Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • mwbr22 Novemba kur. 1-5
  • Marejeo ya Daftari la Mkutano wa Huduma na Maisha

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Marejeo ya Daftari la Mkutano wa Huduma na Maisha
  • Marejeo ya Daftari la Mkutano wa Huduma na Maisha—2022
  • Vichwa vidogo
  • NOVEMBA 7-13
  • NOVEMBA 14-20
  • NOVEMBA 28–DESEMBA 4
  • DESEMBA 12-18
  • DESEMBA 19-25
  • DESEMBA 26–JANUARI 1
Marejeo ya Daftari la Mkutano wa Huduma na Maisha—2022
mwbr22 Novemba kur. 1-5

Marejeo ya Daftari la Mkutano wa Huduma na Maisha

NOVEMBA 7-13

HAZINA ZA NENO LA MUNGU | 2 WAFALME 5-6

“Walio Pamoja Nasi Ni Wengi Kuliko Walio Pamoja Nao”

it-1 716 ¶4

Elisha

Israeli Yaokolewa Kutoka kwa Siria. Wakati wa utawala wa Mfalme Yehoramu wa Israeli, Siria ilivamia Israeli kwa ghafla. Zaidi ya mara moja Elisha alifichua njama za Ben-hadadi wa Pili na kumfunulia Mfalme Yehoramu mbinu zote za Wasiria. Mwanzoni Ben-hadadi alifikiri kulikuwa na msaliti katika kambi yake. Lakini alipogundua chanzo cha matatizo yake, alituma jeshi kubwa Dothani, na kulizingira kwa farasi na magari ya vita ili kumkamata Elisha. (PICHA, Buku la 1, uk. 950) Mtumishi wa Elisha alishikwa na woga, lakini Elisha akasali kwa Mungu afungue macho ya mtumishi wake, “na tazama! eneo lenye milima lilikuwa limejaa farasi na magari ya vita ya moto kumzunguka Elisha pande zote.” Wasiria walipoanza kukaribia, Elisha akasali na kuomba muujiza wa aina tofauti, “Tafadhali, lipige kwa upofu taifa hili.” Kisha Elisha akawaambia Wasiria hivi: “Nifuateni,” lakini hakuhitaji kuwaongoza kwa kuwashika mkono, jambo linaloonyesha upofu huo ulikuwa wa kiakili na si upofu halisi. Hawakumtambua Elisha ambaye walikuwa wamekuja kumkamata, wala hawakutambua mahali ambapo alikuwa akiwapeleka.​—2Fa 6:8-19.

it-1 343 ¶1

Upofu

Ni wazi kwamba upofu ambao jeshi la Wasiria walipata kwa neno la Elisha ulikuwa upofu wa kiakili. Ikiwa askari wote katika jeshi hilo wangekuwa wamepigwa na upofu halisi, wangehitaji kuongozwa kwa mkono. Lakini simulizi hilo linasema kwamba Elisha aliwaambia hivi: “Njia yenyewe si hii, na jiji lenyewe si hili. Nifuateni.” William James anasema hivi kuhusu jambo hilo katika kitabu chake Principles of Psychology (1981, Buku la 1, uk. 59): “Jambo lenye kustaajabisha ni kwamba upofu wa kiakili hutokea wakati ambapo sehemu ya ubongo inayotambua mambo ambayo jicho linaona inaathiriwa. Hilo halimaanishi kwamba macho hayatambui mambo yanayoona, bali yanashindwa kuyaelewa. Kisaikolojia hali hiyo inafafanuliwa kuwa kushindwa kupatanisha mambo ambayo macho yanaona na maana ya mambo hayo; na wakati wowote ambapo sehemu ya ubongo inayopokea habari kutoka kwenye jicho inaposhindwa kuwasiliana na sehemu nyingine za ubongo zinazotathmini habari upofu huo hutokea.” Inaonekana kwamba huo ndio upofu ambao Yehova aliondoa wakati ambapo jeshi la Siria lilipofika Samaria. (2Fa 6:18-20) Huenda pia upofu huo wa kiakili ndio uliowapata wanaume wa Sodoma, kwa kuwa simulizi hilo linaonyesha kwamba badala ya kuhuzunika kwa kupoteza uwezo wao wa kuona, waliendelea kujaribu kutafuta mlango wa nyumba ya Loti.​—Mwa 19:11.

NOVEMBA 14-20

HAZINA ZA NENO LA MUNGU | 2 WAFALME 7-8

“Yehova Alifanya Jambo Lisilotarajiwa”

it-1 716-717

Elisha

Hata hivyo, baadaye, Ben-hadadi wa Pili alivamia, si kwa kundi dogo la wavamizi, bali kwa jeshi kubwa na kulizingira Samaria. Waliendelea kuzingira jiji hilo hadi hali ikawa mbaya sana hivi kwamba angalau kisa kimoja kiliripotiwa kwa mfalme cha mwanamke ambaye alimla mwana wake mwenyewe. Kwa kuwa Mfalme Yehoramu alikuwa mzao wa Ahabu, “mwana . . . wa muuaji,” aliapa kwamba atamuua Elisha. Lakini kiapo hicho kilichotolewa bila kufikiri hakikutekelezwa. Yehoramu alipofika nyumbani kwa nabii huyo akiwa na kamanda wake msaidizi, alisema kwamba amepoteza tumaini la kupata msaada kutoka kwa Yehova. Elisha alimhakikishia mfalme kwamba siku iliyofuata kungekuwa na chakula kingi sana. Kamanda msaidizi wa mfalme alidhihaki utabiri huo, hivyo Elisha akamwambia hivi: “Utaona kwa macho yako mwenyewe, lakini hutakula vyakula hivyo.” Yehova akatokeza kelele iliyosikika katika kambi ya Wasiria, nao wakaamini kwamba jeshi kubwa la mataifa yaliyoungana lilikuwa likija kuwashambulia. Kwa sababu hiyo wakatoroka na kuacha kambi iliyojaa chakula chao chote. Mfalme aliposikia kwamba Wasiria wamekimbia, alimweka kamanda wake msaidizi alinde lango la Samaria, lakini akakanyagwa-kanyagwa na umati wa Waisraeli wenye njaa walioharakisha kwenda kukusanya nyara kutoka kwenye kambi ya Wasiria hivi kwamba akafa. Aliona chakula chenyewe lakini hakula.​—2Fa 6:24–7:20.

Hazina za Kiroho

it-2 195 ¶7

Taa

Wafalme wa Ukoo wa Daudi. Yehova Mungu alimweka rasmi Mfalme Daudi akalie kiti cha ufalme cha Israeli, naye Daudi alithibitika kuwa kiongozi mwenye hekima wa taifa hilo, kwa kufuata mwongozo wa Mungu. Kwa sababu hiyo aliitwa “taa ya Israeli.” (2Sa 21:17) Alipofanya agano la ufalme pamoja na Daudi, Yehova aliahidi hivi: “Kiti chako cha ufalme kitaimarishwa kabisa milele.” (2Sa 7:11-16) Kwa sababu hiyo, watawala wa ukoo wa Daudi kupitia mwana wake Sulemani walikuwa kama “taa” kwa Israeli.​—1Fa 11:36; 15:4; 2Fa 8:19; 2Nya 21:7.

NOVEMBA 28–DESEMBA 4

HAZINA ZA NENO LA MUNGU | 2 WAFALME 11-12

“Mwanamke Mwovu, Aliyejitakia Makuu Aadhibiwa”

it-1 209

Athalia

Kama mama yake Yezebeli, Athalia alimchochea mume wake Yehoramu atende maovu machoni pa Yehova wakati wa utawala wake wa miaka minane. (1Fa 21:25; 2Nya 21:4-6) Pia, kama mama yake alivyotenda, Athalia alimwaga damu ya watu wasio na hatia. Mwana wake mwovu Ahazia alipokufa baada ya kutawala kwa mwaka mmoja, aliwaua wazao wote wa kifalme, isipokuwa Yehoashi aliyekuwa mtoto mchanga. Yehoashi alifichwa na kuhani mkuu na mke wake, ambaye alikuwa shangazi yake. Baada ya hapo, Athalia alijiweka rasmi kuwa malkia kwa miaka sita, m. 905-899 K.W.K. (2Nya 22:11, 12) Wana wake walipora vitu vitakatifu kutoka kwenye hekalu la Yehova na kuvitoa dhabihu kwa Baali.​—2Nya 24:7.

it-1 209

Athalia

Yehoashi alipotimiza umri wa miaka saba, Kuhani Mkuu Yehoyada aliyekuwa akimwogopa Mungu alimtoa nje na kumtawaza kuwa mrithi halali aliyestahili kukalia kiti cha ufalme. Athalia aliposikia kelele zilizokuwa zikitoka hekaluni, alikimbia kwenda huko na alipoona kilichokuwa kikitokea, akapaza sauti, “Ni njama! Ni njama!” Kuhani Mkuu Yehoyada akaagiza kwamba atolewe nje ya eneo la hekalu ili akauawe katika lango la farasi la nyumba ya mfalme; huenda yeye ndiye mtu pekee aliyekuwa hai katika nyumba ya Ahabu. (2Fa 11:1-20; 2Nya 22:1–23:21) Utabiri huo ulithibitika kuwa wa kweli kabisa: “Hakuna neno hata moja la Yehova ambalo Yehova amesema dhidi ya nyumba ya Ahabu litakalokosa kutimia”!​—2Fa 10:10, 11; 1Fa 21:20-24.

