwa kwa ujumla kwamba Pierre Joubert alikuwa ameishi muda mrefu zaidi kuliko wote. Alikufa mwaka wa 1814, akiwa na umri wa miaka 113. Ni kweli kwamba wengine wamesemwa kuwa waliishi muda mrefu zaidi, lakini umri wao haukuthibitishwa kupitia hati zinazoaminika. Hata hivyo, hati sahihi zimethibitisha kwamba watu kadhaa wameishi muda mrefu kuliko Pierre Joubert.
Jeanne Louise Calment alizaliwa Arles, kusini-mashariki mwa Ufaransa, Februari 21, 1875. Kifo chake kilichotokea Agosti 4, 1997—zaidi ya miaka 122 baadaye—kilitangazwa sana. Katika mwaka wa 1986, Shigechiyo Izumi wa Japani alikufa akiwa na umri wa miaka 120. Kitabu Guinness Book of Records 1999 chaorodhesha Sarah Knauss, mwenye umri wa miaka 118, kuwa ndiye mtu mwenye umri mkubwa zaidi kufikia wakati kitabu hicho kilipoandikwa. Alizaliwa Septemba 24, 1880, huko Pennsylvania, Marekani. Wakati Marie-Louise Febronie Meilleur wa Quebec, Kanada, alipokufa mwaka wa 1998 akiwa na umri wa miaka 118, alikuwa amemshinda Sarah kwa siku 26.
Kwa kweli, idadi ya wakongwe imeongezeka sana. Imekadiriwa kuwa idadi ya wenye umri wa miaka 100 au zaidi itaongezeka kufikia zaidi ya milioni 2.2 katika nusu ya kwanza ya karne ijayo! Vivyo hivyo, idadi ya watu wenye umri wa miaka 80 na zaidi iliongezeka kutoka milioni 26.7 mwaka wa 1970 hadi milioni 66 mwaka wa 1998. Hilo ni ongezeko la asilimia 147, ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 60 la jumla ya idadi ya watu duniani.
Na si kwamba tu watu wanaishi muda mrefu zaidi. Wengi pia wanatimiza mambo ambayo watu walio wengi wenye umri wa miaka 20 hawawezi kutimiza. Mwaka wa 1990, John Kelley, mwenye umri wa miaka 82, alimaliza mbio za masafa marefu—shindano la kilometa 42.195—katika muda wa saa tano na dakika tano. Katika mwaka wa 1991, Mavis Lindgren, nyanya mwenye umri wa miaka 84, alimaliza umbali huo katika muda wa saa saba na dakika tisa. Na hivi karibuni, mwanamume mwenye umri wa miaka 91 alimaliza mbio za Masafa marefu za New York City!
Hii haimaanishi kwamba wazee wa nyakati za kale hawakutimiza matendo ya ajabu. Akiwa na umri wa miaka 99, Abrahamu, mzee wa ukoo anayezungumziwa katika Biblia, “alipiga mbio kuwalaki” wageni wake. Akiwa na umri wa miaka 85, Kalebu alitangaza hivi: “Kama nguvu zangu zilivyokuwa wakati huo [miaka 45 mapema], na nguvu zangu ndivyo zilivyo sasa, kwa vita na kwa kutoka nje na kuingia ndani.” Nayo Biblia inasema kumhusu Musa kwamba alipokuwa na umri wa miaka 120, “jicho lake halikupofuka, wala nguvu za mwili wake hazikupunguka.”—Mwanzo 18:2; Yoshua 14:10, 11; Kumbukumbu la Torati 34:7.
Yesu Kristo alisema kuhusu mtu wa kwanza, Adamu, na Noa mjenga-safina kuwa watu wa kihistoria. (Mathayo 19:4-6; 24:37-39) Kitabu cha Mwanzo chasema kwamba Adamu aliishi miaka 930, Noa naye akaishi miaka 950. (Mwanzo 5:5; 9:29) Je, kweli watu wameishi muda mrefu kadiri hiyo? Je, twaweza kuishi muda mrefu zaidi ya huo, labda milele? Tafadhali chunguza uthibitisho katika makala ifuatayo.