Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • lf swali 3 kur. 13-21
  • Maagizo Yalitoka Wapi?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Maagizo Yalitoka Wapi?
  • Maswali Matano Muhimu Kuhusu Chanzo cha Uhai
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • UMBO LA MOLEKULI YENYE KUSTAAJABISHA
  • MFUMO WA PEKEE WA KUHIFADHI HABARI
  • KITABU KISICHO NA MWANDIKAJI?
  • MASHINI ZILIZO MWENDONI
  • “KUSOMA” DNA
  • KWA NINI UKWELI HUU NI MUHIMU?
  • Chunguza Uthibitisho
    Amkeni!—2011
  • Chembe Zako​—Maktaba Iliyo Hai!
    Amkeni!—2015
  • Kuchunguza Chembe kwa Hadubini
    Amkeni!—1999
  • Uhai Ulianzaje?
    Amkeni!—1999
Pata Habari Zaidi
Maswali Matano Muhimu Kuhusu Chanzo cha Uhai
lf swali 3 kur. 13-21

Swali la 3

Maagizo Yalitoka Wapi?

Kwa nini uko jinsi ulivyo? Ni nini kinachoamua rangi ya macho yako, nywele zako, ngozi yako? Namna gani kimo chako, umbo lako, au unavyofanana na mmoja wa wazazi wako au wazazi wote wawili? Ni nini kinachoamua kwamba mwisho wa vidole vyako upande mmoja uwe laini na ule mwingine uwe na kucha?

Katika siku za Charles Darwin, majibu ya maswali hayo yalikuwa fumbo. Darwin mwenyewe alishangazwa na jinsi tabia zinavyopitishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine, lakini hakujua mengi kuhusu sheria ya chembe za urithi wala utendaji wake. Hata hivyo, leo wanabiolojia wametumia miaka mingi kuchunguza chembe za urithi za mwanadamu na maagizo yaliyo ndani ya molekuli yenye kustaajabisha inayoitwa DNA au Deoksiribonyukilia asidi. Bila shaka, swali muhimu ni, Maagizo hayo yalitoka wapi?

Wanasayansi wengi husema nini? Wanabiolojia wengi na wanasayansi fulani hufikiri kwamba DNA pamoja na maagizo yake yaliyopangwa vilitokana na matukio yaliyojitokeza yenyewe ambayo yalifanyika kwa kipindi cha mamilioni ya miaka. Wanasema kwamba hakuna uthibitisho wa ubuni katika maumbile ya molekuli hiyo wala katika habari inayobeba na kuituma wala jinsi inavyofanya kazi.17

Biblia inasema nini? Biblia inasema kwamba kufanyizwa kwa sehemu mbalimbali za mwili wetu—hata wakati zitakapofanyizwa—kunahusisha kitabu cha mfano ambacho chanzo chake ni Mungu. Ona jinsi Mfalme Daudi alivyoongozwa na roho kueleza mambo, akisema hivi kumhusu Mungu: “Macho yako yalikiona kiini-tete changu, na katika kitabu chako sehemu zake zote zilikuwa zimeandikwa, kuhusiana na siku ambazo zilifanyizwa na hakukuwako hata moja kati ya hizo.”—Zaburi 139:16.

Uthibitisho unafunua nini? Ikiwa fundisho la mageuzi ni la kweli, basi inapaswa angalau kuonekana kwamba huenda DNA ilijitokeza yenyewe kupitia mfuatano wa matukio. Ikiwa Biblia inasema kweli, basi DNA inapaswa kutoa uthibitisho wenye kusadikisha kwamba inatokana na Muumba mwenye utaratibu na akili.

Habari za msingi kuhusu chembe za urithi, zinaeleweka kabisa na zinastaajabisha. Basi acheni tufunge safari nyingine kuingia ndani ya chembe. Hata hivyo, wakati huu tutatembelea chembe ya mwanadamu. Wazia unatembelea jumba la makumbusho ambalo limekusudiwa kukufundisha kuhusu jinsi chembe ya aina hiyo inavyofanya kazi. Jumba hilo la makumbusho linawakilisha chembe halisi ya mwanadamu, lakini iliyokuzwa mara 13,000,000 hivi. Ina ukubwa wa uwanja mkubwa sana wa michezo ambao unaweza kutoshea watu 70,000 hivi wakiwa wameketi.

Unaingia ndani ya jumba hilo na kutazama kwa mshangao mahali hapo penye kustaajabisha palipo na maumbo na vitu vingi vya ajabu. Karibu na sehemu ya katikati ya chembe kuna kiini, tufe lenye urefu wa ghorofa 20 hivi. Unaingia humo.

Unaingia kupitia mlango ulio kwenye ngozi ya nje ya kiini, au utando, na kutazama huku na huku. Ndani mna kromosomu 46. Zimepangwa kwa pea zinazofanana lakini zinatofautiana kwa urefu, pea iliyo karibu nawe ina urefu wa ghorofa 12 hivi (1). Kila kromosomu imebonyea katikati, na hivyo inafanana kidogo kama soseji iliyokunjwa lakini nene kama shina la mti mkubwa. Unaona mikanda tofauti-tofauti kutoka upande mmoja hadi mwingine wa kromosomu hiyo ya mfano. Unapokaribia, unatambua kwamba kila mkanda uliolala unagawanywa na mistari iliyo wima. Kati ya mistari hiyo kuna mistari mifupi iliyolala (2). Je, ni rundo la vitabu? Hapana; ni kingo za vitanzi vilivyopangwa na kufungwa pamoja katika safu. Unavuta kitanzi kimoja, nacho kinatoka kwa urahisi. Unastaajabu kuona kwamba kitanzi kimefanyizwa kwa koili ndogo (3), ambazo pia zimepangwa kwa utaratibu mzuri. Ndani ya koili hizo kuna kitu muhimu—kitu kinachofanana na kamba ndefu sana. Ni nini hicho?

UMBO LA MOLEKULI YENYE KUSTAAJABISHA

Acheni tuifananishe sehemu hii ya kromosomu ya mfano na kamba. Ina unene wa sentimita 2.6 hivi. Imefungwa kwa mkazo sana kuzunguka vibiringo (4), ambavyo husaidia kutengeneza koili ndani ya koili. Koili hizo zimeunganishwa kwa kitu kama nguzo ambayo huzishikilia. Maelezo kwenye ubao yanaonyesha kwamba kamba hiyo imepangwa vizuri. Ikiwa ungeivuta kamba hiyo kutoka kwenye kila kromosomu hizo za mfano na kuinyoosha yote kutoka mwisho mmoja hadi mwingine, urefu wake unaweza kufika karibu nusu ya dunia!a

Kitabu kimoja cha sayansi kinauita mfumo huo wa kupanga “mafanikio makubwa ya uhandisi.”18 Je, maoni ya kwamba hakuna mhandisi aliyehusika katika mafanikio hayo yanakusadikisha? Ikiwa jumba hilo la maonyesho lingekuwa na bohari kubwa yenye mamilioni ya bidhaa za kuuza ambazo zimepangwa vizuri sana hivi kwamba ungeweza kupata chochote unachohitaji kwa urahisi, ungesema kwamba hakuna mtu aliyepanga bohari hiyo? Bila shaka hapana! Hata hivyo, utaratibu huo ni wa hali ya chini ukilinganishwa na ule tunaozungumzia.

Kwenye ubao wa maelezo katika jumba la makumbusho, unaalikwa kuchukua kiasi fulani cha kamba hiyo na kuitazama kwa ukaribu (5). Unapoipitisha kwenye vidole vyako, unatambua kwamba hiyo si kamba ya kawaida. Imefanyizwa kwa nyuzi mbili zilizosokotwa pamoja. Nyuzi hizo zimeunganishwa kwa fito ndogo-ndogo zinazoachana kwa nafasi ileile. Kamba hiyo inafanana ngazi iliyosokotwa mpaka ikafanana na ngazi ya mzunguko (6). Kisha unatambua: Mkononi mwako una molekuli ya DNA ya mfano—mojawapo ya maajabu makubwa ya uhai!

Molekuli moja ya DNA iliyopangwa kwa utaratibu pamoja na vibiringo na nguzo zake, hufanyiza kromosomu moja. Vipago vya ngazi huitwa pea za msingi (7). Hivyo hufanya kazi gani? Vyote hivyo ni vya nini? Unapata maelezo rahisi kwenye ubao wa maelezo.

