Historia ya Mashahidi wa Yehova Katika Nyakati za Kisasa
—Ujeremani (inaendelea)
NDUGU na Dada Strenge waliona namna mashahidi wa Yehova walivyokuwa na nafasi ndogo sana ya kupokea haki za kisheria wakati wa miaka hiyo yenye msukosuko. Ndugu Strenge alikamatwa na kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu, naye Dada Strenge, sasa akiwa amebaki peke yake na watoto wake, alitiwa katika hali iliyohitaji atumie nguvu zote alizoweza kukusanya. Atoa habari hizi:
“Shuleni mwanangu alipaswa ajifunze wimbo wa kizalendo na shairi la kizalendo kwa moyo. Kwa kuwa hakuweza kupatanisha jambo hili na imani zake za kidini, alikataa. Mwalimu wake aliagiza vijana wadogo wawili wamwelekeze kwa mwalimu mkuu kama mfungwa, aliyeitwa Bw. Hanneberg, aliyemwambia kidole chake kimepaswa kipigwe mpaka kiwe chenye damu nyingi na kuvimba sana na kiwe cheusi na cha samawati (bleu) hata ‘asiweze tena kukiingiza katika [mkundu] wake.’ Aliendelea kumtisha na kusema asingemwona baba yake tena. Mwishowe akamwuliza kijana huyu wa miaka kumi kama angekataa kufanya utumishi wa kijeshi. Günter akaitaja Biblia na kusema, ‘Yeye achukuaye upanga atatoweka kwa upanga,’ kisha mwalimu mkuu akamwagiza mwalimu wa Günter ‘amwadhibu kama ilivyo kawaida.’ Baadaye mwalimu mkuu alimwambia aende nyumbani, akisema kwamba angeagiza polisi waje kumchukua nyumbani baada ya dakika kumi wakamwingize katika nyumba ya kufunzia adabu. Mwanangu alikuwa ndiyo sasa tu anapofika nyumbani polisi walipoendesha gari kubwa lao mbele ya nyumba yetu. Maafisa kadha walidai waingie kwa nguvu, lakini mimi nikakataa kufungua mlango. Baada ya muda fulani polisi walikwenda kwa jirani yangu, wakidai mwanamke huyu atoe ushuhuda wa kunionyesha mwenye hatia. Kwa kuwa hakutaka kutoa ushuhuda huo wenye kunionyesha mwenye hatia, alilazimishwa kwa muda mrefu mpaka mwishowe akakubali alitusikia tukiimba wimbo na kutoa sala kila asubuhi. Kisha polisi wakaondoka.
“Asubuhi iliyofuata karibu saa 4:30 polisi wakarudi. Kwa kuwa sikutaka kufungua mlango, maafisa wa Gestapo wakapaza sauti: ‘Ewe Mwanafunzi wa Biblia uliyelaaniwa! Fungua!’ Kisha wakamwendea fundi wa kufuli aliyeishi karibu na kumwagiza avunje mlango.
“Akishikilia bastola kifuani mwangu, mmoja wa mawakili wa Gestapo akapaza sauti: ‘Tupe watoto.’ Lakini mimi nikawashikilia sana nao wakanishikilia sana wakitafuta ulinzi. Kwa kuogopa kwamba wangetutenganisha kwa nguvu, tukapiga yowe kwa nguvu sana tupate msaada.
“Dirisha lilikuwa wazi na kundi kubwa la watu wakakusanyika mbele ya nyumba nao wakasikia mayowe yangu ya kukata tamaa: ‘Mimi nilizaa watoto wangu kwa utungu mwingi zaidi nami sitawapa kwenu kamwe. Lazima mnipige na kuniua kwanza.’ Kisha nikazimia kwa kushindwa na wasiwasi. Niliporudiwa na fahamu zangu, nikahojiwa na Gestapo (polisi) kwa saa tatu. Wakajaribu kunifanya nimtie mume wangu hatiani. Hoja zikakatizwa mara kadha na kuzimia-zimia kwangu. Kwa sasa, kundi la watu lililozidi kuwa kubwa mbele ya nyumba liliendelea kuonyesha kwa makelele yao kwamba hawakukubaliana na yaliyokuwa yakiendelea. Mwishowe Gestapo wakaondoka tena, bila ya kutimiza walilokuwa wamekuja kufanya. Sasa walipanga kuchukua watoto kwa siri. Yaelekea kwa kufuata mpango huu niliombwa nionekane mbele ya mahakma ya pekee katika Elbing siku kadha baadaye. Siku iyo hiyo watoto wangu walipaswa waende kwa mlinzi aliyewekwa awaangalie. Mimi nikatazamia mabaya zaidi na kumfikia mlinzi nikiwa na watoto wote wawili siku moja kabla. Akasema binti yangu wa miaka kumi na mitano angetiwa katika kambi ya kazi na Gunter mwenye miaka kumi apewe kwa jamaa ambayo ingemzoeza awe wa Nationalist Socialism (Ujamaa wa Kitaifa). Wakikataa wangeingizwa katika shule ya kufunzia adabu. Kwa wasiwasi wangu nikauliza: “Niambie, tayari tunaishi katika Urusi, au tungali tumo Ujeremani?’ kisha akajibu: ‘Bi. Strenge, mimi nitayapuza uliyosema sasa hivi. Hata mimi ni wa jamaa ya kidini; baba ni mhudumu!’ Nilipoomba binti yangu aruhusiwe hata kukubali uanafunzi wa ufundi mahali fulani, wakili huyu akasema: ‘Mimi sitaki matata yako. Afadhali nishughulike na watoto wengine ishirini kuliko kushughulika na Mwanafunzi wa Biblia mmoja.’”
“Jumamosi ikafika, siku niliyopaswa kwenda Elbing nikatetee imani yangu katika Yehova na ahadi zake. Ili kujiimarisha nipate kueleza yote yaliyokuwa moyoni mwangu, nikamtembelea mume wangu aliyefungwa kabla sijaenda. Alipoletwa, nilimwangukia mikononi. Huzuni yote na matukio yote ya kuogofya ya siku chache zilizopita ilinirudia tena: mume wangu amehukumiwa miaka mitatu gerezani, nimetenganishwa na watoto wangu. Roho yangu ilivunjika nami nilifikia upeo wa uvumilivu. Lakini maneno ya mume wangu yalikuwa kama maneno ya malaika, aliyenifariji kwa kuonyesha yaliyompata Ayubu na taabu zake na hali hakuvunja uaminifu wake kwa Mungu, hata baada ya kupoteza kila kitu, hakumlaumu Mungu juu ya kufanya kosa. Alisimulia namna yeye pia alivyokuwa amebarikiwa na Yehova sana baada ya jaribu kali lililoletwa na kesi nyingi na kujaribiwa. Hii ilinipa nguvu mpya. Sasa nikafika kesini nikiwa hodari kusikia kwa fahari bidii waliyokuwa nayo watoto wangu wakimtolea Yehova na Ufalme wake ushuhuda na imani yao mbele ya waalimu wao na maafisa wengine wakuu. ‘Mahakma ya Ujeremani’ ikaagiza: Kwa kuwa sikulea watoto wangu wakifuata Ujamaa wa Kitaifa, na kwa kuwa niliimba nyimbo pamoja nao kwa kumsifu Yehova, ningehukumiwa kifungo cha miezi minane.”
KAFUKUZWA NA WANADARASA WENZAKE
Ndugu Willi Seitx mwenye umri wa miaka kumi na miwili wa Karlsruhe alipatwa na jambo tofauti. Yeye mwenyewe atoa habari hizi:
“Ni vigumu kwangu kueleza mambo ambayo imenilazimu nivumilie mpaka sasa. Wanafunzi wenzangu shuleni wamenipiga; tuendapo matembezini, lazima niende peke yangu nikiruhusiwa hata kwenda kwenyewe, nami sipaswi niseme na rafiki zangu wa shule, ambao ningali nao. Yaani: ‘Mimi nachukiwa na kufanyiwa mzaha kama mbwa mwenye upele.’ Faraja yangu ya peke yake imekuwa kwamba ufalme wa Mungu utakuja karibuni. . . . ”
Januari 22, 1937, Willi alifukuzwa shuleni “kwa sababu ya kukataa kutoa salamu ya Kijeremani, kuimba nyimbo za kizalendo na kushiriki katika miadhimisho ya shule.”
KAHUKUMIWA KWA KUSALI NA KUIMBA
Max Ruef wa Pocking aligundua pia namna majaribio ya kawaida yalivyofanywa kulazimisha mashahidi wa Yehova wavunje ukamilifu wao. Njia yake ya kujipatia riziki iliharibiwa kabisa. Hati ya kuweka rehani aliyokuwa amechukua kwa kusudi la kurekebisha mijengo ilifutwa. Kwa kuwa hakuweza kulipia hati hiyo mara moja, mali yake yote ilifanyiwa mnada Mei wa 1934.
“Mateso hayakukomea hapo,” asimulia Ndugu Ruef. “Bali, nilishtakiwa kwa uongo na kukokotwa mahakmani viongozi wa siasa walipochochea mambo. Kwa kuwa hakukuwa na la kunishtakia, nilihukumiwa kifungo cha miezi sita na mahakma ya pekee katika Munich kwa sababu nilikuwa nimehusika katika kusali na kuimba kulikopigwa marufuku nyumbani mwangu. Nilianza kutumikia hukumu yangu Desemba 31, 1936. Mke wangu aliyekuwa akitazamia mtoto wa tatu alipokea Reich marks 12 mbali na kodi ya nyumba, ambao haukuwa msaada kwake mwenyewe na watoto wawili wenye umri wa miaka tisa na kumi. Wakati ukafika wake kuzaa mtoto. Wote wawili tuliomba kwamba kutumikia kifungo changu kukatizwe juma chache niweze kuangalia mambo fulani ya lazima. Karibu juma moja kabla mtoto hajazaliwa ombi letu lilikataliwa kama ‘lisilofaa.’”
—(Inaendelea)—Kutoka 1974 Yearbook of Jehovah’s Witnesses.