Kuna Johari Hai Nchini Namibia!
NAMIBIA ina eneo la karibu kilometa 1,500 kandokando ya pwani ya kusini-magharibi mwa Afrika. Pwani yote ya nchi hiyo ina matuta ya mchanga, vilima vya miamba, na nyanda kubwa za changarawe. Kuna johari za rangi mbalimbali miongoni mwa mawe ya fuo za Namibia zenye vijiwe vya mviringo. Hata almasi hupatikana huko pindi kwa pindi. Lakini nchi hiyo ina kitu kingine chenye thamani kuliko mawe hayo. Namibia ina johari hai—watu wa vikundi vyake vingi vya kitaifa.
Wakazi wa mapema zaidi wa Namibia waliongea lugha ambazo kwa pamoja ziliitwa Khoisan. Usemi wao ulijulikana kwa zile sauti za kupiga kidoko. Baadhi ya watu wasemao Kikhoisan leo ni Wadamara wenye ngozi nyeusi, Wanama wafupi wenye ngozi nyeupe, na Wasan, wale wawindaji maarufu. Makabila mengi ya weusi pia yameingia Namibia katika karne za majuzi. Wao hufanyiza vikundi vitatu vikubwa vya kitaifa: Waovambo (kabila kubwa zaidi nchini Namibia), Waherero, na Wakavango. Wazungu walianza kukaa nchini Namibia katika karne ya 19. Wahamiaji wengi zaidi waliwasili baada ya almasi kugunduliwa kwenye mchanga wa jangwani.
Wakazi wa Namibia ni wenye thamani kwa sababu wao ni sehemu ya ulimwengu wa wanadamu ambao Mungu alitolea Mwana wake, akiwafungulia njia ya kupata uhai udumuo milele. (Yohana 3:16) Mamia ya Wanamibia kutoka katika makabila mengi tayari wamekubali ujumbe wa wokovu. Hao wanaweza kulinganishwa na johari hai kwa sababu wako miongoni mwa “vitu vinavyotamaniwa na mataifa yote” ambavyo sasa vinakusanywa na kuingizwa katika nyumba ya Yehova ya ibada.—Hagai 2:7.
Kuchimba Migodi ya Kiroho Kwaanza
Mwaka wa 1928 ndipo johari za kiroho za Namibia zilipoanza kuchimbwa. Mwaka huo, ofisi ya tawi ya Afrika Kusini ya Watch Tower Society ilipeleka fasihi za Biblia zipatazo 50,000 kwa watu kotekote nchini. Mwaka uliofuata, Mkristo mtiwa-mafuta kutoka Afrika Kusini aitwaye Lenie Theron alifuatia upendezi ulioonyeshwa. Kwa miezi minne alisafiri huku na huku katika nchi hiyo kubwa akiwa peke yake, akiangusha vichapo zaidi ya 6,000 vya kujifunza Biblia katika Kiafrikana, Kiingereza, na Kijerumani. Bila shaka kazi yote hiyo haikuwa ya bure.
Kwa kielelezo, mfikirie Bernhard Baade, mchimba-migodi Mjerumani. Mwaka wa 1929 alipata mayai kutoka kwa mkulima ambaye alifunga kila yai kwa ukurasa kutoka katika kichapo cha Watch Tower. Bernhard alisoma kwa hamu kila ukurasa, akitaka kujua ni nani aliyeandika kitabu hicho. Hatimaye akafikia ukurasa wa mwisho, uliokuwa na anwani ya Ujerumani ya Watch Tower Society. Bernhard akaandika akiomba fasihi zaidi naye akawa Mnamibia wa kwanza kuikubali kweli.
Wafanyakazi wa Wakati Wote Wawasili
Mwaka wa 1950, wamishonari wanne waliozoezwa katika Shule ya Biblia ya Gileadi ya Watchtower waliwasili Namibia. Idadi ya wamishonari ikaongezeka hadi wanane kufikia mwaka wa 1953. Walitia ndani Dick na Coralie Waldron, wenzi wa ndoa Waaustralia ambao bado wanatumikia nchini humu kwa uaminifu. Wapiga-mbiu wa Ufalme wengine wa wakati wote kutoka Afrika Kusini na ng’ambo pia wameshiriki katika kuchimba johari za kiroho za Namibia. Wamishonari wengine, pamoja na wahitimu wa Shule ya Mazoezi ya Kihuduma, wametumwa Namibia.
Jambo jingine linalochangia ukuzi wa kiroho nchini Namibia ni kule kutafsiriwa na kuchapishwa kwa fasihi za Biblia katika lugha kubwa za kienyeji, kama vile Kiherero, Kikwangali, Kikwanyama, Kinama/Damara, na Kindonga. Tangu mwaka wa 1990, jijini kuu Windhoek kumekuwa na ofisi nzuri ya kutafsiri na makao ya wafanyakazi wa wakati wote wa kujitolea. Karen Deppisch, ambaye ameshiriki na mume wake katika kazi ya wakati wote ya kueneza evanjeli katika sehemu mbalimbali za Namibia, asema hivi: “Watu wengi hushangaa tunapowapatia fasihi katika lugha yao wenyewe, hasa wakati ambapo ni vichapo vichache sana vya aina yoyote vinavyopatikana katika lugha hiyo hasa.”
Kung’arisha Johari
Baadhi ya johari halisi za Namibia zimeng’arishwa na ule mwendo wa mawimbi na mchanga kwa mamileani ya wakati. Lakini, bila shaka, michakato hiyo ya kiasili haitokezi johari hai. Huhitaji jitihada ili wanadamu wasio wakamilifu ‘wauweke mbali utu wa hapo zamani’ na kujivika utu mpya ulio kama wa Kristo. (Waefeso 4:20-24) Kwa kielelezo, kuabudu wazazi wa kale waliokufa ni utamaduni uliokolea miongoni mwa makabila mengi ya Namibia. Watu ambao hawafanyi vitendo vya kuabudu wazazi wa kale waliokufa mara nyingi hunyanyaswa na washiriki wa familia na majirani. Watu wajifunzapo kutoka katika Biblia kwamba wafu “hawajui neno lo lote,” hukabili mtihani. (Mhubiri 9:5) Jinsi gani?
Shahidi Mherero aeleza hivi: “Ilikuwa vigumu sana kuitii kweli. Nilikubali kujifunza Biblia na Mashahidi wa Yehova, lakini ilichukua muda mrefu kabla sijatumia mambo niliyokuwa nikijifunza. Kwanza, nililazimika kujaribu ili kuona kama ingekuwa salama ikiwa singeendelea kufanya mambo ya kitamaduni. Kwa kielelezo, ningeendesha gari kupitia sehemu fulani za Namibia bila kusimama na kuweka jiwe kwenye kaburi au kuinua kofia yangu kwa kuwasalimu wafu. Hatua kwa hatua, nikasadikishwa kwamba hakuna kitu kingenipata ikiwa singewaabudu wazazi wa kale waliokufa. Nina furaha kama nini kwamba Yehova amebariki jitihada zangu za kusaidia familia yangu na watu wengine wenye kupendezwa wajifunze kweli!”
Uhitaji wa Wachimba-Migodi wa Kiroho
Kabla ya kufika kwa wamishonari mwaka wa 1950, kulikuwa na mhubiri mmoja tu wa habari njema nchini Namibia. Idadi imeongezeka mfululizo kufikia 995. Hata hivyo, bado kuna kazi nyingi ya kufanywa. Kwa hakika, maeneo mengine hata hayajahubiriwa. Je, unaweza kutumikia mahali ambapo wapiga-mbiu wa Ufalme wenye bidii wanahitajiwa sana? Basi, tafadhali, vuka uingie Namibia, utusaidie kung’arisha johari zaidi za kiroho.—Linganisha Matendo 16:9.
[Ramani/Picha katika ukurasa wa 26]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
AFRICA
NAMIBIA
[Picha]
Namibia ni nchi yenye johari zenye kupendeza
[Hisani]
Ramani: Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.; Almasi: Courtesy Namdek Diamond Corporation
[Picha katika ukurasa wa 26]
Habari njema yahubiriwa kwa vikundi vyote vya kikabila vya Namibia
[Picha katika ukurasa wa 28]
Je, unaweza kutumikia mahali ambapo wapiga-mbiu wa Ufalme wanahitajiwa sana?