MFUMO WA PEKEE WA KUHIFADHI HABARI

Kulingana na ubao wa maelezo, ili kuelewa DNA, lazima mtu aelewe kwanza vile vipago, yaani, fito zinazounganisha sehemu mbili za ngazi. Wazia ngazi ikiwa imekatwa mara mbili. Kila kipande kina vipago vinavyotokeza. Vipago hivyo ni vya aina nne tu. Wanasayansi huviita A, T, G, na C. Wanasayansi walishangaa kugundua kwamba mpangilio wa herufi hizo hutuma habari kwa njia fulani iliyofupishwa.

Huenda unajua kwamba mawasiliano ya Morse yalianzishwa katika karne ya 19 ili watu waweze kuwasiliana kwa njia ya telegrafu. Mfumo huo ulitumia “herufi” mbili tu—nukta na kistari. Hata hivyo, “herufi” hizo zingeweza kutumiwa kuwakilisha maneno au sentensi nyingi. Mfumo wa DNA una herufi nne. Mpangilio wa herufi hizo—A, T, G, na C—hufanyiza “maneno” yanayoitwa codons. Codons zimepangwa katika “maghorofa” yanayoitwa chembe za urithi. Kwa wastani, kila chembe ya urithi ina herufi 27,000. Chembe hizo pamoja na mitanuko iliyo kati yake huungana na kufanyiza vitu kama sura za kitabu—kromosomu mojamoja. Kromosomu 23 zinahitajika ili kutengeneza “kitabu” kizima—habari zote kuhusu chembe za urithi za kiumbe kilicho hai.b

Chembe za urithi zingekuwa kitabu kikubwa. Kingekuwa na habari nyingi kadiri gani? Kwa ujumla, chembe za urithi za mwanadamu hufanyizwa kwa pea za msingi au vipago bilioni tatu hivi kwenye ngazi ya DNA.19 Wazia ensaiklopedia kadhaa ambazo kila moja ina zaidi ya kurasa 1,000. Chembe za urithi zinaweza kujaza mabuku 428 ya aina hiyo. Ukiongeza nakala ya pili iliyo katika kila chembe utapata jumla ya mabuku 856. Ikiwa ungechapa mabuku hayo ya chembe hizo za urithi wewe mwenyewe, ingekuwa kazi ya kudumu—bila likizo—ambayo ingekuchukua miaka 80 hivi!

Bila shaka, kazi ya aina hiyo ingekuwa yenye kuchosha tu. Ungeweza jinsi gani kujaza mamia ya mabuku makubwa kwenye kila moja ya chembe zako ndogo sana trilioni 100? Kushindilia habari nyingi kadiri hiyo na kwa njia bora hivyo ni jambo linalopita uwezo wetu.

Profesa fulani wa sayansi ya molekuli na kompyuta alisema: “Gramu moja ya DNA, ambayo ikikaushwa inaweza kuchukua ujazo wa sentimita moja ya mchemraba, ina habari nyingi kama zile zinazoweza kutoshea katika diski trilioni moja hivi.”20 Hilo linamaanisha nini? Kumbuka kwamba DNA ina chembe za urithi, maagizo yanayofanyiza mwili wenye kustaajabisha wa mwanadamu. Kila chembe ina maagizo kamili. DNA ina habari nyingi sana hivi kwamba chembe zinazotoshea kwenye kijiko cha chai zinaweza kubeba maagizo yanayotosha kufanyiza idadi ya wanadamu wote walio hai leo, mara 350! DNA inayohitajika kufanyiza watu bilioni saba wanaoishi duniani leo haiwezi hata kufanyiza utando mwembamba kwenye kijiko hicho.21

KITABU KISICHO NA MWANDIKAJI?

Licha ya maendeleo katika kupunguza ukubwa wa vitu, hakuna kifaa chochote cha kuhifadhi habari kilichotengenezwa na mwanadamu kinachoweza kukaribia uwezo wa DNA. Hata hivyo, tunaweza kuilinganisha na diski. Fikiria hili: Huenda diski ikatushangaza kwa sababu ya muundo wake mzuri, sehemu yake ya juu inayong’aa, mpangilio wake mzuri. Tunaona uthibitisho ulio wazi kwamba watu wenye akili waliitengeneza. Namna gani ikitiwa habari—si habari yoyote tu bali habari yenye kueleweka, maagizo kamili ya kujenga, kudumisha, na kufanyia marekebisho mitambo tata? Habari hiyo haibadilishi uzito au ukubwa wa diski hiyo. Hata hivyo, habari hiyo ndiyo sehemu muhimu zaidi ya diski hiyo. Je, maagizo hayo yaliyoandikwa hayakusadikishi kwamba kuna mtu mwenye akili anayehusika? Je, maandishi hayahitaji mwandikaji?

Tunaweza kuilinganisha DNA na diski au kitabu. Kitabu kimoja kinachozungumzia chembe za urithi kinasema: “Kusema kweli, kulinganisha chembe za urithi na kitabu hata si usemi wa kitamathali. Ni kweli kabisa. Habari za kielektroniki hufanyiza kitabu . . . Na ndivyo na chembe za urithi.” Mwandikaji huyo aongezea: “Chembe za urithi ni kitabu chenye ujuzi mwingi kwa sababu katika hali nzuri kinaweza kujinakili na kujisoma chenyewe.”22 Hilo linatokeza sehemu nyingine muhimu ya DNA.

MASHINI ZILIZO MWENDONI

Ukiwa umesimama kwa utulivu, unashangaa ikiwa kwa kweli kiini cha chembe kimesimama tuli kama jumba la makumbusho. Kisha unaona ubao mwingine wa maelezo. Juu ya chombo cha glasi kuna DNA ya mfano yenye maandishi yanayosema: “Bonyeza Kitufe Upate Ufafanuzi.” Unabonyeza kitufe, naye msimuliaji anasema: “DNA inatimiza angalau kazi mbili muhimu. Kwanza inatokeza nakala yake. Lazima DNA inakiliwe ili kila chembe mpya iwe na nakala kamili ya habari zilezile za chembe za urithi. Tafadhali tazama onyesho hili.”

Mashini inayoonekana kuwa tata inaingia kupitia mlango ulio upande mmoja wa ubao wa maelezo. Ni roboti nyingi zilizounganishwa pamoja. Mashini hiyo inaenda kwa DNA, inajipachika, na kuanza kusonga pamoja na DNA kama vile gari-moshi linavyofuata reli. Inasonga kwa kasi hivi kwamba huwezi kuona kwa urahisi kinachoendelea, lakini unaweza kuona kwamba nyuma yake sasa kuna kamba mbili zilizokamilika za DNA badala ya moja.

Msimuliaji anaeleza: “Hii ni njia rahisi sana ya kuonyesha kinachoendelea DNA inapojinakili. Kikundi cha molekuli zinazoitwa vimeng’enya husafiri pamoja na DNA, kwanza zinajigawanya katika sehemu mbili, kisha zinatumia kila uzi kama kigezo cha kutengeneza uzi mwingine mpya unaofanana nao. Hatuwezi kukuonyesha sehemu zote zinazohusika—kama vile kifaa ambacho hutangulia mashini ya kunakili na kukata upande mmoja wa DNA ili iweze kujizungusha kwa urahisi bila kujifunga. Wala hatuwezi kukuonyesha jinsi DNA ‘inavyosahihishwa’ mara kadhaa. Makosa yanagunduliwa na kusahihishwa kwa usahihi wa hali ya juu sana.”—Ona picha katika ukurasa wa 16 na 17.

Msimuliaji anaendelea: “Kile tunachoweza kukuonyesha waziwazi ni mwendo. Uliona roboti hii ikisonga kwa mwendo wa kasi sana, sivyo? Kimeng’enya husonga kwenye ‘njia’ ya DNA kwa kiwango cha vipago au pea za msingi 100 hivi kwa kila sekunde.23 Ikiwa ‘njia’ hiyo ingekuwa na ukubwa wa reli, ‘injini’ hiyo ingekuwa ikikimbia kwa mwendo wa zaidi ya kilomita 80 kwa saa. Katika bakteria, mashini za kunakili zinaweza kusonga kwa kasi mara kumi zaidi ya mwendo huo! Katika chembe ya mwanadamu, mamia ya mashini hizo za kunakili hufanya kazi katika sehemu tofauti-tofauti kando ya ‘njia’ ya DNA. Mashini hizo hunakili chembe zote za uhai kwa saa nane tu.”24 (Ona sanduku “Molekuli Inayoweza Kusomwa na Kunakiliwa,” katika ukurasa wa 20.)

“KUSOMA” DNA

Roboti za kunakili DNA zinabingirika na kuondoka jukwaani. Mashini nyingine inatokea. Hiyo pia inasonga katika mtanuko wa DNA, lakini polepole. Unaona kamba ya DNA ikiingia upande mmoja wa ile mashini na kutokea upande mwingine—bila kubadilika. Lakini uzi mmoja mpya unatokea kwenye tundu tofauti la mashini hiyo kama mkia unaoota. Ni nini kinachoendelea?

Tena msimuliaji anafafanua: “Kazi ya pili ya DNA ni kurekodi. DNA haiondoki ndani ya kiini. Hivyo basi, chembe zake za urithi—viambato vya protini vinavyofanyiza mwili wako—zinaweza kusomwa na kutumiwa jinsi gani? Mashini hiyo ya vimeng’enya inapata mahali kando ya DNA ambapo chembe ya urithi ilikuwa imewashwa na kemikali zinazoingia kutoka nje ya kiini cha chembe. Kisha mashini hiyo inatumia molekuli inayoitwa RNA (ribonucleic acid) kutengeneza nakala ya chembe hiyo ya urithi. Molekuli ya RNA inafanana sana na uzi mmoja wa DNA, lakini zinatofautiana. Kazi yake ni kuchukua habari zilizo ndani ya chembe za urithi. Molekuli ya RNA inapokea habari hiyo ikiwa ndani ya mashini ya kimeng’enya, kisha inaondoka kwenye kiini na kwenda kwa mojawapo ya ribosomu ambapo habari hiyo itatumiwa kutengeneza protini.”

Unapoendelea kutazama onyesho hilo, unajawa na mshangao. Unavutiwa sana na jumba hilo la makumbusho na ujuzi wa waliochora ramani yake na kujenga mitambo yake. Lakini namna gani ikiwa jumba hilo lote pamoja na vifaa vyote vilivyomo vingeanza kutenda, vikionyesha kazi nyingi mbalimbali zinazofanyika ndani ya chembe ya mwanadamu wakati uleule mmoja? Hilo lingekuwa onyesho lenye kustaajabisha kama nini!

Hata hivyo, unagundua kwamba mambo hayo yote yanayofanywa na mashini ndogo lakini tata sana yanaendelea sasa hivi ndani ya chembe zako trilioni 100! DNA yako inasomwa, ikitoa maagizo ya kutengeneza mamia ya maelfu ya protini tofauti-tofauti zinazofanyiza mwili wako—vimeng’enya vyake, tishu, viungo, na kadhalika. Sasa hivi DNA yako inanakiliwa na kusahihishwa ili kupata maagizo mengine mapya yatakayosomwa katika kila chembe mpya.

KWA NINI UKWELI HUU NI MUHIMU?

Acheni tujiulize tena, ‘Maagizo yote hayo yalitoka wapi?’ Biblia inasema kwamba “kitabu” hiki pamoja na maandishi yake yanatokana na Mwandikaji anayepita uwezo wa mwanadamu. Je, kauli hiyo imepitwa na wakati au haipatani na sayansi?

Fikiria hili: Wanadamu wanaweza hata kujenga jumba hilo ambalo tumezungumzia? Ikiwa wangejaribu, wangekumbana na matatizo mengi. Mambo mengi kuhusu chembe za urithi za mwanadamu na jinsi zinavyofanya kazi hayajaeleweka bado. Wanasayansi bado wanajaribu kuelewa mahali chembe zote za urithi zinapatikana na kazi zake. Nazo chembe za urithi zina sehemu ndogo tu ya uzi wa DNA. Namna gani ile mitanuko mingine isiyo na chembe za urithi? Wanasayansi wameiita mitanuko hiyo, DNA zisizohitajiwa, hata hivyo, hivi karibuni wamekuwa wakirekebisha maoni hayo. Huenda mitanuko hiyo ikadhibiti jinsi na kwa kadiri gani chembe za urithi zinavyotumika. Hata kama wanasayansi wangetengeneza mfano kamili wa DNA na mashini za kunakili na kusahihisha, je, wangeweza kuufanya ufanye kazi kama DNA halisi?

Mwanasayansi mashuhuri Richard Feynman aliacha ujumbe huu ubaoni muda mfupi kabla ya kifo chake: “Kile ambacho siwezi kutengeneza, sikielewi.”25 Unyenyekevu wake unavutia na maneno yake ni ya kweli kabisa kuhusiana na DNA. Wanasayansi hawawezi kutengeneza DNA pamoja na uwezo wake wa kujinakili na kujirekodi; wala hawawezi kuielewa kikamili. Hata hivyo, wengine hudai kwamba wanajua ilijitokeza yenyewe bila kuelekezwa. Je, kweli uthibitisho ambao umechunguza unaunga mkono kauli hiyo?

Wasomi fulani wameamua kwamba uthibitisho huo una maana tofauti. Kwa mfano, Francis Crick, mwanasayansi aliyegundua kwamba DNA inafanana na ngazi ya mzunguko, aliamua kwamba molekuli hiyo imepangwa kwa utaratibu sana hivi kwamba haiwezi kuwa ilijitokeza yenyewe bila kufuata mpangilio maalum. Alipendekeza kwamba huenda viumbe fulani wenye akili kutoka nje ya dunia vilituma DNA duniani ili kuanzisha uhai.26

Hivi karibuni zaidi, mwanafalsafa mashuhuri Antony Flew, aliyeunga mkono fundisho la kwamba hakuna Mungu kwa miaka 50, alibadili maoni yake. Akiwa na umri wa miaka 81 alikiri kwamba mtu fulani mwenye akili aliumba uhai. Kwa nini alibadili maoni yake? Baada ya kuichunguza DNA. Alipoambiwa kwamba huenda maoni yake mapya yasikubaliwe na wanasayansi, inasemekana Flew alijibu: “Inasikitisha. Maishani mwangu nimeongozwa na kanuni . . . fuata uthibitisho, popote utakapokuelekeza.”27

Una maoni gani? Uthibitisho unaelekeza wapi? Wazia kwamba umepata chumba cha kompyuta katikati mwa kiwanda. Kompyuta hiyo inaendesha programu tata inayoelekeza kazi zote kiwandani. Isitoshe, programu hiyo daima inatuma maagizo kuhusu jinsi ya kuunda na kudumisha kila mashini, nayo inajinakili na kujisahihisha. Uthibitisho huo utakusaidia ufikie mkataa gani? Kwamba kompyuta hiyo na programu yake vilijitengeneza vyenyewe, au kwamba vilitengenezwa na watu wenye utaratibu na akili? Uthibitisho uko wazi.

[Maelezo ya Chini]

a Kitabu Molecular Biology of the Cell hutumia kipimo tofauti. Kinasema kwamba kujaribu kupanga nyuzi hizo ndefu ndani ya kiini cha chembe ni kama kujaribu kupanga uzi mwembamba sana wenye urefu wa kilomita 40 ndani ya mpira wa tenisi—lakini kwa utaratibu mzuri hivi kwamba kila sehemu ya uzi huo inaweza kufikiwa kwa urahisi.

b Kila chembe ina nakala mbili kamili za chembe za urithi, jumla ya kromosomu 46.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 20]

MOLEKULI INAYOWEZA KUSOMWA NA KUNAKILIWA

DNA inaweza kusomwa na kunakiliwa bila kukosea jinsi gani? Kemikali nne zinazotumika katika ngazi ya DNA—A, T, G, na C—hufanyiza kila kipago cha ngazi kwa kujipanga kwa mpangilio uleule: A na T, G na C. Ikiwa upande mmoja wa kipago ni A, nyakati zote ule upande mwingine ni T; na nyakati zote G hukutana na C. Kwa hiyo, ikiwa una upande mmoja wa ngazi, unaujua ule upande mwingine. Upande mmoja wa ngazi ukiwa GTCA, lazima ule upande mwingine uwe CAGT. Vipago hivyo nusu-nusu hutofautiana kwa urefu, lakini vinapoungana, vinafanyiza vipago kamili vyenye urefu ulio sawa.

Kujua ukweli huo kuliwasaidia wanasayansi kugundua ukweli mwingine kuhusu molekuli hii yenye kustaajabisha: DNA ina uwezo wa kunakiliwa tena tena. Mashini ya kimeng’enya ambayo hunakili DNA huchukua elementi zinazoelea za zile kemikali nne kutoka kwenye kiini. Kisha inazitumia kukamilisha kila kipago kwenye uzi uliogawanyika wa DNA.

Hivyo basi, molekuli ya DNA ni kama kitabu kinachosomwa na kunakiliwa tena na tena. Kwa wastani, katika maisha ya mwanadamu, nakala za DNA hufanyizwa mara 10,000,000,000,000,000 hivi. Inashangaza kwamba licha ya kufanyizwa mara nyingi hivyo, nakala hizo hufanana sana na za awali.28

[Sanduku katika ukurasa wa 21]

UKWELI WA MAMBO NA MASWALI

◼ Ukweli wa mambo: Molekuli ya DNA imetiwa ndani ya kromosomu kwa njia yenye utaratibu sana hivi kwamba imeitwa “mafanikio ya kihandisi.”

Swali: Utaratibu wa aina hiyo ungeweza kujitokezaje wenyewe bila kuelekezwa?

◼ Ukweli wa mambo: Hakuna kompyuta yoyote leo iliyo na uwezo mkubwa wa kuhifadhi habari kama DNA.

Swali: Ikiwa mafundisanifu wa kompyuta hawawezi kuwa na matokeo kama hayo, kitu kisicho na akili kingeweza kufanya hivyo jinsi gani bila kuongozwa?

◼ Ukweli wa mambo: DNA ina maagizo yote yanayohitajika kutokeza mwili usio na kifani wa mwanadamu na kuudumisha katika maisha yake yote.

Swali: Maandishi hayo yangetokeaje bila mwandikaji, programu hiyo ingetokeaje bila mtengenezaji wa programu?

◼ Ukweli wa mambo: Ili DNA ifanye kazi, lazima inakiliwe, isomwe, na kusahihishwa na kikundi cha molekuli tata zinazoitwa vimeng’enya, ambavyo lazima vishirikiane kwa utaratibu wa hali ya juu na upesi sana.

Swali: Je, unaamini kwamba mitambo ya hali ya juu sana na yenye kutegemeka inaweza kujitokeza yenyewe? Bila uthibitisho kamili, je, hiyo haingekuwa sawa na kuwa na imani bila msingi?

[Mchoro katika ukurasa wa 14, 15]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

“Mafanikio ya uhandisi”

Jinsi DNA Inavyopangwa

Kupanga DNA ndani ya kiini ni mafanikio makubwa ya kihandisi—kama vile kupanga uzi wenye urefu wa kilomita 40 ndani ya mpira wa tenisi

[Mchoro katika ukurasa wa 16, 17]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Kutoa Nakala

Jinsi DNA Inavyonakiliwa

1 Sehemu hii ya mashini ya kimeng’enya hugawanya DNA katika nyuzi mbili tofauti

2 Sehemu hii ya mashini huchukua uzi wa DNA na kuutumia kama kigezo cha kutengeneza uzi wenye nyuzi mbili

3 Kibanio chenye umbo la mviringo ambacho huongoza na kuimarisha mashini ya kimeng’enya

4 Nyuzi mbili zilizokamilika za DNA zinatengenezwa

Ikiwa DNA ingekuwa na ukubwa wa reli, mashini ya kimeng’enya ingesafiri kwa mwendo wa zaidi ya kilomita 80 hivi kwa saa

[Mchoro katika ukurasa wa 18, 19]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Kurekodi

Jinsi DNA “Inavyosomwa”

1 Hapa DNA haijanyooshwa. Uzi unaoonekana hupeleka habari kwa RNA

2 RNA “husoma” DNA, na kuchukua habari zilizo ndani ya chembe ya urithi. DNA huiambia mashini ya kurekodi mahali itakapoanzia kurekodi na itakapomalizia

3 Ikiwa na habari nyingi, RNA huondoka kwenye kiini cha chembe na kwenda kwenye ribosomu, ambapo inapeleka maagizo kuhusu jinsi ya kutengeneza protini tata

4 Mashini ya kurekodi

[Picha katika ukurasa wa 18]

Gramu moja ya DNA ina habari nyingi zinazoweza kutoshea katika diski trilioni moja

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki