Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w00 10/1 kur. 30-31
  • ‘Mbuzi-Mwitu Avutiaye’

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • ‘Mbuzi-Mwitu Avutiaye’
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2000
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2000
w00 10/1 kur. 30-31

‘Mbuzi-Mwitu Avutiaye’

WENGI wetu hatungetumia kivumishi -enye kuvutia kumfafanua mbuzi. Huenda tukawafikiria mbuzi kuwa wanyama wenye manufaa ambao hula chochote na ambao hutufaidi kwa nyama tamu na maziwa bora—lakini hatungewaona kuwa wenye kuvutia.

Hata hivyo, Biblia humfafanua mke kuwa “ayala apendaye na paa apendezaye [“mbuzi-mwitu avutiaye,” NW].” (Mithali 5:18, 19) Solomoni, mwandishi wa kitabu cha Mithali, alichunguza kwa makini sana wanyama-mwitu wa Israeli, kwa hiyo bila shaka alikuwa na sababu nzuri ya kutumia usemi huo. (1 Wafalme 4:30-33) Kama baba yake Daudi, labda alikuwa amechunguza mbuzi-mwitu waliokuwa wakija mara kwa mara katika eneo lililo karibu na Engedi, karibu na pwani za Bahari ya Chumvi.

Makundi madogo ya mbuzi-mwitu wanaoishi katika Jangwa la Yudea lililo karibu hutembelea chemchemi ya Engedi. Kwa kuwa ndiyo chemchemi ya maji pekee katika eneo hilo kame, Engedi pamekuwa mahali penye maji panapopendwa sana na mbuzi-mwitu kwa karne nyingi. Kwa kweli, neno Engedi labda lamaanisha “chemchemi ya mwanambuzi,” uthibitisho wa kuwapo kwa mbuzi wachanga mahali hapo mara kwa mara. Mfalme Daudi alikimbilia hapa aliponyanyaswa na Sauli, ijapokuwa ilimbidi akae kama mkimbizi “juu ya majabali ya mbuzi-mwitu.”—1 Samweli 24:1, 2.

Huko Engedi bado waweza kuona mbuzi-mwitu wa kike, akitelemka kwa madaha kwenye bonde majabalini anapomfuata beberu kwenda penye maji. Ndipo unapoweza kufahamu ulinganisho wa mbuzi-mwitu wa kike na mke mwaminifu-mshikamanifu. Hali yake ya asili ya uanana na madaha yake pia huashiria sifa za kike. Neno “-enye kuvutia” ladokeza sura nzuri na yenye madaha ya mbuzi-mwitu huyo.a

Lazima mbuzi-mwitu wa kike awe mstahimilivu na vilevile mwenye madaha. Kama Yehova alivyomweleza Ayubu, mbuzi-mwitu huzaa majabalini, mahali pasipofikika ambapo huenda pakawa na chakula kidogo sana na halijoto kali sana. (Ayubu 39:1) Yajapokuwa magumu hayo, yeye hutunza wazao wake na kuwafundisha jinsi ya kupanda na kuruka katikati ya majabali kwa wepesi kama afanyavyo yeye. Pia mbuzi-mwitu huyo hulinda watoto wake kwa ushujaa dhidi ya wanyama-wawindaji. Mchunguzaji mmoja alimwona mbuzi-mwitu akimzuia tai kwa nusu saa, huku mtoto wake akichutama chini yake ili kupata ulinzi.

Mara nyingi wake na akina mama Wakristo hulazimika kulea watoto wao katika hali ngumu sana. Kama mbuzi-mwitu, wanajitoa bila ubinafsi kutimiza daraka hilo walilopewa na Mungu. Nao hujitahidi kishujaa kulinda watoto wao na hatari za kiroho. Kwa hiyo, Solomoni hadunishi wanawake hata kidogo kwa usemi huo, bali kwa kweli alikuwa akivuta uangalifu kwa madaha na urembo wa mwanamke—sifa za kiroho ambazo hung’aa hata katika mazingira yaliyo magumu zaidi.

[Maelezo ya Chini]

a Kulingana na The New Brown-Driver-Briggs-Gesenius Hebrew and English Lexicon, katika muktadha huu neno la Kiebrania chen, linalotafsiriwa “-enye kuvutia,” humaanisha ‘umbo na sura ya madaha.’

[Picha katika ukurasa wa 30, 31]

Mke na mama Mkristo huonyesha sifa nzuri za kiroho anapotimiza madaraka yake aliyopewa na Mungu

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki