Mabaki ya Mwasia Yapatikana Italia ya Kale
MTU mwenye asili ya Asia Mashariki alifika jinsi gani katika Milki ya Roma, miaka 2,000 iliyopita? Hilo ndilo swali ambalo wataalamu wa vitu vya kale walikabili baada ya kufanya uvumbuzi wenye kuvutia huko Italia ya kusini mwaka wa 2009.
Eneo hilo lilikuwa ni makaburi ya Roma ya kale huko Vagnari, kilomita 60 magharibi ya Bari. Mabaki ya mifupa ya watu 75 ilifukuliwa. Uchunguzi wa mifupa hiyo ulionyesha kwamba wengi wa watu hao walizaliwa katika eneo hilo. Hata hivyo, mifupa ya mtu mmoja iliwashangaza watafiti hao. Uchunguzi wa DNA ya mitokondria katika mifupa hiyo ulionyesha kwamba mama ya mtu huyo alikuwa wa asili ya Asia ya Mashariki.a Mabaki hayo yalionyesha kuwa mtu huyo aliishi katika karne ya kwanza au ya pili W.K. Kulingana na ripoti ya uvumbuzi huo, “hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza kwa mifupa ya mtu mwenye asili ya Asia ya Mashariki kugunduliwa katika Milki ya Roma.” Hivyo, mtu huyo alikuwa nani?
Ripoti hiyohiyo inasema, “Unapoona mabaki hayo kwa mara ya kwanza huenda ukamhusisha mtu huyo na biashara ya hariri iliyokuwa imesitawi kati ya China na Roma.” Hata hivyo, inafikiriwa kwamba biashara hiyo ilihusisha madalali, au watu wa kati, kwa hiyo, hakuna yeyote aliyekuwa akisafiri kilomita zote 8,000 kati ya China na Italia.
Tunaweza kujifunza nini kutoka katika eneo ambako mabaki hayo yalipatikana? Katika nyakati za kale, Vagnari lilikuwa eneo la kijijini lenye nyumba za kifalme, ambalo lilimilikiwa na mfalme. Katika eneo hilo wafanyakazi waliyeyusha chuma na pia kutengeneza vigae vya udongo wa mfinyanzi. Wengi wao walikuwa watumwa, na inawezekana kwamba mtu huyo wa Mashariki alikuwa mtumwa pia. Kwa kweli, hakuzikwa kama tajiri. Wavumbuzi walipata chungu kimoja tu kati ya vitu alivyozikwa navyo. Walipata pia mabaki ya mtu mwingine aliyezikwa juu yake.
Kwa nini uvumbuzi huo ni wa maana? Kuenea kwa Ukristo katika karne ya kwanza kulitegemea umbali ambao watu wa kale wangeweza kusafiri. Biblia inaripoti kwamba baada ya siku ya Pentekoste, mwaka wa 33 W.K., habari njema zilifikishwa maeneo ya mbali na wageni waliokuwa wakitembelea Yerusalemu. (Matendo 2:1-12, 37-41) Angalau mifupa hiyo inadokeza kwamba katika kipindi hicho watu fulani walikuwa wakisafiri kutoka Asia ya Mashariki hadi katika eneo la Mediterania.b
[Maelezo ya Chini]
a Uchunguzi wa DNA ya mitokondria hauwezi kutoa habari yoyote kuhusu asili ya baba.
b Pia, kuna uthibitisho kwamba watu wa Ulaya walisafiri kwenda Asia ya Mashariki. Ona makala “Wamishonari Wangesafiri Hadi Wapi Upande wa Mashariki?” katika gazeti la Mnara wa Mlinzi la Januari 1, 2009.
[Ramani katika ukurasa wa 29]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
ROMA
Vagnari
Bahari ya Mediterania
ASIA YA MASHARIKI
BAHARI YA PASIFIKI
[Picha katika ukurasa wa 29]
Mabaki ya mifupa ya mtu wa Asia ya Mashariki iliyofukuliwa katika eneo la makaburi ya Roma ya kale
[Hisani]
© Su concessione del Ministero per i Beni e le Attività Culturali-Direzione Regionale per i Beni Culturali e Paesaggistici della Puglia-Soprintendenza per i Beni Archeologici della Puglia