Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g 11/11 kur. 4-6
  • Chunguza Uthibitisho

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Chunguza Uthibitisho
  • Amkeni!—2011
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Je, Habari Tata Inaweza Kujiandika Yenyewe?
  • Ni Nani Aliyefanyiza “Maktaba” Hiyo?
  • Je, Kweli Ni DNA “Zisizohitajika”?
  • Kazi ya DNA “Zisizohitajiwa”
  • Maagizo Yalitoka Wapi?
    Maswali Matano Muhimu Kuhusu Chanzo cha Uhai
  • Chembe Zako​—Maktaba Iliyo Hai!
    Amkeni!—2015
  • Je, Kuna DNA Zisizohitajiwa?
    Amkeni!—2005
  • Uhai Ulianzaje?
    Amkeni!—1999
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—2011
g 11/11 kur. 4-6

Chunguza Uthibitisho

UKO katika kisiwa kilicho mbali sana ambacho hakina watu. Unapotembea ufuoni, unaona maandishi “John 1800” yakiwa yamechongwa kwenye mwamba. Kwa kuwa kisiwa hicho kiko mbali na hakina watu, je, ungekata kauli kwamba maandishi hayo yalitokezwa na mmomonyoko uliosababishwa na upepo au maji? Bila shaka la! Ungekata kauli kwamba mtu fulani alichonga maandishi hayo. Kwa sababu gani? Kwanza, kwa sababu nambari na herufi zinazoonekana waziwazi, hata kama zimeandikwa katika lugha ya kigeni, haziwezi kujitokeza zenyewe. Pili, maandishi hayo yana maana, na hilo linaonyesha kwamba yaliandikwa na mtu mwenye akili.

Kila siku, tunapata habari zilizoandikwa katika njia mbalimbali—kama vile maandishi ya vipofu (Braille) au herufi za alfabeti, na pia michoro, noti za muziki, maneno, ishara za mkono, mawimbi ya redio, na programu za kompyuta zinazotumia binari, yaani, nambari moja kadhaa na sufuri kadhaa. Habari inaweza kupitishwa kwa njia yoyote ile, iwe ni kwa mawimbi ya mwangaza au ya redio au iwe imeandikwa kwa wino kwenye karatasi. Vyovyote vile, kwa kawaida watu hutambua kwamba habari muhimu iliandikwa na mtu fulani mwenye akili, lakini inashangaza kwamba wengi wanashindwa kutambua hilo habari hiyo inapokuwa imeandikwa ndani ya chembe iliyo hai. Wanamageuzi wanasema kwamba habari iliyo ndani ya chembe ilijitokeza au kujiandika yenyewe. Lakini, je, hilo ni kweli? Hebu chunguza uthibitisho.

Je, Habari Tata Inaweza Kujiandika Yenyewe?

Kiini cha kila chembe iliyo hai katika mwili wako kina habari fulani yenye kustaajabisha inayoitwa deoksiribonyukilia asidi, au kwa ufupi DNA. Habari hizo zimehifadhiwa katika molekuli ndefu yenye nyuzi mbili inayofanana na ngazi iliyojipinda. DNA yako ni kama maagizo ya upishi, au programu ambayo inaongoza kutokezwa, kukua, kudumishwa, na kujigawanya kwa matrilioni ya chembe zinazofanyiza mwili wako. Molekuli za DNA zimefanyizwa kwa molekuli ndogo zinazoitwa nukliotidi. Molekuli hizo ndogo zinawakilishwa na herufi A, C, G, na T, ikitegemea kemikali zinazozifanyiza.a Kama herufi za alfabeti, herufi hizo nne zinaweza kuunganishwa katika njia mbalimbali na kufanyiza “sentensi,” yaani maagizo ambayo huongoza kunakiliwa kwa molekuli ya DNA na utendaji mwingine ndani ya chembe.

Habari yote iliyohifadhiwa katika DNA yako inaitwa genome. Herufi fulani zinapatikana tu katika DNA yako kwa kuwa DNA yako ina habari kukuhusu wewe tu kama vile, rangi ya macho yako, rangi ya ngozi yako, umbo la pua lako, na kadhalika. Kwa ufupi, genome yako inaweza kufananishwa na maktaba kubwa yenye habari kuhusu kila sehemu ya mwili wako, ambayo inakufanyiza wewe.

“Maktaba” hiyo ni kubwa kadiri gani? Ina urefu wa “herufi,” au nukliotidi, bilioni tatu hivi. Kulingana na Mradi wa Kuchunguza Chembe za Urithi za Mwanadamu, ikiwa herufi hizo zingeandikwa kwenye karatasi, zingejaza mabuku yapatayo 200, kila buku likitoshana na kitabu chenye anwani na nambari za simu chenye kurasa 1,000.

Hilo linatukumbusha sala moja iliyoandikwa miaka 3,000 hivi iliyopita. Sala hiyo inayopatikana katika kitabu cha Biblia cha Zaburi 139:16 inasema hivi: “Macho yako yalikiona kiini-tete changu, na katika kitabu chako sehemu zake zote zilikuwa zimeandikwa.” Bila shaka, mwandikaji huyo hakuwa akizungumzia mambo kwa njia ya sayansi, lakini kwa maneno rahisi anazungumzia hoja sahihi inayoonyesha hekima na nguvu za ajabu za Mungu. Sala hiyo ni tofauti kabisa na maandishi ya kale ya kidini yaliyojaa hekaya na ushirikina!

Ni Nani Aliyefanyiza “Maktaba” Hiyo?

Ikiwa ni jambo linalopatana na akili kuamini kwamba maandishi “John 1800” yaliyochongwa kwenye mwamba yaliandikwa na mtu mwenye akili, je, haipatani na akili hata zaidi kuamini kwamba habari tata sana na iliyo muhimu inayopatikana kwenye DNA iliandikwa na mtu mwenye akili? Isitoshe, habari ni habari haidhuru inapatikana wapi au imepitishwa kwa njia gani. Donald E. Johnson, ambaye ni mtaalamu wa kompyuta na habari alisema kwamba kulingana na sheria za kemia na fizikia, habari au mfumo unaochanganua habari hauwezi kujitokeza wenyewe. Na inapatana na akili kwamba kadiri habari ilivyo tata, ndivyo inavyohitaji mtu mwenye akili zaidi kuiandika. Mtoto anaweza kuandika “John 1800.” Lakini ni mtu mwenye akili inayopita ya mwanadamu anayeweza kuandika maagizo ya uhai. Isitoshe, “kadiri tunavyojifunza kuhusu mwili wa mwanadamu, ndivyo uvumbuzi huo mpya unavyozidi kututatanisha,” linasema jarida Nature.

Kusema kwamba maktaba tata yenye habari za DNA ilijitokeza yenyewe bila kuelekezwa na mtu yeyote hakupatani na akili na ufahamu wa wanadamu.b Imani hiyo haina msingi.

Wakijaribu kuonyesha kwamba hakuna Mungu, nyakati nyingine wanamageuzi wamefikia mkataa ambao baadaye ulionekana kuwa wenye makosa. Fikiria kwa mfano maoni ya kwamba asilimia 98 hivi ya habari zilizo katika DNA yetu “hazihitajiki.” Hilo linamaanisha kwamba maktaba hiyo ya maagizo ina mabilioni ya maneno yasiyo na maana.

Je, Kweli Ni DNA “Zisizohitajika”?

Kwa miaka mingi, wanabiolojia waliamini kwamba DNA ina maagizo ya kutengeneza protini peke yake. Hata hivyo, baada ya muda, iligunduliwa kwamba ni asilimia 2 tu ya DNA iliyo na maagizo ya kutengeneza protini. Asilimia ile nyingine 98 ya DNA hufanya kazi gani? Watu wengi walikata kauli kwamba DNA hizo zisizojulikana “hazihitajiwi kwa sababu ni habari za ziada zilizosalia baada ya mageuzi kukamilika,” akasema John S. Mattick, profesa wa Biolojia ya Molekuli katika Chuo Kikuu cha Queensland huko Brisbane, Australia.

Mwanamageuzi Susumu Ohno, ndiye aliyeanzisha usemi “DNA ‘zisizohitajiwa.’” Katika makala yake yenye kichwa “DNA Nyingi Sana ‘Zisizohitajiwa’ Katika Genome Yetu” (“So Much ‘Junk’ DNA in Our Genome”), alisema kwamba mfuatano wa DNA zinazosalia “ni mabaki ya majaribio ya kiasili ambayo hayakufanikiwa. Dunia imejaa mabaki ya wanyama waliotoweka zamani; je, ni ajabu kwamba mwili wetu umejaa mabaki ya chembe za urithi ambazo hazihitajiwi tena?”

Nadharia ya kwamba kuna DNA “zisizohitajiwa” iliathiri kwa njia gani uchunguzi wa chembe za urithi? Wojciech Makalowski, mwanabiolojia wa molekuli anasema kwamba maoni hayo “yaliwazuia watafiti wengi wasichunguze DNA [zisizohitajiwa] ambazo hazitengenezi protini,” isipokuwa wanasayansi wachache sana ambao, “wakiwa katika hatari ya kudhihakiwa, walichunguza DNA hizo ambazo hazikuwa zimewahi kuchunguzwa. Kwa sababu ya uchunguzi wao, maoni kuhusu DNA zisizohitajiwa . . . yalianza kubadilika mwanzoni mwa miaka ya 1990.” Anaongezea kusema kwamba siku hizi wanabiolojia huziona DNA hizo ambazo zilisemekana hazihitajiwi kuwa “hazina ya chembe za urithi.”

Mattick anasema kwamba nadharia ya DNA zisizohitajiwa ni mfano bora zaidi unaoonyesha jinsi watu hufuata maoni ya watu wengi “badala ya kuchunguza mambo ya hakika.” “Kukosa kutambua matokeo ya kukata kauli kwa njia hiyo,” anaongezea, “kunaweza kuwa mojawapo ya makosa makubwa zaidi katika biolojia ya molekuli.” Ni wazi kwamba mikataa ya kisayansi inapaswa kufikiwa kwa kutegemea uthibitisho uliopo si kwa kufuata maoni ya watu wengi. Kwa msingi wa hilo, uthibitisho wa hivi karibuni umefunua nini kuhusu kazi ya DNA “zisizohitajiwa”?

Kazi ya DNA “Zisizohitajiwa”

Kiwanda cha kutengeneza magari hutumia mashini kutengeneza sehemu za magari. Tunaweza kufananisha sehemu hizo na protini katika chembe. Kiwanda hicho pia kinahitaji vifaa na mifumo ambayo itaunganisha sehemu hizo hatua kwa hatua na mitambo ya kuongoza, au kudhibiti kuunganishwa kwa sehemu hizo. Ndivyo ilivyo na utendaji ndani ya chembe. Watafiti wanasema kwamba hiyo ndiyo kazi ya DNA “zisizohitajiwa.” Nyingi ya DNA hizo zina maagizo ya molekuli tata inayoitwa RNA (ribonucleic acid), ambayo hudhibiti ukuzi na utendaji wa chembe.c Mwanabiolojia na mwanahisabati Joshua Plotkin, anasema hivi katika gazeti Nature: “Kuwepo kwa molekuli hizo zinazodhibiti ukuzi kunaonyesha kwamba uelewaji wetu wa mambo ya msingi . . . ni mdogo sana.”

Ili kiwanda kifanye kazi vizuri kinahitaji pia mfumo mzuri wa mawasiliano. Ndivyo ilivyo na chembe. Tony Pawson, mtaalamu wa chembe katika Chuo Kikuu cha Toronto huko Ontario, anaeleza: “Badala ya kutumia njia rahisi na ambazo hazijaungana, chembe hutumia mtandao tata sana wa kupitisha habari,” na hivyo kufanya mfumo wote “kuwa tata sana” kuliko ilivyodhaniwa awali. Kwa kweli, kama alivyosema mtaalamu mmoja wa chembe za urithi katika Chuo Kikuu cha Princeton, “utendaji na maagizo yanayoongoza yale yanayotukia ndani ya chembe na kudhibiti jinsi chembe zinavyofanya kazi pamoja bado ni fumbo.”

Kila uvumbuzi mpya kuhusu chembe unaonyesha utaratibu na ustadi wa hali ya juu. Hivyo basi kwa nini watu wengi bado wanashikilia dhana ya kwamba uhai na mfumo wa habari wa hali ya juu ulitokezwa na mageuzi yasiyo na mpangilio?

[Maelezo ya Chini]

a Kila nukliotidi imefanyizwa kwa mojawapo ya kemikali nne za msingi: (A) adenine, (C) cytosine, (G) guanine, na (T) thymine.

b Inasemekana kwamba mageuzi yanatokana na mabadiliko katika chembe za urithi wa vitu vilivyo hai. Mambo hayo yatazungumziwa kwa ufupi katika makala inayofuata.

c Utafiti wa hivi karibuni unaonyesha kwamba RNA ndefu ambazo hazitokezi protini ni tata sana na kwamba zinahitajiwa kwa ukuzi wa kawaida. Watafiti wamegundua kwamba kasoro fulani katika RNA hizo zinahusianishwa na magonjwa mengi kama vile aina fulani za kansa, magonjwa ya ngozi, na hata ugonjwa wa Alzheimer. DNA ambazo hapo awali zilionekana kuwa “hazihitajiwi” huenda zikatumiwa katika kugundua na kutibu magonjwa mbalimbali!

[Sanduku katika ukurasa wa 5]

DNA YAKO NI NDEFU KADIRI GANI?

DNA katika chembe moja mwilini mwako inaponyooshwa ina urefu wa mita 2 hivi. Ikiwa ungechukua DNA zote zilizo katika matrilioni ya chembe mwilini mwako na kuzinyoosha na kuziunganisha moja baada ya nyingine, inakadiriwa kwamba zingekuwa na urefu wa kutoka duniani hadi kwenye jua na kurudi karibu mara 670. Kusafiri umbali huo kwa mwendo wa nuru kutachukua saa 185 hivi.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki