Marejeo ya Daftari la Mkutano wa Huduma na Maisha
JANUARI 7-13
HAZINA ZA NENO LA MUNGU | MATENDO 21-22
Kutafuta Hazina za Kiroho
nwtsty habari za utafiti—Mdo 22:16
uoshe dhambi zako kwa kuliitia jina lake: Au “safisha dhambi zako na uliitie jina lake.” Mtu atasafishwa dhambi zake, si kwa maji yanayotumiwa kumbatiza, bali kwa kuliitia jina la Yesu. Kufanya hivyo kunahusisha kuwa na imani katika Yesu na kuonyesha imani hiyo kwa matendo ya Kikristo.—Mdo 10:43; Yak 2:14, 18.
JANUARI 14-20
HAZINA ZA NENO LA MUNGU | MATENDO 23-24
Kutafuta Hazina za Kiroho
nwtsty habari za utafiti—Mdo 23:6
mimi ni Farisayo: Baadhi ya watu waliokuwepo walimjua Paulo. (Mdo 22:5) Wangeelewa kwamba kwa kujiita mwana wa Mafarisayo, alikuwa akionyesha kwamba alikuwa na elimu na utamaduni kama wao. Walielewa kwamba Paulo hakuwa akijitambulisha kimakosa, kwa kuwa Mafarisayo katika Sanhedrini walijua kwamba alikuwa amegeuka na kuwa Mkristo mwenye bidii. Lakini katika muktadha huu, maneno ya Paulo kuhusu kuwa Farisayo hayapaswi kueleweka kihalisi; Paulo alikuwa akionyesha kwamba kama Mafarisayo yeye pia aliamini kuna ufufuo tofauti na Masadukayo ambao hawakuuamini. Kwa kufanya hivyo, alitaja jambo alilokubaliana na Mafarisayo waliokuwepo. Inaonekana alitumaini kwamba kuzusha suala hilo lililobishaniwa sana kungefanya baadhi ya washiriki wa Sanhedrini waunge mkono hoja zake, na mbinu yake ilifanikiwa. (Mdo 23:7-9) Maneno ya Paulo kwenye Mdo 23:6 pia yanalingana na jinsi alivyojieleza alipojitetea baadaye mbele ya Mfalme Agripa. (Mdo 26:5) Na alipowaandikia Wakristo wenzake jijini Filipi akiwa Roma, kwa mara nyingine Paulo alitaja kwamba zamani alikuwa Farisayo. (Flp 3:5) Pia inapendeza kuona jinsi Wakristo wengine ambao zamani walikuwa Mafarisayo wanavyorejelewa katika Mdo 15:5.—Tazama habari za utafiti kwenye Mdo 15:5.
nwtsty habari za utafiti—Mdo 24:24
Drusila: Alikuwa binti mdogo zaidi na wa tatu wa Herode anayetajwa kwenye Mdo 12:1, yaani, Herode Agripa wa Kwanza. Alizaliwa mwaka wa 38 W.K. hivi na alikuwa dada ya Agripa wa Pili na Bernike. (Tazama habari za utafiti kwenye Mdo 25:13 na Kamusi, “Herode.”) Gavana Feliksi alikuwa mume wake wa pili. Mwanzoni aliolewa na Mfalme Azizus wa Emesa ambaye alikuwa Msiria, lakini alimtaliki na kuolewa na Feliksi mwaka wa 54 W.K., yaani, alipokuwa na umri wa miaka 16 hivi. Inawezekana alikuwepo Paulo alipozungumza mbele ya Feliksi “kuhusu uadilifu na kujizuia na hukumu itakayokuja.” (Mdo 24:25) Feliksi alipomwachia Festo cheo cha gavana, alimwacha Paulo akiwa mfungwa kwa sababu “alitamani kukubaliwa na Wayahudi,” na watu fulani wanafikiri alifanya hivyo ili kumpendeza mke wake mwenye umri mdogo, ambaye alikuwa Myahudi.—Mdo 24:27.
JANUARI 21-27
HAZINA ZA NENO LA MUNGU | MATENDO 25-26
Kutafuta Hazina za Kiroho
nwtsty habari za utafiti—Mdo 26:14
kuipiga teke michokoo: Mchokoo ni fimbo yenye ncha inayotumiwa kumwelekeza mnyama. (Amu 3:31) Maneno “kuipiga teke michokoo” ni methali inayopatikana katika vitabu vya Kigiriki. Inatusaidia kupiga picha ya ng’ombe dume mkaidi anayekataa kuelekezwa na mchokoo kwa kuupiga teke na hivyo kujiumiza. Sauli alitenda kwa njia kama hiyo kabla ya kuwa Mkristo. Kwa kupigana na wafuasi wa Yesu, ambao walikuwa na kibali cha Yehova Mungu, Paulo alikuwa karibu kujiumiza vibaya sana. (Linganisha Mdo 5:38, 39; 1Ti 1:13, 14.) Katika Mhu 12:11, “michokoo ya kuongozea ng’ombe” inatajwa kwa njia ya mfano, ikirejelea maneno yanayosemwa na mtu mwenye hekima ambayo yanamchochea msikilizaji kufuata shauri.
nwt kamusi
Mchokoo. Fimbo ndefu yenye ncha kali ya chuma, iliyotumiwa na wakulima kumwongoza mnyama kwa kumdungadunga nayo. Maneno ya mtu mwenye hekima yanayomchochea msikilizaji kutii ushauri wenye hekima yanafananishwa na mchokoo. “Kuipiga teke michokoo” ni maneno yanayoleta taswira ya ng’ombe dume mkaidi anayekataa kufuata mwongozo wa mchokoo kwa kuupiga teke, na hivyo kujiumiza mwenyewe.—Mdo 26:14; Amu 3:31.
JANUARI 28–FEBRUARI 3
HAZINA ZA NENO LA MUNGU | MATENDO 27-28
Kutafuta Hazina za Kiroho
nwtsty habari za utafiti—Mdo 27:9
kufunga kwa Siku ya Kufunika Dhambi: Au “mfungo wa majira ya kupukutika.” Tnn., “ule mfungo.” Neno la Kigiriki linalotafsiriwa “ule mfungo” linarejelea ile sheria moja tu kuhusu kufunga katika Sheria ya Musa, yaani, kufunga katika kipindi cha Siku ya Kufunika Dhambi kila mwaka, ambayo pia inaitwa Yom Kippur (Kiebrania, yohm hak·kip·pu·rimʹ, “siku ya kufunika”). (Law 16:29-31; 23:26-32; Hes 29:7; tazama Kamusi, “Siku ya Kufunika Dhambi.”) Neno “kujitesa,” linalotumiwa kuhusiana na Siku ya Kufunika Dhambi, linaaminiwa kuwa linamaanisha kujinyima kwa njia mbalimbali, kutia ndani kufunga. (Law 16:29, maelezo ya chini.) Matumizi ya neno “kufunga” katika Mdo 27:9 yanalingana na wazo la kwamba njia kuu ya kujinyima katika Siku ya Kufunika Dhambi ilikuwa kutokula. Kufunga kwa Siku ya Kufunika Dhambi kulikuwa mwishoni mwa Septemba au mwanzoni mwa Oktoba.
nwtsty habari za utafiti—Mdo 28:11
Wana wa Zeu: Kulingana na hekaya za Kigiriki na Kiroma, “Wana wa Zeu” (Kigiriki, Di·oʹskou·roi) walikuwa Castor na Pollux, mapacha wa mungu Zeu (Jupiter) na Malkia Leda kutoka Sparta. Walisemekana kuwa walifanya mambo mengi kutia ndani kuwalinda mabaharia na kuwaokoa walipokabili hatari baharini. Habari hizo kuhusu sanamu iliyokuwa upande wa mbele wa meli hiyo ni uthibitisho mwingine kwamba simulizi hilo liliandikwa na mtu aliyejionea mambo hayo.