Marejeo ya Daftari la Mkutano wa Huduma na Maisha
MEI 8-14
HAZINA ZA NENO LA MUNGU | 2 MAMBO YA NYAKATI 20-21
Hazina za Kiroho
it-1 1271 ¶1-2
Yehoramu
Yehoramu hakutenda kwa uadilifu kama Yehoshafati baba yake, na sababu moja ilikuwa uvutano mbaya wa Athalia, mke wake. (2Fa 8:18) Yehoramu aliwaua kaka zake sita na baadhi ya wakuu wa Yuda lakini hakuishia hapo, alisababisha watu wa Yuda waache kumwabudu Yehova na wakaanza kuabudu miungu ya uwongo. (2Nya 21:1-6, 11-14) Kipindi chote cha utawala wake kilikuwa chenye matatizo. Kwanza, Waedomu waliasi; kisha watu wa Libna wakaasi dhidi ya Yuda. (2Fa 8:20-22) Nabii Eliya alimtumia Yehoramu barua na kumwonya: “Yehova anawaletea pigo kubwa watu wako, wana wako, wake zako, na mali zako zote.” Zaidi ya hilo, alimwambia hivi Mfalme Yehoramu: “Utashikwa na magonjwa mengi, kutia ndani ugonjwa wa matumbo, mpaka ugonjwa huo utakaposababisha matumbo yako yatoke nje, siku baada ya siku.”—2Nya 21:12-15.
Maneno hayo yote yalitimia. Yehova aliwaruhusu Waarabu na Wafilisti washambulie Yuda na wakawachukua mateka wake na wana wa Yehoramu. Yehova alimruhusu mwana wa mwisho wa Yehoramu, Yehoahazi (ambaye pia anaitwa Ahazia) kubaki, na alifanya hivyo kwa sababu tu ya agano la Ufalme ambalo alikuwa amefanya pamoja na Daudi. “Baada ya mambo hayo yote, Yehova akampiga kwa ugonjwa wa matumbo usioweza kupona.” Miaka miwili baadaye, “matumbo yake yalitoka nje” na hatimaye akafa. Kwa hiyo mwanamume huyo mwovu akafikia mwisho wake na “hakuna mtu yeyote aliyesikitishwa na kifo chake.” Alizikwa katika Jiji la Daudi “lakini si katika makaburi ya wafalme.” Ahazia mwana wake akaanza kutawala baada yake.—2Nya 21:7, 16-20; 22:1; 1Nya 3:10, 11.
MEI 15-21
HAZINA ZA NENO LA MUNGU | 2 MAMBO YA NYAKATI 22-24
“Yehova Huwathawabisha Watu Wanaotenda kwa Ujasiri”
it-1 379 ¶5
Mazishi, Makaburi
Kuhani Mkuu Yehoyada ambaye alikuwa mwadilifu alizikwa katika “Jiji la Daudi pamoja na wafalme.” Yeye ndiye mtu pekee ambaye si wa ukoo wa kifalme kuzikwa katika makaburi ya wafalme.—2Nya 24:15, 16.
Hazina za Kiroho
it-2 1223 ¶13
Zekaria
12. Mwana wa Kuhani Mkuu Yehoyada. Baada ya kifo cha Yehoyada, Mfalme Yehoashi aliacha ibada ya kweli, na kuwasikiliza watu waliompa ushauri mbaya badala ya kuwasikiliza manabii wa Yehova. Zekaria, binamu ya Yehoashi (2Nya 22:11), aliwapa watu wa Yuda onyo la moja kwa moja, lakini watu hawakutubu na kumrudia Yehova, badala yake walimpiga mawe Zekaria katika ua wa hekalu. Alipokuwa akifa, Zekaria alisema maneno haya: “Yehova na ashughulikie jambo hili na kukulipiza kisasi.” Unabii huo ulitimizwa kwa sababu nchi ya Siria ilileta uharibifu mkubwa Yuda na pia Yehoashi aliuawa na watumishi wake wawili “kwa sababu alikuwa amemwaga damu ya wana wa kuhani Yehoyada.” Septuajinti ya Kigiriki na Vulgate ya Kilatini zinasema kwamba Yehoashi aliuawa ili kulipiza damu ya “mwana” wa Yehoyada. Hata hivyo, maandishi ya Wamasora na Peshitta ya Kisiria, zinasema “wana,” huenda wingi huo unaonyesha utukufu na ubora wa mwana wa Yehoyada, yaani, Zekaria ambaye alikuwa nabii na kuhani pia.—2Nya 24:17-22, 25.
MEI 22-28
HAZINA ZA NENO LA MUNGU | 2 MAMBO YA NYAKATI 25-27
“Yehova Anaweza Kukupa Nyingi Zaidi Kuliko Hizo”
it-1 1266 ¶6
Yehoashi
Mfalme wa Yuda alikodi wanajeshi elfu mia moja kutoka kwa Yehoashi ili wakamsaidie kupigana na Waedomu. Hata hivyo, “mtu fulani wa Mungu wa kweli” alishauri kwamba wanajeshi hao warudishwe nyumbani hata ingawa tayari walikuwa wamelipwa talanta mia moja za fedha (dola 660,600). Wanajeshi hao walikasirika sana labda kwa sababu walitazamia kwamba wangepata nyara vitani. Waliporudi kwenye ufalme wa kaskazini walivamia majiji ya ufalme wa kusini wakitokea Samaria (huenda walitumia jiji hilo kama kituo chao) mpaka Beth-horoni na kuchukua nyara nyingi.—2Nya 25:6-10, 13.
JUNI 5-11
HAZINA ZA NENO LA MUNGU | 2 MAMBO YA NYAKATI 30-31
“Kukutana Pamoja Kunatunufaisha”
it-1 1103 ¶2
Hezekia
Bidii Yake kwa Ajili ya Ibada ya Kweli. Hezekia aliwekwa kuwa mfalme akiwa na miaka 25 na punde baada ya hapo alionyesha bidii yake kwa ajili ya ibada ya kweli. Hatua ya kwanza aliyochukua ni kufungua na kuirekebisha hekalu. Aliwaita makuhani na Walawi na kuwaambia: “Ninatamani moyoni mwangu kufanya agano pamoja na Yehova Mungu wa Israeli.” Hilo lilikuwa agano la kuwa waaminifu, ni kana kwamba agano la Sheria lilikuwa likizinduliwa upya katika Yuda, kwa sababu hata ingawa bado lilikuwepo lilikuwa limepuuzwa. Alifanya kazi kubwa ya kuwapanga Walawi na majukumu yao, na alirejesha pia mipango kwa ajili ya ala za muziki na nyimbo za sifa. Ulikuwa mwezi wa Nisani, mwezi ambao walipaswa kuadhimisha Pasaka, lakini hekalu halikuwa safi na vilevile makuhani na Walawi hawakuwa safi. Kufikia Nisani 16, hekalu lilikuwa safi na vyombo vyake vilikuwa vimerudishwa. Kisha dhabihu za kufunika dhambi zilihitaji kutolewa kwa ajili ya Waisraeli wote. Kwanza, wakuu walileta dhabihu za dhambi kwa ajili ya ufalme, hekalu, na watu, kisha watu walitoa maelfu ya dhabihu za kuteketezwa.—2Nya 29:1-36.
it-1 1103 ¶3
Hezekia
Kwa sababu watu hawakuwa safi, hawangeweza kuadhimisha Pasaka wakati ambapo iliadhimishwa kwa ukawaida, basi Hezekia alitumia fursa ya kuadhimisha Pasaka mwezi mmoja baadaye, jambo lililoruhusiwa na sheria. Aliwaalika watu wa Yuda na pia wa Israeli kupitia wakimbiaji ambao walipeleka barua kotekote nchini kuanzia Beer-sheba mpaka Dani. Wajumbe hao walidhihakiwa na watu wengi; lakini baadhi ya watu, hasa kutoka Asheri, Manase, na Zabuloni, walijinyenyekeza na kuhudhuria mwadhimisho huo, pia baadhi ya watu kutoka Efraimu na Isakari walihudhuria. Isitoshe, waabudu wengi wa Yehova ambao hakuwa Waisraeli walihudhuria pia. Inaelekea haikuwa rahisi kwa waabudu wa Yehova walioishi katika ufalme wa kaskazini kuhudhuria. Wao pia walikabili upinzani na dhihaka kama ilivyokuwa kwa wajumbe, kwa sababu ufalme wa makabila kumi ulikuwa umezama katika upotovu wa maadili na ibada ya sanamu na pia ulikuwa ukishambuliwa na Waashuru.—2Nya 30:1-20; Hes 9:10-13.
it-1 1103 ¶4-5
Hezekia
Baada ya Pasaka, Waisraeli waliadhimisha Sherehe ya Mikate Isiyo na Chachu kwa siku saba wakiwa na shangwe nyingi hivi kwamba kutaniko lote likaamua kuendeleza sherehe hiyo kwa siku saba zaidi. Licha ya hatari waliyokabili katika kipindi hicho, Yehova aliwabariki hivi kwamba “kulikuwa na shangwe nyingi Yerusalemu, kwa maana tangu siku za Sulemani mwana wa Daudi mfalme wa Israeli, jambo kama hilo halikuwa limeonekana Yerusalemu.”—2Nya 30:21-27.
Hizo hazikuwa hisia za muda mfupi tu kwa sababu baada ya kukutanika walichukua hatua ili kurudisha ibada ya kweli. Baada ya sherehe hiyo, Waisraeli hao walivunjavunja nguzo takatifu, wakabomoa mahali pa juu na madhabahu, na wakaikatakata miti mitakatifu katika nchi yote ya Yuda na Benjamini, na hata katika Efraimu na Manase. (2Nya 31:1) Hezekia aliwawekea mfano mzuri kwa kumpondaponda yule nyoka wa shaba aliyetengenezwa na Musa, kwa maana Waisraeli walimwabudu na kumfukizia moshi wa dhabihu. (2Fa 18:4) Baada ya mwadhimisho huo mkubwa, Hezekia alihakikisha ibada safi inaendelezwa kwa kupanga makuhani katika vikundi vyao na kufanya mipango ya kutegemeza utumishi hekaluni; aliwahimiza watu watii Sheria kwa kutoa sehemu ya kumi na mazao ya kwanza kwa ajili ya Walawi na makuhani, na watu walifanya hivyo kwa moyo wote.—2Nya 31:2-12.
JUNI 12-18
HAZINA ZA NENO LA MUNGU | 2 MAMBO YA NYAKATI 32-33
“Waimarishe Wengine Wakati wa Taabu”
it-1 204 ¶5
Ashuru
Senakeribu. Senakeribu, mwana wa Sargoni wa Pili, alishambulia ufalme wa Yuda katika mwaka wa 14 wa utawala wa Hezekia (732 K.W.K.). (2Fa 18:13; Isa 36:1) Hezekia alimwasi Mfalme wa Ashuru kwa kuvunja makubaliano ambayo mfalme huyo alikuwa amefanya na Ahazi, baba ya Hezekia. (2Fa 18:7) Kwa sababu hiyo Senakeribu alishambulia sehemu kubwa ya Yuda, inasemekana alishinda majiji 46 ya Yuda (linganisha Isa 36:1, 2) na kisha akiwa amepiga kambi Lakishi, alimwamuru Hezekia alimpe faini ya talanta 30 za dhahabu (dola 11,560,000 hivi) na talanta 300 za fedha (dola 1,982,000 hivi). (2Fa 18:14-16; 2Nya 32:1; linganisha Isa 8:5-8.) Licha ya kwamba Hezekia alilipa faini hiyo, Senakeribu aliwatuma wasemaji wake na kudai watu wa Yerusalemu wajisalimishe. (2Fa 18:17–19:34; 2Nya 32:2-20) Baadaye, Yehova aliwaangamiza wanajeshi 185,000 wa Ashuru katika usiku mmoja na hivyo, Mwashuru huyo mwenye majivuno alilazimika kurudi Ninawi. (2Fa 19:35, 36) Akiwa huko, watoto wake wawili walimuua kisha Esar-hadoni, mwana wake mwingine akawa mfalme. (2Fa 19:37; 2Nya 32:21, 22; Isa 37:36-38) Matukio hayo yote isipokuwa kuangamizwa kwa majeshi ya Waashuru yalirekodiwa kwenye mche wa Senakeribu na pia kwenye mche wa Esar-hadoni.—PICHA, Buku la 1, uk. 957.
JUNI 19-25
HAZINA ZA NENO LA MUNGU | 2 MAMBO YA NYAKATI 34-36
“Je, Unanufaika Kikamili Kutokana na Neno la Mungu?”
it-1 1157 ¶4
Hulda
Hilkia, kuhani mkuu alipata “kitabu cha sheria” kazi ya kurekebisha hekalu ilipokuwa ikiendelea. Baada ya kusikia kitabu hicho kikisomwa, Yosia alituma watu wakatafute ushauri wa Yehova. Walienda kwa Hulda, naye aliwaambia ujumbe uliotoka kwa Yehova, yaani, taifa hilo lililoasi lingepata msiba kwa sababu ya kutotii kama “kitabu” kilivyosema. Kwa kuongezea, Hulda alisema kwamba kwa sababu Yosia alikuwa amejinyenyekeza mbele za Yehova, hangeona msiba huo bali angezikwa na mababu zake na kulazwa kwa amani katika kaburi lake.—2Fa 22:8-20; 2Nya 34:14-28.