Hazina za Kiroho

t-1 1265-1266

Yehoashi

Baada ya hapo, maadamu Kuhani Mkuu Yehoyada alikuwa hai na kutenda kama baba na mshauri wa Yehoashi, mfalme huyo mwenye umri mdogo alifanikiwa. Alipokuwa na umri wa miaka 21 alifunga ndoa, naye akaja kuwa na wake wawili. Mmoja wa wake zake aliitwa Yehoadani. Kupitia wake zake, Yehoashi alipata wana na mabinti. Kwa njia hiyo, ukoo wa Daudi ambao ungetokeza Masihi, uliokuwa karibu kuangamizwa, ukafanywa imara tena.​—2Fa 12:1-3; 2Nya 24:1-3; 25:1.

DESEMBA 12-18

HAZINA ZA NENO LA MUNGU | 2 WAFALME 16-17

“Subira ya Yehova Ina Mipaka”

it-2 908 ¶5

Shalmanesa

Kuitawala Israeli. Wakati wa utawala wa Mfalme Hoshea wa Israeli (m. 758-740 K.W.K.), Shalmanesa wa Tano aliingia Palestina na Hoshea akawa kibaraka wake na kuanza kumlipa ushuru kila mwaka. (2Fa 17:1-3) Hata hivyo, baadaye Hoshea alikosa kulipa ushuru huo na ikagunduliwa kwamba alikuwa akipanga njama na Mfalme So wa Misri. (Ona SO.) Kwa sababu hiyo, Shalmanesa alimfunga gerezani Hoshea na baada ya hapo akalizingira Samaria kwa miaka mitatu. Jiji hilo lililokuwa na ngome imara lilianguka, nao Waisraeli wakapelekwa utekwani.​—2Fa 17:4-6; 18:9-12; linganisha Ho 7:11; Eze 23:4-10.

it-1 414-415

Utekwa

Sababu kuu iliyoongoza kwenye ufalme wa kaskazini wa Israeli wa makabila kumi na ufalme wa kusini wa Yuda wa makabila mawili kupelekwa utekwani ilikuwa moja: wote waliacha ibada ya kweli ya Yehova na kushiriki ibada ya miungu ya uwongo. (Kum 28:15, 62-68; 2Fa 17:7-18; 21:10-15) Yehova aliwatumia manabii ambao waliyaonya mataifa yote mawili lakini hawakusikiliza. (2Fa 17:13) Hakuna yeyote kati ya wafalme wa ufalme wa makabila kumi ya Israeli aliyewahi kuondoa kabisa ibada ya uwongo iliyoanzishwa na Yeroboamu, mfalme wa kwanza wa taifa hilo. Yuda, ufalme wa kusini wa makabila mawili, haukusikiliza maonyo ya moja kwa moja kutoka kwa Yehova wala kuzingatia kwamba Israeli lilikuwa limepelekwa utekwani kwa sababu hiyo. (Yer 3:6-10) Hatimaye, wakaaji wa falme zote mbili walipelekwa utekwani hatua kwa hatua.

Hazina za Kiroho

it-2 847

Msamaria

Neno “Wasamaria” linaonekana kwa mara ya kwanza katika Maandiko baada ya kutekwa kwa ufalme wa makabila kumi ya Samaria mwaka wa 740 K.W.K.; lilitumiwa kuwatambulisha wale walioishi katika ufalme wa kaskazini kabla ya utekwa ili kuwatofautisha na wageni walioletwa baadaye kutoka katika maeneo mengine ya Milki ya Ashuru. (2Fa 17:29) Inaonekana kwamba Waashuru hawakuwaondoa Waisraeli wote, kwa kuwa simulizi kwenye 2 Mambo ya Nyakati 34:6-9 (linganisha 2Fa 23:19, 20) linaonyesha kwamba wakati wa utawala wa Mfalme Yosia bado kulikuwa na Waisraeli fulani nchini humo. Baada ya muda, neno “Wasamaria” likaja kumaanisha wazao wa wale walioachwa Samaria na watu walioletwa nchini humo na Waashuru. Kwa sababu hiyo baadhi yao walikuwa watoto waliozaliwa katika ndoa za Waisraeli na wageni hao. Miaka mingi baadaye, neno hilo lilirejelea watu wa dini fulani, badala ya kumaanisha watu wa kabila au taifa fulani. Neno “Msamaria” lilirejelea mtu wa dhehebu la kidini lililoanzishwa katika eneo la kale la Shekemu na Samaria, na mafundisho ya msingi ambayo walifuata yalikuwa tofauti na ya dini ya Kiyahudi.​—Yoh 4:9.

DESEMBA 19-25

HAZINA ZA NENO LA MUNGU | 2 WAFALME 18-19

“Jinsi Wapinzani Wetu Wanavyojaribu Kutudhoofisha”

yb74 177 ¶1

Sehemu ya 2​—Ujerumani

Inashangaza kwamba maofisa wa SS, ambao mara nyingi walitumia ujanja mkubwa kujaribu kumfanya mtu kutia sahihi tangazo hilo, mara nyingi walimgeuka mtu huyo baada ya kutia sahihi na kumdhulumu hata zaidi kuliko walivyofanya awali. Karl Kirscht anathibitisha jambo hilo: “Mashahidi wa Yehova walishughulikiwa kwa ujanja wa hali ya juu kuliko mtu mwingine katika kambi za mateso. Ilifikiriwa kwamba mbinu hiyo ikitumiwa watashawishiwa kutia sahihi tangazo hilo. Tuliombwa tena na tena tufanye hivyo. Kuna baadhi ya wale ambao walitia sahihi, lakini, katika visa vingi walilazimika kusubiri zaidi ya mwaka mzima kabla ya kuachiliwa huru. Katika kipindi hicho mara nyingi walitukanwa waziwazi na maofisa wa SS kwa kuwa walikuwa wanafiki na waoga na walilazimishwa kutembea kuwazunguka ndugu zao kana kwamba ni ‘gwaride la heshima’ kabla ya kuruhusiwa kuondoka kambini.”

Hazina za Kiroho

it-1 155 ¶4

Vitu vya Kale Vilivyochimbuliwa

Kwa mfano, Biblia inasema kwamba Mfalme Senakeribu wa Ashuru aliuawa na wanawe wawili, Adrameleki na Shareza, na kwamba mwana wake mwingine, Esar-hadoni, ndiye aliyemrithi na kuwa mfalme. (2Fa 19:36, 37) Hata hivyo, maandishi fulani ya kumbukumbu ya Babiloni yanasema kwamba Tebethi 20, Senakeribu aliuawa na mwana wake wakati wa uasi. Berossus, aliyekuwa kuhani wa Babiloni wa karne ya tatu K.W.K., na Nabonido, aliyekuwa mfalme wa Babiloni wa karne ya sita K.W.K., walisema jambo hilohilo, kwamba Senakeribu aliuawa na mwana wake mmoja tu. Hata hivyo, katika kipande kilichogunduliwa hivi karibuni cha Bamba la Esar-hadoni, mwana wa Senakeribu aliyemrithi, Esar-hadoni anasema waziwazi kwamba ndugu zake (wingi) waliasi na kumuua baba yao kisha wakakimbia. Philip Biberfeld, anasema hivi kuhusu hilo katika kitabu Universal Jewish History (1948, Buku la 1, uk. 27): “Maandishi hayo ya Kumbukumbu ya Babiloni, Nabonido, na Berossus walikosea; ni simulizi la Biblia tu ndilo lililokuwa sahihi. Hata habari ndogo zilizotajwa humo zilithibitishwa na maandishi ya Esar-hadoni na hivyo likathibitika kuwa sahihi zaidi kuhusu tukio hilo katika historia ya Wababiloni na Waashuru kuliko maandishi ya Wababiloni wenyewe. Hiyo ni hoja muhimu sana tunapochunguza vyanzo vingine vya wakati huo ambavyo havipatani na maandishi ya Biblia.”

DESEMBA 26–JANUARI 1

HAZINA ZA NENO LA MUNGU | 2 WAFALME 20-21

Hazina za Kiroho

it-2 240 ¶1

Timazi

Timazi inaweza kutumiwa katika ujenzi ili kuhakikisha jengo limenyooka au kupima ikiwa linaweza kudumu kwa muda mrefu. Yehova alitabiri kwamba angetumia “kamba iliyotumika kupima Samaria na kutumia timazi iliyotumiwa kupima nyumba ya Ahabu” dhidi ya Yerusalemu lililoasi. Mungu alikuwa amewapima Wasamaria na nyumba ya Mfalme Ahabu na kugundua walikuwa wabaya au wamepinda kimaadili, na hivyo akawaangamiza. Vivyo hivyo, Mungu angehukumu Yerusalemu na watawala wake, angefichua uovu wao, na kuliangamiza jiji hilo. Mambo hayo yalitukia katika mwaka wa 607 K.W.K. (2Fa 21:10-13; 10:11) Nabii Isaya aliwajulisha watu hao waovu waliojigamba na watawala wa watu wa Yerusalemu kuhusu uharibifu uliokuwa ukija na kuhusu tangazo la Yehova: “Nitaifanya haki kuwa kamba ya kupimia na uadilifu utakuwa kifaa cha kusawazishia.” Viwango vya haki ya kweli na uadilifu wa kweli vingefunua ni nani waliokuwa watumishi wa kweli wa Mungu na ni nani ambao hawakuwa, na matokeo yangekuwa ama kuokolewa au kuangamizwa.​—Isa 28:14-19.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki