Ujenzi wa Kimataifa wa Majumba ya Ufalme Katika Nchi Fulani za Ulaya
1 Kazi ya Mashahidi wa Yehova ilikuwa imepigwa marufuku katika miongo ya miaka iliyopita katika nchi kadhaa za Ulaya, kutia ndani Ulaya Mashariki. Marufuku ilikuwa kali katika nchi nyingi. Ilikuwa vigumu kufanya mikutano hadharani, na mara nyingi haikuwezekana kuwa na Jumba la Ufalme la kufanyia mikutano. Hata hivyo, katika miaka ya majuzi, ‘BWANA ametutendea mambo makuu, tumekuwa tukifurahi.’—Zab. 126:3.
2 Mashahidi wa Yehova walianza kupata uhuru hatua kwa hatua mwaka wa 1983. Nchi ya Poland na Hungaria zilihalalisha dini ya Mashahidi wa Yehova mwaka wa 1989. Dini ya Mashahidi wa Yehova ilihalalishwa nchini Urusi mwaka wa 1991. Tangu wakati huo, wameongezeka sana nchini Urusi na katika nchi nyingine zilizokuwa sehemu ya Muungano wa Sovieti. Kati ya Machi 1996 na Oktoba 1998, Baraza Linaloongoza liliidhinisha maombi ya mikopo 359 ya ofisi za tawi za nchi 11 huko Ulaya kwa ajili ya Majumba ya Ufalme.
3 Unapotazama picha katika nyongeza hii, tafakari mambo makuu ya ajabu ambayo Yehova amewafanyia watu wake. (Zab. 136:4) Utafurahi kujua kwamba pesa ambazo zimechangwa na ndugu ulimwenguni pote hutumiwa kwa njia inayofaa kabisa, kupatana na maneno ya Yesu katika Yohana 13:35: “Kwa hilo wote watajua kwamba nyinyi ni wanafunzi wangu, mkiwa na upendo miongoni mwenu wenyewe.”
4 Rumania ni mojawapo ya nchi za Ulaya zinazofaidika na mpango wa kusaidia kujenga Majumba ya Ufalme katika nchi zenye matatizo ya uchumi. Majumba ya Ufalme 36 yamejengwa katika nchi hiyo tangu Julai 2000. Nchini Ukrainia, ramani ileile ya ujenzi ilitumiwa katika ujenzi wa karibu Majumba yote ya Ufalme 61 yaliyojengwa mwaka wa 2001, na yale 76 yaliyojengwa mwaka wa 2002. Pesa ambazo zimechangwa kwa ajili ya Hazina ya Majumba ya Ufalme zimetumiwa kujenga mamia ya Majumba ya Ufalme huko Bulgaria, Kroatia, Makedonia, Moldova, Urusi, Serbia na Montenegro.
5 Kujenga Majumba ya Ufalme katika nchi fulani si kazi rahisi, na kazi nyingi hufanywa kabla ya ujenzi wenyewe kuanza. Mara nyingi matayarisho hayo huchukua muda mrefu. Isitoshe, gharama ya kujenga Jumba la Ufalme katika sehemu hiyo ya Ulaya ni ya juu sana kuliko gharama ya ujenzi katika sehemu mbalimbali za Afrika na Amerika Kusini. Hata hivyo, kwa sababu ya ongezeko kubwa la idadi ya waabudu wa Yehova, mamia ya Majumba ya Ufalme bado yanahitajiwa katika nchi za Ulaya zenye matatizo ya uchumi!
6 Inafurahisha sana kuona jinsi Majumba mengi ya Ufalme yanavyojengwa kwa haraka! Mambo mengi yaliyoonwa yanaonyesha kwamba watu wanaoishi karibu na Majumba hayo ya Ufalme wamepata ushahidi mzuri kupitia ujenzi huo. Katika maeneo fulani watu wenye mamlaka huvutiwa kuona jinsi wajenzi wanavyokubali kwa utayari kufuata matakwa ya kisheria ya ujenzi.
7 Kwa kufaa, Isaya alitoa unabii kuhusu ongezeko la ibada ya kweli wakati wetu. Mungu alitabiri hivi kupitia nabii huyo: “Mimi, BWANA, nitayahimiza hayo wakati wake.” (Isa. 60:22) Bila shaka Yehova ameleta ongezeko huko Ulaya Mashariki katika miaka kumi iliyopita. Yehova na aendelee kubariki jitihada zetu za kujenga Majumba ya Ufalme hata haraka zaidi katika nchi nyingi, huku tukiendelea kutoa michango kwa ajili ya Hazina ya Majumba ya Ufalme! Kwa njia hiyo Majumba ya Ufalme mengi zaidi yatajengwa katika nchi zenye matatizo ya uchumi. Ujenzi huo utachangia ongezeko la ibada ya kweli katika sehemu nyingi za Ulaya, na ushahidi mkubwa utatolewa hadi “ncha ya dunia.”—Mdo. 13:47.
[Picha katika ukurasa wa 3]
Jengo lenye Majumba kadhaa ya Ufalme Moscow, Urusi
[Picha katika kurasa za 4-6]
Majumba Mapya ya Ufalme Huko Ulaya Mashariki
Strumica, Makedonia
Daruvar, Kroatia
Bitola, Makedonia
Sokal, Wilaya ya Lviv, Ukrainia
Sofia, Bulgaria
Krasnooktyabrskiy, Eneo la Maykop, Urusi
Bački Petrovac, Serbia na Montenegro
Plovdiv, Bulgaria
Tlumach, Wilaya ya Ivano-Frankivsk, Ukrainia
Rava-Ruska, Wilaya ya Lviv, Ukrainia
Stara Pazova, Serbia na Montenegro
Zenica, Bosnia na Herzegovina
Sokal, Wilaya ya Lviv, Ukrainia
Zhydachiv, Wilaya ya Lviv, Ukrainia