Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • yb90 kur. 148-197
  • Barbados, West Indies

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Barbados, West Indies
  • 1990 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
  • Vichwa vidogo
  • Kupanda Mbegu za Ukweli wa Ufalme
  • Kumbukumbu za Siku Zenye Kusisimua
  • Bidii Isiyopungua
  • Kuifikia Jamii ya Weupe
  • Manufaa Kutoka kwa Hotuba za Watu Wote
  • Mbegu Zaanguka Kwenye Visiwa Vingine
  • Mwanzo Katika St. Vincent
  • Msaada Zaidi Waandaliwa
  • Kupapasa-papasa kwa Ajili ya Mungu na Kumpata
  • Basi Zilizokodishwa kwa Ajili ya Kazi ya Kutoa Ushuhuda
  • Mashahidi Wajasiri
  • Kipofu Asaidia Wengine Waone
  • Tengenezo la Kitheokrasi Wakati wa Vita ya Ulimwengu 2
  • Wahitimu wa Gileadi Wawasili
  • Ziara ya Msimamizi
  • Hawakuacha
  • Astahiwa kwa Kazi ya Ufuataji Haki
  • Kazi ya Ufalme Yaanza Mwendo Katika St. Lucia
  • Ugonjwa wa Baharini Wakati wa Safari Kwenye Mkusanyiko
  • Ziara Kutoka Makao Makuu
  • Ile “Dini Isiyoamini Moto wa Mateso”
  • Kueneza Visiwa vya Grenadine kwa Ushuhuda
  • Msaada Baada ya Kimbunga Janet
  • Uhamaji Wawa na Uvutano Juu ya Ukuzi
  • Uchaguzi Bora, Baraka Kubwa Zaidi
  • Baada ya Light, Kazi ya Kufuatia
  • Marekebisho-upya Yapepeta Nje Wale Wasiotosheka
  • Tawi Jipya Lapangwa Kitengenezo
  • Mabadiliko ya Kisiasa Kutuzunguka
  • Wahitimu wa Gileadi Waweka Kielelezo Kizuri
  • Mkusanyiko wa Kimataifa Katika Bridgetown
  • Utumishi wa Redio wa Bure Watokeza Ushuhuda
  • Kuepuka Vikengeusha-Fikira
  • Kusimulia Sifa ya Yehova Katika Visiwa
1990 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
yb90 kur. 148-197

Barbados, West Indies

KARIBUNI Barbados—“bara la samaki arukaye,” na njia-lango ya West Indies. Je! wewe ulijua kwamba kisiwa hiki kidogo ni mojapo nchi zilizo na wakazi wenye kusongamana zaidi katika ulimwengu? Eneo la ardhi yacho ambalo ni kilometa za mraba 430 hivi linakaliwa na watu zaidi ya 253,500. Lakini kama vile mithali isemavyo, “Vitu vizuri huja vikiwa katika vifurushi vidogo,” na hakika ndivyo ilivyo katika kisiwa hiki kilicho upande wa mashariki zaidi ya vinginevyo vyote vya vikundi vya visiwa vya Karibea.

Pwani ya mashariki ya Barbados huandaa mandhari yenye kuvutia ya vilima vyenye kuteremka kwa utaratibu ikitazama kutoka juu mawimbi meupe ya Bahari Atlantiki isiyotulia, hali pwani ya magharibi ina kingo za fuo nyeupe ambazo hupigwa-pigwa kwa wanana na yale maji matulivu zaidi ya Bahari ya Karibea.

Wakati mmoja miwa ilikuwa ndiyo “mfalme” wa uchumi katika Barbados. Hata hivyo, hivi majuzi zaidi, utalii umekuwa ndiyo njia kuu ya kuchuma fedha. Kila mwaka kisiwa hiki hukaribisha maelfu ya wageni, ambao huzidi idadi yote ya watu wacho.

Kutoka wakati ambao Barbados ililowewa na wakoloni Waingereza katika 1627 W.K. kufika wakati wa kupewa kwayo uhuru katika 1966, ufungamano imara uliendelezwa pamoja na Uingereza, na baadaye, pamoja na Kanisa Anglikana. Ni kwa kadiri gani jambo hilo liliathiri maisha ya kila siku? Wakati mmoja sheria ilitungwa ikitaka ‘sala za jamaa na hudhurio kwenye kanisa.’ Sala za asubuhi na za jioni zilifanywa kuwa za lazima. Kushindwa kokote kutii kulitokeza faini ya kilo 18 za sukari. Kila mtu aliwekewa sharti la kujipatanisha na amri hiyo pamoja na nidhamu ya kanisa bila kuziacha hata kidogo. Jambo hilo lilimwongoza mwanahistoria mmoja kuwaeleza Wabarbado kuwa ‘wameshupazwa na wanga na Uanglikana.’ Hata hivyo, hali imebadilika kidogo, kwa kuwa sasa kuna farakano na madhehebu mbalimbali 141 za “Kikristo.” Je! imani ya kweli ingeweza kusitawi katika ngome ya kidini kama hiyo?

Kupanda Mbegu za Ukweli wa Ufalme

Katika 1905, miaka tisa kabla ya kusimamishwa kwa Ufalme wa Kimesiya katika mbingu, Joseph Brathwaite alianza kutoa ushuhuda katika Barbados akiwa kolpota, kama wafanya kazi wa wakati wote miongoni mwa Mashahidi wa Yehova walivyoitwa wakati huo. Yeye alikuwa amejifunza ukweli katika British Guiana (sasa ni Guyana). Kabla ya muda mrefu kupita, watu wenye njaa ya ukweli kama vile Algernon Symmonds na Maud, mke wake, wakakubali ule ujumbe wenye nderemo wa Ufalme. Wote wawili, pamoja na Juliet Shepherd, walibatizwa katika 1909. Waldemar (ambaye baadaye akawa Bi. Vere Rice) binti mchanga wa akina Symmonds akajiunga upesi na wazazi wake katika kugawanya trakti za Biblia.

Hawa Wanafunzi wa Biblia wa mapema walikuwa na tamaa yenye kuwaka ya kuongea na wengine juu ya yale ambayo walikuwa wamejifunza. Roho ya uharaka na kujidhabihu iliwasukuma wagawanye vichapo vya Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi walipokuwa wakipeleka ujumbe kwenye vijiji vingi kisiwani. Dada Rice anasimulia hivi: “Papi [baba yake], ambaye aliendesha biashara katika Bridgetown, mji mkuu, alikuwa akitumia nyumbu wake na kigari kusafirisha kikundi cha Wanafunzi wa Biblia kilichokuwa kikishiriki kazi ili kueneza zile wilaya za nchi. Sisi tulikuwa tukienda nje sana-sana wakati wa miisho-juma. Yule nyumbu maskini hakupata pumziko jingi, na hivyo alikuwa akisimama mara nyingi njiani tukirudi nyumbani—iwe ni kwa sababu ya uchovu au ushupavu tu sisi hatukuweza kujua. Kama tokeo, sisi tulikuwa tukirudi nyumbani usiku sana Jumapili, nyakati nyingine kupita usiku wa manane. Hata hivyo ilikuwa lazima niamke kesho yake asubuhi kwenda shule.”

Kumbukumbu za Siku Zenye Kusisimua

Miongoni mwa wale ambao utendaji wao hurudi nyuma kufika hizo nyakati za mapema ni Dada Lina Gaul, ambaye kwa kufahamiwa sana anaitwa “Mami Gaul” na wachanga na wazee pia. Ingawa kumbukumbu lake si jepesi kama katika nyakati za hapo kwanza, oh, jinsi yeye hupenda kukumbuka hizo siku zenye kusisimua na kufikiria matendo mazuri ajabu ya Yehova ya kushughulika na watu wake! Sasa akiwa katika miaka yake ya 90, Mami Gaul hukumbuka wakati, huko nyuma katika 1910, baba na mama yake walipopokea trakti moja kutoka kwa Bw. Thomas, mwalimu wa shule. Kwa msaada wa trakti hiyo na nyinginezo zilizochapwa na Wanafunzi wa Biblia, upesi jamaa ile ikajifunza ukweli kuhusu moto wa mateso, nafsi, Utatu, na mafundisho mengine. Haikuwachukua muda mrefu kukata vifungo vyote na Kanisa la Misheni ya Kikristo katika Kijiji cha Wafanya Kazi, na upesi wakashirikiana na eklesia (au kundi) ya Wanafunzi wa Biblia iliyokutana kwenye Na. 40 Barabara Roebuck katika Bridgetown. Kufikia 1911 wazazi wake wote wawili walikuwa tayari kwa ubatizo, na mwaka uliofuata Lina akazamishwa pia.

Dada Gaul na wazazi wake, Alexander na Josephine Payne walionwa na washiriki wao wa hapo kwanza wa Misheni ya Kikristo kuwa “kondoo waliopotea njia,” na jitihada zilifanywa ‘kuwarudisha.’ Kwa kusudi hilo, misheni ile ilifanya mikutano ya watu wote pale pale mbele ya nyumba ya akina Payne na kumsihi Bwana awarudishe kwenye zizi la Misheni ya Kikristo.

Dada Gaul, akiwa na tabasamu yenye kupendeza na macho yenye kumeremeta, hukumbuka pindi moja wakati rafiki mkubwa zaidi wa mama yake wa hapo kwanza kutoka ile misheni alipotumwa kwenye nyumba yao. Kana kwamba anasikia yale mazungumzo yote kwa mara nyingine tena, yeye husimulia hivi:

“‘Dada Payne,’ akasema rafiki ya mamangu, ‘Mimi nina ujumbe wako kutoka kwa Bwana.’

“‘Je! wewe ulimwona? Yeye alionekanaje?’ Mama akajibu katika kupinga.

“‘Yeye ni mtu mrefu mweupe, amevalia [mavazi] meupe, anampanda farasi mweupe, naye awaambia mrudi kwenye Jumba la Kijiji cha Wafanya Kazi.’

“Jibu kali la mama lililofuata lilikomesha haraka jitihada zao za kutufanya turudi kwenye Kanisa Misheni. Alisema hivi: ‘Basi, wewe rudi ukamwambie “mtu” huyo kwamba mimi, Josephine Payne, nasema kwamba mimi sirudi.’”

Akina Payne, pamoja na watu wengine mmoja mmoja wenye kushirikiana na Wanafunzi wa Biblia katika miaka hiyo ya mapema, walikutana na dhihaka nyingi na upinzani wenye kuendelea. Hata hivyo, imani yao ilikuwa imara. Katika kutazama nyuma, sisi tunaweza kuthamini swali hili lililozushwa katika Maandiko: “Ni nani aliyeidharau siku ya mambo madogo?” (Zek. 4:10) Pasipo shaka, kusudi la Yehova la kufanya jina lake litangazwe katika dunia yote linatia ndani kisiwa hiki kidogo katika West Indies.

Dada Gaul angali anatumikia kwa bidii naye hajakosa kamwe kuhubiri habari njema hata mwezi mmoja tangu ubatizo wake katika 1912. Ingawa amepatwa na ugonjwa wa kupooza mwili mara mbili, unaotajwa kienyeji kuwa “kupitwa,” yeye angali anadumisha akili timamu naye hutafuta sikuzote fursa za kushiriki habari njema pamoja na wengine.

Bidii Isiyopungua

Dada Waldemar Rice, mfanya kazi mwingine mwenye juhudi, ametoa ukweli kwa watu wa kila hadhi ya maisha kwa matokeo mazuri kwa muda wa miongo saba iliyopita. Yeye ana ustadi wa kutumia Kibarbado, au kilugha cha “Kibaja,” kwa matokeo mazuri. Kufahamiana kwake kikamili na misemo ya kienyeji huongeza uzuri kwenye utoaji wake wa ushuhuda bila kuupunguzia adhama, na idili yake nyingi kwa ajili ya tumaini la Ufalme linaposemwa kwa lugha ya kienyeji, hufanya watu watake kusikiliza. Anaposema na watu wa malezi ya cheo cha chini juu ya hali za ulimwengu zenye kuzorota, yeye husema hivi: “Dis worl’ in bare turmoil, dah is de troof, when um in trouble in one place, um is starvation in another or riots in yonder.”

Yeye ni mjasiri na asiyeogopa katika kutetea ukweli, na kielelezo hiki kimetia moyo vijana wengi kwa muda wa miaka iliyopita. Ingawa nguvu zake za kimwili zimepungua, bidii ya Dada Rice kwa utumishi wa Yehova hubaki ikiwa yenye nguvu nyingi kama zamani mpaka kufikia mwaka wa 87 wa maisha yake.

Kuifikia Jamii ya Weupe

Kama vile visiwa vingi vya West Indies vilivyo, wakazi wa Barbados sana-sana ni wazao wa watumwa weusi wa Kiafrika—asilimia 90 ya idadi ya watu. Miongoni mwa watu wa kwanza kati ya weupe kukubali ukweli alikuwa Lucy Gooding, ambaye wakati mmoja jamaa yao iliishi lilipo sasa jengo la tawi na Jumba la Ufalme moja katika Bridgetown.

John Benjamin alipeleka ujumbe wa Ufalme kwa akina Goodings jioni moja katika 1910. Wakiwa Waanglikana thabiti, walishtuka kuelezewa ukweli wa Biblia kuhusu baadhi ya imani zao zenye thamani kubwa. Wakiwa wanahangaika, walisema na mhudumu wao. “Sababu gani mfadhaikie mambo haya?” akajibu. “Yasahauni na mshikamane na kanisa.” Badala ya hivyo, wao wakajiuzulu.

Kwa kuwa Dada Gooding alikuwa na utu ulio imara sana na aliweza kueleza ukweli waziwazi, yeye alikuwa katika mstari wa mbele katika kazi ya Ufalme kwa miaka mingi. Kutoka siku za mapema zaidi, nyumba yake ilitumika kuwa makao ya misionari kwa njia isiyo rasmi kwa ajili ya wawakilishi wa pekee wa Sosaiti waliozuru Barbados.

Miongoni mwa hawa Mashahidi wa mapema, hamkuwa na ubaguzi au kutopatana. Migawanyiko ya kikabila au kijamii haikujipenyeza kamwe katika hadhi zao kama vile ilivyofanya katika jamii nyinginezo. Wakale wote ambao wangali miongoni mwetu wanakuwa wepesi kusimulia ithibati ya upendo imara sana na ufungamano waliohisi, na wangali wanahisi, kuelekea mmoja na mwingine. Ni kama alivyosema Yesu: “Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi.”—Yoh. 13:35.

Dada wa kambo wa Lucy Gooding, Winifred Heath, hukumbuka hizo siku za mapema na mabadiliko aliyolazimika kufanya yeye mwenyewe ili kuwa mtumishi wa Yehova anayekubalika. Hujicheka akumbukapo hivi kwa kuaibika: “Jamani, mimi nilizoea kutusi kama mvua samaki.” Kwa sababu mabadiliko hayo yalifanyika polepole, yeye hakupata kubatizwa katika ile miaka ya mapema lakini alifanya hivyo katika 1940 wakati kukusanywa kwa wale “kondoo wengine” kulipokuwa kumeanza.

Manufaa Kutoka kwa Hotuba za Watu Wote

Hotuba za watu wote zimetimiza fungu lenye umaana katika kueneza ukweli. Alfred Joseph, ambaye mwanzoni alitoka Guyana, alipata kukutana na ukweli kwa mara ya kwanza kwenye mhadhara wa Biblia uliotolewa katika mahali peupe katika Brandons Beach, karibu na bandari ya Bridgetown. Watu wapatao 50 walikuwa katika hadhirina kusikiliza ile hotuba “Wafu Wako Wapi?” Mwanzo huu wa elimu yake ya Biblia ulioongoza kwenye ubatizo wake katika 1915, ambao ulifanyiwa karibu na mahali pale pale ambapo alisikia mhadhara wa Biblia kwa mara ya kwanza.

Yesu alisema hivi: “Mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru.” (Yoh. 8:32) Sasa kwa kuwa Ndugu Joseph alikuwa huru kiroho, yeye angeweza kusaidia wengine wapate uhuru uo huo. Kwa kupendeza, katika 1516, kwa Leseni ya Kifalme ya Hispania, njia ilikuwa imefunguliwa kwa ajili ya biashara ya utumwa kutoka Afrika iliyohalalishwa kisheria, ambayo iliendelea kwa zaidi ya karne tatu na nusu. Lakini, pengine kwa ukweli ulioonekana kidogo kuwa kinyume kabisa, Alfred Joseph na William R. Brown wa Jameika, wote wawili wakiwa wazao wa watumwa Waafrika, walienda Afrika kuonyesha njia iongozayo kwenye uhuru wa kiroho kwa maelfu mengi ya watu waishio Afrika Magharibi. Hivyo, katika Juni 29, 1915, Ndugu Joseph aliondoka kwa meli akachukue kazi ya kondrati katika Sierra Leone, ambako pia alijitolea kufanya kazi ya kueneza habari njema za Ufalme.

Wakati Ndugu Joseph aliporudi Barbados miaka 18 baadaye, aliongoza katika kutoa hotuba mahali peupe. Pindi moja, yeye alichukua kikundi cha akina ndugu na dada wakafanyie kazi Waverly Cot katika parishi ya St. George. Kama ilivyokuwa desturi yao, walitumia asubuhi wakihubiria watu katika nyumba zao na kuwaalika kwenye mkutano wa watu wote ambao ungefanywa alasiri. Jumba la umma lilikodishwa kwa kusudi hilo. Hata hivyo, mara tu mhadhara ulipoanza, akina ndugu na dada peke yao wakiwa ndani, washiriki wa Jeshi la Kanisa la Church of St. Luke walikusanyika pale pale upande wa nje wakiwa na dramu ya besi, au “bumu” pamoja na dramu-birika. Kupigwa kwa dramu kwa makelele mengi, pamoja na kuimba kulikusudiwa kuzuie mnenaji asisikike. Umati ukakusanyika. Makelele yalikuwa mengi mno. Ndugu Joseph, akiwa bila vikuza-sauti, hakuweza kusikika hata kidogo.

Ndipo, kwa mshangao mkubwa wa akina ndugu na ule umati uliokuwa upande wa nje, kukanya mvua kubwa ya ghafula. Hata hivyo, mbingu zilikuwa zimekuwa bila mawingu, bila ishara yoyote ya dhoruba iliyokuwa ikija. Kwa kuwa jumba lile walimokuwa wanakusanyika akina ndugu ndipo mahali pekee palipotoa kinga, watu wote waliokuwa wamekusanyika nje, kutia na wale waliokuwa wakipiga dramu, wakaja mbiombio ndani ya jumba, ambalo lilijaa pomoni mara hiyo. Kila mmoja alikaa kwa ajili ya mhadhara wa saa nzima na pia wakaufurahia. Wakati akina ndugu walipoondoka kwa safari yao ya kuelekea nyumbani, walivumbua kwamba kwa njia yenye kushangaza mvua ilikuwa imekunya katika eneo lile tu lilipokuwa jumba!

Mbegu Zaanguka Kwenye Visiwa Vingine

Kwa wakati uliopo ofisi ya tawi katika Bridgetown, Barbados, huelekeza kazi ya kuhubiri Ufalme katika visiwa vingine vitano: Bequia, Carriacou, Grenada, St. Lucia, na St. Vincent. Visiwa hivi viko magharibi mwa Barbados—vyote vikiwa ndani ya mwendo wa kilometa 253.

Grenada, ambacho ndicho kisiwa kilicho mbali zaidi upande wa kusini-magharibi, ni chenye ukubwa wa kilometa za mraba 311 tu, kikiwa na idadi ya wakazi wenye urafiki 112,000. Grenada ilijipatia jina la kubandikwa “Kisiwa cha Vikolezo” kwa sababu ya kuwako wingi wa vikolezo vyenye harufu tamu-tamu kama vile mdalasini, karafuu, maharagwe tonka, cocoa, na basibasi.

Mbegu za ukweli zilipandwa katika kisiwa hiki chenye kupendeza katika ule mwaka ambao Vita ya Ulimwengu 1 ilifyatuka. Elias James akiwa mfanya kazi mhamiaji katika Panama alikuwa amekubali ujumbe wa Ufalme wa Mungu na akawa amekuwa mhubiri aliye wakfu na kubatizwa. Akiwa na hamu nyingi ya kushiriki ukweli na wale wa kisiwa cha kwao, alirudi huko katika 1914. Kabla ya muda mrefu kupita alikutana na Bw. Briggs, Mbarbado aliyeishi Grenada. Upesi Briggs akakubali ujumbe wa Ufalme.

Karibu na wakati huu, wafanya kazi wenye bidii katika Barbados walikuwa wakituma trakti na vipande vingine vya fasihi kwa wale waliojuana nao katika “visiwa vya chini zaidi.” Judith Callender, ambaye alitumikia Yehova kwa uaminifu mpaka kifo chake miaka kadhaa iliyopita, alisimulia kwamba mjomba wake “Popie” alikuwa akitumia Francis, baba yake trakti, ambaye alikuwa Mbarbado, wakati alipoishi pamoja naye katika Grenada. Naye baba yake, alishiriki habari njema pamoja na Wabarbado wenzake.

Miongoni mwa wale waliokubali ukweli alikuwa Chriselda James, dada mkwe wa Elias James. Yeye alifaulu kulea jamaa ya watoto kenda katika ukweli ijapokuwa upinzani wenye kuendelea wa mume wake. Watoto wote kenda wakapata kuwa Mashahidi waliobatizwa. Akiwa mmoja wa waliodai kuwa washiriki wa wapakwa-mafuta, alithibitika kuwa Mkristo mshikamanifu na mwenye kuvumilia mpaka kifo chake katika 1986, akiwa na umri wa miaka 87. Watatu wa watoto wake walikufa mbele yake, lakini wale wengine wote wangali wanatenda, wawili wao wakiwa wanatumika wakiwa mapainia wa kawaida na mmoja akiwa mzee na painia wa pekee.

Wahudumu wasafirio wanakumbukwa pia kwa ushiriki wao katika kazi ya Ufalme katika Grenada. Miongoni mwao walikuwa A. T. Johnson, W. R.  Brown, na E. J. Coward. Utumishi wa Ndugu Coward katika mashariki ya Karibea ulifanikiwa kwa kila kiwango. Hata hivyo, haukuepuka jicho lenye kijicho la makasisi. Wakitumia kwa faida yao ule woga uliokuwako wakati wa Vita ya Ulimwengu 1, maadui wa ukweli walisababisha uvumi mwovu uenee ukidokeza kwamba E. J. Coward alikuwa jasusi Mjeremani! Chini ya mkazo huu kutoka kwa makasisi, wakuu wa serikali waliamrisha Ndugu Coward aondoke West Indies ya Uingereza. Hivyo huduma yake hapa ikakomeshwa ghafula. Baada ya ono hilo, Sosaiti ikang’amua kwamba hakuna Mwanafunzi wa Biblia kutoka United States angepata kuruhusiwa kwa urahisi kuingia visiwa hivyo. Kwa hiyo mipango ikafanywa ili Ndugu George Young, Mkanada, apelekwe kule katika 1922.

Kwa muda wa miaka iliyopita mikusanyiko ilihudhuriwa sana-sana na watu wenye umri mkubwa, hivyo watu walianza kurejezea hii kuwa ile “dini ya watu wazee.” Hata hivyo, roho yao ilikuwa changa na yenye hamu nyingi. Halikuwa jambo lisilo la kawaida kwa wafanya kazi hawa wenye kujitoa kutembea kilometa 8 na zaidi, nyakati nyingine katika mvua kubwa ya kitropiki, wakahudhurie mikutano ya kila juma.

Njoo pamoja nasi sasa tuvukapo kwenda St. Vincent, kilometa 118 tu kaskazini mwa Grenada, tukaone namna kazi ilivyoanza huko.

Mwanzo Katika St. Vincent

St. Vincent, kisiwa chenye kuvutia cha eneo la kilometa za mraba 388 na ambacho ndicho makao ya bustani za usitawishaji mimea zilizo za zamani zaidi katika Karibea ya mashariki, kilitembelewa na Ndugu A. T. Johnson katika 1913. Wakati huo, Ethel na Maud Thompson na baba yao walionyesha upendezi fulani katika ujumbe wa Ufalme. Miaka fulani baadaye, Philippa La Borde, Mtrinidadi, akalowea katika kisiwa kile.

Kuna msemo wa kimashamba miongoni mwa wakulima katika West Indies ambao mara nyingi umethibitika kuwa kweli: “Mbegu iliyoanguka huzaa zaidi ya ile iliyopandwa.” Kwa maneno mengine, mbegu iliyoanguka kwa nasibu huzaa zaidi ya ile iliyopandwa kimakusudi. Kutoa kielelezo, katika 1918, alipokuwa akipekua mifuko ya mumeye kabla ya kufua, Philippa alipata trakti ya Biblia ambayo mumeye alikuwa amepewa na W. R. Brown. Trakti hii iliamsha upendezi. Wote wawili, yeye na mumeye walijifunza na wakakubali ukweli na kisha wakabatizwa katika Agosti 1, 1918. Miaka michache baadaye, wakati fulani kabla ya 1923, walikwenda St. Vincent kwa sababu za kiafya. Walikusudia kukaa huko miezi michache tu, lakini ikawa kwamba walikaa kwa miaka mingi.

Akikumbuka mawazo yake ya kwanza wakati walipokwenda St. Vincent, Philippa hutaarifu hivi: “Barabara za mji zilikuwa hazikutengenezwa vizuri na zilikuwa zenye mavumbi-mavumbi, lakini watu walikuwa wenye urafiki sana, na hilo ndilo lililokuwa jambo la maana.” Kwa muda wa miaka 50 iliyofuata, Dada La Borde, ambaye alitajwa kwa ukawaida kuwa “Mama Lab” kotekote katika kisiwa kile, aliweza kupeleka ujumbe wa Ufalme kwa wakuu wa serikali wenye vyeo vya juu zaidi—kwa sababu alikuwa amekuwa mwalimu wa nasari kwa baadhi yao. Yeye alionekana mdogo na dhaifu, lakini alikuwa na utu imara na alikuwa na uwezo wa kueleza kweli za Biblia katika njia nyepesi na yenye kupatana na akili.

Uwezo wake wa kuchukua hatua ya kwanza na busara yake vilionekana wazi katika ile njia ambayo katika hiyo alimsaidia Marion Dunn, mwenyeji wa St. Vincent, kufikia hatua ya ubatizo. Bi. Dunn alikuwa amekutana na ukweli kwa mara ya kwanza katika Kyuba katika 1914. Upesi baada ya hapo, alirudi St. Vincent, lakini ndipo akakutana na upinzani mkali na wenye kuendelea kutoka kwa mpwa wake aliyeishi naye. Kwa sababu ya roho ya kutaka kulipa kisasi ya mpwa wake, Bi. Dunn alisitasita kuweka maisha yake wakfu kwa Yehova na kuonyesha hilo kwa ubatizo wa maji. Hata hivyo, baada ya Dada La Borde kutoa kitia-moyo na msaada wa Kimaandiko, mipango ilifanywa kumbatiza Marion Dunn faraghani nyumbani mwa Dada La Borde katika 1935. Miaka mingi baadaye, Dada La Borde aliwaza hivi: “Nilijifunza mengi sana kwa kufanya kazi pamoja na Dada Dunn, yaani, saburi na unyenyekevu.”

Msaada Zaidi Waandaliwa

John C. Rainbow, kutoka makao makuu ya Sosaiti katika United States, alipewa mgawo katika 1924 wa kutumia juma moja pamoja na Mashahidi wale katika St. Vincent. Ziara yake iliandaa kitia-moyo kizuri kwa akina dada hawa waaminifu na pia kwa wale waliohudhuria mihadhara yake kwenye Maktaba Carnegie katika Kingstown, mji mkuu.

Katika ziara yake ya pili kupitia visiwa vile, George Young alitua pia katika St. Vincent asaidie akina dada hawa. Wakati huo, katika 1932, ile Photo-Drama of Creation ilionyeshwa katika Maktaba Carnegie na ikapokewa vizuri sana. Kwa kweli, kwa dai la umma, mipango ilifanywa kuwe na wonyesho wa pili, wakati huu katika nyumba ya mahakama ya mji mkuu. Ndugu Young alifanya mfululizo wa hotuba za watu wote na akasaidia akina dada kupanga kitengenezo funzo la kila juma la Mnara wa Mlinzi. Ili kusaidia kuendeleza ibada ya kweli miongoni mwa watu hawa wanyenyekevu, yeye alianzisha pia huduma ya nyumba kwa nyumba katika kisiwa hiki.

Kupapasa-papasa kwa Ajili ya Mungu na Kumpata

Wakati wa miaka ya vita ya 1939 hadi 1945, jambo fulani lilisitawi katika St. Vincent ambalo hakika hutoa kielezi cha mwelekezo wa kimalaika katika kukusanya watu wa mfano wa kondoo. Kule juu ya milima ya Riley ni mahali ambapo mtu anaweza kutazama kusini na kupata mwono mzuri wa kisiwa Bequia umbali wa kilometa zapata 16 au anaweza kutazama kaskazini na kupata mwono wenye kutia kizunguzungu wa Bonde Mesopotamia lililo chini tu. Kule juu ya milima hii kiliishi kikundi cha watu wenye mioyo myeupe ambao walikutana kwa ukawaida kujifunza juu ya Mungu. Ingawa kiliongozwa vibaya, bado walikuwa ‘wakipapasa-papasa kwa ajili ya Mungu.’ (Linganisha Matendo 17:26, 27.) Leonard Pope, askofu wa kikundi hiki, pamoja na kiongozi Albert Forbes na kundi la “Watikisaji,” kama walivyojiita wenyewe, walikuwa wamekuja kuthamini vichapo vya Mnara wa Mlinzi nao walikuwa wakivitumia katika mikutano yao.

Siku moja katika 1942, Rupert G. Wyllie alitua kusikiliza Leonard Pope alipokuwa akihubiri katika eneo lililoitwa Paul’s Lot katika Kingstown. Pope alikuwa akihubiri kwa sauti kubwa, lakini kutokana na yale aliyosema, Wyllie, aliyekuwa msomaji wa fasihi ya Mnara wa Mlinzi, alijua kwamba Pope lazima awe alikuwa akisoma fasihi ile ile. Licha ya hivyo, katika mkono wa Pope, ambao alikuwa akitumia kufanya ishara zenye kufika mbali, mlikuwa kitabu alichokuwa akirejezea mara kwa mara, akidai kwamba kilithibitisha mambo aliyokuwa akisema. Wyllie alikumbuka akifikiri, ‘Ni kweli yeye ni Mtikisaji, lakini sasa anasema jambo linalostahiki kusikilizwa.’ Baadaye, alipokuwa akisema na Wyllie, Pope alisema hivi: “Kwapasa kuwe mahali katika Kingstown pa kujifunza haya.” Wyllie alijua akina Dada La Borde na Dunn na kwa hiyo akaelekeza Pope kwao. Pope alikutana na wale akina dada na akajifunza zaidi juu ya ukweli. Upesi yeye na kundi lake la watu wanane walikuwa wakitembea zile kilometa 8 kuja Kingstown kwa ajili ya funzo la kila juma la Mnara wa Mlinzi.

Katika 1944 wakati wa ziara kwenye St. Vincent ya Gilbert Talma, mwangalizi wa tawi wa Sosaiti katika Trinidadi, wote wanane walibatizwa kwenye Edinboro Beach. Hata hivyo, haikuwa mpaka 1947 kwamba kikundi hiki cha Mashahidi katika Riley kikaundwa kitengenezo kuwa kundi la pili katika St. Vincent. La kwanza lilikuwa katika Kingstown. Mwaka uliofuata baadhi ya wale ambao hapo kwanza walikuwa “Watikisaji” wakawa mapainia wa wakati wote nao wakatoa ushuhuda wenye matokeo mazuri katika maeneo ya milima-milima ya nchi.

Wa mwisho wa wale wanane wa kwanza kabisa katika kikundi cha “Askofu” Pope, Leonora Forbes, ajapokuwa na miguu iliyolemazwa na ugonjwa yabisi kavu, aliendelea kuwa na ushiriki wenye kutenda katika kueneza habari njema za Ufalme mpaka kifo chake katika Machi 1988. Yeye alikuwa chanzo kizuri ajabu cha kitia-moyo kwa wachanga na wazee pia.

Wakati uwanja mdogo wa ardhi uliokuwa juu ya kilima ulipotolewa kwa ujenzi wa Jumba la Ufalme, wafanya kazi hawa wenye bidii-nyendelevu walifanya kazi kwa bidii. Mahali hapo pa ujenzi palikuwa na mwono wenye fahari, lakini lilikuwa jambo gumu kujenga hapo. Akina ndugu na dada walibeba vifaa vya ujenzi juu ya vichwa vyao kuvileta kwenye mahali pa ujenzi—umbali wa kilometa 2.4 kutoka kwenye mto na pia kutoka mahali palipo karibu zaidi ambapo barabara inapatikana. Mwishowe jumba likakamilika, la kwanza kumilikiwa na ndugu zetu katika kisiwa hicho. Njia ya kufikia Jumba la Ufalme hili lenye kuvutia ilikuwa kwa vikanyagio ambavyo vilikuwa vimekatwa katika udongo wa kilima. Bila shaka, wakati wa majira ya mvua vikanyagio hivi vilikuwa vikiwa vyenye kuteleza sana sana, na hesabu fulani ya waangalizi wasafirio wameteleza na kuteremka mpaka chini ya kilima—wakiwa wamesimama ama vingine!

Kabla ya kwenda St. Lucia, tutarudi Barbados kidogo tuone maendeleo ya kazi huko.

Basi Zilizokodishwa kwa Ajili ya Kazi ya Kutoa Ushuhuda

Makolpota (sasa wanaitwa mapainia) walikuwa wakifanya kazi kubwa sana ya kugawanya fasihi ya Biblia. Cuthbert Blackman, sasa akiwa katika mwaka wake wa 77, alikuwa mmoja wa mapainia 10 katika Barbados katika 1931, na kulikuwako wengine 44 walioshiriki kazi kadiri wakati na hali zilivyoruhusu.

Leo wakazi wa Barbados wanatumikiwa vizuri na mfumo wa barabara za kisasa. Kwa kweli, hata ingawa kinaelezwa kuwa “kilometa 34 urefu na upana wa kadiri,” kisiwa hiki kina barabara za kilometa 1,280 zilizotengenezwa kwa zege ama asfalti. Hata hivyo, miaka 50 iliyopita usafiri ulikuwa tofauti sana na ulivyo sasa. Kulikuwako kona nyingi hatari barabarani, ambazo zilikuwa masalio ya mfumo wa barabara wa karne ya 17 ambao ulikuwa umetengenezwa hasa kwa ajili ya mikokoteni ya kukokotwa na nyumbu. Kwa sababu hiyo, Ndugu Blackman husimulia, “Sisi tuliterema vya kutosha kuwa na utumishi wa mkokoteni wa Ndugu Edwin Hackett uliokokotwa na Harry, farasi wake mwaminifu.”

Hata hivyo, njia nyingine za usafiri zilipopata kuwa za kawaida zaidi, akina ndugu wakaanza kukodi mabasi kwa ajili ya kazi ya kutoa ushuhuda. Katika njia hii parishi zote 11 za kisiwa kile zingeweza kuenezwa kwa utaratibu katika kazi ya kutoa ushuhuda wa vikundi. Kwa wakati fulani akina ndugu walitumia kadi za kutolea ushuhuda ili kuelezea sababu ya ziara zao. Baadaye, mirekodio ya mahubiri ya Ndugu Rutherford ilipigiwa wenye nyumba juu ya mashine yenye kubebeka ya kupiga sahani za santuri, na mashine zenye kutumia utepe zilitumiwa kwa ajili ya idadi kubwa zaidi ya wasikilizaji.

Kwa kawaida, watu katika kisiwa huamka asubuhi na mapema. Alfred Joseph alikumbuka kwamba asubuhi moja yeye na ndugu wengine waliamua kuanza mapema kazi ya kutoa ushuhuda katika Holetown, mji wenye idadi ndogo ya watu katika pwani ya magharibi. Waliangika mashine yao yenye kutumia utepe juu ya mti ili sauti iweze kufika mbali katika hewa tulivu ya asubuhi na hivyo ifikie watu zaidi. Njia hii ya kushambulia ilitokeza itikio la mara hiyo. Ndugu Joseph alisema hivi: “Sajini mmoja wa polisi alionekana upesi katika mandhari ile, akitujulisha kwamba alikuwa ametumwa na ‘Reverendi’ na kwamba ilitupasa kukomesha programu yetu ya elimu ya Biblia. Sisi tulimtia moyo asikilize kwa dakika chache. Alipoona kwamba sisi hatukuwa wenye kukosa utaratibu kwa njia yoyote—isipokuwa kuanza mapema—na kwamba hakukuwa na jambo lolote baya kuhusu ujumbe wetu wa Ufalme, akaondoka.”

Mashahidi Wajasiri

Bidii na ujasiri wa akina ndugu, pamoja na kupiga moyo konde kwao kutoa ushuhuda kikamili, ilikuwa alama ya wakati huo. Ilikuwa ni kana kwamba Mashahidi hawa wa mapema walipeleka ujumbe mpaka kwenye malango. Wakiwa na hamu nyingi ya kufunua unafiki na mvurugo katika Jumuiya ya Wakristo, walifanikiwa katika kufanya watu wengi watue na kufikiri kwa uzito, jambo ambalo kwa kawaida hawangefanya.

Kutoa kielelezo, wakati “Reverendi” mmoja aitwae Ince wa Kanisa Nazareti la St. Lawrence katika Kanisa la Kristo, Barbados, aliposikia juu ya safari za Ndugu Joseph katika Afrika, alialika Ndugu Joseph ahutubie kundi lake juu ya maisha katika Afrika. “Mimi nilikubali mara hiyo,” akumbuka Ndugu Joseph, “nami nikaafikiana naye kusema kwa saa moja. Nilitumia sehemu kubwa ya wakati nikisimulia juu ya huduma yangu katika Sierra Leone na njia ya maisha kule. Lakini ndipo nilipohisi inanipasa kusema jambo fulani juu ya mafundisho fulani ya Biblia. Nilimwomba ‘Reverendi’ Ince na katekista wake wafuatane na maandiko niliyokuwa nikitumia kama vile Ezekieli sura ya 34 na Isaya sura ya 28. Kisha, nikiwa mwenye ujasiri zaidi, nilimwalika Ince asome Isaya 56:10, 11. [“Walinzi wake ni vipofu, wote pia hawana maarifa, wote ni mbwa walio bubu . . . ”] Basi, hiyo ilikuwa kupita kiasi, kwa kuwa mara hiyo yeye aliomba wimbo uimbwe. Hata hivyo, kabla ya kundi kuanza, mimi nikaendelea na kichwa changu.

“Kwenye fursa ile ile iliyofuata, yeye akaomba michango ikusanywe. Sasa, je, wewe unaweza kuwazia mimi nikishindana naye hata katika jambo hili, na nikifanya hivyo mle mle ndani ya kanisa lake? Lakini, mimi nilifanya hivyo! Waona, mpangilio wa Sosaiti ulikuwa umepenya ndani sana akilini mwangu—‘Viti ni bure hakuna kukusanya michango’—nami singeweza kuruhusu fursa hii iponyoke bila kusema jambo fulani juu ya hilo. Mimi nilijulisha wazi kundi zima kwamba hatungekusanya hata peni moja na kwamba mimi ningelipia gharama ya umeme uliotumiwa wakati wa mkutano huu. Hatimaye, hakuna michango iliyokusanywa hata kidogo.

“Niliuliza kundi kama lingependa mimi niwahutubie tena, katika pindi nyingine. Itikio lilikuwa ndiyo bila shaka. Hata hivyo, ‘reverendi’ wao hakunialika tena kamwe.

“Wakati fulani baada ya tukio hilo, niliweka mashine yenye kutumia utepe mahali peupe, upande wa nyuma kabisa wa Kanisa Nazareti lile lile nikapiga mirekodio ya Jaji Rutherford. Kama tokeo, wakati kundi lilipokusanyika kwa ibada, wengi hawakwenda ndani, bali, walikaa nje kusikiliza mhadhara uliorekodiwa. Iwe ilikuwa sana-sana ni udadisi au ni kwa sababu ya kupendezwa halisi, singeweza kusema, lakini ningeweza kusema hili: ‘Kundi langu’ lililokuwa nje lilikuwa kubwa zaidi ya lile lililokuwa ndani ya kanisa.”

Kufikia 1936 kulikuwako makundi manne ya Mashahidi wa Yehova katika Barbados—moja katika Bridgetown na moja katika kila parishi za Kanisa la Kristo, St. George, na St. Philip.

Kipofu Asaidia Wengine Waone

Watu wengi kotekote katika kisiwa walikuwa wakikubali ukweli. Walikuwa wakifanya hivyo kwa kusimama mbele ya kampuni, kama yalivyoitwa makundi wakati huo, wakikataa katakata uhusiano wao wa hapo kwanza na Jumuiya ya Wakristo na kufanya tangazo la kujitoa kabisa (wakfu) kwa utumishi wa Bwana. Baadaye, walikuwa wakionyesha hilo kwa uzamisho wa maji. Mmoja wa wale waliofanya hivyo katika miaka ya mwisho-mwisho ya 1930 alikuwa kipofu, Cecil Alleyne.

Cecil alifanya tangazo lake la peupe katika kikao tofauti. Akiwa pasta msaidizi wa Kanisa Nazareti katika Blades Hill, St. Philip, tayari alijua vifungu vingi vya Andiko. Lakini alikuwa hajapata kamwe kufahamu kile “kigezo cha maneno yenye afya.” (2 Tim. 1:13, NW) Hata hivyo, wakati Ndugu Blackman alipomtolea ushuhuda, hata ingawa Cecil alikuwa kipofu, haikumchukua muda mrefu kuona ukweli. Sasa alihisi kuchukizwa juu ya ile miaka mingi ya nuru ya elimu ya kiroho aliyokuwa amepoteza katika ushirika wake na Kanisa Nazareti. Muda mfupi baada ya hapo, alisimama katika kanisa na kufanya tangazo lake kwamba hangeendelea kushirikiana nao lakini kwamba alikuwa amekuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova. Wengi waliohudhuria walitoa machozi na kumsihi asiondoke, kwa kuwa alikuwa amependwa sana nao. Lakini katika muda wa miaka mingi iliyofuata, wengi wa hao hao walijitia katika ibada ya kweli kama tokeo la kutolewa ushuhuda na Ndugu Alleyne.

Yeye alijua zile wilaya vizuri sana, kwa kuwa hakuwa amezaliwa akiwa kipofu. Wakati ambao alikuwa akiongozwa kotekote katika eneo, alijua alipokuwa hasa na ni nani aliyeishi katika nyumba yoyote ile ambayo huenda akawa anaipita wakati ule. Bidii yake yenye kutokeza na ucheshi vilimfanya apendwe na wengi kwa njia yenye kuthaminika. Yeye alikuwa na njia yenye kuvutia watu, ikitegemezwa na kicheko chenye kuambukiza wengine, ambacho kilikuwa kikikazia mambo ya Kimaandiko aliyokuwa akizungumzia na pia kikaandaa kituo chenye kuburudisha ili kuruhusu mambo hayo yapenye ndani. Sana-sana yeye ndiye aliyewezesha baadaye kundi zuri lianzishwe katika Blades Hill. Mmoja wa wale aliohubiria na ambaye alisaidia sana alikuwa Oswald Batson, ambaye alipata kuwa painia na baadaye akatumikia akiwa mwangalizi wa mzunguko kisha mwangalizi wa wilaya katika vile visiwa sita vya eneo la tawi mpaka kifo chake katika 1957. Ndugu Alleyne amekufa pia.

Tengenezo la Kitheokrasi Wakati wa Vita ya Ulimwengu 2

Kihistoria mwaka 1938 ulikuwa wenye maana kubwa kwa watu wa Yehova ulimwenguni pote. Mwaka huo ulitia alama utambuzi wa uhitaji wa tengenezo la kitheokrasi kabisa. Katika Karibea ya mashariki, kama ilivyokuwa ulimwenguni pote, kulikuwako ukazaji wa muundo wa kitengenezo. Jambo hilo lilikuwa kweli kweli na uongozi wa kimungu, kwa kuwa lilichangia umoja uliohitajiwa kusaidia Wakristo wa kweli kudumisha kutokuwamo wakati wa pambano la ulimwengu ambalo lilifuata upesi.

Hata ingawa visiwa hivi havikuhusika moja kwa moja katika uhasama, vikiwa makoloni ya Uingereza viliandaa idadi fulani ya wanaume wenye kuvaa yunifomu kwa utumishi wa kijeshi. Hata hivyo, ndugu zetu walijitenga na utendaji wa vita wakatoa jitihada zao kwa ajili ya kuelekeza watu kwenye Ufalme wa Yehova kuwa tumaini pekee la aina ya binadamu. Hata ingawa hakukuwa marufuku rasmi juu ya vichapo vya Sosaiti, wakuu walitumia vyeo vyao vya juu kuwekea mipaka uingizaji wa fasihi, rekodi, hati, na ugavi mwingineo ambao ungekuwa wenye usaidizi kwa utendaji wa Ufalme.

Uhaba wa fasihi ukatokea. Kwa hiyo vichapo vyovyote vile walivyopokea akina ndugu vilitumiwa kwa uangalifu sana. Dada Lucy Gooding na wengine wachache katika Barbados wakawa waandishi wenye kujitoa sana, wakirudufisha na kugawanya kwa akina ndugu makala za funzo za gazeti lolote la Mnara wa Mlinzi walilopokea. Yenye kuonyesha shukrani za kutoka moyoni, pamoja na kuonyesha mwelekeo wa wote wale waliokuwa wakishirikiana wakati huo, ni maneno haya ya Dada La Borde wa St. Vincent: “Sisi tunashukuru Yehova na Dada yetu mpendwa Gooding, aliyeshiriki pamoja nasi wito wa kimbingu, kwamba tuliweza kwenda sambamba na habari iliyo ya karibuni zaidi.”

Baada ya vita kumalizika, ombi lilitolewa kwa serikali iruhusu vichapo vya Sosaiti viingizwe nchini tena. Upesi baada ya hapo, upakizi ukapokewa, na hakuna ugumu wowote ambao umepata kuonwa tangu wakati huo.

Wahitimu wa Gileadi Wawasili

Nchi nyingi, kutia na Barbados, sasa zilikuwa katika hali ya kuweza kupokea baraka isiyotazamiwa. Kuanzia 1945, wahitimu wa Shule ya Biblia ya Gileadi ya Mnara wa Mlinzi waliwasili. Hiyo iliipa kazi kichocheo kikuu kama nini!

James na Bennett Berry, ndugu wawili wa kimwili, na Franklyn Lamar Pate walianza kutumikia wakiwa wamisionari katika Novemba 1945. Pia walitumikia vile visiwa vingine ambavyo sasa viko chini ya tawi hili wakiwa waangalizi wa mzunguko, ambao wakati huo waliitwa watumishi kwa akina ndugu. Kwa kushiriki pamoja na akina ndugu yale mazoezi mazuri waliyopokea katika Gileadi, maendeleo yenye kuonekana wazi yalionekana katika kiwango cha kufundisha, ndani ya makundi na katika huduma ya shambani pia.

Kwa mara ya kwanza akina ndugu katika Barbados walithamini manufaa ya kuzungumzia mafungu yote yaliyoratibiwa ya habari ya funzo iliyogawiwa kwa wakati uliowekwa. Hilo lilikuwa lenye manufaa hususa kwa Kundi la Bridgetown, ambamo roho ya ugomvi ilikuwa imesitawi miongoni mwa baadhi ya watu mmoja mmoja. Roho hiyo iliyofanyiwa maendeleo ilisaidia kuleta ukuzi zaidi wa kiroho. Hesabu fulani ya wapya na wachanga zaidi wakaanza kushirikiana na kundi.

Kufikia sasa yalikuwako makundi sita katika Barbados, yakiwa na wahubiri watendaji 72. Hudhurio la Ukumbusho kwa mwaka huo lilikuwa 199. Kwa wakati uliopo, Grenada iliripoti wahubiri 15, wakiwapo 22 kwa ajili ya Ukumbusho.

Ziara ya Msimamizi

Katika 1946 baada ya vita, msimamizi wa Sosaiti, Nathan H. Knorr, na aliyekuwa wakati huo makamu wa msimamizi, Frederick Franz, wakazuru West Indies kwa mara ya kwanza. Hata hivyo, katika pindi hii, kisiwa pekee kilichotembelewa kilikuwa Trinidadi, ambacho kiliangalia kazi ya Ufalme katika visiwa vyote vya Karibea ya mashariki.

Ni msisimuko na uthamini ulioje uliobubujika wakati barua ilipopokewa kutoka ofisi ya tawi katika Port of Spain, Trinidadi. Ikipelekewa makundi yote, barua hii ilisoma hivi kwa sehemu: “Mkusanyiko utapangwa, na mkutano wa watu wote Ndugu Knorr akiwa msemaji. Haitawezekana Ndugu Knorr na Franz kuzuru visiwa vingine katika safari hii, kwa hiyo tafadhali waarifuni akina ndugu. . . . Ingekuwa vizuri watumishi wa kampuni na mapainia waje, ikiwa wanaweza. Hii itakuwa fursa nzuri ajabu kwa akina ndugu katika West Indies kukutana pamoja na msimamizi na makamu wa msimamizi wa Sosaiti na kupata habari nyingi zenye thamani juu ya kusogeza mbele utumishi wa Ufalme.”

Hata hivyo, manufaa za programu ya mkusanyiko huo zilishirikiwa hata na wale ambao hawakuweza kufanya safari hiyo kwenda Trinidadi. Ili kuwezesha hilo, mkusanyiko mkubwa ulifanyiwa Barbados katika Oktoba wa mwaka huo. Kufikia wakati huo Joshua Steelman, mhitimu mwingine wa Gileadi, alikuwa amewasili, naye alikuwa na ushiriki katika programu ya mkusanyiko. Kwenye mkusanyiko huo akina ndugu walipokea habari kwamba wangekuwa wakipata ziara za ukawaida kwa makundi zikifanywa na “watumishi kwa akina ndugu,” wanaoitwa sasa waangalizi wa mzunguko. Kilele cha hudhurio kilikuwa 902. Huo ulikuwa ndio mwanzo wa enzi ya mikusanyiko mikubwa zaidi iliyopangwa vizuri katika Barbados.

Miongoni mwa wale walioimarishwa na mkusanyiko huo walikuwa akina ndugu Gall, St. Clair na Frank. Ile roho ya kweli ya painia ambayo wamisionari hao walionyesha iliwavutia sana sana hivi kwamba wao pia wakachukua utumishi wa painia. Katika 1950 Frank Gall na Fitz Gregg wakawa Wabarbado wa kwanza kualikwa wahudhurie Shule ya Gileadi. Baada ya kuhitimu darasa la 16, wote wawili walipewa mgawo kwenda British Honduras (sasa ni Belize).

Ndugu wenyeji walipokuwa wakijitumikisha kabisa, nyakati nyingine kupita ilivyo kawaida, Yehova alimimina baraka nyingi juu yao. Dudley Mayers, mwenye umri wa miaka 81, anakumbuka miaka hiyo naye hutusimulia hivi: “Tulikuwa kumi tu katika kikundi chetu kidogo katika Hall’s Village, St. James, kutia washiriki wanne wa jamaa yangu. Kwa kuwa mmoja wa akina ndugu alikuwa mzee sana na akina dada walikuwa wengi, mimi niliwekwa rasmi kwenye madaraka yote ya mtumishi katika kampuni, kama tulivyoliita kundi wakati ule. Baadaye, tulihamia Cave Hill, St. Michael, zapata kilometa 5 kutoka mahali tulipokuwa mwanzoni, na tokea wakati huo na kuendelea mambo yalianza kufanya maendeleo kikweli kufikia hatua ambapo leo sisi tuna wahubiri 135 na zaidi ya 200 huhudhuria mikutano yetu ya Jumapili.” Ndugu Mayers mwenyewe, ingawa amekuwa na mapigo matatu ya moyo, huendelea kutumikia kwa ukawaida akiwa painia msaidizi.

Hawakuacha

Iliwachukua wamisionari wakati fulani kujipatanisha na hali za kienyeji na kupata kadiri fulani ya kinga mwilini kwa magonjwa ya kienyeji. Wengi wao hawakuacha bali walikaa katika migawo yao.

Kielelezo chenye kutokeza cha mmoja ambaye hakuacha na kuondoka na ambaye amekuja kupendwa sana na akina ndugu ni Sven Johansson. Yeye na Richard Ryde walipewa mgawo kutumikia wakiwa wamisionari katika Grenada katika Machi 1949. Ndugu Johansson, ambaye hapo mwanzoni alitoka Sweden, anakumbuka wakati alipopata homa ya maleria. Kwa kutokujua huo ulikuwa ugonjwa gani, alijaribu kujitibu homa ya mafua vizuri kadiri ile yeye akiwa mseja alijua, lakini hatimaye aling’amua kwamba ugonjwa wake ulikuwa mkali kuliko vile alivyokuwa amewazia. Anaandika hivi: “Wakati daktari aliponileta chini ya uangalizi wake, ilikuwa ni kuchelewa mno. Kila mtu alifikiri ningekufa. Richard Ryde, misionari mwenzangu, hata aliandikia Ndugu Knorr juu ya mipango ya mazishi. Ndugu Knorr alijibu mara hiyo kwamba yeye apaswa kuhakikisha kwamba nimepata utunzaji wa kitiba ulio bora zaidi unaopatikana.

“Hatimaye, nikapona. Kisha mwenzangu akawa mgonjwa jinsi iyo hiyo. Tulikuwa wagonjwa pamoja kwa kurudia-rudia. Nyakati nyingine sote wawili tulikuwa wagonjwa na kulala kitandani wakati ule ule mmoja. Ili kuamua ni nani angeamka kumtunza mwingine na kufanya kazi za nyumbani zilizohitajiwa kabisa, tulikuwa tukilinganisha joto la mwili. Yule aliye na joto la juu zaidi alipata kukaa kitandani. Kwa miaka mingi tuling’ang’ana na homa hii yenye kusumbua na yenye kurudi mara kwa mara. Kwa habari yangu, ilinichukua miaka minane kabla ya kupona kabisa.”

Astahiwa kwa Kazi ya Ufuataji Haki

Ndugu Johansson alitumikia si Grenada tu, ambako alioa dada mwenyeji, bali pia St. Vincent. Katika 1951 yeye na mke wake walikwenda St. Vincent, ambako walitumikia wakiwa mapainia wa kawaida kwa miaka kadhaa. Hata hivyo, mara tu alipokaa na kutulia alijulishwa na mkuu wa polisi kwamba alikuwa na siku tano za kuondoka kisiwani. Katika mahoji yaliyofuata pamoja na mkuu huyo, yeye aliambiwa kwamba alitangazwa rasmi kuwa asiyetakikana kwa sababu alikuwa jasusi wa kigeni. Ndugu Johansson alimweleza kwamba alikuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova naye hakuhusika katika siasa. Mkuu huyo wa polisi alibaki akiwa imara kabisa.

Ndugu Johansson aliandika hivi: “Rufani yangu pekee ilikuwa kwenda kumwona msimamizi wa kisiwa. Baada ya kufanya mwadi, niliweza kusema na msimamizi kwa dakika 30. Yeye alithibitisha yale ambayo mkuu wa polisi alikuwa ameniambia mapema, yaani, kwamba mimi sasa nilikuwa mgeni asiyetakikana. Ndipo msimamizi huyo akajulisha wazi kwamba mimi nilikuwa nikipinga Wakatoliki; yeye mwenyewe akiwa Mkatoliki, alihisi kwa nguvu sana juu ya jambo hilo. Mimi nilimhakikishia kwamba sikuwa nikipinga Wakatoliki. Nilitaja kwamba kinyozi wangu alikuwa Mkatoliki na kwamba mimi nilitembelea Wakatoliki katika nyumba zao kuongea nao juu ya Biblia. Mwishowe, alisema hivi: ‘Bw. Johansson, mimi nimesikia kwamba wewe unajua kutengeneza redio vizuri sana. Mimi nina redio mbili zinazohitaji kutengenezwa. Nitazituma kwako kesho uzitengeneze. Unaweza kukaa kisiwani.’ Ndipo akainua simu, akampigia simu mkuu wa polisi, na kumpa maagizo kwamba napaswa kuruhusiwa kukaa kisiwani.”

Zaidi ya mara moja, ushuhuda mzuri ulitokana na uhakika wa kwamba Ndugu Johansson alikuwa mfano mzuri katika kazi yake ya kimwili. Mfanya biashara mmoja alitaka mtu mfuataji haki mwenye kutegemeka wa kutengeneza redio zilizoharibika. Yeye alichukua redio mbili zinazofanana ambazo zilikuwa katika hali nzuri, akakata waya katika mfumo wa kila moja. Kisha akapeleka hizo redio mbili kwa mafundi wawili ambao yeye aliwafikiria kuwa miongoni mwa wale walio bora zaidi katika kazi yao. Wakati Ndugu Johansson aliporudisha ile redio aliyokuwa amepelekewa atengeneze, alitia ndani risiti ya kudai malipo ya dola 2.40 (senti 88, U.S.), akitaarifu kwamba ni kwa ajili ya kuchomelea waya iliyokuwa imekatika. Yule fundi mwingine alipeleka risiti ya dai la malipo kwa ajili ya kubadili tyubu na sehemu nyingine. Ndugu Johansson alipata kazi ya mtengeneza redio kwa ajili ya shirika hilo la biashara.

Wakati wa miaka 39 ambayo Ndugu Johansson amekuwa katika visiwa hivi, ameshiriki kazi ya mzunguko, wilaya, na painia wa pekee. Kwa sasa anakaa Barbados naye anatumikia akiwa painia wa kawaida na mshiriki wa Halmashauri ya Tawi inayoangalia kazi katika visiwa hivi. Ijapokuwa alipatwa na pigo la moyo kali sana hivi majuzi, sasa amepata nafuu. Moyo wake, ukiwa umedhoofika kidogo, unataka afanye mambo kwa mwendo wa polepole zaidi. Kielelezo chake kwa muda wa miaka iliyopita hukumbusha wengi lile elezo la Paulo kwenye 2 Wakorintho 6:4-6, NW: “Katika kila njia tunajipendekeza wenyewe kuwa wahudumu wa Mungu, kwa uvumilivu wa mengi, kwa dhiki, kwa visa vya uhitaji, kwa magumu, . . . kwa ustahimilivu, kwa fadhili, kwa roho takatifu, kwa upendo bila unafiki.”

Kazi ya Ufalme Yaanza Mwendo Katika St. Lucia

St. Lucia, kilicho umbali wa kilometa 192 kaskazini-magharibi mwa Barbados, ni kisiwa cha kitropiki chenye kupambwa kwa majani-majani na chenye kuvutia cha wakaaji 120,000. Kikiwa chenye sifa sana kwa sababu ya vilele viwili vya mlima Gros Piton na Petit Piton vyenye umbo la mviringo-chini, ambavyo hutokeza baharini, kisiwa hicho kinajulikana sana kwa zao la ndizi na nazi kavu.

Katika 1947 St. Lucia kilianza kutokeza tunda la Ufalme pia. Shahidi wa kwanza mwenyeji alikuwa Leanna Mathurin. Wakati mwanamke huyu alipokubali ukweli, alikuwa akiishi katika Demerara, Guyana. Yeye aliandikia Ndugu Knorr, akiuliza kama kuna jambo lolote ambalo angeweza kufanya kusaidia kueneza habari njema katika St. Lucia. Baada ya kupokea jibu la Ndugu Knorr lenye kutia moyo, alihamia Micoud, kijiji kimoja kilicho umbali wa kilometa 48 kutoka Castries, mji mkuu.

Miaka miwili baadaye, wamisionari waliozoezwa Gileadi—Lloyd Stull na William Cammers wakawasili. Hao wawili, pamoja na Leanna Mathurin, wakawa ndio jumla ya idadi ya Mashahidi wa Yehova kisiwani.

Dada huyu mwenye bidii, akiwa anafahamiana vizuri na lugha patois ya kienyeji, ambayo ni mchanganyiko wa Kifaransa na Kiingereza, alifikia watu wengi wa mashambani akiwa na faraja kutoka kwa Maandiko. Kutokana na fedha zake mwenyewe alijenga Jumba la Ufalme dogo. Vyumba viwili viliongezwa kwalo, kimoja katika kila upande. Yeye mwenyewe alikaa katika kimoja na kile kingine aliweka kando kwa ajili ya wahudumu wasafirio. Ingawa ana umri wa miaka 82, angali anatumikia kwa bidii akiwa painia wa kawaida.

St. Lucia, kikiwa sana-sana kinatawalwa na Ukatoliki, kilitokeza ushindani fulani fulani kwa wamisionari katika kupata makao yanayofaa, lakini Ndugu Stull asema hivi: “Sisi tulichukua oni la kwamba kila kitu tulichohitaji kingeandaliwa katika huduma ya nyumba kwa nyumba.” Na hakika, wakati baada ya wakati mahitaji yao ya lazima yalitimizwa.

Katika muda wa miaka iliyopita wamisionari zaidi walipelekwa St. Lucia. Miongoni mwao walikuwa Fred Dearman kutoka United States na William na Edith Honsinger kutoka Kanada, ambao wangali wanatumikia kwa uaminifu katika migawo yao. Baraka za Yehova zimedhihirika kikweli juu ya kazi zao ngumu za upendo, kwa kuwa sasa kuna Majumba ya Ufalme manne mazuri yakitumikia mahitaji ya makundi matano na wahubiri wayo 380 wenye bidii.

Ugonjwa wa Baharini Wakati wa Safari Kwenye Mkusanyiko

Katika ile miaka ya mapema, ili kufika kwenye mikusanyiko katika vile visiwa mbalimbali, akina ndugu walilazimika kutumia vyombo vya matanga, merikebu kubwa zenye mbio, majahazi, au chombo chochote kilichosafiri baharini kati ya visiwa vile. Hakukuwa na utumishi wowote wa ndege wenye kutegemeka uliounganisha visiwa vile. Wale waliokuwa mabaharia hodari, kusafiri baharini hakukutokeza ugumu wowote. Lakini kwa wengine kama Ndugu Stull, mara nyingi lilithibitika kuwa ono lenye kugonjwesha.

Mtu fulani alieleza mojawapo safari hizo katika njia hii: “Ndugu Stull, alipata kuwa mgonjwa sana merikebuni kwa kuwa hakuwa baharia hodari. Zaidi ya hilo, kufanya jambo baya kuwa baya zaidi, ile ambayo ingalikuwa safari ya siku moja ilichukua siku tatu kwa sababu ya mchafuko wa bahari.

“Ilikuwa lazima kulala kwenye sitaha, kwa kuwa mizigo ilikuwa imewekwa ndani ya ngama na upenu wa merikebu. Kilikuwapo chandarua cha kujikinga mvua, lakini hatimaye mvua na mnyunyizo wa maji ya bahari yalikuwa yakiingia ndani. Ndugu Stull alikuwa mgonjwa sana hivi kwamba yeye hakuwa na nguvu za kufikia mahali pa kujikinga, hivyo wakati ulio mwingi alikuwa bila kinga kutokana na mvua na jua. Wakati wa mchana, jua lilipokuwa likiwaka, tulikuwa tukimviringisha upande mmoja apate kukauka, kisha ule upande mwingine mpaka alipokuwa amekauka—hadi kile kipindi kingine cha hali mbaya ya hewa, wakati ambapo jambo ilo hilo lingerudiwa.”

Ono hilo lenye kusumbua-sumbua liliendelea mpaka akina rafiki walipokuja karibu vya kutosha kuweza kuona kisiwa cha mkusanyiko. Lakini hata wakati huo hakukuwa na kitulizo. Mkondo ulibadilika nayo merikebu ikapeperushwa baharini, isionekane tena. Wakati mwishowe walipotia gudini, kilikuwa kitamaushi kama nini kujua kwamba maofisa wa uhamiaji na wa forodhani walikuwa wamekwisha ondoka vituoni mwao! Kwa hiyo akina ndugu wakalazimika kutumia usiku mwingine ndani ya merikebu.

Richard Ryde, ambaye makao yake yalikuwa Grenada akiwa misionari, alipatwa pia na ono la magumu ya kusafiri kati ya visiwa. Alikuwa ameratibiwa atumikie akiwa mwenyekiti wa mkusanyiko katika Barbados. Alisafiri kwa meli kutoka Grenada kwenda St. Vincent, akitumaini kuunganisha safari kwenda Barbados. Akijua mabadiliko-badiliko ya safari za kati ya visiwa, aliruhusu wakati wa kutosha ili aweze kushiriki kazi ya kabla ya mkusanyiko. Hata hivyo, kwa sababu ya hali za bahari, Ndugu Ryde aliwasili Barbados kuwahi tu kusikiliza hotuba ya watu wote! Wakati ile merikebu aliyokuwa akisafiria ilipokaribia Barbados, wale waliokuwa merikebuni wangeweza kuona bara katika pindi kadha wa kadha. Hata wangeweza kutambua watu wakitembea ufuoni. Lakini mikondo na upepo mbaya viliwazuia kuifikia. Mabaharia washirikina waliona matukio hayo kuwa dalili mbaya nao wakatundika misalaba, lakini wapi. Kwa chukizo lenye kueleweka, Ndugu Ryde akawaambia, “Kina bwana, hamhitaji misalaba—mnahitaji mota nyingine.”

Ziara Kutoka Makao Makuu

Akina ndugu walifurahishwa kama nini na habari katika 1949 kwamba Ndugu Knorr, akiwa katika safari yake ya pili kupitia Karibea, angezuru Barbados! Wakati huu, Milton Henschel, pia kutoka wafanya kazi wa makao makuu, angeandamana naye. Mkusanyiko wa wilaya wa kati ya visiwa ambao ungefanyiwa Steel Shed ulipangwa ulingane na ziara hiyo.

Hudhurio kwenye hotuba ya watu wote, “Wakati Umesonga Sana Kuliko Unavyodhani!” lilikuwa 3,000. Hesabu hiyo haikupitwa kwa miaka mingine 25. Wakati wa mkusanyiko huo Ndugu Knorr alizungumza pia pamoja na mapainia habari ambayo ingeletea visiwa hivyo faida za kiroho—taraja la mazoezi ya Gileadi.

Ile “Dini Isiyoamini Moto wa Mateso”

Upendo mkubwa wa watu kwa Biblia umefumwa ndani ya utamaduni wa maisha ya Wabarbado. Hilo, pamoja na hali ya kujua kusoma na kuandika iliyoenea kote na tamaa nyingi ya kutaka kujifunza, hufanya huduma ya nyumba kwa nyumba iwe ushindani wenye kupendeza. Ni mara chache mtu anapokosa kusikilizwa. Badala ya hivyo, huenda akapata kwamba mazungumzo motomoto ya kidini yanasitawishwa, yakihitaji maarifa mengi ya kujua Biblia na utumizi wayo wa ufundi.

Kwa wakati fulani, hasa wakati wa miaka ya 1960 na 1970, mara nyingi watu walikuwa wakiwasema Mashahidi kuwa ile “dini isiyoamini moto wa mateso.” Mmoja wa ndugu zetu hukumbuka kwamba Gertrude Linton alikuwa akisemwa na watu mtaani kuwa “Gertie Asiyeamini Moto wa Mateso.” Kwa wazi hiyo ilikusudiwa ikwaze watu waliokuwa wakionyesha upendezi katika ujumbe wetu. Kwa hiyo ikawa lazima kuwa na sehemu katika programu ya kusanyiko la mzunguko kuonyesha jinsi ya kushughulika na kipingamizi hiki kwa kutumia King James Version. Maandiko ya Biblia kama vile Zaburi 55:15; 86:13; Isaya 14:9; na Yona 2:2, pamoja na marejezo ya pambizoni yanayoambatana nayo katika King James Version yalitumiwa. Kwa kuwa nyumba zilizo nyingi zilikuwa na tafsiri hiyo yenye marejezo ya pambizoni, akina ndugu waliweza kusababu na watu kutoka kwa Biblia zao wenyewe na kuwasaidia kuona kwamba moto wa mateso unaotajwa katika Maandiko si mahali pa mateso ya moto bali ni kaburi. Kwa wazi njia hii ilithibitika kuwa yenye kufanikiwa, kwa kuwa ni vigumu kusikia kipingamizi hicho tena.

Kueneza Visiwa vya Grenadine kwa Ushuhuda

Sasa vile visiwa vikubwa katika eneo la tawi hili vilikuwa vikipata ushuhuda mwingi. Lakini vile visiwa vidogo zaidi vinavyotapakaa katikati ya Grenada na St. Vincent vilihitaji uangalifu pia. Visiwa hivi vinaitwa Grenadine.

Siku hizi mtu anayesafiri kwa ndege katika eneo hili hawezi kamwe kukosa kuona visiwa hivi. Hata hivyo, ili kuvifikia miaka mingi iliyopita, Sosaiti ilinunua merikebu ya meta 20 iliyoitwa Sibia. Ilikuwa katika Machi 18, 1950, kwamba kikundi cha wamisionari cha kimataifa kilitia nanga nje ya kisiwa cha Carriacou, kilicho kikubwa zaidi cha visiwa Grenadine. Miongoni mwa mabaharia hao walikuwamo Arthur Worsley, Stanley Carter, Ronald Parkin, na Gust Maki, aliyetumikia akiwa nahodha—wote wakiwa wapiga-mbiu ya habari njema wenye bidii. Kabla ya muda mrefu kupita wale watu 7,000 katika kisiwa hiki cha kilometa za mraba 34 walikuwa wamepokea ushuhuda uliopangwa kitengenezo kwa mara ya kwanza.

Akina ndugu walipata kwamba, wajapokuwa peke yao kwa kulinganishwa, mlikuwamo roho ya uchangamfu wa kutoka moyoni miongoni mwa watu. Hawakuwa na vitu vingi kimwili, lakini hilo halikuhangaisha wamisionari kwa kuwa wao walikuwapo pale ili kutoa na kushiriki. Kwa hiyo ili kusaidia watu hao wanyenyekevu, mara nyingi wamisionari walibadilishana Biblia na fasihi nyingine na mazao ya kienyeji ya njugu, mahindi, na mboga. Katika Agosti 29, 1950, Shahidi wa kwanza mwenyeji, dada mmoja, akabatizwa. Katika Septemba 22, 1952, kundi lilipangwa kitengenezo. Leo kundi hilo moja lina wahubiri zaidi ya 43, bila kutaja wahubiri wengi ambao wamehama kutoka kisiwani na ambao sasa wako Ulaya, Amerika Kaskazini, na visiwa vingine vya Karibea.

Kingine cha visiwa vya Grenadine ambacho huhifadhi uzuri wacho wa kimashamba usioharibiwa ni Bequia. Sibia ilisafiri kuingia ndani ya bandari yacho yenye kuvutia, Port Elizabeth, katika Aprili 5, 1950. Wakati wa miaka iliyofuata, ziara kumi zilifanywa na Sibia kwenye kisiwa hiki cha wakaaji 6,000. Leo, kundi imara la wahubiri wapatao 20 huangalia kupendezwa kisiwani humo.

Katika 1953 msimamizi wa Sosaiti alikubali merikebu kubwa zaidi inunuliwe, chombo chenye kutumia mota kilichoitwa Le Cheval Noir, kichukue mahali pa Sibia. Jina lilibadilishwa liwe lenye kufaa zaidi, Light (Nuru), ambalo liliwakilisha kikweli kusudi la chombo hicho chenye rafardha mbili. Mlikuwamo nafasi kwa watu wanane kuishi ndani yacho. Hata kingeweza kusafirisha kufikia watu 50 katika safari fupi za kati ya visiwa, na mara nyingi hilo lilifanywa kiliposafirisha wahubiri kati ya visiwa kuhudhuria mikusanyiko.

Msaada Baada ya Kimbunga Janet

Katika Septemba 1955, Kimbunga Janet kilikumba visiwa vya Barbados, Bequia, Carriacou, Grenada, na St. Vincent. Kama vile dume mwenye kasirani, upepo huo, ukiwa katika mwendo wenye nguvu kadiri ambayo haijapata kuonwa kamwe katika kumbukumbu za watu wanaoishi katika eneo hilo, uling’oa miti na nyumba. Kabla ya kuendelea kaskazini zaidi, Janet kilivumisha trilioni nyingi za nguvu-farasi za kani yenye kuharibu juu ya visiwa hivi kwa juma kamili. Asilimia tisini ya nyumba na majengo katika Carriacou ziliangushwa chini au kuharibiwa.

Upendo ambao akina ndugu walionyesha kuelekea wale walioathiriwa na kimbunga hicho ulikuwa wenye kutokeza kweli kweli. “Wakati wa kimbunga hicho sisi tulikuwa pamoja na chombo Light katika eneo la Puerto Riko,” akasema Gust Maki. “Akina ndugu na dada katika Puerto Riko walitupatia mavazi mengi pamoja na vyakula tupelekee akina ndugu katika Carriacou.” Akikumbuka itikio la watu, yeye aliendelea kusema hivi: “Kwa kuwa makanisa yote katika Carriacou yaliharibiwa, hakukuwa na ibada za kidini kwa majuma kadhaa. Padri Mkatoliki alionekana akienda kwenye nyumba za washiriki wake kuwatolea Ushirika kabla ya kuondoka kisiwani. Padri Mwanglikana alitembelea nyumba ya mwanamtaa kuomba pesa ili kanisa litengenezwe; wakati ule ule mtu huyu alikuwa akiishi katika chumba cha jikoni kilichokuwa kibanda. Mwanamke huyu alisikika akisema, ‘Askofu wangu anakuja kuomba pesa, hali Mashahidi wa Yehova wanakuja kusaidia washiriki wao.’”

Uhamaji Wawa na Uvutano Juu ya Ukuzi

Ile miaka ya kutoka 1950 kufika 1970 ilibadili kigezo cha ukuzi na usitawi wa tengenezo kotekote katika eneo la tawi. Watu kutoka kotekote katika Karibea mashariki walihisi uhitaji wa kuhamia nchi zilizositawi zaidi kutafuta “maisha bora” na hali za kiuchumi zilizoendelea. Ndivyo ilivyokuwa hasa kwa habari ya Wabarbado. Katika pindi ya miaka 30, Barbados iliripoti jumla ya upungufu wa idadi ya watu 74,000.

Hali ya kiuchumi ya ndugu zetu haikuwa tofauti na ile ya watu wengine. Wengi walijikuta wakiumia katikati ya madai mawili yenye kubana—ule uhitaji wa kuandalia jamaa zao chakula, mavazi, na nyumba, na ule uhitaji muhimu zaidi wa kutanguliza mambo ya kiroho na kudumisha umoja wa kijamaa katika ibada ya kweli. Hali hiyo ilitokeza kadiri kubwa ya michunguzo ya nafsi kwa vichwa vya jamaa visiwani.

Makundi mengi yalidhoofishwa sana na mwondoko wa baadhi ya akina ndugu ambao ndio waliokuwa wahubiri wenye bidii zaidi. Katika visa fulani, mfululizo wa kutokuwapo kwa mshiriki mmoja wa jamaa kulichangia kutoaminika katika ndoa, na ili kutengeneza ufa wa ndoa, nidhamu pamoja na mwongozo kutoka kwa wazee ulitakwa. Uhakika wa kwamba jamaa haikuwa pamoja ulichangia kufanya watoto kuwa wakosaji, katika visa fulani. Kadiri miaka ilivyopita, wahamaji wenye kurudi walikuwa katika hali nzuri zaidi kifedha katika visa vilivyo vingi, lakini kwa sababu ya dhara lililofanywa kwenye mahusiano ya jamaa na hasara ya kiroho, baadhi yao walipata wakijiuliza, ‘Ulikuwa wema gani hata hivyo?’

Uchaguzi Bora, Baraka Kubwa Zaidi

Hata hivyo, walikuwako wale ambao walikinza vivutio vya kiuchumi, wakadumisha jamaa zao pamoja, na kuvumilia zile nyakati ngumu. Walijitahidi zaidi tu katika njia zao za kupata riziki nao walibarikiwa sana kwa kufanya hivyo. Fikiria wawili wa wale walioweka vielelezo bora—Milton Alleyne na Fitz Hinds.

Ingawa alikuwa kondrakta stadi na mwenye ujuzi, Milton Alleyne alikinza ile hisi yenye nguvu ya kutaka kuhama. Yeye alikaa katika ujamii ili aweze kusaidia jamaa yake katika njia zaidi ya zile za kiuchumi tu na ili aweze kusaidia ndugu wenyeji. Yeye alidumisha jamaa yake ikiwa pamoja na sasa anapata shangwe ya kuwa na watoto wake wote wanne wakiwa wakfu na kubatizwa na wakiwa watendaji katika ukweli. Wawili wanatumikia sasa wakiwa mapainia wa kawaida na mmoja akiwa painia wa pekee. Ndugu Alleyne sasa hutumikia akiwa mwangalizi msimamizi wa Kundi la Hillaby katika Barbados.

Fitz Hinds pia alionyesha uvumilivu wenye saburi. Yeye amekuwa katika mstari wa mbele katika utendaji wa kitheokrasi, akiandaa uongozi kundini wa miaka zaidi ya 36. Kwa sasa anatumikia akiwa kiongozi wa Funzo la Mnara wa Mlinzi katika Sugar Hill, Barbados, yeye pia amekuwa na shangwe ya kusaidia jamaa yake yote ikue katika ukweli. Wana wake watatu wote ni watumishi wa huduma, na mmoja wa binti zake ni painia wa kawaida. Wengine wa jamaa hushiriki kwa ukawaida utumishi wa painia msaidizi nyakati mbalimbali katika mwaka.

Kwa furaha, inaweza kusemwa kwamba kile kigezo cha miaka ile ya 1950 kufika 1970 kimegeuzwa. Sasa ni wachache zaidi wa wale ndugu wenye bidii na wanaostahili zaidi hufikiria kuhama kwa sababu za kiuchumi pekee.

Baadhi ya wale ambao wametwaa pendeleo la utumishi wa wakati wote wamependelewa kuwa na mazoezi ya Shule ya Gileadi. Inachangamsha moyo kufikiria uhakika wa kwamba tawi la Barbados limepeleka wafanya kazi kumi wa wakati wote Gileadi katika muda wa miaka iliyopita. Ili kuratibu kazi inayopanuka kwa haraka visiwani, wawili wa wahitimu ambao walipewa migawo tena hapa, A. V. Walker na O. L. Trotman, sasa hutumikia katika Halmashauri ya Tawi pamoja na Sven Johansson.

Ni wazi kwamba kazi ya kufanya wanafunzi imesonga mbele vizuri. Akina ndugu wamepata uwezo wa kitengenezo uliohitajiwa nao wametwaa madaraka zaidi kuhusiana na kazi ya Bwana katika hizi siku za kumalizia za huu mfumo mbovu wa mambo.

Baada ya Light, Kazi ya Kufuatia

Wale wamisionari waliokuwa katika ile merikebu Light walifanya kazi yenye thamani visiwani. Hata hivyo, kulikuwako kizuizi kimoja. Katika visiwa hivi vidogo, watu walihangaikia sana ni nani angebatiza vitoto vyao baada ya kuzaliwa na ni nani angewafanyia zile kawaida za ibada za mwisho au kuwazika wafapo. Watu wenye kupendezwa waliojifunza pamoja na wamisionari, ambao baadhi yao walifikia hatua ya kuacha kanisa lao, walihisi wameachwa peke yao wakati wamisionari walipong’oa nanga na kusafiri kwenda kwenye kisiwa kingine. ‘Ni nani atazika wafu wetu sasa?’ wakataka kujua. Hivyo wakarudia kanisa lao.

Kwa sababu hiyo, kufikia 1957 Light makao ya kimisionari ya Sosaiti yenye kuelea baharini ilikuwa imemaliza kazi yayo nayo iliuzwa. Wale wamisionari waliokuwamo merikebuni walipewa migawo kwingineko. Sasa jukwaa ilikuwa imetayarishwa kwa wafanya kazi wa wakati wote wenye makao barani wafuatie kupendezwa kulikoonyeshwa.

Stanley na Ann Carter walipewa mgawo kwenda St. George’s, Grenada. Kwa ushikamanifu na uaminifu walifanya kazi ya kujitaabisha ili kuimarisha akina ndugu. Upesi ile idili iliyotokezwa na wale Mashahidi wenye bidii katika jiji ikaongoza kwenye uhitaji wa mahali pakubwa zaidi pa kukutania. Jumba la Ufalme zuri lilijengwa mahali panapoelekeana na ile bandari yenye kuvutia ya St. George’s nalo liliwekwa wakfu na Robert Wallen wa wafanya kazi wa makao makuu wakati alipozuru akiwa mwangalizi wa eneo la dunia katika Machi 1964.

Marekebisho-upya Yapepeta Nje Wale Wasiotosheka

Uandalizi wa Sosaiti katika 1961 kwa ajili ya mazoezi zaidi kwa njia ya Shule ya Huduma ya Ufalme kwa mapainia wa pekee, wamisionari, na wazee katika kundi ulisaidia sana kuimarisha kazi kitengenezo. Ulisaidia ndugu wenye kustahili kuthamini thamani ya kutia jitihada kukaa pamoja na migawo yao badala ya kuhama kwa sababu ya manufaa za kiuchumi. Uangalifu ulihitaji kutolewa pia kwa habari ya hali zilizohusu wahubiri ambao maisha yao hayakuwa safi kiadili. Nyakati nyingine visa hivyo havikuwa vikishughulikiwa mara hiyo. Kwa hiyo, ule mtaala wa mwezi mmoja ulioandaliwa katika Bridgetown, Barbados, na Kingstown, St. Vincent, ulitoa lile rekebisho-upya la Kimaandiko lililohitajiwa katika maoni.

Wengine walilalamika wakati marekebisho yalipofanywa, lakini wengine walishukuru kwa unyenyekevu kuweza kutumikia Yehova katika cheo chochote. Kama kielelezo, Reuben Boyce anakubali kwamba ndugu mwingine alipochukua daraka la kuwa mwangalizi msimamizi badala yake katika Kundi la Bridgetown, Barbados, hilo lilikuja “likiwa mshangao mkubwa” kwake. Lakini yeye alilikubali kuwa lilifanyika kwa mwelekezo wa Yehova au ruhusa Yake. Kwa upande mwingine, mmoja ambaye hatembei tena katika njia ya ukweli alimwendea Ndugu Boyce kwa hisia-mwenzi za kujisingizia na kusema hivi: “Ilitukia nini? Jamani, kwani walikuondoa?”

Ndugu Boyce aliitikia, “Unamaanisha nini?”

Ndipo yule aliyekuwa akijaribu kuchochea kutoridhika akataarifu hivi: “Hiyo haitoshi! Utafanya nini kwa sababu hiyo?”

Jibu la Ndugu Boyce lilirudisha wonyesho wa mwelekeo wa ushikamanifu wa walio wengi wa akina ndugu wakati aliposema hivi: “Angalia, Bwana! Hili si jambo la kuzungumziwa. Wakati Sosaiti inapomweka mtu rasmi kwenye cheo katika kundi, wao hawakuambii kwamba watakuweka rasmi; hivyo wakati wanapokuondoa, hufanyi matata—wewe unaendelea tu kama kawaida. Kwa hivyo mimi sioni lolote la kuwekea kinyongo.” Nalo likakomesha mazungumzo.

Kwa muda wa miaka iliyopita Ndugu Boyce ameendelea kudumisha ushikamanifu wake kwa Yehova na tengenezo Lake na kunufaishwa na nidhamu iliyohitajiwa. Sasa akiwa kipofu kabisa na mwenye kusonga sana katika umri, anatumikia akiwa mzee. Katika miaka yake ya baadaye amekuwa pia na baraka ya mke wake, ambaye hapo kwanza alikuwa asiyeamini, kuwa Shahidi aliye wakfu na kubatizwa.

Tawi Jipya Lapangwa Kitengenezo

Miongoni mwa Habari za Kitheokrasi katika toleo la Februari 1966 la Huduma ya Ufalme (Chapa ya Trinidadi) mlikuwamo tangazo fupi lakini lenye maana kubwa: “Ofisi ya tawi mpya ilianza kutenda kazi Januari 1, 1966, katika Barbados kuangalia kazi katika Barbados, Bequia, Carriacou, Grenada, St. Lucia na St. Vincent.” Kufikia wakati huo hesabu ya Mashahidi katika visiwa hivi sita ilijumlika kuwa 1,084. Wahubiri hawa walikuwa na mgawo wa kuhubiria idadi ya watu iliyounganishwa ya zaidi ya nusu milioni. Bila shaka, ushuhuda mwingi ulikuwa tayari umetolewa.

Wamisionari wawili walipelekwa Barbados kupanga kitengenezo makao ya kimisionari ambamo ofisi ya tawi ingekuwa. Hao walikuwa Benjamin na Beryl Mason. Ndugu Mason alikuwa amehudhuria madarasa ya 2 na 39 ya Gileadi. Chapa yake ilikuwa bidii kwa huduma. Yeye alionekana ameinama kidogo, na kwa kuwa alikuwa na tabia ya kuwa mwenye ucheshi, alikuwa akisema kwamba sababu ya kuinama kwake ilikuwa “kusonga mbele katika utumishi wa Bwana.”

Tokea pale mwanzo walo wenyewe, lile tawi jipya lilianza mara hiyo kutoa uangalifu zaidi wa kibinafsi kwa akina ndugu, likiangalia zaidi mahitaji yao. Pia kuwa na ofisi ya tawi pale pale katika ujamii wa kisiwa kulimaanisha kupata ugavi wa kundi kwa urahisi zaidi, bila kulazimika kuagiza kutoka Trinidadi na kisha kutegemea utumishi wa upakizi usiotegemeka kati ya visiwa. Haikuchukua muda mrefu kwa ndugu wote katika tawi kuzoelea kuwa sehemu ya ile “jamaa ya tawi” jipya.

Sasa ulikuwa wakati kwa Sosaiti kutia mizizi yenye kudumu katika Barbados. Kisehemu kizuri cha ardhi katika Bridgetown kilinunuliwa kitumiwe kwa ajili ya ofisi ya tawi jipya, kao la kimisionari, na Jumba la Ufalme. Kilikuwa ni kisehemu cha ardhi kile kile ambacho kilikuwa kimekuwa kitovu cha utendaji mwingi wa kitheokrasi kwa zaidi ya miaka 50—makao ya Lucy Gooding.

Ofisi ya tawi ya Barbados iko mahali panapofaa sana katika Bridgetown, jengo moja la mjini kutoka ofisi kuu ya posta na wapata mwendo wa kutembea kwa miguu wa dakika kumi kutoka bandari ya Bridgetown. Mara nyingi sura safi, na nzuri ya majengo hayo huzungumziwa na watu wanapopita—watu ambao pia walitazama jitihada ya ujamii ya Mashahidi katika ujenzi. Makundi yote yalishiriki katika ujenzi wenyewe, na jambo hilo lenyewe lilikuwa ushuhuda mkubwa.

Ule uratibu wa kazi ya ujenzi katika majengo ya tawi na ushirika uliotokeza ulifanya akina ndugu wafikiri kwa uzito zaidi juu ya ujenzi wa Majumba ya Ufalme uliohitajiwa sana. Kwa ghafula waling’amua kwamba ustadi ulipatikana kwa urahisi miongoni mwa akina ndugu kisiwani. Hivyo, katika muda wa miezi 18 baada ya majengo ya tawi kuwekwa wakfu, Majumba ya Ufalme mapya manane yalijengwa katika eneo la tawi. La kwanza kuwekwa wakfu lilikuwa katika Cave Hill, Barbados; mengine yakafuata katika Castries, St. Lucia, pamoja na Grenville, Grenada, kutaja machache tu. Katika eneo lote la tawi sasa kuna Majumba ya Ufalme 28, hivyo kuwezesha makundi yote 33 kukutana katika majengo yanayomilikiwa na akina ndugu.

Mabadiliko ya Kisiasa Kutuzunguka

Kuanzia 1958 yalikuwako mabadiliko makubwa ya kisiasa kotekote katika West Indies. Visiwa kumi vya West Indies, kutoka Jameika katika kaskazini-magharibi kufika Trinidadi katika kusini, viliunganishwa katika muungano wa kisiasa. Lakini ukakosa kufanikiwa, na hivyo ukafumuliwa katika Mei 1962. Badala ya visiwa hivi vyote kuendelea kuelekea uhuru wa kisiasa vikiwa taifa moja, kila kimoja kiliachwa kifuatie uhuru wacho chenyewe. Hivyo, Barbados kikawa taifa huru katika Novemba 30, 1966. Grenada, St. Lucia, na St. Vincent vilifanya hivyo baadaye.

Hata hivyo, matukio haya ya kisiasa hayakuathiri uhusiano miongoni mwa akina ndugu katika vile visiwa mbalimbali. Kabla na tangu uhuru wa kisiasa kwa visiwa hivi, sikuzote akina ndugu wamejitahidi kuishi kupatana na kanuni ya Biblia ya kutokuwamo. Wao wanajua vizuri sana kwamba Kristo alisema hivi kuhusu wafuasi wake: “Wao si sehemu ya ulimwengu, kama vile mimi si sehemu ya ulimwengu.” (Yoh. 17:16, NW) Pia wameongozwa na maneno ya mtume Paulo: “Ikiwa inawezekana, kwa kadiri ambavyo inawategemea nyinyi, iweni wenye kuamanika pamoja na watu wote.” (Rum. 12:18, NW) Kwa kuwa akina ndugu hawakuhusika kisiasa bali walidumisha kutokuwamo kwao kabisa, wamekuja kustahiwa sana, hata ingawa hawapendwi, na serikali ya kisiwa chao. Nyakati fulani, wanasiasa huudhikia akina ndugu kwa kutofanya ule wanaoudhania kuwa wajibu wa kiraia, hasa wakati wa machaguzi ya kimahali. Hata hivyo, akina ndugu hawajapata kamwe kuwa na matatizo mazito juu ya jambo hili.

Katika pindi chache, baadhi ya watoto wa Mashahidi wametishwa kufukuzwa shuleni kwa kujizuia kufanya nadhiri na kula viapo vya utii wa kisiasa. Hilo lilipotokea, ilisaidia kurejezea wasimamizi wa shule, hasa wale walio katika Barbados, kwenye baadhi ya mambo ya katiba ya kisiwa. Wakati wenye mamlaka ya shule walipokumbushwa juu ya haki zilizohakikishwa humo, ni mara chache tulipokuwa na magumu zaidi. Ile broshua Shule na Mashahidi wa Yehova imethibitika kuwa kifaa bora cha kufanya msimamo wetu uwe wazi kwa wasimamizi na walimu wa shule.

Wahitimu wa Gileadi Waweka Kielelezo Kizuri

Visiwa vyote vimenufaishwa na waangalizi wasafirio na wamisionari waliozoezwa Gileadi. Kila mmoja wa hawa amechangia kwa uthabiti uenezaji wa habari njema na uimarishaji wa makundi.

Katika 1960 John na Lynne Mills walikuja Barbados kutoka Trinidadi kufanya kazi ya mzunguko. Na waliifanya kwa kufanikiwa kwa miaka mingi, huku wakiwa na mtoto mchanga.

Richard na Gay Toews waliwasili Barbados katika Februari 21, 1967, wachukue mgawo wao wa kimisionari. Mwaka uo huo Ndugu Toews aliwekwa rasmi asimamie tawi, naye aliangalia vizuri daraka hilo kwa miaka 13. Kama vile mtume Paulo alivyokuwa amemwagiza Timotheo afanye, akina ndugu waliokuwa katika tawi wakati huo walifanya kazi ya kusitawisha na kuzoeza ndugu wenyeji, badala ya wamisionari wa kigeni, wachukue madaraka na kuangalia migawo muhimu.—2 Tim. 2:2.

Gay Toews, dada mpole na mwenye bidii ya kufanya kazi, alithibitika kuwa misionari mzuri wakati wa ile miaka ambayo alikaa Barbados. Alikuja kufahamiana sana na semi za “Kibaja” naye alizitumia mara nyingi katika huduma yake ya nyumba kwa nyumba, hata ingawa nahau za Kibarbado hazikusikika jinsi ile ile zilipotamkwa kwa ulimi wa Mkanada! Yeye alifanikiwa sana katika kuwaelekeza wenye kupendezwa kwenye tengenezo. Kwa sababu ya afya mbaya, baada ya wakati Ndugu Toews na Gay, mke wake, walirudi Kanada ambako sasa wanashiriki kazi ya wilaya.

Kwa sasa tawi la Barbados lina wamisionari kumi na makao matano ya kimisionari. Wanne wa wale waangalizi watano wasafirio wamezoezwa Gileadi. Wengi wa wale wanaotumikia sasa katika utumishi wa wakati wote husema kwamba mojawapo mambo yaliyowachochea wachukue utumishi wa wakati wote ni kile kielelezo chema cha wamisionari.

Kwa msaada huu wote wa kimisionari, ongezeko lingaliweza kuwa kubwa zaidi kama haikuwa kwa sababu ya hali ya ukosefu wa adili ya nyakati hizo. Katika kisiwa kimojapo, asilimia 78 ya watoto wote wenyeji huzaliwa nje ya kifungo cha ndoa. Ingawa dini za Jumuiya ya Wakristo zinakuwa tayari kukubali kwa urahisi ile inayoitwa eti adili mpya, watu wa Yehova hawawezi kufanya hivyo. Katika jitihada ya kulipa staha ya kijamii tokeo la ngono kama hizo za ovyoovyo, serikali ya kisiwa kimoja, iliondoa neno haramu (la kuwaeleza watoto waliozaliwa nje ya kifungo cha ndoa) kutoka vitabu vya kisheria, katika hati ya Mgeuzo wa Sheria ya Jamaa ya hivi majuzi. Kwa hiyo ndugu zetu wamelazimika kukazia ushikamano kwa viwango vya juu vya Yehova vya adili.

Mkusanyiko wa Kimataifa Katika Bridgetown

Ishara nzuri ya ukuzi, ukomavu, na kimo cha kiroho cha akina ndugu katika Barbados ilionyeshwa katika kuwa wakaribishaji wa mmoja wa mfululizo wa mikusanyiko ya kimataifa katika 1978. Akina ndugu walisisimuliwa kuwa na pendeleo hilo, ambalo lilithibitika kuwa fanikio kubwa sana. Wajumbe wengi sana hivyo kutoka ng’ambo walikuwa hawajapata kamwe kuhudhuria mkusanyiko wa aina yoyote katika Barbados. Wajumbe walikuja kutoka mataifa 28.

Ushuhuda mzuri ulitolewa katika mahoteli na kwingineko mamia haya ya wajumbe walipochangamana na watu wa Barbados. Kama tokeo, zaidi ya 6,000 walikuwapo kwa ajili ya hotuba ya watu wote, ambayo ilitolewa na Karl Adams kutoka Betheli ya Brooklyn. Jack Barr na Mildred, mke wake, kutoka London, Uingereza, walihudhuria pia, naye Ndugu Barr aliongoza sehemu kadhaa muhimu za programu. Wakati huo alikuwa akingojea hati rasmi ambazo zingemruhusu aingie United States ili aweze kutumikia akiwa mshiriki wa Baraza Linaloongoza.

Utumishi wa Redio wa Bure Watokeza Ushuhuda

Katika Barbados wakati suala, zoea, au mwadhimisho vinapokuwa vichwa vya mazungumzo, kwa kawaida uandalizi unafanywa ili maoni yanayotofautiana yazungumziwe hewani kwa stesheni za redio. Njia hii ya mazungumzo ya umma imetumiwa kwa matokeo mazuri na watu wa Mungu kutaarifu msimamo wetu juu ya masuala mbalimbali, nalo tokeo la jambo hilo limekuwa kukomeshwa kwa maoni mabaya juu ya kazi yetu. Katika pindi moja tulialikwa kupeleka mwakilishi akatumikie akiwa sehemu ya kikoa ambacho kingezungumzia maswali katika programu ya kuuliza maswali kwa kupiga simu kuhusu habari ya Krismasi, kwa kuwa sisi hatushiki mwadhimisho huo.

Askofu wa Kanisa Anglikana alikuwamo katika kikoa hicho. Kabla ya programu kwenda hewani, ndugu aliyewakilisha Mashahidi alimwendea askofu na kumuuliza anavyopaswa kuitwa. Askofu huyo alieleza kwamba angeweza kuitwa Baba, Askofu, au Reverendi. Ndugu yetu alieleza kwa upole kwamba yeye hangeweza kutumia wowote wa mitajo hiyo ya cheo kwa sababu Biblia haiafikiani na zoea kama hilo. Kwa wazi kasisi huyo aliudhika, kwa hiyo alikwenda kwa msawazishi wa programu na kutaarifu kwamba hangeonekana katika programu hiyo pamoja na Shahidi huyo—ingekuwa ama yeye ama Shahidi. Kwa kuwa ndugu aliyewakilisha Mashahidi alikuwa ndiye peke yake katika kikoa hicho ambaye hakuafikiana na mwadhimisho wa Krismasi, ilikuwa lazima abaki. Hivyo kasisi yule aliondoka studio akiwa ameudhika na kutahayarika sana.

Wakati suala la kutiwa damu mishipani na zoea la ugoni-jinsia-moja yalipokuwa vichwa vya mazungumzo, kwa mara nyingine tena Mashahidi walialikwa wapeleke wawakilishi wakatumikie katika vikao mbalimbali na kutoa maoni ya Biblia.

Kuepuka Vikengeusha-Fikira

Inaweza kusemwa kwa urahisi kwamba tengenezo la kitheokrasi la mahali hapa limetoka mbali wakati wa miaka 84 iliyopita. Ingawa watu wa Mungu hawajapata kuzuiwa kwa njia iliyopangwa kitengenezo katika visiwa hivi, Shetani Ibilisi, hasimu yetu mwenye hila, ametumia vyombo vingine. Yeye ametumia mitego ya hila zaidi—ukosefu wa adili, kutafuta-tafuta makosa, na tafrija yenye kupita kiasi.

Kama kielelezo, mchezo wa kisiwani unaopendwa na watu wengi sana ni kriketi. Unafuatiwa kwa hamu nyingi sana, sana hivi kwamba mwandikaji mmoja alionelea hivi: “Kriketi sana sana ni dini kuliko kuwa mchezo.” Mashabiki wenye idili hufuatia mchezo huo katika redio, televisheni, au kwa kuwapo mwenyewe kwenye uwanja wa mchezo wa kriketi “uliotakaswa” katika Kensington Oval, Barbados. Lakini walio wengi wa akina ndugu, wakijua hali ya mchezo huo yenye kumaliza sana wakati, wamejitahidi kudumisha oni lenye usawaziko kuelekea hii na namna nyinginezo za tafrija ambazo zinaweza kujipenyeza ndani ya maisha ya kiroho ya mtu.

Itikio kwa kazi ya painia msaidizi wakati wa Aprili huonyesha kwamba ndugu zetu hujitahidi kikweli kuweka masilahi ya Ufalme kwanza. Katika Aprili 1988 tawi la Barbados liliripoti kilele cha mapainia wasaidizi 1,009. Hiyo inamaanisha kwamba kwa wastani kulikuwako zaidi ya mapainia wasaidizi 32 kwa kila kundi katika vile visiwa sita vilivyo chini ya uangalizi wa tawi. Wote pamoja, asilimia 46 ya akina ndugu walijitia katika namna fulani ya utumishi wa wakati wote wakati wa mwezi huo. Pasipo shaka utendaji huo wa bidii ulichangia uhakika wa kwamba katika Aprili wa mwaka huo tawi lilibarikiwa kuwa na kilele kipya cha wahubiri 2,571.

Kusimulia Sifa ya Yehova Katika Visiwa

Historia ya Mashahidi wa Yehova sasa ni sehemu ya historia ya Barbados. Hilo bara lililo kama askari aliye kimya aliye kwenye mwingilio wa Bahari ya Karibea limetoa sauti kwa habari njema za Ufalme wa Mungu kwa miongo minane iliyopita. Na kwa sababu ya sauti hiyo kubwa, kisiwa hicho kimekuwa njia-lango kikweli kwa maelfu mengi ambao wamekuja kushangilia “majira ya kuburudisha” kupitia kupata uhusiano mzuri pamoja na Yehova Mungu na Mwana wake, Kristo Yesu.—Mdo. 3:19, NW.

Wakati mrefu uliopita mnabii Isaya aliandika hivi: “Mwimbieni Yehova wimbo mpya, sifa yake toka ncha za dunia . . . Acheni wamhesabie Yehova utukufu, na katika visiwa acheni wasimulie hata sifa yake.” (Isa. 42:10, 12, NW) Sala ya muungano ya wapiga mbiu ya Ufalme wote 2,571 katika eneo hili la tawi ni kwamba baraka ya Yehova iendelee kuwa juu ya jitihada zao za kusimulia sifa yake.

[Sanduku/Ramani katika ukurasa wa 150]

Muhtasari wa Tawi la Barbados

Mji Mkuu wa Barbados: Bridgetown

Lugha Rasmi: Kiingereza

Dini Kubwa: Anglikana

Idadi ya Watu Iliyounganishwa: 629,184

Wahubiri: 2,571

Mapainia: 299

Makundi: 33

Hudhurio la Ukumbusho: 8,065

Ofisi ya Tawi: Bridgetown

[Ramani]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

BAHARI ATLANTIKI

BARBADOS

Bathsheba

Holetown

Bridgetown

ST. LUCIA

Castries

Micoud

ST. VINCENT

Kingstown

BEQUIA

Port Elizabeth

GRENADINES

CARRIACOU

GRENADA

Grenville

St. George’s

BAHARI YA KARIBEA

[Picha ya ukurasa mzima katika ukurasa wa 148]

[Picha katika ukurasa wa 153]

Lina “Mami” Gaul, kushoto, na Waldemar Rice, Mashahidi wa mapema katika Barbados

[Picha katika ukurasa wa 155]

Lucy Gooding, ambaye nyumba yake ilitumiwa kuwa makao ya misionari

[Picha katika ukurasa wa 156]

Winfred Heath, aliyebadili maisha yake ili astahili kubatizwa katika 1940

[Picha katika ukurasa wa 158]

Chriselda James wa Grenada alilea watoto kenda katika ukweli

[Picha katika ukurasa wa 159]

E. J. Coward, kutoka makao makuu ya Brooklyn, alitumikia visiwa vya Karibea ya mashariki

[Picha katika ukurasa wa 161]

Philippa “Mama Lab” La Borde, Shahidi tangu 1918, alitumika katika St. Vincent kwa miaka 50

[Picha katika ukurasa wa 165]

Cuthbert Blackman alitumia mkokoteni wenye kukokotwa na farasi kwa ajili ya kazi ya painia

[Picha katika ukurasa wa 170]

Frank Gall, kushoto, mmojapo Wabarbado wa kwanza wahitimu wa Gileadi, na Dudley Mayers aliyesaidia kufanyiza makundi ya mapema katika Barbados

[Picha katika ukurasa wa 173]

Richard Ryde, kushoto, na Sven Johansson walipelekwa Grenada wakiwa wamisionari katika 1949

[Picha katika ukurasa wa 175]

Lloyd Stull, mmojapo wamisionari wa kwanza kupelekwa St. Lucia

[Picha katika ukurasa wa 180]

“Sibia,” merikebu ya meta 20 iliyo- tumiwa katika kazi ya kimisionari

[Picha katika ukurasa wa 183]

“Light,” chombo cha rafardha mbili kilichochukua mahali pa “Sibia”

[Picha katika ukurasa wa 184]

Washiriki wa Halmashauri ya Tawi: A. V. Walker, kushoto; O. L. Trotman; na Sven Johansson

[Picha katika ukurasa wa 188]

Benjamin na Beryl Mason, waliosaidia kupanga kitengenezo kao la kimisionari

[Picha katika ukurasa wa 191]

Richard na Gay Toews, wamisionari waliopewa mgawo Barbados katika 1967, sasa wanatumikia Kanada

[Picha katika ukurasa wa 192]

Majengo ya tawi na Jumba la Ufalme katika Bridgetown, Barbados

[Picha katika ukurasa wa 193]

“Imani Yenye Ushindi” Mkusanyiko wa Kimataifa wa 1978, Stediamu ya Kitaifa, Barbados

[Picha katika ukurasa wa 194]

Pwani Bathsheba, katika upande wa Barbados wa Bahari Atlantiki

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki