Mkutano wa Kila Mwaka Oktoba 2, 1999
MKUTANO WA KILA MWAKA wa washiriki wa Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania utafanywa Oktoba 2, 1999, kwenye Jumba la Kusanyiko la Mashahidi wa Yehova, 2932 Kennedy Boulevard, Jersey City, New Jersey. Mkutano unaotangulia wa washiriki peke yao utafanywa saa 3:15 asubuhi, ukifuatwa na ule mkutano wa jumla wa kila mwaka saa 4:00 asubuhi.
Washiriki wa Shirika hilo wanapaswa kuijulisha Ofisi ya Mwandishi sasa juu ya badiliko lolote la anwani zao lililotokea mwaka uliopita ili zile barua za kawaida zenye taarifa na hati za kuwakilisha ziweze kuwafikia mwezi wa Julai.
Hati za kuwakilisha, watakazopelekewa washiriki pamoja na taarifa ya mkutano wa kila mwaka, zinapasa kurudishwa ili ziifikie Ofisi ya Mwandishi wa Sosaiti kabla ya Agosti 1. Inampasa kila mshiriki ajaze mambo yote yaliyo katika hati yake ya kumwakilisha na kuirudisha upesi, akitaarifu ikiwa atakuwapo mkutanoni yeye binafsi au la. Habari zinazotajwa katika kila hati ya kuwakilisha zinapaswa kutaja waziwazi jambo hilo, kwa kuwa ndizo zitakazotegemewa ili kujua ni nani watakaokuwapo binafsi.
Inatarajiwa kwamba kipindi kizima, kutia ndani ule mkutano rasmi na ripoti mbalimbali, kitamalizika mwendo wa saa 7:00 alasiri. Hakutakuwa na kipindi cha alasiri. Kwa sababu nafasi ni ndogo, itawezekana kuingia kwa kuwa na tikiti tu. Hakutakuwa na mpango wa kuunganisha majumba mengine kwa simu ili kuusikia mkutano wa kila mwaka.